Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MTIHANI: Mwakinyo, wenzake na msoto nyuma ya nondo

MWAKINYO Pict

Muktasari:

  • Duniani kote watu wanafahamu mchezo wa ngumi umejaa ‘unyama’ kutokana na watu wake wengi hasa wachezaji kwa maana ya mabondia kutoka kwenye maisha ya hali ya chini na tumaini pekee kwao ni nguvu zao ili kufikia mafanikio wanayotaka.

KATIKA maisha unaweza kufanya jambo likachafua taswira nzima ya jina na uhalisia wako, huenda kwa akili zako timamu au kwa kusingiziwa, lakini kitendo cha kuhusika tayari heshima inakuwa imepungua.

Duniani kote watu wanafahamu mchezo wa ngumi umejaa ‘unyama’ kutokana na watu wake wengi hasa wachezaji kwa maana ya mabondia kutoka kwenye maisha ya hali ya chini na tumaini pekee kwao ni nguvu zao ili kufikia mafanikio wanayotaka.

Angalia historia ya bondia wa zamani duniani, Muhammad Ali namna alivyoishi maisha ya ubishi na misimamo mikali na wakati mwingine kuonekana mtukutu kupindukia.

Lakini pia mwangalie Mike Tyson ‘Iron’ alivyokuwa mkorofi kupindukia kabla kufungwa gerezani miaka sita kwa kesi ya kubaka hukumu ambayo aliitumikia miaka mitatu kabla ya kutoka kwa msamaha ambao kiasi fulani ulirekebisha taswira ya maisha yake.

Matukio yenye utata kwa mabondia yapo kila sehemu ingawa ukweli ni kwamba sheria za mchezo huo haziruhusu kujishughulisha na ugomvi mitaani japo tabia hiyo imekuwa ngumu kupotea.

Tanzania ilimpoteza bondia Thomas Mashali kutokana na kupigwa hadi kufa na kundi la vijana kwa madai ya wizi 2016.

Lakini, tukio la karibuni linamhusu bondia Hassan Mwakinyo anayeshikiliwa katika Kituo cha Polisi Chumbageni, Tanga, akituhumiwa kumshambulia mtu anayedaiwa kuingia katika eneo lake bila ridhaa yake akimtuhumu kuwa ni mwizi na kumsababishia kile kinachodaiwa kuwa majeraha mwilini mwake.

Mwakinyo anashikiliwa na jeshi hilo tangu Alhamisi, Machi 6, 2025, huku mtu anatedaiwa kumshambulia akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo mjini Tanga.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mabondia wa Tanzania ambao waliwahi kushikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na matukio mbalimbali waliyowahi kuyafanya.

MWAKI 02

FRANCIS CHEKA

Mwaka 2015, bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka ‘SMG’ alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kumpiga meneja wake wa baa yake, Bahati Kibanda.

Cheka alitiwa hatiani kwa kumpiga na kumsababishia maumivu makali Kibanda ambaye alikwenda hapo kudai fedha zake katika baa aliyokuwa anaifanyia kazi mjini Morogoro.

Cheka ambaye alikuwa anashikilia mkanda wa WBF wakati huo alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro kwa shitaka hilo lililosomeka kuwa ni la shambulio la kudhuru mwili na kujeruhi.

Mbali ya hukumu ya kifungo cha miaka mitatu, mahakama ilimuamuru alipe fidia ya Sh1 milioni ambapo hata hivyo bondia huyo alitumikia kifungo hicho kwa kukaa gerezani siku 42 kabla ya kukata rufaa ya hukumu hiyo, kisha akahukumiwa kifungo cha nje.

Baada ya kutoka gerezani, Cheka aliendelea na mchezo huo kabla ya kuachana nao 2018 baada ya kupigwa knockout (KO) na Dullah Mbabe, akaenda zake kwa mama yake nchini Msumbiji anakoishi hadi sasa.

Bondia huyo aliachana na mchezo huo akiwa amepigana mapambano 49, akifanikiwa kushinda 34 kati ya hayo 18 ni kwa knockout na kupigwa mara 13, kati hayo manane kwa knockout huku akitoka sare mawili.

MWAKI 03

HASSAN MWAKINYO

Bahari imechafuka upande wa bingwa wa WBO Afrika, Hassan Mwakinyo kutokana na kuendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumshambulia Mussa Ally, mkazi wa Sahare mjini Tanga anayedaiwa kumtuhumu kuwa mwizi.

