MJUAJI: Yanga imedhulumiwa fainali

WIKI iliyopita niliandika kuhusu Yanga na leo naandika tena kuhusu mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania.

Sio upendeleo kama wengine wanavyonitumia ujumbe na kuniambia, la hasha. Yanga inastahili kuandikwa katika kipindi hiki.

Moja ya sababu kubwa ni kuweka historia sawa, kumbuka Yanga imefika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya miaka 30 kwa timu ya Tanzania kufikia hatua hiyo. Simba ilicheza fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993.

Je, lini tena timu ya Tanzania itafikia hatua kama huyo au zaidi? Itachukua tena miaka 30 au timu zetu zitakuwa zimeshapata uzoefu? Tusubiri na kuona.

Jana Jumamosi usiku Yanga ilikuwa inacheza mchezo wa pili wa fainali dhidi ya USM Alger ya Algeria, matokeo ni kama ulivyosikia.


MIAKA 55 ILIYOPITA

Miaka 55 iliyopita, Yanga ilibeba ubingwa wa Ligi ya Taifa ya Tanzania (sasa Ligi Kuu ya Tanzania) na kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Klabu Bingwa (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) barani Afrika mwaka 1969.

Kumbuka Yanga ilibeba ubingwa wa Ligi ya Taifa kwa miaka mitano mfululizo baada ya Sunderland (Simba) kuchukua mara mbili mfululizo msimu wa 1964/ 65 na 1965-66 na mara ya tatu mwaka 1967 ubingwa ukaenda kwa Cosmopolitan.

Chama cha Soka cha Tanzania (FAT) kilikuwa bado kichanga sana kwani kilijiunga na CAF mwaka 1964.


MAANDALIZI BABU KUBWA

katika kujiandaa na uwakilishi wa nchi, Yanga ilifunga safari kwenda Romania ikiwa na Kocha Peter Mandawa kufanya katika maandalizi ya msimu ‘Pre-sesson’ kwa takribani mwezi mzima. Iliporudi nchini ilirudi na Kocha Mromania, Proffesa Victor Stansceluscu.

Ziara hii ilikuwa na matunda mazuri kwa Yanga kwani iliisaidia kufanya kufanya vizuri kwenye mashindano hayo ya Afrika tangu hatua ya awali.

Katika mchezo wa kwanza, Yanga ilikuwatana na timu kutoka Madagascar, Fitarikandro. Yanga ilishinda mabao 4-0 nyumbani na ilipoenda ugenini ikakubali kichapo cha mabao 2-0 kusonga mbele, ikaenda raundi ya kwanza.


HAWA HAPA SAINT GEORGE

Katika raundi ya kwanza Yanga ilikutana na timu kutoka Ethiopia, Saint George. Mchezo wa kwanza ulikuwa ni ugenini ikalazimisha sare tasa. Katika mchezo wa marudiano ikaipiga bila huruma timu hiyo mabao 5-0 na moja kwa moja kutingia robo fainali.

Mara ya pili tena, Yanga iliifunga Saint George maboa mengi, jumla yalikuwa ni 8-3 mwaka 1998 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezo wa kwanza ulikuwa sare ya mabao 2-2 Ethiopia na hapa nyumbani Yanga iliichapa 6-1.

Yanga ilifanikiwa kucheza hatua ya makundi na kupangwa kundi F na timu za Asec Mimosa, Manning Rangers, Raja Casablanca na Young Africans.


CHUKUA HISTORIA HII

Kumbuka hadi kufikia hapa Yanga ilikuwa ni timu ya kwanza kuwakilisha nchi kimataifa ugenini.

Ndio, Simba ikiwa unatumia jina la Sunderland ilishindwa kuwakilisha nchi baada ya chama cha soka nchini, kushindwa kupeleka jina Chama cha Soka Afrika (AFC, sasa CAF).

Cosmopolitan iliwakilisha nchi lakini kwa mchezo mmoja tu wa hapa nyumbani dhidi ya timu ya Jeshi la Somali na kushindwa kwenda kucheza mechi ya ugenini kutokana na ukata.

Historia ya pili, Yanga ikawa timu ya kwanza ya Tanzania kuingia Robo fainali


YANGA YADHULUMIWA HAPA

Katika mchezo wa robo fainali Yanga ilikutana na timu kutoka Ghana, Asante Kotoko.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa mjini Kumas, Yanga ilipata sare ya bao 1-1. Na katika marudiano jijini Dar es Salaam Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) matokeo yakawa yaleyale sare 1-1.

 Baada ya matokeo hayo ikabidi ukachezwe mchezo wa mwisho wa timu hizo katika uwanja huru 'neutral ground'. Utaratibu wa kupigiana penalti haukuwepo. Gemu ikanda kuchezwa Ethiopia ambayo nayo ikaisha kwa sare.

Hapo sasa ndipo Yanga ilipodhurumiwa ikaamuliwa irushwe shilingi ili iamue nani aende nusu fainali.


UDANGANYIFU ULIFANYIKA

Manahodha wa pande zote mbili walishuhudia mwamuzi akirusha shilingi, kapteni wa Asante Kotoko alifanya ujanja kwani baada ya shilingi kutua na kung’amua walikuwa wamekosa aliikimbilia na kuinyakuwa na kisha kushangilia na kumfanya kapteni wa Yanga Abdulrahaman kupigwa na butwaa pamoja na kwamba shilingi iliangukia upande wake.

Ndipo Yanga ikadhulumiwa nafasi ya kuwa timu ya kwanza kuingia nusu fainali, rekodi iliyokuja kuwekwa na watani zao, Simba mwaka 1974, labda ingeweza kutinga hata fainali na kubeba kombe kabisa. Nimesema labda.


KITWANA MBAYA SANA

Straika wa Yanga, Kitwana Manara ‘Popat’ aliingia kwenye orordha ya wafungaji bora akiwa mfungaji bora namba tisa akiwa na mabao mawili.