MPAPASO WA MASAU BWIRE: Hiki ndicho kipimo kizuri kwa Ruvu

KLABU ya soka ya Ruvu Shooting FC, imesema, msimu huu wa ligi 2022 imejipanga vizuri zaidi na lengo lao ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mwenyekiti wa klabu hiyo yenye masikani yake Mlandizi, Kibaha mkoani Pwani, Kanali Peter Eliasi Mnyani, aliuambia Mpapaso kwamba, tofauti na msimu uliopita, msimu huu kikosi cha timu yake kimeandaliwa vilivyo, ni kikosi bora, chenye ushindani wa kutosha.

Kanali huyo wa jeshi, ambaye pia ni Mkuu wa Kikosi cha Jeshi (CO), 832 KJ, Ruvu JK, ilipo kambi ya timu hiyo, alisema, msimu uliopita klabu yake ilionekana dhaifu baada ya wachezaji wake wa kutumainiwa 11, katikati ya msimu kwenda kozi ya kijeshi.

Alisema, baadhi ya wachezaji hao wamerudi, tayari wamejiunga na kikosi, wachezaji saba, wamemaliza kozi yao Septemba 30, 2022 na muda wowote watajiunga na wenzao klabuni.

Klabu hiyo msimu huu katika mechi tano ilizocheza, imeshinda tatu, imefungwa mbili, ina jumla ya alama tisa, ipo nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu unaoongozwa na mabingwa watetezi, Yanga Afrika.

Ruvu Shooting katika mechi ya awali, ikiwa ugenini dhidi ya Ihefu, ilipata ushindi wa bao 0-1, ikafungwa na Mtibwa mabao 2-1, mchezo uliochezwa Uwanja wa Manungu, Morogoro.

Baada ya hapo, ilifungwa tena ugenini katika Uwanja wa Kassim Majaliwa, Ruangwa-Lindi, bao 1-0 na mwenyeji Namungo.

Mechi mbili za nyumbani zilizofuata ikicheza Uwanja wa Uhuru, Ruvu Shooting ilishinda zote, dhidi ya Polisi Tanzania bao 1-0 na dhidi ya Coastal Union mabao 2-1.

Matokeo hayo yamejenga imani, matumaini na kujiamini kwa viongozi, benchi la ufundi na wechezaji kiasi cha kuwapa uhakika wa kufanya vizuri zaidi msimu huu na pengine kuchukua kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza.

Klabu hiyo yenye wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wazawa, imejipambanua katika kufikia malengo ya ubingwa tofauti na klabu nyingine ambazo zimekuwa zikipambana kutokushuka tu daraja.

Akizungumza na Mpapaso, mmoja wa walezi wa klabu hiyo, Meja Jeneral Mabele, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), alisema, pamoja na kufurahishwa na matokeo mazuri ya klabu hiyo, ataisapoti kwa kiasi kikubwa kuhakikisha inafikia malengo.

Kikubwa alichokihimiza na kukisisitiza mlezi huyo wa Ruvu Shooting, ni umoja, ushirikiano na mshikamano utakaowapatia nguvu ya pamoja, kuwawezesha kufikia mafanikio na kutwaa ubingwa.

Ruvu Shooting wanaamini kwamba, ligi ikisimamiwa ipasavyo, kwa mujibu wa kanuni, sheria zikafuatwa, waamuzi wakazitafsiri vilivyo, kila klabu ikapata inachostahili kutokana na uwezo wake, usawa na haki vikafuatwa, inao uwezo mkubwa wa kutwaa ubingwa wa Tanzania.

Ligi ya msimu uliopita, Ruvu Shooting, maarufu, Barcelona ya Bongo, wazee wa PTK +Fukunyua, waliponea tundu la sindano kushuka daraja, sababu ikiwa wacheza 11 walioondoka katika ya ligi kwenda katika mafunzo ya kijeshi.

Msimu huu wamethibitisha kuwa na kikosi bora baada ya kufanya usajili mzuri, lakini pia kurejea kwa wachezaji hao ambao walikwenda kozi na sasa kutengeneza kikosi cha ushindani, chenye uwezo wa kushindana na kupata ushindi dhidi ya timu yoyote.

