MPAPASO WA MASAU BWIRE: Mpapaso ulianza hivi, karibuni tuliamshe

AHLAN Wa Sahlan... wasomaji wa Mwanaspoti kwa mara ya kwanza na kuanzia sasa nitakuwa nanyi kila Jumamosi katika gazeti hili pendwa la michezo na burudani nchini na ukanda wa Afrika Mashariki.
Naushukuru uongozi kwa kuniamini na kunipa nafasi hii ya kuwasiliana, kuwasilisha maoni, mtazamo na mchango katika maendeleo ya michezo hususan soka ndani ya Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla wake.
Katika jambo lolote linalofanywa kwa malengo fulani popote na yeyote awe mtu mmoja mmoja, taasisi na hata serikali, mbali na mafanikio, changamoto pia huchomoza, mpira wa miguu popote duniani hata katika baadhi ya mataifa yaliyofanikiwa kisoka changamoto zipo, haziepukiki.
Katika safu hii nitajitahidi kwa kushirikiana na wadau wengine kuwalisha lishe bora wasomaji kuhusu mpira wa miguu, mafanikio na changamoto zilizopo ili kwa pamoja, kwa maoni na ushauri wenu tushughulike nazo katika mpira wa miguu ili kama sio kuziondoa kabisa basi tuzipunguze kwa kiasi kikubwa. Safu hii pia inalenga kutoa burudani kwenye mpira wa miguu na ndilo kusudio hasa. Wadau, wapenzi na mashabiki wa soka wataburudika kila sehemu inapotajwa soka, mitandaoni na kwenye vyombo vya habari yakiwemo magazeti, redio na televisheni iwe ni burudani tu - burudani ambayo itahitimishwa na shughuli yenyewe uwanjani, japo kwenye mchezo wenyewe baada ya kumalizika wengine watakaopata matokeo hasi, burudani hiyo, itageuka kuwa msumari wa moto ndani ya mioyo yao.
Mpapaso wa Masau Bwire utakupapasa hasa kulainisha na kukuweka vizuri mno kifikra, kiuelewa na kiweledi pia kuhusu soka letu. Kikubwa tu, kaa mkao wa kupapaswa kupitia mpapaso wa Masau Bwire.
Kabla hujakutana na mpapaso wenyewe ni vizuri ukamfahamu Masau Bwire mwenyewe ni nani huyu? Maisha na shughuli zake, japo kwa ufupi.
Masau Bwire ni yatima aliyezaliwa miaka kadhaa iliyopita katika Kijiji cha Mwiruruma, Kata ya Iramba, Tarafa ya Kenkombyo, Wilaya ya Bunda mkoani Mara mwenye umri unaotosha kuitwa babu japo bado sina mjukuu na wazazi wangu, Bwire Wakuru Kuliga (baba) na Nyakwesi Mabamba Mtaki (mama).
Masau ni Mjita moja ya kabila lenye ustaarabu mkoani Mara - kabila la watu wapole na wanyenyekevu, wasiotaka kuonea wala kuonewa, wakweli na wenye kaubishi kidogo hasa wana-poutetea ukweli na kile wanachokiamini wasioyumbishwa, wenye kujiamini. Masau ni mtoto wa mwisho kuzaliwa kwa mama yake kati ya watoto 12 aliozaa na wa 19 kati ya 20 waliozaliwa na baba yake aliyekuwa na wake wawili - Nyakwesi (mama’ke) na Nyamahindi Maindi (Bi mdogo wa mzee Bwire). Wote ni marehemu.
Ninayo elimu ya ualimu, ninafundisha Shule ya Msingi Makumbusho iliyopo Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam na kabla ya hapo nimefundisha shule za msingi nyingine katika manispaa hiyo ya Kinondoni ambazo ni Mburahati, Gilman Rutihinda, Mapinduzi na Tandale kazi niliyoianza mwaka 1994.
Pia ninayo taaluma ya habari tangu mwaka 2002. Nimefanya kazi ya uandishi wa habari katika vyombo mbalimbali vya habari - magazeti na redio hata televisheni nilifanya ila kwa muda mfupi sana. Nilikuwa nikipeleka habari katika televisheni ya Taifa (TVT) kwa wakati huo.
Magazeti ambayo nimefanya nayo kazi kwa kuandika habari ni Majira, Dar Leo, Tanzania Leo, Sura ya Mtanzania, Kulikoni na Mawio. Kwa upande wa redio nilizofanyia kazi kwa kuripoti matukio mbalimbali ni Redio Times, Wapo FM, Morning Star, Uhuru FM, N.Y.U na Top Radio.
Miongoni mwa waandishi wa habari mahiri niliofanyanao kazi enzi hizo ni Mobhare Matinyi, Joseph Kulangwa, Titus Kaguo, John Mapinduzi, Boniface Wambura, Daniel Chongolo, Hassan Abbas na Manyerere Jackton. Wengine ni Jackline Liana, Lucy Mayenga, Amir Mhando, Eben-ezer Mende, Said Mwinshehe, Frank Balile, Selemani Mbughuni, Dina Ismail, Shija Richard, Kulwa Mzee, Eliza Mmasi, Joyce Magoti, Deo Myonga, Peter Mwenda na Zahoro Mlanzi.
Vilevile nimekuwa ofisa Habari na Mawasiliano wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (Cerefa) tangu 2004 nilipoteuliwa chini ya Mwenyekiti wake Imani Madega hadi 2012 nilipobadilishiwa majukumu kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wakati huo mwenyekiti wa Corefa akiwa Hassan Othman ‘Hassanoo’, nafasi niliyodumu nayo hadi 2020.