Mwakinyo aliwekwa mahabusu tangu Machi 6, mwaka huu ambapo Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga kupitia Kaimu Kamanda wa Polisi, Almachius Mchunguzi, lilisema bondia huyo anatuhumiwa kumshambulia na kumjeruhi Mussa aliyejitambulisha kuwa ni mvuvi.

Kijana anadaiwa kujeruhiwa alipopita kwenye makazi ya Mwakinyo huku kamanda akibainisha kuwa uchunguzi utakapokamilika watatoa taarifa kwa vyombo vya habari ikiwa ni sambamba na kumfikisha mahakamani ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

Kamanda Mchunguzi alisema walimkamata Mwakinyo kwa tuhuma za kumjeruhi mvuvi, ambapo ni tuhuma za jinai akifafanua kuwa mtu yeyote akifanya makosa kama hayo bila kuangalia nafasi yake kwenye jamii inatakiwa achukuliwe hatua za kisheria na suala la umaarufu haliwezi kubadili kile kilichotendeka.

Mwakinyo amecheza mapambano 27 akiwa ameshinda 24, kati ya hayo 17 ni kwa knockout, amepigwa mapambano matatu kati ya hayo mawili yakiwa kwa knockout.

Bondia huyo mwenye hadhi ya nyota tatu ndiyo namba moja kwenye uzani wa middle kati ya mabondia 49 kwa uzito huo wakati duniani akiwa wa 25 kati ya mabondia 1999 huku akiwa na uwezo wa kupiga kwa knockout asilimia 70.

MWAKI 01

FADHILI CHAMILE

Huenda siyo maarufu na hana jina kubwa, lakini Fadhili Chamile ni mmoja kati ya mabondia wachanga waliokuwa na uwezo mkubwa akipotea kwa tuhuma ya kesi ya mauaji.

Miaka mitatu iliyopita bondia huyo alikuwa ni mmoja kati ya watu sita waliokamatwa na kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya kinyozi aliyefahamika kwa majina ya Mwinyi Mpeku katika tukio lililotokea Manzese, Dar es Salaam.

Tukio hilo ambalo lilitokea katika mitaa ya Manzese, huku chanzo cha mauaji hayo kikitajwa kuwa Mwinyi alipigiwa kelele za mwizi, jambo lililosababisha kupokea kipigo kilichosababisha kifo chake.

Inaelezwa kuwa katika kumpiga ndipo vijana wa bodaboda wanaoegesha katika eneo lilipotokea tukio hilo ambao wanadaiwa kushiriki akiwemo Chamile ambaye ni mmoja wa waendesha bodaboda kwenye kijiwe hicho ambaye kwa sasa inadaiwa anatumikia kifungo.

Kabla ya tukio hilo, Chamile alicheza mapambano 15 akiwa amefanikiwa kushinda sita kati ya hayo mawili kwa knockout, akipigwa katika mapambano matatu huku akitoka sare sita.


BATO TWEVE

Kama uliusikia ule msala wa jaribio la utekaji wa mfanyabiashara Deogratius Tarimo katika eneo la Kiluvya, Dar es Salaam, basi bondia Bato Tweve alidaiwa kuwa mmojawao.

Tweve mwenye rekodi ya kucheza mapambano sita akiwa ameshinda manne kati ya hayo mawili kwa knockout, huku akipigwa mara mbili - moja kwa knockout alitambuliwa kuhusika katika tukio hilo kupitia taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es salaam kupitia Kamanda Jumanne Muliro kabla ya kupelekwa mahakamani.


ISAAC MWAIFANI

Katika mchezo wa ngumi za kulipwa, wengi wanamuita ‘Jitu la Mtumba’ ambaye ni kiboko ya Shaban Kaonekana.

Mwaifani mwenye rekodi ya kucheza mapambano saba akiwa amefanikiwa kushinda manne, kati ya hayo mawili kwa knockout na kutoka sare mara tatu ilhali hajawahi kupigwa, alikuwa ni miongoni mwa mabondia watatu waliokamatwa na Jeshi la Polisi katika sakata la jaribio la utekaji dhidi ya mfanyabiashara, Deogratius Tarimo.


BENKI MWAKALEBELA

Rekodi zinaonyesha kwamba Benki Mwakalebela amecheza mapambano 15 ya ngumi akiwa amefanikiwa kushinda 13 kati ya hayo 10 akiondoka na ushindi wa knockout, huku akipigwa mara mbili - zote ikiwa ni knockout.

Mwakalebela ni mmoja kati ya mabondia watatu waliokaa rumande kabla ya kupelekwa mahakamani katika sakata la jaribio la utekaji dhidi ya mfanyabiashara Deogratius Tarimo ambalo lilitikisa katika Jiji la Dar es Salaam.