Mtendawema: Una Mayele, Feitoto unakosaje ubingwa?

HUENDA kwa kizazi cha sasa ni ngumu kumtambua, lakini kwa wale vijana wa zamani waliokuwa vichaa wa soka jina la Willy Mtendemema sio geni kwao.
Wanamkumbuka mwamba huyu aliyekuwa beki wa kati ya Yanga aliyejijengea jina na heshima kubwa kwenye familia ya soka kwa uwezo wake uwanjani katika kukaba washambuliaji hatari, kuanzisha mashambulizi na utamu zaidi ni umaridadi aliokuwa nao.
Ilikuwa ni nadra kumuoa Mtendamema ambaye majina yake kamili ni Williams Huberts Mtendamema akiwa kachafuka, licha ya kuifanya kazi yake kwa ufanisi kwa dakika zote 90 ama 120 za pambano la soka.
Wenzake walikuwa wakimuita ‘bishoo’, neno lililokuwa likimtambulisha mtu maridadi, yaani sharobaro wa kisasa, kutokana na kupenda kwake kunyoa nywele kwa mtindo wa panki, huku akitembea kwa kudundika kama anayeiogopa ardhi.
Licha ya kuwa bishoo, lakini Mtendamema alikuwa mmoja ya mabeki visiki enzi akicheza akitumia akili, maarifa na kipaji na ni nadra kumuona akitumia nguvu kama ilivyo desturi wa mabeki wa kati wa zamani waliozoea vurugu.
Mwanaspoti limemuibukia beki huyo wa kimataifa wa Tanzania aliyeanza kucheza soka klabu ya AICC kabla ya kuonwa na mabosi wa Jangwani na kumbeba miaka 1990 na kufunguka mambo mengi.
Amezungumzia safari yake kisoka na jinsi anavyoiangalia Yanga ya sasa na kueleza ni miujiza pekee inayoweza kuinyima ubingwa msimu huu kutokana na kuwa na majembe ya maana yenye uwezo wa kuipa matokeo ya kusisimua.
MTENDAMEMA
Beki huyo aliyekuwa na mwili wa kimichezo, kuna baadhi wanadhani jina la Mtendamema ni a.k.a pengine kwa jinsi alivyokuwa akicheza kwa ustaarabu kama baba paroko, lakini ukweli hilo ni jina lake halisi.
“Mimi naitwa Williams Huberts Mtendamema,” anasema kwa upole kuonyesha jina hilo lilivyobeba maisha yake halisi, yaliyojaa huruma na hofu ya Mungu kwa kila jambo analolifanya.
Mtendamema ni jina la ukoo wa baba yake (Huberts), ambaye alisomea upadri, lakini hakuifanya kazi hiyo, kutokana na kupingwa na mama yake ambaye ni bibi wa staa huyo.
“Bibi mzaa baba alimkataza mzee asifanye kazi ya upadri alitaka aoe ili azae watoto ukoo upanuke, ndipo alipomuoa mama yangu ambaye naye baba yake alikuwa mzee wa kanisa kwa kifupi ukoo wetu wote ni watu wa dini, ukiwaona ndugu zangu ni kama mimi.”
Mwanaspoti liligundua uhalisia wa jina hilo la Mtendemema wakati wa mahojiano yaliyofanyika nje ya ofisi zake zilizopo Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, kwani jamaa ni mtaratibu, mkarimu na muda mwingi anasisitiza utu.
“Kuna wakati huruma yangu inaniponza, wapo wanaoitumia vibaya kwa kujinufaisha na kuniumiza, ila sijaacha kumtegemea Mungu na kuwasamehe,” anasema.
Anasema wazazi wake waliotangulia mbele za haki, walimjenga kutoyumbishwa na vitu vinavyoweza kuondoa utu wa mtu.
“Kilichonisaidia wakati nacheza Yanga sikutafuta umaarufu, bali umaarufu ulinifuata wenyewe, nilijitambua napaswa kufanya nini, hata mke niliyeoa hakujua kabisa soka, alikuwa binti wa kawaida kabisa mtaani kwetu,” anasema.
