Mondi, Zari wanaupiga mwingi Afrika Mashariki

Mondi, Zari wanaupiga mwingi Afrika Mashariki

TAKWIMU zinaonyesha hadi Aprili 2022 watumiaji wa mitandao ya kijamii duniani walifikia bilioni 4.65 ambao ni sawa na asilimia 58.7 ya idadi ya watu duniani, huku watumiaji wapya milioni 326 wakijiunga katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.

Inakadiriwa kwa siku duniani kote watu hutumia saa bilioni 10 kwenye mitandao ya kijamii ambazo ni takribani miaka milioni 1.2 ya kuishi binadamu.

Facebook ndio mtandao wenye watumiaji wengi kwa mwezi ambao ni bilioni 2.9, YouTube bilioni 2.5, WhatsApp bilioni 2, Instagram bilioni 1.4, WeChat bilioni 1.2 na TikTok bilioni 1.

Hadi sasa, Diamond Platnumz na mzazi mwenziye, Zari The Bosslady ndiyo mastaa pekee Afrika Mashariki waliofikisha wafuasi (followers) zaidi ya milioni 10 Instagram.

Zari kutokea nchini Uganda ambaye anaishi Afrika Kusini na familia yake, amempiku Miss Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu ambaye anashika nafasi ya pili akiwa na wafuasi milioni 9.8.

Hadi Aprili, 2021 mcheza Filamu wa Kenya, Lupita Nyong’o ndiye alikuwa akiongoza kwa wafuasi Afrika Mashariki upande wa wanawake akiwa nao milioni 9, huku Zari akifikisha idadi hiyo na Wema Sepetu akiwa nao milioni 8.6 kwa kipindi hicho.

Ikumbukwe mtandao wa Instagram ulianzishwa Oktoba 2010 na Kevin Systrom na Mike Krieger, Aprili 2012 ulinunuliwa na kampuni ya Facebook ambayo sasa inajulikana kama Meta Platforms.

Kwa ujumla anayeongoza Afrika Mashariki ni msanii wa Bongofleva toka WCB Wasafi, Diamond mwenye wafuasi milioni 14.9, akifuatiwa na Mwanahabari kutoka Tanzania pia, Millard Ayo mwenye milioni 11.6 na Zari milioni 10.8.

Mcheza soka kutoka Misri anayekipiga Liverpool, Mohamed Salah ndiye staa mwenye wafuasi wengi Instagram barani Afrika akiwa nao milioni 51.9, akifuatiwa na mwimbaji wa Nigeria, Davido mwenye milioni 24.6.

Hadi mwishoni mwa 2015, Diamond alikuwa ndiye msanii mwenye wafuasi wengi zaidi Instagram barani Afrika akiwa nao milioni 1.5, kufikia Septemba 2016 akaondolewa kwenye nafasi hiyo na Davido aliyefikisha wafuasi 2.9 kwa wakati huo.

Mchezaji wa Man United kutoka Ureno, Cristiano Ronaldo ndiye binadamu mwenye wafuasi wengi Instagram duniani kote akiwa nao milioni 466, wanaomfutia ni Kylie Jenner milioni 357, Lionel Messi milioni 348 na Selena Gomez milioni 335.

Baada ya kuanzishwa Instagram mwaka 2010 mtandao huo ulipata watumiaji milioni 1 ndani ya miezi miwili, hadi kufikisha mwaka mmoja tayari ilikuwa na watumiaji milioni 10, hadi sasa unatumika katika lugha 32 duniani kote.

Nchi ya India ndio inaongoza duniani kuwa na watumiani wengi wa Instagram wakifikia milioni 253.5, kisha Marekani milioni 155.7, Brazil milioni 122.5, Indonesia milioni 99.9, Uturuki milioni 54.4 na Japan milioni 47.3. Na kati ya watumiaji wa Instagram duniani kote ambao ni bilioni 1.4, asilimia 48.1 ni wanawake, huku wanaume wakiwa asilimia 51.9.