Mrisho Ngassa: Nilivaa jezi ya Yanga kwa hasira

Mrisho Ngassa: Nilivaa jezi ya Yanga kwa hasira

Muktasari:

  • MRISHO Khalfan Ngassa ni winga anayekubalika katika soka la Bongo na sehemu nyingi. Ni winga mwenye kasi awapo kwenye majukumu. Ngassa amecheza soka kwa mafanikio akiwa na timu tofauti hasa Yanga.

MRISHO Khalfan Ngassa ni winga anayekubalika katika soka la Bongo na sehemu nyingi. Ni winga mwenye kasi awapo kwenye majukumu. Ngassa amecheza soka kwa mafanikio akiwa na timu tofauti hasa Yanga.

Katika mawinga bora wa Ligi Kuu Bara miaka ya karibuni, basi Ngassa ni miongoni mwao hata kama kwa sasa hayupo timu kubwa.

Ngassa ni kati ya wachezaji waliotunza viwango muda mrefu, huku akiwa na msaada mkubwa ndani ya timu alizopitia hata timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, akiwa ndiye mfungaji wa muda wote Stars akifunga mabao 25 ambayo hayajafikiwa na mchezaji mwingine.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti yaliyofanyika nyumbani kwake Boko jijini Dar es Salaam, Ngassa amezungumza mambo mengi kwenye maisha ya soka.


AZIZ ANTA AMPOKEA

Ngassa alianza kucheza soka la ushindani Ligi Kuu 2008 alipojiunga na Kagera Sugar ambako alipelekwa na kocha Silvester Marsh (sasa marehemu).

“Marsh ndio alinitoa Mwanza na kunipeleka Kagera, Mungu ampumzishe sehemu salama kiukweli, nilienda pale nikiwa bado mdogo mdogo.”

Winga huyo anasema Kagera Sugar alikutana na wachezaji wakongwe akiwemo Azizi Anta, lakini hakuvunjika moyo kwani walikuwa wakimchukulia kama mdogo wao.

“Nilikuwa najifunza kutoka kwao vitu vingi sana, ukweli nilikuwa naongezea vitu vyangu na vyao kuwa bora muda wote ninapokuwa uwanjani,” anasema Ngassa ambaye alidumu kagera kwa mwaka mmoja tu na kutua Yanga.


AGONGANISHA watani

Baada ya kung’ara na Kagera Sugar ukiwa ni msimu wake wa kwanza, Ngassa aliziingiza vitani timu za Simba na Yanga baada ya kuonyesha kuhitaji saini yake.

Anasema alifuatwa na baadhi ya watu wa Yanga moja kwa moja na kumwambia wanamhitaji huku Simba nao wakihitaji huduma yake.

“Yanga walikuja moja kwa moja, Simba sijui walimtuma nani na alichelewa kuja, sasa wakati natoka kusaini Yanga narudi kambini ndio naambiwa viongozi wa Simba na wao walikuja kuniulizia,” anasema.

“Licha ya kuhitajika Simba sikuingia tamaa ya kusaini mikataba miwili kwa sababu nilikuwa najua kitu nafanya.”


AMKUMBUKA MANJI

Ngassa anasema baada ya kutua Yanga alisaini miaka miwili kuitumikia, huku akiweka wazi muda wote aliokuwa nao ulikuwa na maisha ya furaha.

“Hakukuwa na maisha ya manenomaneno, muda wote ni furaha nilipokuwa pale enzi hizo tukiwa na Yusuf Manji (mwenyekiti wa wakati huo).

“Meneja wangu wakati huo Muddy Mtabora alinipigia simu na kunitakia kila la heri katika mapambano yangu, nyumbani pia walikuwa wakiniombea muda wote katika kufanikiwa.”

Mwanaspoti lilimuuliza staa huyu swali la kizushi, vipi kuhusu pesa ya usajili aliyoipata Yanga? Ngassa aligoma kutaja akiweka wazi kuwa ilimsogeza kimaisha.


mikononi mwa YUSUPH BAKHRESA

Baada ya kucheza Yanga miaka miwili na kuchukua makombe mbalimbali aliaachana nayo na kujiunga Azam FC. Baada ya kutua Azam, Ngassa anasema aliku-tana na maisha mazuri yaliyomfanya acheze soka kwa utulivu, lakini pia akipata ushauri mzuri kutoka kwa Yusuph Bakhresa, mmoja wa mabosi wa timu hiyo.

“Yusuph alikuwa ni mtu wangu wa karibu, alikuwa ananishauri vitu vingi vya msingi kisoka na hata kimaisha muda nilipokuwa pale.”


