Mjue Mkenya Bernice, mpishi wa pilau Arsenal

GUMZO linaloendelea kwenye mitandao Kenya na Afrika Mashariki ni uvumi wa kuacha kazi wa mpishi wa Arsenal ambaye ni raia wa nchi hiyo, Bernice Kariuki.

Uvumi huo uliibuka baada ya Bernice kuposti andiko kwenye akaunti yake ya Facebook baada ya  mechi ya mwisho ya msimu ya Arsenal, Mei 28 waliposhinda mabao 5-0.
Andiko hilo liliibua taharuki kwamba ameachana na Arsenal baada ya kudumu nayo miaka miwili,lakini akaibuka na kukanusha hilo kupitia kwa mwandishi wa NTV Kenya, Alex Chamwada. "Ni habari za uzushi, mimi ni mpishi binafsi, nimeajiriwa na kampuni binafsi inayotoa huduma Arsenal."

Katika mahojiano yake ya hivi karibuni, Bernice alifichua namna alivyopata kazi katika klabu ya Arsenal, akihudumia kikosi cha kwanza kwa mapenzi makubwa.

Bernice ni kati ya wapishi 27 pale Arsenal wanaoshughulika na maandalizi ya msosi wa kikosi cha kwanza cha kocha Mikel Arteta aliyeukosa ubingwa dakika za lala salama.
Chini ya uongozi wa Mpishi Mkuu wa Arsenal, Darren Taylor, majukumu ya Bernice ni kuandaa misosi ya kikosi cha kwanza tu na benchi la ufundi.

Mbali na hilo, Bernice ametwika jukumu la kuaanda vyakula vyepesi vya kumpiga busti au kumrejeshea mchezaji nguvu kabla na baada ya mechi. Aidha yeye ndiye mwenye jukumu la kuandaa menyu kikosi kinapokuwa na safari ya nje ya nchi hususan ikizingatiwa mataifa tofauti yana aina tofauti ya vyakula.

PILAU, CV VILIVYOMBEBA
Baada ya kuondoka Kenya, Bernice alipata udhamini wa masomo katika Chuo cha Westminster Kingsway College jijini London alikosomea sanaa ya upishi (Culinary Arts). Alipofuzu aliajiriwa kwenye mahoteli ya nguvu Uingereza zinazotembelewa na watu wenye nafasi na pesa zao kama vile The Lanesborough, The Dorchester na The Waldorf Hilton iliyoko jijini London.

“Wengi wameanza kunifahamu kwasababu nipo Arsenal, lakini pia nimewahi kuwa mpishi wa klabu ya Tottenham Hotspurs."
Anakiri ni msosi mmoja alioandaa kwenye karamu moja mwaka juzi iliyohudhuriwa na Pierre-Emerick Aubamayeng kipindi hicho akiwa bado Arsenal, ndio iliyompa kazi.

“Nilialikwa kwenye pati moja ya Krismasi kuandaa msosi na huko ndiko nilikutana na Auba ambaye sasa yupo Chelsea. Niliandaa vyakula vingi ikiwemo pilau. Sasa kwenye pati, nikamwomba Auba kama anaweza kunisaidia nipate kazi Arsenal. Sikujua pilau niliyoandaa ilikuwa imebamba sana.

"Aliupenda sana ukizangatia ulikuwa wali, ila wenye utofauti kwa namna nilivyoandaa. Alichoniambia pale ni kwamba, tutaanza kwanza kwa yeye kuniajiri kama mpishi wake sababu alifurahishwa sana na ule msosi,” anasema Bernice mwenye miaka 51.

Huu ukawa mwanzo wa uhusiano mzuri na baadaye, Aubameyang aliweza kumtambulisha kwa uongozi wa upishi wa Arsenal na kutokana na kuwa kazi yake inaonekana, ikawa rahisi kupata kazi.
Kocha Arteta alipokabidhiwa timu, alianza kubadilisha mambo kibao ikiwemo suala la lishe kwa wachezaji wake ili kuhakikisha wanampa huduma anayopata. Ni kwenye harakati hizi, ikatokea naye Bernice alikuwa akisaka kazi kule na baada ya uwezo wake kuonekana, hata Arteta alifurahia na kupendekeza aongezwe kwenye timu.


MAISHA YA UPISHI, MASTAA
“Ukiachia mbali wachezaji mastaa, nimekutana hata na familia ya kifalme mara si moja. Ukumbuke niliwahi pia kufanya kazi Dorchester ambayo nafikiri ndio hoteli kubwa zaidi duniani na tena ya staha. Pale ni watu mashuhuri tu ndio huingia,” alisema.
Akiwa na zaidi ya miaka 15, kwenye taaluma hii, Bernice ni Private Chef. Anasema; "Private Chef ni mpishi aliyejiajiri. Kwa hiyo hata Arsenal ni kama kibarua. Sijaajiriwa kwa mkataba wa kudumu,” alifafanua. Ukiwa Private Chef, unaunda timu ya wapishi wataalamu waliobobea kwenye nyanja mbalimbali ya upishi. Nipo kwenye timu ya wapishi 90 na yupo bosi juu. Sasa hapa kila mmoja wetu huenda kutafuta kazi, na ukipata unawaita wenzako mnasaidiana majukumu,” anasimulia Bernice.

