Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtaomba po!... Moto wa Simba si mchezo, Yanga, Azam  kwa mbaaali

Po Pict
Po Pict

Muktasari:

  • Msimu huu unaonekana kuwa mgumu zaidi kwani hadi sasa tumeshuhudia timu zote zimeonja ladha ya kipigo angalau kimoja wakiwemo wakongwe Simba na Yanga.

VITA ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara sambamba na tuzo nyingine binafsi inaonekana kuwa ngumu kutokana na ushindi uliopo hadi sasa.

Msimu huu unaonekana kuwa mgumu zaidi kwani hadi sasa tumeshuhudia timu zote zimeonja ladha ya kipigo angalau kimoja wakiwemo wakongwe Simba na Yanga.

Yanga ambayo juzi ilifungwa juzi 3-1 na Tabora United nyumbani, namba zake katika uwanja wa nyumbani zinamuhukumu wakati wenzao Simba nyumbani fresh.

Wakati Nyumbani mambo yakiwa magumu, Yanga ugenini wamefanya kweli.

Ni wazi kila mmoja anafahamu kwamba Simba ndiyo vinara wa Ligi Kuu Bara kwa sasa wakati timu hiyo ikikusanya pointi 25 ikifuatiwa na Yanga yenye 24, kila moja ikicheza mechi 10.

Wakongwe hao wa soka la Bongo, wamekuwa wakikimbizana kila mmoja akipigia hesabu ubingwa wa ligi hiyo unaoshikiliwa na Yanga ambao ni mabingwa watetezi.

Simba ilirejea kileleni baada ya kukosekana hapo kwa takribani siku 56 kwani mara ya mwisho ilishushwa Septemba 11 mwaka huu. Ikarejea Novemba 6.

Ikiwa hivi sasa Ligi Kuu Bara imesimama kwa takribani wiki mbili kupisha mechi za kuwania kufuzu Afcon 2025, tayari tumemaliza mzunguko wa 11 licha ya kwamba kuna baadhi ya timu zimecheza mechi pungufu ya hizo kutokana na sababu mbalimbali.

Ukiangalia Simba kati ya mabao 21 yaliyofungwa na timu hiyo, kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ahoua ametisha kwa kuhusika katika mabao 9 akifunga matano na asisti nne.

Kule Fountain Gate ambapo kuna kinara wa mabao ndani ya Ligi Kuu Bara mpaka sasa, Seleman Mwalimu aliyefunga sita, wanaye mwamba mwingine Salum Kihimbwa ambaye ndiye amehusika kwenye mabao mengi.

Kihimbwa ambaye anacheza nafasi ya winga kikosini hapo, amehusika kwenye mabao saba kati ya 20 yaliyofungwa na timu hiyo huku akifunga matatu na asisti nne.

Baada ya kumalizika kwa mzunguko wa 11, tunakupitisha katika mambo kadhaa yaliyojiri katika ligi hiyo hadi sasa.

PO01
PO01

SIMBA NYUMBANI FRESH

Ukiangalia kwa timu zinazotumia vizuri uwanja wake wa nyumbani, Simba imeonekana kuwa juu ya wenzake kwani imefanikiwa kukusanya pointi nyingi zaidi ambazo ni 13 ikicheza mechi sita, imeshinda 4, sare moja na kupoteza moja.

Wapinzani wao wa jadi, Yanga katika mechi za Nyumbani, wameshinda tatu na kupoteza mbili kati ya tano walizocheza na kukusanya pointi tisa. Katika msimamo wa timu zilizofanya vizuri zaidi Nyumbani, Simba inashika nafasi ya kwanza wakati Yanga ni ya sita. Kipigo cha juzi dhidi ya Tabora United ndiyo kimewatibulia zaidi, endapo wangeshinda wangekuwa nyuma ya Simba kwa tofauti ya pointi moja

Wakati Simba ikifanya vizuri nyumbani, Pamba Jiji inatia huruma kwani mechi tano haijashinda hata moja ikiwa ndiyo timu pekee haijaonja ladha ya ushindi nyumbani, ikiambulia sare nne na kupoteza moja ikikusanya pointi nne, inafuatiwa na KenGold iliyoshinda moja Nyumbani, sare mbili na kupoteza mbili katika mechi tano na kukusanya pointi tano.