DILI mbili majuu

Ngassa anasema watu wengi wamekuwa hawajui ukweli kuhusu safari kwenda kujaribu soka la kulipwa nje.

Winga huyo anaanza kwa kugusia safari ya Marekani katika Klabu ya Seattle Sounders iliyokuwa ni mpango maalumu wa Serikali za Marekani na Tanzania.

“Wakati ule wa kipindi cha Rais Jakaya Kikwete ndio nilipata fursa ya kwenda. Hayakuwa majaribio kama watu wengi walivyokuwa wanadhani, nilienda kwa ajili ya mechi ile tu na baada ya mechi basi niliambiwa nirejee nyumbani, nilikaa wiki mbili na kila siku kulikuwa na posho ya Dola 100,” anasema.

Kuhusu dili la West Ham, anasema alipelekwa na Yusuph na alipofika ha-kupata muda mzuri wa kufanya mazoezi.

“Unajua watu wanashindwa kuelewa, wanadhani timu za wenzetu ni kama huku tu kwamba mchezaji katoka nje moja kwa moja anaingia katika timu ya kwanza kufanya majaribio, kule haipo hivyo lazima ufanye kwa vijana kwanza”.

“Nil-ienda kwenye majaribio, lakini nilifanya nao mazoezi siku moja - tena keshokutwa yake walikuwa na mechi. Tulifanya fitinesi zaidi halafu pia kule kila mtu ana mchezaji wake.

“Lakini watu waliongea kuhusu hilo, mara sijui nimeshindwa kumaliza kuku mzima... hapana, hivyo vitu sio vya kweli kabisa. Ukweli ni kwamba hawakupata kabisa muda wa kuniona kwani nilikuwa nafanya mazoezi na timu zao za vijana, lakini watu wanaongea sana na hauwezi kuwakataza.”


JEZI YA YANGA

Ngassa, licha ya kuwa na mkataba na Azam, kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki dhidi ya Azam na AS Vita ya DR Congo alionekana amevaa jezi ya Yanga baada ya mpira kumalizika Julai 2012. Katika mchezo huo ambao Ngasa alifunga bao lililoipeleka Azam fainali kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Vita alikwenda kwenye jukwaa la mashabiki wa Yanga baada ya mchezo kumalizika na kushangilia pamoja nao.

Mmoja wa mashabiki hao alimpa jezi ya Yanga na Ngassa aliivaa juu ya jezi ya Azam na kutoka nje, huku akiwaacha wachezaji na makocha wakiwa uwanjani wakifurahia kufuzu.

“Ujue kabla ya ule wa mchezo kulikuwa na maneno ya hovyo tunaongelewa mimi na Sure Boy (Aboubakar Salum), nilikuwa naumia kutajwa kitu ambacho sihusiki nacho na huwa napenda sana haki.

“Ile mechi niliingia nikitokea benchi na nilifunga, sasa baada ya bao lile na tukio lililokuwa linazungumzwa wakati natoka nilivalishwa jezi na shabiki, niliona nimalizie, niliwaomba radhi viongozi wa Azam lakini kutokana na maneno ya pembeni hawakuniamini,” anasema.

Ngassa anasema walipoingia fainali na kucheza na Yanga, mabosi wake walimtaka kocha asimpange kikosi cha kwanza. “Walisema nisipangwe kutokana na madai kuwa mimi ni Yanga, lakini mwisho wa siku tulipoteza ule mchezo niliingia kama dakika 10 za mwisho”.


MKOPO SIMBA

Kitendo cha kuvaa jezi ya Yanga kiliwatibua mabosi Azam kiasi cha kumtoa kwa mkopo Simba ambapo anaweka wazi kwamba kulikuwa na ofa mbili - Simba na Yanga, lakini waliamua aende Simba. “Mabosi ndio waliamua wapi niende japo najua ilikuwa kama wanafanya kwa kukomoa, lakini kama mchezaji kazi kwangu ni popote”.


ISHU YA EL MEREIKH

Iliwahi kudaiwa kwamba Ngassa aliwahi kukwepa dili la kusajiliwa na El Mereikh ya Sudan, licha ya kuwekewa pesa nyingi mezani. Lakini, anaweka wazi siri iliyomfanya ashindwe kwenda timu hiyo.

“Unajua wakati namaliza mkopo wangu Simba, kabla ya wiki kumaliza mkataba kilichotokea ni kwamba Yanga walinipa donge nono na nilisaini mkataba, Simba walitaka kuniongezea mkataba ilishindikana, hata wa Sudan nao walipokuja pia nilishindwa kusaini nao,” anasema.