 “Kwa staili hii, utapiga pesa ndefu sana sababu ni tofauti na kuajiriwa sehemu moja tu. Kwa staili hii, unakuwa na wateja wengi sana sababu kumbuka ni kundi na kila mpishi anatafuta kazi akipata anawaita wenzake kusaidiana. Malipo huwa mazuri sana. Mimi ni 'hasla', unajua Wakenya tulivyo eeh.”


UPISHI ARSENAL SIO RAHISI
Kwa timu kubwa kama Arsenal, ina takriban wachezaji wasiopungua 25 wanaounda kikosi cha kwanza. Ukiongeza hao na kikosi cha chipukizi na vile vile kikosi cha timu ya wanawake ni takribani wachezaji 118 kabla ya kuongeza benchi za ufundi.

“Tunazungumzia kijiji cha watu, zaidi ya 600 kwenye klabu. Kwa maana hiyo tuna zaidi ya wapishi 90, huku 27 wakitengewa rasmi majukumu ya kikosi cha kwanza. Na kule sio tu upishi, ni upishi wa kiafya. Kiwango cha mafuta, chumvi lazima viwe sahihi. Juisi zao lazima ziwe na virutubisho sahihi na majukumu yote hayo yanatuangukia sisi. Kila kitu sisi huandaa kwa uhalisia,” anasema.

“Halafu wachezaji hawali chakula sawa. Kwa hiyo ni jukumu lako kujua nani anakula nini na kwa kiasi gani na umwandalie. Kuna mtu atakuwa ameongeza kilo anatakiwa kupunguza, huyo msosi wake utakuwa tofauti na anayepaswa kuongeza kilo au yule anayeuguza majeraha. Kwa hiyo hatupiki chakula chochote tu,” alifafanua.

Kwa ujumla msosi unaolipwa sana Arsenal na wachezaji ni samaki. Kibarua chake Arsenal huanza saa tisa asubuhi.
“Pamoja na kikosi changu huwa tunaanza kwa kuzitengeneza zile samaki kwa ajili ya mapishi sababu unapaswa kumwandaa samaki jiko likiwa bado baridi. Kisha baada ya pale, tunawandalia wachezaji vinywaji vya protini sababu wao hukimbia kila siku asubuhi kwa hiyo, wanapofika uwanjani saa 10 asubuhi, wanakuta tayari. Watu hawajui tu, hawa wachezaji huamka mapema sana,” alisema.
Baada ya kukimbia, watarejea tena uwanjani, na kumkuta Bernice na wenzake wamewaandalia kifungua kinywa.

“Watakula na mara nyingi huwa ni omelette (msosi wamayai) na ovacado, kisha wapumzike wakisubiri vikao vya mazoezi ambavyo huanza saa tano asubuhi,” alisema aliyekulia maisha magumu kwenye mtaa duni wa Jericho.
“Mimi ni demu wa ghetto, Jeri W412, pale Lumumba Drive karibu na Ofafa Jericho (Nairobi). Nilisomea shule ya Msingi Makadara na nilipita mitihani yangu nikaitwa Precious Blood Riruta. Ni shule nzuri sana kila Mkenya anajua hilo ila sikupenda sababu ilikuwa shule ya watoto wa kitajiri. Halafu nilitokea ghetto na unajua watoto wa ghetto walivyo wakorofi kutokana na kupitia maisha magumu. Nakumbuka nikifukuzwa kwenye muhula wa kwanza,” anasimulia.

Baada ya pale, babake alimpeleka kijijini kwao Nyandarua, “Nikawekwa kwenye shule ya kawaida sana iliyoitwa Magomano na kwangu mimi nilipenda maisha ya kijijini sababu babu na nyanyangu walikuwepo.”

Miaka minne baadaye alipomaliza kidato cha nne mwaka 1990, babake alimtafutia kazi Mombasa.
“Nilimwambia baba mimi sikai Kenya, anitafutie pesa niondoke, na ndivyo niliishia kujikuta Sweden nikiwa na miaka 19 tu. Huko ndiko nilianza kusomea upishi. Baada ya hapo ndio nikahamia Uingereza,” alisema. Mpango wake kwasasa ni kufungua shule ya upishi Kenya, ili kukuza kizazi kijacho cha wapishi.