5 ZA JUU WAKALI NYUMBANI

                                       P       W      D      L       F       A       Pts

1.Simba                        6         4        1        1        16      3        13

2.Singida BS                6         3        2        1        7        3        11

3.Fountain Gate          6         3        2        1        13      10      11

4.Tabora United           5         3        1        1        4        3        10

5.KMC                           5         3        1        1        4        5        10



5 ZA CHINI DHAIFU NYUMBANI

                                       P        W      D      L       F       A       Pts

12. Kagera Sugar         5        2        1        2        4        4        7

13.TZ Prisons               6        2        1        3        5        7        7

14.Namungo                 5         2        0        3        3        5        6

15.KenGold                    5         1        2        2        5        7        5

16.Pamba Jiji                5         0        4        1        3        4        4

PO02
PO02

YANGA ZAO UGENINI

Wakati Simba wakitamba nyumbani kwa kukusanya pointi nyingi, Yanga wametisha ugenini kwa kushinda mechi zote tano walizocheza wakipata pointi 15 wakifunga mabao sita, hawajaruhusu nyavu zao kutikiswa.

Hata hivyo, Simba nao ugenini wapo vizuri kwani katika mechi nne walizocheza wameshinda zote wakikusanya pointi 12, wakifunga mabao matano, hawajaruhusu bao lolote. Tofauti yao ipo katika mabao ya kufungua, Yanga inayo sita na Simba matano.

Kwa timu ambazo hazijaonja ladha ya ushindi ugenini kuna Dodoma Jiji, Coastal Union, Tanzania Prisons, JKT Tanzania, Kagera Sugar na KenGold.


5 ZA JUU WAKALI  UGENINI

                                   P        W      D      L       F       A       Pts

1.Yanga                     5        5        0        0        6        0        15

2.Azam                      6        4        2        0        8        0        14

3.Singida BS              4        4        0        0        6        1        12

4.Simba                      4        4        0        0        5        0        12

5.Tabora United 6      2        1        3        8        12      7


5 ZA CHINI DHAIFU UGENINI

                                      P        W      D      L       F       A       Pts

12.Coastal Union        5        0        3        2        4        6        3

13.Namungo                5        1        0        4        2        7        3

14.JKT Tanzania          5        0        2        3        1        5        2

15.Kagera Sugar          5        0        1        4        2        7        1

16.KenGold                   6        0        0        6        2        13      0

PO04
PO04

WAZAWA NOMA SANA

Katika raundi 11 zilizochezwa, hadi sasa yamefungwa jumla ya mabao 164, kati ya hayo matatu ni ya kujifunga. Katika orodha ya mabao, wachezaji wazawa wameonekana kukimbiza wakifunga 96, huku wageni wakifunga mabao 65.

Seleman Mwalimu wa Fountain Gate ndiye amewabeba wazawa akifunga mabao sita akiongoza chati ya jumla ya ufungaji.

Mwalimu ameyafunga mabao hayo dhidi ya Namungo (Agosti 29, 2024), KenGold           (Septemba 11, 2024), Dodoma Jiji (Septemba 15, 2024), Kagera Sugar (Septemba 27, 2024) Tanzania Prisons (Oktoba 1, 2024) na KMC (Oktoba 21, 2024).

Chini ya mwalimu, kwa wachezaji wazawa anayefuatia ni nyota mwingine wa Fountain Gate Edgar William mwenye manne. Wengine ni Paul Peter (Dodoma Jiji), Maabad Maulid (Coastal Union), Nassor Saadun, Joshua Ibrahim (KenGold), Salum Kihimbwa (Fountain Gate) na Offen Chikola (Tabora United) wenye matatu kila mmoja.

