Molinga afunguka kwanini ametua Namungo



WAKATI klabu za Ligi Kuu Bara zikikamilisha usajili saa chache kabla ya dirisha la usajili kufungwa, Namungo FC ilimtambulisha mshambuliaji kutoka DR Congo, David Molinga katika ukurasa wa Instagram kuwa tayari imeinasa saini ya mchezaji huyo ambaye msimu uliopita allikuwa akiitumikia Zesco United ya Zambia.

Msimu wa 2019-2020, Molinga alikuwa akiichezea Yanga na hadi anaondoka Jangwani alikuwa amefanikiwa kufunga mabao 11 katika Ligi Kuu, huku akiwa mfungaji bora wa timu hiyo katika msimu huo, ingawa uongozi uliamua kuachana na mshambuliaji huyo ambaye alikuwa ameitumikia timu hiyo kwa msimu mmoja.

Hata hivyo, wakati anaicheza Yanga, Molinga aliwahi kuifunga Namungo FC mabao mawili katika sare ya 2-2.

Bao la mwisho kuifungia Yanga ilikuwa katika mchezo wa mwisho wa ligi msimu wa 2019/20 dhidi ya Lipuli kwenye Uwanja wa Samora dakika ya 39.

Baada ya kuondoka Yanga alijiunga na Zesco United ya Zambia aliyodumu nayo msimu mmoja tu - kabla ya kuamua kujiunga na Namungo FC. Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti kutoka DR Congo, nyota huyo alifunguka mambo mbalimbali ikiwemo namna alivyopata dili la kuchezea Zesco.

“Unajua huyu kocha ambaye alikuja Azam FC msimu uliopita, George Lwandamina kabla hajaondoka Zambia ndiye alinihitaji niende kucheza Zesco United. Nilikuwa nimemalizana na Yanga. Kwa hiyo ilikuwa rahisi kwenda kusaini timu yake,” anasema Molinga


MAISHA NDANI YA ZESCO

Akizungumzia maisha yake katika timu ya Zesco, Molinga anasema: “Nilipoenda nilimkuta Lwandamina na ndiye aliyetaka nisajiliwe pale. Kwa hiyo mwanzoni mambo yalienda vizuri tu, lakini alipoondoka kuja Azam mambo yalibadilika, kwa sababu kocha aliyekuja alikuwa hanipi nafasi ya kuanza mara kwa mara.

“Nilisaini mkataba wa miaka miwili ambao ulipaswa kwisha 2022, lakini nimecheza mwaka mmoja tu - msimu wa 2020/21. Ulivyoisha niliamua kuomba kuondoka kwa sababu nilikuwa sioni nafasi ya kuendelea kucheza kikosi cha kwanza, ingawa viongozi wa Zesco waliniambia tukae chini tuzungumze tuyamalize, nilikataa kubaki nikaomba kuondoka.”


UJIO NDANI YA NAMUNGO FC

Mchezaji huyo alizungumzia kilichomsukuma kutua Namungo, akisema: “Nilipata ofa kutoka nchi kadhaa ndani ya Afrika kabla ya kupokea ofa ya Namungo FC, lakini ilipokuja ofa ya Namungo FC niliamua kuikubali. Niliachana na zile dili nyingine kwa sababu nilikuwa naona ni vizuri kuja kucheza Tanzania - sehemu ambayo nimewahi kucheza.

“Kwangu niliona mazingira (ya Tanzania) hayatakuwa yamebadilika ukilinganisha na sehemu nyingine ambazo ningeenda kucheza.

“Nimesaini mkataba wa mwaka mmoja tu kwa sababu niliwaambia viongozi wa timu ninahitaji kuwekeza nguvu nyingi msimu huu wa kwanza kuona mambo yataendaje na kama kila kitu kikienda vizuri nitaongeza mkataba.”


MO BANKA, MAKAME

Kuhusu usajili uliofanywa na Namungo, nyota huyo anasema: “Huwezi kuamini, yaani nilivyojua kuwa kina Banka na Makame

wamesaini Namungo FC nilifurahi sana, kwa sababu nimecheza nao Yanga.

“Nilikuwa nafurahi kucheza timu moja na Banka hata tulivyokuwa tukicheza Yanga iwe mazoezini au kwenye mechi. Kiukweli naona tutakuwa na ushirikiano mkubwa baina yetu kwa kuwa tunajuana vizuri.

“Najua Obrey Chirwa pia amesajili. Ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa na ligi ya Tanzania, lakini ujio wangu Namungo ni kuja kuongezea uzoefu wangu ndani ya klabu ili tuweze kuisaidia kufikia malengo waliyojiwekea msimu mpya, ingawa suala la mchezaji gani aanze kikosi cha kwanza ni uamuzi na kazi ya kocha mwenyewe.

“Moja ya suala lililonivutia kujiunga Namungo ni malengo waliojiwekea msimu huu mpya. Kwanza timu yetu ina malengo ya kuwa miongoni mwa timu zitakazofanya vizuri kwenye ligi ili kupata nafasi ya kushiriki tena michuano ya kimataifa, hilo ndio lengo letu kubwa.

“Lakini mpira unahitaji hamasa sana na ninaona kikosi chetu kitakuwa na hamasa kubwa, kwa sababu tuna malengo ya kugombania ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ingawa najua watu wanaweza kuona ni jambo lisilowezekana. Mimi nakuhakikishia kwamba hilo jambo linawezekana kabisa.

“Naweza kukupa mfano mdogo tu, msimu uliopita kwenye La Liga ukiachana na masuala ya kiufundi, Atletico Madrid ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi kutokana na hamasa waliyokuwa nayo ambayo ndio ilichangia kwa kiasi fulani kuzishinda Real Madrid na FC Barcelona.”


MFUNGAJI BORA YANGA

Molinga alikuwa mfungaji bora Yanga msimu aliocheza, hivyo anaelezea juu ya hilo alipotua Namungo.

“Nimekuja kufanya kazi na moja ya kazi yangu Namungo ni kufunga mabao mengi ili kuisaidia ifanye vizuri katika ligi na kombe la FA,” anasema na kufafanua juu ya tetesi za kutaka kurejea Yanga.

“Ni kweli wakati nipo Zesco United nilikuwa nawasiliana na baadhi ya viongozi wa Yanga na kweli kulikuwa na mpango huo wa kuja kucheza Yanga tena, lakini unajua Yanga inapenda kusajili wachezaji wenye majina makubwa. Kwa hiyo kuna vitu vingi vilitokea na sitaweza kuvisema, lakini nashukuru Mungu nimerudi tena Tanzania.

“Hivyo kurudi au kutorudi Yanga siwezi kulizungumzia kwa sasa. Ni Mungu pekee ndiye anayejua nini kitatokea siku zijazo, ngoja kwanza nijikite zaidi na Namungo FC, halafu hayo mambo mengine tutaweza kuyazungumza siku zijazo.”


IMEANDIKWA NA ABDULGHAFAL ALLY