Monica, humwambii kitu kwa Diarra

Ndiye kipa pekee ambaye hajaruhusu nyavu zake kutikiswa katika mechi tano ambazo ameidakia timu ya Fountain Gate Princess hadi sasa kwenye Ligi Kuu Bara ya Wanawake.

Anaitwa Monica Chebet, raia wa Kenya ambaye anaamini kama ataendelea kupewa nafasi kikosi cha kwanza, basi anataka kuweka rekodi ikiwemo kuchukua tuzo ya kipa bora.

Monica ambaye amesajiliwa na Fountain Gate msimu huu akitokea Wadadia Women inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya, alianza kikosi cha kwanza walipoichapa Yanga Princess bao 1-0 kisha akaiongoza Fountain kuifumua Amani Queens mabao 4-0. Alidaka walipoibamiza Mkwawa Queens mabao 2-0. Hakucheza timu yake ilipochapwa mabao 2-1 na Simba, kisha akarejea langoni walipoitandika Alliance Girls mabao 4-0 na akakaa langoni walipowafunga watani zao wa jadi Baobab Queens kwa bao 1-0 na hakudaka timu yake ilipotoka suluhu na Ceasiaa Queens.

“Nimekuwa nikifanya mazoezi binafsi pindi timu inapokuwa haina mazoezi, kwa muda huo ndio maana nina kiwango bora kwani najua kama huna bidii huwezi kuwa vizuri uwanjani,” anasema Monica.

“Kama timu inafanya mazoezi jioni mimi na baadhi ya makipa wenzangu tumekuwa tunafanya mazoezi yetu binafsi asubuhi na yote ni kuhakikisha naendelea kuwa katika ubora mkubwa kwa sababu nimepania kuweka rekodi na hata kuchukua tuzo ya kipa bora,” anasema Monica ambaye aliwahi kuingia tatu bora Kenya kwenye tuzo ya makipa msimu uliopita.


ANAMKUBALI SANA DIARRA

Unaambiwa licha ya kwamba Monica ana ubora kwa upande wa wanawake, lakini kumbe kuna baadhi ya maujuzi anachukua kutoka kwa kipa wa Yanga ya wanaume, Djigui Diarra ambaye ni raia wa Mali.

Diarra ndiye kipa anayemvutia zaidi Monica kwenye Ligi Kuu Bara na anasema amekuwa akimfutilia mno jinsi anavyoanzisha mashambulizi, alivyo mtulivu golini lakini kubwa zaidi anavyojiamini langoni.

“Namkubali sana Diarra ni kipa mzuri na napenda anavyojiamini anapokuwa golini. Huwa namfuatilia sana na kuna baadhi ya vitu najifunza kutoka kwake kwa ajili ya kunijenga ili na mimi niwe kipa mzuri,” anasema.

Kwa upande wa wanawake, Monica anavutiwa zaidi na kipa wa Simba Queens, Gelwa Yona.


FOUNTAIN UBINGWA INAWEZEKANA

Licha ya kwamba Funtain Gate hivi sasa imeanza kushuka taratibu kwenye msimamo wa ligi baada ya mwanzoni mwa ligi kuonekana iko moto na kukaa kileleni kwa wiki kadhaa, hata hivyo jambo hilo halimpi presha Monica ambaye anaamini ligi bado na timu yake inaweza kutwaa ubingwa.

“Sawa, kwa sasa tumeshuka, lakini bado ubingwa uko wazi. Muhimu ni kuongeza juhudi ili kurejea nafasi ya kwanza kwani kama tukijibidisha bado tuna nafasi ya kubeba ubingwa msimu huu,” anasema Monica.


WAKENYA WENGI TANZANIA BARA

Monica anasema kuwepo kwa wachezaji wengi Wakenya kwenye Ligi Kuu Bara ni kutokana na ushindani wa ligi na pesa wanayopata.

“Ligi ya Tanzania ina ushindani sana lakini kubwa wanalipa vizuri tofauti na Kenya, ndio maana unaona wachezaji wengi tumekuja hapa.

“Pia ligi hii kwa sasa inafuatiliwa sana na mechi nyingine zinaonyeshwa (kwenye runinga) hivyo inatupa fursa ya kuonekana nje na kupata timu kwenye mataifa mengine,” anasema kipa huyo.

Monica anasema alikuwa akiifuatilia sana ligi ya Tanzania na alitamani kucheza Fountain Gate aliyopo hivi sasa pamoja na Simba Queens.

“Nilikuwa na marafiki wengi ambao nafahamiana nao hapa Tanzania akiwemo kipa mwenzangu wa Fountain Gate, Caroline Rufaa ambaye tumesoma pamoja na tumecheza pamoja Kenya sasa yeye alisababisha nikawa nafuatilia mechi za ligi ya wanawake ya hapa.

“Nilikuwa najisemea kuwa lazima siku moja nije kucheza ligi ya hapa na kiukweli kuna timu mbili nilizilenga zaidi ambazo ni Fountain na Simba kwa sababu niliona zina wachezaji wenye uwezo mkubwa,” anasema Monica ambaye bado ana ndoto siku moja ya kucheza timu vigogo hapa nchini.


OPAH BALAA

Monica anasema tangu aanze kucheza ligi ya Bongo hakuna straika anayemvutia na hatari kama Opah Clement wa Simba Queens akidai mchezaji huyo ana balaa.

“Opah ni straika hatari na ana sifa tatu. Kwanza ana kazi, pia ni mzuri akiwa na mpira huwa hapotezi kirahisi na tatu akiwa mbele ya goli hafikirii chochote zaidi ya kufunga,” anasema Monica.


MAISHA FOUNTAIN

Monica anafurahishwa na jinsi anavyopata ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzake ndani na nje ya uwanja pamoja na viongozi wa klabu hiyo, lakini anafurahi zaidi kwa sasa kujifunza kula wali maharage.

“Ushirikiano ninaopata hapa ni mkubwa sana na najihisi kama niko Kenya tu na chakula ninachopenda sana ni wali maharage.

“Unajua wali maharage Kenya upo, lakini sio wengi wanaupenda kwa sababu tumezoea sana ugali lakini hapa Tanzania dah! Watu wanapenda sana wali maharage sasa imenifanya na mimi kuzoea chakula hicho na kukipenda, “anasema Monica.