Prime
Madrid asiyefunzwa na mama yake hufunzwa na ulimwengu
HADI Xabi Alonso atakapowaweka sawa tayari watakuwa wamefundishwa na ulimwengu katika kiasi cha kutosha. Rafiki zangu wazee wa Galacticos. Real Madrid. Jumatano mchana Madrid, asiyefunzwa na mama yake hufunzwa na ulimwengu, walikuwa wakifunzwa adabu tena pale New Jersey Marekani.
Kwetu ilikuwa usiku pale New Jersey ilikuwa mchana kweupe ingawa Madrid mpira walikuwa hawauoni. Luis Enrique Martinez alikuwa katika ubora wake na vijana wake. Pasi nyingi kila wakati na kukabwa kwingi kila wakati. Madrid hawakuuona mpira ingawa ilikuwa mchana.
Labda Rais wa Madrid, Florentino Perez atakuwa amejifunza kitu. Namna anavyochanwa na soka la kisasa katika nyakati hizi. Akili yake ya kwanza ni kuvunja kabati kwa mastaa wakubwa duniani, lakini mpira wa kisasa bado hajauweza.
Amemuita Alonso awaweke sawa waingie katika dunia ya mpya ya mpira, lakini tayari ameshapata aibu ya kutosha. Kwa miaka mingi sijawahi kuona Madrid wakipitia aibu ya namna hii. inaanzia jinsi wanavyofundishwa mpira na Barcelona kule kwao.
Kocha wa Barcelona ni Mjerumani. Hans Flick. Hata hivyo, anafundisha mpira wa Kihispaniola. Barcelona wakiwa hawana mpira wanautaka haraka. Wakiwa nao wanabadilishana nafasi kwa haraka. Eneo pekee ambalo watu wanaweza kuleta ubinafsi wa kukokota ni kule mwishoni. Kule kwa kina Lamine Yamal na Rafinha.
Kila siku Madrid wanachezea bao nyingi kwa Barcelona. Sio tu kwamba wanafungwa lakini wanadhalilishwa. Ndani yao wana kina Vinicius Junior na Kylian Mbappe. Kila bao la Barcelona linapoingia wanaonekana wazi kwamba wanakuwa wamefadhaika.
Baada ya kufunzwa na ulimwengu kule Hispania walikuja kufunzwa na ulimwengu na Arsenal. Kocha wa Emirates ni Mhispaniola mwingine ambaye ameuiga mpira wa Pep Guardiola. Unaachia kwa haraka na wakati hauna mpira unaudai kwa haraka. Mnaudai pamoja. Hakuna kuleta ustaa.
Madrid walipotea London, kisha wakamaliziwa Santiago Bernabeu. Hakukuwa na ubishi wowote kwamba Arsenal walikuwa bora kwa dakika 180. Hata bao la Madrid lilitokana na kosa binafsi la William Saliba. Bao la pili la Gabriel Martinelli ulikuwa msumari mwingine katika jeneza la Madrid.
Jumatano mchana Madrid wakaingia katika anga za Mhispaniola mwingine, Luis Enrique Martinez. Zilikuwa hesabu rahisi tu. Arsenal ambaye ni mbabe wa Madrid aliteketezwa vilivyo na PSG katika mechi mbili za nusu fainali London na Paris. Madrid angemuweza wapi mbabe wa Arsenal?
Na ndicho kilichotokea. Tulikwenda mapumziko PSG akiongoza kwa mabao matatu. Kipindi cha pili wakamaliziwa bao la nne. Kama kawaida kamera ziliwavuta Mbappe, Vinicius na Jude Bellingham wakishika viuno baada ya kila bao kuingia. Walikuwa wanafunzwa na ulimwengu kwa mara nyingine.
Sina shaka Alonso atawanyoosha Madrid. Lakini anahitaji ruhusa maalumu kutoka kwa Perez. Ukitaka kucheza mpira wa PSG au Arsenal unaweza kuwa na mastaa wako, lakini inabidi wawe wanashika adabu kweli kweli. Hauhitaji wachezaji wanaosubiri waletewe mpira kuonyesha vipawa vyao. Hizo zilikuwa enzi za kina Ronaldinho sio leo.
Mastaa wengi wakubwa hawawi bora wakati timu haina mpira. Lakini kwa sasa kwa mifumo ya hawa Wahispaniola unalazimika kujikaza. Mikel Arteta aliachana na Mesut Ozil na Pierre Emerick Aubamayeng tukamshangaa. Hata hivyo, Arsenal walikuwa bora zaidi mastaa hawa walipoondoka.
Itazame PSG ya mastaa ilivyokuwa ovyo. Walikuwepo Lionel Messi, Neymar na Mbappe, lakini taji la Ulaya lilikuwa ndoto. Luis Enrique Martinez akaanza mradi wake mpya kwa kuwachukua kina Vitinha na Fabian Luiz ambao sio wachezaji wa kariba ya Mbappe.
Ametengeneza timu ambayo kwa mara nyingine imefundisha adabu Madrid. Kwanza walifundisha adabu wengine na kuchukua ubingwa wa Ulaya, lakini sasa wanaelekea kuchukua ubingwa wao wa dunia. Chelsea kuna timu ya kuwazuia PSG pale? Sijaiona.
Na sasa Mzee Florentino katika umri wa miaka 78 anafundishwa adabu na walimwengu. Hajawahi kusahau sera yake ya Galacticos. Anapenda kwenda nayo kila mahali. Kuanzia wakati ule wa kina Luis Figo, Zinedine Zidane, Ronaldo de Lima, David Beckham na wengineo.
Hata hivyo, sasa hivi anafunzwa adabu na mpira wa kisasa. Anapowakimbilia kina Mbappe mahasimu wake Barcelona wao wanawakuza kina Pedri, Lamine Yamal na Gavi wakitokea La Masia. Na bado anapokea vichapo.
Alonso atawanyoosha kina Mbappe, lakini Perez anapaswa kumpa ruhusa. Tatizo Perez anawaza biashara. Anawaza maduka yake. Mastaa lazima wacheze kwa sababu za kibiashara. Kocha anataka lazima wakabe uwanjani ndipo wacheze.
Tatizo linaweza kutokea hapo. Akiwa na Bayer Leverkusen maisha ya Alonso yalikuwa rahisi na ndio maana akawapa ubingwa wao wa kwanza katika historia ya Bundesliga. Kila mchezaji anamsikiliza. Kila mchezaji anamuelewa.
Pale Madrid itafika mahali Alonso anaweza kuona Vinicius na Mbappe hawawezi kucheza kwa wakati mmoja. Perez atakubali? Yeye anawataka wote uwanjani kwa sababu za kibiashara. Anawataka wote uwanjani kwa ajili ya kuongezeka kwa viingilio.
Hata hivyo, mpira mzuri na maridadi kama ule wa PSG ndio ambao unaweza kuiongezea viingilio Real Madrid na pia mauzo ya jezi. Tatizo Perez hawezi kuwafikiria wachezaji kama kina Vitinha katika ubongo wake, lakini ndio wachezaji wanaomudu staili za kina Alonso.
Tusubiri na kuona, lakini ukweli ni kwamba Madrid imefunzwa sana na ulimwengu katika miezi ya karibuni. Haishangazi kuona Mzee Perez akaenda zake Ujerumani kumfuata Alonso na kumrudisha Hispania. Anaamini ana kitu kile kile ambacho Pep Guardiola anacho, Arteta anacho, Luis Enrique anacho. Na hata Cesc Fabregas anacho pale Como.