Nilianza kwa kujitolea kuisemea Ruvu Shooting 2003 ilipoanzishwa. Nimedumu kuwa msemaji wake mpaka sasa, milima, mabonde na dhoruba nyingi nilizokutana nazo ndani ya timu hii zilinijenga, kunikomaza na kuniimarisha kisoka.
Miaka ya karibuni wadau, wapenzi na mashabiki wa soka walio wengi wamekuwa wakiniita kwa jina la ‘Mzee wa Kupapasa’, jina walilonipachika kutokana na kauli yangu ya kupapasa ambayo nimekuwa nikiitumia kuisemea timu yangu kabla na baada ya mchezo.
Wengi wao wamekuwa wakihoji maana halisi ya neno hilo, chimbuko lake na sababu hasa ya kulitumia katika kusema kwangu miongoni mwao wakijaribu kulipatia tafsiri mbaya.
Kwa kuwa safu hii imebebwa na neno hilo, papasa (mpapaso) ni vizuri nikiliweka wazi kidogo maana yake halisi, sababu ya kulitumia katika kauli zangu ndani ya timu yangu ya Ruvu na pengine chimbuko lake ili unapopapaswa na Mpapaso wa Masau Bwire katika safu hii usishtukeshtuke mithili ya mtoto anayeugua degedege. Tafsiri halisi ya neno ‘papasa’ katika Kamusi za Kiswahili ni kitenzi chenye maana ya kupitisha mkono polepole na juu juu ya kitu kama afanyavyo mtu asiyeweza kuona.
Sentensi ambayo naweza kuitumia kujenga maana halisi ya neno papasa katika bongo za Wabongo wengi, wenye tafsiri potofu kuhusu neno hili naweza kusema kwamba ‘umeme ulipozimika usiku, nilipapasa kuta kwenda jikoni kutafuta mshumaa na kiberiti’.
Kumbe, kupapasa ni kutafuta ili ukipate kitu ambacho umeshindwa kukiona baada ya macho yako kushindwa kuona aidha kipofu au kwenye giza ukipapasa, utakipata na utakitwaa.
Chimbuko na sababu ya neno hilo papasa kuanza kulitumia katika timu yangu ya Ruvu ilikuwa hiyo hiyo, ya kukitafuta ambacho kwa macho ya kawaida imeshindikana kukiona.
Neno hili Papasa nilianza kulitumia 2017 wakati huo mbali na timu yangu ya Ruvu Shooting kucheza vizuri, tulikuwa hatupati matokeo chanya kwa uchezaji wa kawaida. Tulishindwa kupata ushindi, hivyo ikabidi sasa tupapase ili tukipate (ushindi) ambacho tumeshindwa kukiona na kukipata kwa njia ya kawaida. Nakumbuka mwaka huo 2017 tulikuwa na mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Majimaji ya Songea katika uwanja wa Majimaji, Songea nilisafiri kwa ndege kutoka Dar es Salaam hadi Mbeya, kutoka Mbeya hadi Songea nikatumia daladala.
Nikiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam ndipo dhana hii ya kupapasa kuitumia katika usemaji wangu ilianzia.
Pale uwanjani, Terminal 2 kuna mageti mawili ya ukaguzi - chini na juu kuingia eneo la kusubiria ndege kuondoka. Hapo ndipo nilipata wazo la kupapasa kutokana na ukaguzi niliofanyiwa na wahudumu na askari waliokuwepo siku hiyo.
Kabla ya kuingia katika eneo hilo la kusubiria ni lazima ufanyiwe ukaguzi, upite kwenye mashine za skana ili kama una kitu chochote cha hatari kupitia mashine hizo kiweze kuonekana kwa mashine hizo kutoa mlio fulani kuonyesha kwamba una kitu kisicho cha kawaida.
Siku hiyo nilikuwa na simu za mkononi saba na kwa kuwa ni za mkononi nilizishika mkononi. Nadhani ziliwatisha walinzi wale, wakanihisi gaidi fulani au mtu fulani hivi mwenye kujishughulisha na biashara haramu. Sikukaguliwa kitoto nilikaguliwa mpaka mapigo ya moyo nayo yakashtuka.
Nilipitishwa kwenye zile mashine za skana mara tano, simu zangu nililazimika kuzifungua mpaka line niliambiwa nitoe. Mbali na mashine, askari mmoja alitumia mikono yake kunipapasa mwili mzima.
Wakati wakiendelea kunifanyia upekuzi huo wa maana, abiria wenzangu waliokuwa wakinifahamu waliutafsiri kama udhalilishaji. Mtu mmoja ambaye nilimfahamu askari wa jeshi la wananchi aliyekuwa amevaa kiraia aliwafuata na kuwauliza kama wananifahamu. Aliwasihi wasiendelee kunipekua maana wananidhalilisha akiwahakikishia mimi ni mtu mwema.
Baada ya hapo nikatambua kwamba kumbe kupapasa ni kila kitu. Mashine za skana si lolote, kupapasa ndiyo ufumbuzi wa kupata kisichopatikana kwa njia za kawaida. Nilipozungumza na vyombo vya habari niliwaambia tu kwamba, “tunakwenda Songea kuwapapasa Majimaji.”
Mpapaso wa Masau Bwire katika safu hii utakupapasa katika muktadha huo. Nikuombe kila Jumamosi usikose kupitia safu hii maana utapigwa msasa, utapapaswa kila eneo na utalainika na kuwa mwepesi, mwenye weledi katika soka ndani na nje ya Tanzania.