Kwa upande wa nyota wa kigeni, Jean Charles Ahoua wa Simba anaongoza akifunga matano akiwafunga Fountain Gate (Agosti 25, 2024), Dodoma Jiji (Septemba 29, 2024), Namungo (Oktoba 25, 2024) na KMC (Novemba 6, 2024) alipofunga mawili. Kati ya mabao hayo, mawili ni ya penalti dhidi ya Dodoma Jiji na KMC.

Wanaomfuatia Ahoua kwa wageni ni Peter Lwasa (Kagera Sugar – 4), Elvis Rupia (Singida Black Stars), Maxi Mpia Nzengeli (Yanga) na Marouf Tchakei (Singida Black Stars) ambao kila mmoja ana matatu.


WAMEJIWEKA WENYEWE

Katika harakati za mapambano ndani ya uwanja, mambo mengi yanatokea ambapo Kipindi cha kuokoa hatari wachezaji wanajikuta wakijifunga.

Waliokutana na msala huo wapo watatu ambao ni kipa wa Dodoma Jiji, Daniel Mgore aliyejifunga dhidi ya Mashujaa katika mchezo uliopigwa Agosti 17, 2024. Wengine ni Fredy Tangalo wa KMC aliyejifunga Septemba 19, 2024 katika mchezo dhidi ya Azam na Kelvin Kijili wa Simba aliyefanya hivyo dhidi ya Yanga, Oktoba 19, 2024.


WAPISHI WA MABAO

Katika kusaka mabao, kuna wale wapishi ambao ndiyo wakali wa kuwatengenezea nafasi wenzao kucheka na nyavu ambapo hadi sasa, kuna nyota watatu wapo pale juu.

Wachezaji hao wenye asisti nyingi ni Jean Charles Ahoua wa Simba, Feisal Salum (Azam) na Salum Kihimbwa (Fountain Gate), hawa wote wanazo nne kila mmoja.

PO05
PO05

SPIDER MFALME MPYA

Msimu uliopita, kipa wa Coastal Union, Ley Matampi alimaliza ligi akiwa na clean sheet 15 akaibuka kinara upande huo akifuatiwa na Djigui Diarra wa Yanga aliyekuwa na 14.

Msimu huu, Matampi hajaanza vizuri akiwa na clean sheet moja peke huku kipa wa Simba ambaye ni ingizo jipya, Moussa Camara akionekana kuanza kujitengenezea ufalme wake.

Camara ambaye amefanikiwa kucheza mechi zote kumi za Simba kwa dakika 900, ameruhusu mabao matatu pekee dhidi ya Coastal Union (2) na Yanga (1), huku akiondoka na clean sheet 8.

Kipa huyo raia wa Guinea, amezikusanya clean sheet hizo katika mchezo dhidi ya Tabora United, Fountain Gate, Azam, Dodoma Jiji, Tanzania Prisons, Namungo, Mashujaa na KMC.


KADI NYEKUNDU 7

Msimu huu hadi sasa, zimeonyeshwa kadi saba kwa wachezaji tofauti ndani ya Ligi Kuu Bara zikiwemo mbili kwa makipa, Denis Richard (JKT Tanzania) na Victor Sochima (Tabora United). Kadi ya kwanza alionyeshwa beki wa Azam, Cheikh Sidibe. Wengine ni Saleh Masoud (Pamba Jiji), Ibrahim Elias (KMC), Ibrahim Hamad 'Bacca' (Yanga) na Abalkassim Suleiman (Fountain Gate). Hakuna timu ambayo hadi sasa yenye kadi nyekundu mbili.

PO03
PO03

PENALTI 26

Katika mechi 81 zilizochezwa, zimepigwa penalti 26, kati ya hizo 19 zimejaa nyavuni na 6 wapigaji wakikosa. Timu ya kwanza kufaidika na mkwaju wa penalti ni Namungo ilipocheza dhidi ya Tabora United, Agosti 25 mwaka huu ambapo Djuma Shaban akafunga.

Waliokosa katika hizo penalti stia ni Moubarack Amza (Namungo), Djuma Shabani (Namungo FC), Heritier Makambo (Tabora United), Hassan Dilunga (JKT Tanzania), Maabad Maulid (Coastal Union) na Stephen Aziz Ki (Yanga).