Kipimo chao kikubwa ni mchezo wa keshokutwa, Jumatatu, Oktoba 3, 2022 itakapocheza dhidi ya Yanga SC, mchezo ambao utachezwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Ruvu SShootin inautumia uwanja huo kama wa nyumbani baada ya uwanja wao wa mabatini kufungiwa.

Mchezo huo, pamoja na ugumu uliopo hasa kwa upande wao, kutokana na usajili wa kibabe walioufanya Klabu ya Yanga SC, bado wana hakika, na wanaamini wataibuka na ushindi wa kishindo.

Ruvu Shootin imesema ushindi dhidi ya Yanga SC ni muhimu sana kwao kwani, utaenda kuwapa historia mpya katika soka la Tanzania, Mosi kuifunga klabu ambayo haijafungwa kwa kipindi kirefu, lakini pia, utaifanya iongoze ligi.

Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa, miongoni mwa makocha wachache wazawa wenye elimu, uwezo na ubora wa hali ya juu ya kufundisha soka, ameuthibitishia Mpapaso kwamba, msimu huu ni wa kikosi chake kufanya vizuri katika Ligi Kuu na kupenya kucheza Mashindano ya CAF

Mkwasa ametamba na kusema, klabu zote ni za kawaida, ziko sawa, maandalizi ya kila klabu ndiyo yataiwezesha kufanya vizuri au vibaya.

Alisema klabu yake imeandaliwa na iko vizuri kila eneo na idara, anachokifanya kama kocha, nikuwaongezea maarifa, mbinu na uwezo wachezaji wake ili waweze kushinda dhidi ya klabu pinzani.

Mashabiki wa klabu hiyo, pamoja na kuisapoti timu yao hiyo kwa hali na mali, kilio chao ni uwanja wao wa Mabatini kufungiwa, hivyo kuwawia vigumu kusafiri hadi Dar es Salaam kwenda kutoa hamasa ya ushangiliaji.

Mashabiki hao wameuomba uongozi wa klabu hiyo, kufanya kila linalowezekana kuhakikisha Uwanja wa Mabatini unafunguliwa ili mashabiki wao waweze kujitokeza kwa wingi kuishangilia katika uwanja wake wa nyumbani.

Katika hilo la uwanja kufunguliwa, uongozi wa klabu hiyo chini ya mwenyekiti wake, Kanali Mnyani, kwa ushirikiano na mmoja wa walezi wa klabu hiyo, Brigadier General Mabena, walisema wanashughulikia kwa haraka ili uwanja huo uweze kuboreshwa na kuanza kutumika kwa michezo ya nyumbani ya klabu hiyo.

Hayo ni malengo makubwa ya klabu hiyo ya Ruvu Shooting, katika soka la Bara ambayo viongozi wake wamejinadi na kujipiga vifua wakiamini watayafikia kwani ndiyo dhamira yao.

Klabu zikiwa na mtazamo chanya kama inavyoonesha Ruvu Shooting, ligi itakuwa na msisimko, ushindani utakuwa mkali, inawezekana ubingwa usiwe wa kutabiliwa kwa klabu mbili tu za Simba SC na Yanga SC, ikawa kwamba klabu yoyote, iliyojipanga na kujiandaa vizuri.

Changamoto zilizoelezwa na uongozi wa Barcelona hiyo ya Bongo, ambazo zimekuwa kilio cha wengi, Mpapaso unatoa rai kwa mamlaka husika kusimama kidete kuhakikisha inaziondosha ili ligi yetu ubora wake uwe wa viwango vya juu.

Mpapaso unaiombea na kuitakia kila la kheri klabu hiyo ya Ruvu Shooting iweze kufikia malengo yake, ilete mabadiliko ya kimtazamo katika soka letu. Kwani haipendezi kila siku ubingwa ni wa Simba SC na Yanga SC, wengine ni wasindikizaji tu, kwa kufanya hivyo, ligi itakuwa bora kwakuwa ushindani utakuwa mkali sana.