Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msingi mkubwa wa soka ni kuwa na akademi

Muktasari:

  • Ingawa tunaongea soka kila kukicha, lakini bado hakujawa na misingi ya kulifanya likue zaidi kwa maana ya uwekezaji wa kutosha kuanzia kwenye miundombinu na vipaji ambavyo vipo vingi nchini.

SOKA ni moja ya michezo pendwa na unaokua kwa kasi nchini. Soka linapendwa tangu miaka ya zamani lilipoanzishwa na ukuaji wake umepitia hatua nyingi na kuzalisha nyota kibao na kutoa ajira kwa vijana wengi.

Ingawa tunaongea soka kila kukicha, lakini bado hakujawa na misingi ya kulifanya likue zaidi kwa maana ya uwekezaji wa kutosha kuanzia kwenye miundombinu na vipaji ambavyo vipo vingi nchini.

Kama wadau wa soka, tunaamini ukuaji wa soka na maendeleo yake kwa jumla kunahitajika mambo mengi lakini kikubwa ni miundombinu ya kuwezesha ukuaji huo.

Tanzania ikishirikiana na Kenya na Uganda ndiyo wenyeji wa fainali za Afcon 2027 na kwa sasa maandalizi yanaendelea. Timu zake za taifa hazijawa na matokeo mazuri zinaposhiriki mashindano hayo makubwa Afrika na moja ya sababu kubwa ni kukosa wachezaji wenye uzoefu wa kutosha.

Kwa nchi zote hususan Tanzania, kuna nyota wachache sana wanaocheza soka la kulipwa kwenye mataifa yaliyoendelea na kukua kisoka.

Ni wazi tumeona jinsi walivyoisaidia Stars kwenye kufuzu na kushiriki Afcon ya Morocco na kama kuna la kujifunza kwenye michuano hiyo kuna mifano mingi ya mataifa yaliyoshiriki kwa jinsi yamefanya vizuri kutokana na uwepo wa nyota wanaokipiga kwenye nchi zilizokua kisoka.

Ni wazi mawakala wengi duniani wanapenda kusaka vipaji kutoka kwenye akademi za soka na kama zitakuwa katika mazingira mazuri ya kukuza vipaji, watafika na kujionea na kuondoka na baadhi kwenda kuimarishwa zaidi.

Nchi kama Senegal imebeba taji la Afcon 2025, siyo kwa kubahatisha. Siyo kwa kuokotaokota tu wachezaji, bali kwa kutambua ubora wao kutokana na kile wanachokifanya kwenye ligi kubwa wanazocheza Ulaya na mabara mengine.

Ligi ya Senegal haina ubora kulinganisha na Tanzania, lakini timu ya taifa ina ubora kutokana na uthubutu walioufanya wa kupeleka vijana nje ya nchi kusakata soka la kulipwa.

Vijana hao waliandaliwa kwenye akademi za soka nchini mwao na kisha kuuzwa nje na sasa wanalisaidia taifa lao.

Siyo Senegal pekee, mataifa mengi ya Afrika Magharibi na Kaskazini yanatambua umuhimu wa kuwekeza katika soka la vijana na kuwa na akademi za kutosha, kwani zinawasaidia baadaye kuwa na timu nzuri za taifa.

Wachezaji mfano Lionel Messi, Xavi, Iniesta, Frenkie de Jong, Johan Cruyff na Cristiano Ronaldo walipata mafunzo ya awali katika mazingira ya akademi ambayo yalizingatia maendeleo ya muda mrefu.

Tofauti na huku, nyota wengi wanaanzia mitaani tu bila kupata mafunzo ya soka na hivyo hawana misingi ya kuwafanya wawe imara kwa muda mrefu.

Inaweza ikawa siyo kwa ajili ya Afcon 2027, ila kukawepo na akademi nyingi za kusaidia kuendeleza vijana kuanzia chini. Akademi ambazo zitakuwa zinatangazwa ili kuvutia mawakala wa soka kuja kujionea vipaji vya soka nchini.

Akademi ambazo zitawafunza vijana misingi ya soka, taaluma ya soka, nidhamu, lishe, ulinzi wa afya na mbinu nyingine.

Bado hatujachelewa kwa sababu vipaji vinazaliwa kila siku na la kufanya ni kuhakikisha kunakuwepo na akademi za kutosha.