Waliopata ni Djuma Shabani (Namungo), Heritier Makambo (Tabora United), Maabad Maulid (Coastal Union), Shedrack Asiegbu (Tabora United), Salum Kihimbwa (Fountain Gate), Hassan Dilunga (JKT Tanzania), Jean Charles Ahoua (Simba), Nurdin Chona (Tanzania Prisons), Stephane Aziz KI (Yanga), Leonel Ateba (Simba), Marouf Tchakei (Singida BS), Ismail Mgunda (Mashujaa), Morice Chukwu (Tabora United), Feisal Salum (Azam FC), Joshua Ibrahim (KenGold), Heritier Lulihoshi (Dodoma Jiji), Jumanne Elifadhili (Tanzania Prisons), Morice Chukwu (Tabora United) na Jean Charles Ahoua (Simba).

Katika penalti 26, Tabora United ndiyo iliyofaidika zaidi ikiwa nazo tano, zikiwa ni nyingi kuliko timu zote hadi sasa, ikifuatiwa na Simba na Namungo ambazo kila moja ina 3. Yanga inazo mbili kama ilivyo kwa Coastal Union, JKT Tanzania na Tanzania Prisons. Timu ambazo hazija hata penalti moja ni KMC Kagera Sugar na Pamba wakati Azam, Fountain Gate, Mashujaa, Dodoma Jiji, Sngida Black Stars na KenGold zikiambulia mojamoja.

Kwa upande mwingine, Fountain Gate, Tabora United, Coastal Union na KenGold ndio timu zilizopigiwa penalti nyingi hadi sasa ambapo kila moja imewatokea mara tatu.


WASIKIE BODI YA LIGI

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Almas Kasongo, amesema msimu huu ushindani ni mkubwa kulinganisha na msimu uliopita, hiyo inachangiwa na namna timu nyingi zilivyojiimarisha.

Kasongo alibainisha kwamba, ushindani wa sasa utaongezeka zaidi miezi mitatu ya mwisho wakati ligi ikielekea ukingoni kwa maana ya Machi, Aprili na Mei mwakani.

“Ligi imekuwa na ushindani mkubwa kulinganisha na msiu uliopita, tulipofika hapa unaweza kuona timu zote angalau zimepoteza mechi moja, msimu uliopita Kipindi kama hiki kuna timu zilikuwa hazijapoteza.

“Pia unaweza kuona ushindani mkubwa uliopo huku baadhi ya mechi zikiamulia dakika za jioni, hii inadhihirisha ushindani ni mkubwa.

“Kile ambacho Watanzania walikuwa wakikitarajia kukiona katika ligi yao ushindani ndio huu.

“Matarajio yetu ni kuona mzunguko wa pili ushindani utakuwa mkubwa hasa mwezi Machi, Aprili na Mei kwa sababu ndiyo Kipindi ambacho timu zinapigia hesabu ubingwa, zingine hazitaki kushuka daraja wala kuwepo katika play off,” alisema Kasongo.


MSIMAMO ULIVYO

                             P       W      D      L       F       A       Pts

1.Simba                10      8        1        1        21      3        25

2.Yanga               10      8        0        2        14      4        24

3.Singida BS        10      7        2        1        13      4        23

4.Azam                10      6        3        1        13      3        21

5.Fountain Gate  11      5        2        4        20      20      17

6.Tabora United 11      5        2        4        12      15      17

7.KMC                11      4        2        5        8        16      14

8.Mashujaa          10      3        4        3        9        7        13

9.Dodoma Jiji      11      3        4        4        9        10      13

10.Coastal            11      3        3        5        9        10      12

11.JKT Tanzania 9       2        4        3        7        8        10

12.TZ Prisons     10      2        4        4        5        8        10

13.Namungo       10      3        0        7        5        12      9

14.Kagera Sugar  10      2        2        6        6        11      8

15.Pamba Jiji       11      1        5        5        6        13      8

16.KenGold        11      1        2        8        7        20      5