“Hakuna kitu kibaya kama kutokuwa mwaminifu. Nilitaka uaminifu na ndio maana sikutaka kusaini mkataba timu mbili tofauti japo watu wengi hawaelewi hilo.”


ATIMKIA SAUZI, APATA MAJANGA

Baada ya kusaini mkataba Yanga, Ngassa aliichezea msimu mmoja na baadaye alitimkia Afrika Kusini kucheza soka la kulipwa Klabu ya Free State.

Anasema akiwa na timu hiyo maisha yalikuwa mazuri, lakini shida ilitokea alipopata majeraha ya nyama za paja kwani ndio mlango wa kutokea ulipokuwa.

“Nilipoumia akaja kocha mpya, yule kocha alikuja na wachezaji wake wengine wapya, kwa hiyo akawaambia viongozi tu kwamba yeye ana wachezaji wengine wazuri wanaoweza kucheza nafasi yangu.

“Basi kutokana na kuwa na majeraha wale Wasauzi waliamua kuachana na mimi, nikarudi nyumbani nikajitibia na kuwa sawa.”


WAARABU HAWAKUMVUMILIA

Ngassa baada ya kupona majeraha alitimkia Oman alikojiunga na Fanja FC.

Akiwa na Fanja, anasema maisha yalikuwa mazuri lakini alijikuta katika wakati mgumu baada ya kupata majeraha huku akiwa hajagongana na mtu yeyote uwanjani. “Nilikuwa kule na Danny Lyanga, nakumbuka baada ya kufunga bao na kurejea nyumbani basi nilijiona naumwa ghafla mguu unavimba,” anasema.

“Nilipowaambia viongozi wangu waliniona kama vile naringa baada ya kuona nimefunga na kufanya vizuri, lakini haikuwa hivyo.”

Ngassa anasema viongozi wa timu hiyo walitaka afanyiwe upasuaji, lakini aligoma na ndipo walichukia zaidi juu ya kitendo hicho.

“Sikutaka nifanyiwe upasuaji zaidi ya kupaka dawa za kuchukua, baadaye waliniambia nirudi nyumbani basi nikaja kujitibia mwenyewe.”


TIMU NDOGO

Akizungumzia tofauti ya timu ndogo na kubwa, anasema ipo lakini anachukulia kama njia ya kufanikisha jambo analopanga.

“Utofauti upo na wala sikuwahi kujisikia vibaya nilipokuwa nacheza hizo timu ndogo, kwani nilikuwa najua siku moja nitarudi kucheza timu kubwa.”


ADAI PESA YANGA

Winga huyu anamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuweka nguvu pia katika soka kwani wachezaji wazawa wanadhurumiwa.

“Unakuta mchezaji wa kigeni akiwa anadai kabla hajaondoka atalipwa pesa zake zote, lakini mchezaji mzawa inakuwa tofauti kabisa. Binafsi timu niliyomaliza nayo mkataba (Yanga) bado kuna sehemu yangu ya pesa nawadai, kwa hiyo naomba Rais wa sasa pia ageukie na huku kwenye soka kuna mambo mengi.

“Nadhani akitilia mkazo itafika wakati wachezaji wataacha tabia za kuomba kodi kwa watu fulani, kwani watakuwa wanapata stahiki zao kwa wakati,” anasema.


YANGA MAFANIKIO

Mchezaji huyu watu wengi huwa wanamhusisha ni shabiki mkubwa wa Yanga, lakini hilo liko hivi, “hakuna mchezaji ambaye anakuwa ni shabiki wa timu fulani, kazi yangu ni mpira na nimecheza timu tofauti na kufanya vizuri.”

Ngassaa akiwa Yanga timu hiyo ilimpa mafanikio makubwa na kubadilisha maisha yake. “Ukweli ni kwamba pesa zao zilibadilisha maisha yangu kiujumla, siwezi kusema ni kiasi gani lakini Yanga imenipa mabadiliko.”


KIKOSI CHAKE BORA

Ngassa anataja kikosi chake bora kuwa ni Aishi Manula, Yassin Mustapha, Erasto Nyoni, Joseph Onyango, Jonas Mkude , Tusila Kisinda, Feisal Salum, John Bocco, Mrisho Ngassa na Simon Msuva.


TIMU ALIZOCHEZA

Ngassa kachezea Kagera Sugar, Yanga, Azam FC, Simba, Free States, Fanja FC, Mbeya City, Ndanda FC na Gwambina FC.