Anafunguka mengi, huku akishauri mastaa wa sasa wanaocheza beki ya kati, kuachana na soka la rafu, badala yake wajifunze maarifa na mbinu zitakazowasaidia wasitumie nguvu nyingi wakati wa uwajibikaji.
“Soka linahitaji akili zaidi ili mashabiki waburudike, ili wacheze kwa akili wanapaswa kujituma kwa bidii mazoezini na siyo kufanya vitu kwa kubahatisha vinavyowafanya kuwa na hasira muda wote uwanjani,” anasema.
KIDOGO ATUE SIMBA
Anasema kabla ya kujiunga na Yanga mwaka 1991, Simba ilikuwa ya kwanza kuhitaji huduma yake, lakini chelewachelewa yao ikawapa nafasi vijana wa Jangwani kumbeba kiulaini.
Anasema ilikuwa kipindi cha michuano ya Kombe la AICC iliyokuwa ikifanyika kila mwaka miaka ya nyuma jijini Arusha, ndipo alipoonwa na klabu zote akiwa na timu ya AICC iliyo Daraja la Tatu.
Michuano hiyo ilikuwa ikishirikisha klabu za Tanzania na zile za Kenya na Uganda na mwaka 1989 Simba na Yanga zilivaana fainali na Yanga kushinda kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Joseph Machela.
“Nilifuatwa na kocha Abdallah Kibadeni, akaniambia anataka niichezee Simba, ila hakunipa mkataba zaidi ya mali kauli, tofauti na Yanga ambao kocha Syllersaid Mziray (marehemu) akanichukua na kunipeleka Dar es Salaam.”
ALIVYOTUA YANGA
Anasema anakumbuka baada ya michuano ya AICC kumalizika, viongozi wa Yanga walimfuatilia zaidi walipoenda jijini humo (Arusha) kucheza mechi ya ligi dhidi ya Ndovu, kabla ya mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara.
Anasimulia kabla ya mechi hiyo, Yanga ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya AICC iliyokuwa Daraja la Tatu na ndipo wakapata muda wa kuzungumza naye.
“Ilikuwa ni kawaida timu yoyote ya Ligi Kuu (enzi hizo Daraja la Kwanza) ikija Arusha kucheza na Ndovu, sisi AICC tulikuwa tunatangulia kucheza nao mechi ya kirafiki, tulipocheza na Yanga viongozi na benchi la ufundi likaona kipaji changu,” anasema na kuongeza;
“Wakamaliza mechi yao na Ndovu, wakaondoka kurejea Dar es Salaam, ikapita kama wiki ndipo marehemu Mziray akaja kunichukua kurudi naye Dar, ili kufanya nao mazungumzo na kjiunga nao.”
YANGA YA SASA
Anasema Yanga ya sasa ni tofauti na ya misimu mitatu nyuma, kwamba sasa unaweza kuona kila mchezaji anawajibika ipasavyo kwenye nafasi yake, huku kukiwa na ushindani mkubwa wa namba kwa sababu wachezaji wengi waliopo kikosini wana ubora wa hali ya juu.
Mtendamema anaamini ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu upo mikononi mwa Yanga, endapo kama wachezaji hawatabweteka.
“Mchezaji kama Fiston Mayele ni mkombozi wa timu, straika kazi yake ni kufunga, na anapokuwa msumbufu kwa mabeki, akikabwa inawapa nafasi wachezaji wengine kufunga.” anasema gwiji huyo wa zamani wa timu ya taifa.
Anasema kikosi cha Yanga kwa kuwa na wachezaji wenye vipaji vikubwa kama Mayele, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Saidi Ntibazonkiza, Khalid Aucho, Yannick Bangala, Dickson Job, Bakari Nondo Mwamnyeto na makipa Djigui Diarra na Aboutwalib Mshery na wengineo, Yanga ina kila sababu ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu kama wachezaji hao watadumisha nidhamu ya kila mchezo.
Kwa upande wa Simba, Mtendamema anasema anawaelewa sana Shomary Kapombe na Rally Bwalya.
“Japo hatajwi sana ila Bwalya kwa jicho la soka ni mchezaji hatari zaidi, anafanya kazi kubwa zaid,” alisema.
Usikose mwendelezo wa makala haya kesho.