Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mechi za heshima lala salama Championship

Muktasari:

  • Mechi hizo za raundi ya 29, zitatoa taswira na picha halisi ya timu zitakazocheza ‘Play-Off’ ya kubakia Championship kwa msimu ujao wa 2026-2027 na moja itakayoshuka moja kwa moja daraja ikiungana na Hausung FC ya Njombe inayoburuza mkiani.

BAADA ya kushuhudia Geita Gold na Kagera Sugar zikirejea Ligi Kuu, Ligi ya Championship inaendelea tena kesho Jumapili kwa mechi zote nane kupigwa kwenye viwanja mbalimbali, huku zikiwa ni za heshima na lala salama kwa msimu wa 2025-2026.

Mechi hizo za raundi ya 29, zitatoa taswira na picha halisi ya timu zitakazocheza ‘Play-Off’ ya kubakia Championship kwa msimu ujao wa 2026-2027 na moja itakayoshuka moja kwa moja daraja ikiungana na Hausung FC ya Njombe inayoburuza mkiani.

Kagera Sugar ambayo tayari imekata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, baada ya kuifunga KenGold ya jijini Mbeya mabao 3-0, itakuwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba kuikaribisha Gunners ya Dodoma iliyochapwa 2-0, dhidi ya Bigman FC.

Kagera iliyo nafasi ya pili na pointi 68, baada ya kudumu katika Ligi Kuu kwa miaka 20, tangu iliposhiriki mwaka 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024/2025, ikishinda mechi tano, sare nane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15 na pointi 23.

Timu hiyo inayonolewa na aliyekuwa nyota wa Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, Juma Kaseja aliyewahi kuitumikia pia Kagera akiwa ni mchezaji na kocha wa makipa, amekirejesha kikosi hicho Ligi Kuu, baada ya mwenendo mzuri tangu mwanzo.

Kwa upande wa vinara wa Ligi hiyo, Geita Gold yenye pointi 71, baada ya kuifunga Songea United mabao 3-1 na kurejea Ligi Kuu itakuwa kwenye Uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga kucheza dhidi ya Stand United iliyochapwa bao 1-0 na Mbeya Kwanza.

Geita Gold iliyoshuka daraja msimu wa 2023/2024, msimu uliopita wa 2024-2025, wa Championship ilimaliza nafasi ya nne na pointi 56, ikiwa na aliyekuwa Kocha Mohamed Muya na kushindwa kurejea Ligi Kuu, baada ya kufeli mechi za ‘Play-Off’.

Timu hiyo ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu dhidi ya Stand United, ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudiwa ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2, kisha kuchapwa ugenini 2-0.

Hata hivyo, baada ya kushindwa kupanda Ligi Kuu msimu uliopita wa 2024-2025, hatimaye kikosi hicho kinachofundishwa na Kocha Mkuu Zubery Katwila kimefanikisha malengo hayo, huku kikipigania kumaliza mabingwa katika mechi mbili zilizobaki.

Msimu wa 2024/2025, Stand ilimaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara, ikianza kwa kuiondosha Geita Gold iliyomaliza ya nne na pointi 56, katika Ligi ya Championship kwa jumla ya mabao 4-2.

Baada ya Stand kuitoa Geita Gold, ikacheza ‘Play-Off’ nyingine na Fountain Gate iliyotolewa pia hatua hiyo na maafande wa Tanzania Prisons kwa jumla ya mabao 4-2, ambapo kikosi hicho kilikwama kupanda baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-1.

Kwa upande wa Fountain, ilimaliza nafasi ya 14 na pointi 29 katika Ligi Kuu msimu wa 2024/2025 na kukutana na Tanzania Prisons iliyomaliza ya 13 na pointi 31, kwenye mechi ya mtoano na kikosi hicho cha maafande kushinda jumla ya mabao 4-2.

Kwenye Uwanja wa Majimaji Ruvuma, wenyeji Songea United baada ya kufungwa mabao 3-1, dhidi ya Geita Gold, itaikaribisha Hausung FC ya Njombe inayoburuza mkiani na pointi tisa, ambayo tayari imekuwa ni timu ya kwanza kushuka rasmi daraja.

Maafande wa Polisi Tanzania baada ya kuchapwa bao 1-0, dhidi ya Mbuni FC ya Arusha, itakuwa kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi kucheza na Mbeya Kwanza, yenye kumbukumbu nzuri baada ya timu hiyo kuichapa Stand United ‘Chama la Wana’ bao 1-0.

Polisi iliyokuwa nafasi ya nne, inakutana na Mbeya Kwanza inayoshika nafasi ya tatu huku timu zote zikiwa na pointi 60, ambazo zimejihakikishia nafasi nne za juu, ambapo zitacheza mechi ya play-off (mtoano) ili kuisaka tiketi ya kurejea Ligi Kuu.

Msimu wa 2024/2025, haukuwa mzuri sana kwa Polisi baada ya kumaliza nafasi ya 10, katika Ligi ya Championship na pointi zake 33, ikishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13 na safu ya ushambuliaji ilifunga mabao 44 na kuruhusu 33.

Kikosi hicho kinapambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022/2023, kilipomaliza nafasi ya 15 na pointi zake 25, kufuatia kushinda mechi sita tu, sare saba na kupoteza 17, kikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.

Mbeya Kwanza iliyouzwa katika Halmashauri ya Manispaa ya mjini Tabora ikitokea Lindi ilipoweka kambi msimu wa 2024/2025, ilishuka daraja msimu wa 2021/2022, ilipomaliza mkiani, baada ya kikosi hicho kukusanya jumla ya pointi 25 kibindoni.

Msimu huo, Mbeya Kwanza ilishinda mechi tano tu, sare 10 na kupoteza 15, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 39, ikiungana na Biashara United iliyomaliza nafasi ya 15 na pointi 28, ikiwa na kazi nyingine kubwa ya kupambana kurejea Ligi Kuu Bara.

Kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Chunya jijini, Mbeya, KenGold iliyochapwa mabao 3-0, dhidi ya Kagera Sugar itakuwa na kibarua cha kupambana na kikosi cha B19 FC kinachoingia na kumbukumbu nzuri baada ya kutoka kuifunga Barberian FC 1-0.

African Sports ya Tanga iliyotoka kuchapwa mabao 2-0 na TMA FC ya Arusha, itakuwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga kucheza na Bigman FC ya Lindi, yenye morali kubwa baada ya mechi iliyopita nyumbani kuifunga Gunners FC ya Dodoma 2-0.

Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, TMA FC itaikaribisha Barberian FC iliyochapwa mechi ya mwisho bao 1-0, dhidi ya B19 FC, ambapo ikiwa itapoteza tena itashuka rasmi daraja na kuungana na kikosi cha Hausung FC ya Njombe. 

Mechi ya mwisho kesho Jumapili ya kuhitimisha raundi ya 29, itapigwa kwenye Uwanja wa Filbert Bayi Pwani, ambapo wenyeji maafande wa Transit Camp iliyoichapa Hausung FC bao 1-0, itacheza dhidi ya Mbuni FC iliyoifunga Polisi Tanzania pia 1-0.