MJUAJI: Salim Bawaziri avunja pambano la Simba na Yanga

MACHI 16, 1969, mjini Dar es Salaam katika Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) maelfu ya watu walikuwa wamefurika kwa wingi kwa ajili ya kuona mchezo wa Sunderland na Yanga.

Hata hivyo, kwa bahati mbaya sana mchezo huo haukuchezwa. Unadhani kisa kilikuwa nini? Fuatana na Mjuaji...


NINI CHANZO

Baada ya mchezo huo kutochezwa, mashabiki hao walishindwa kujua wamlaumu nani kwa kutochezwa kwa mchezo huo, kati ya Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT, sasa TFF) na klabu ya Sunderland.

Mchezo huo haukuchezwa baada ya klabu ya Sunderland kugoma kutokana kuyakataa maelekezo ya FAT.

Sababu kubwa iliyowafanya Wekundu wa Msimbazi kugomea mchezo huo ni kitendo cha African Sports ya Tanga kumchezesha kipa Salim Bawaziri katika mchezo wa Ligi ya Taifa (sasa Ligi Kuu).

Unaweza kushangaa ilikuwaje, Bawaziri alikuwa ni kipa wa African Sports ya Tanga, aliwezaje kuvunja pambano hilo la watani wa jadi, Sunderland na Yanga?

Sunderland ilitoa taarifa mapema kuhusu mchezo huo kuwa isingeweza kuingiza timu uwanjani ikikishinikiza Chama cha Soka Tanzania (FAT) kutangaza marekebisho ya sheria mpya za ligi hiyo.

Timu hiyo ilisema isingeshiriki mchezo huo na mwingine wa Ligi ya Taifa dhidi ya Coastal Union kama FAT haitatangaza sheria mpya za ligi hiyo.

Taarifa ya Sunderland ilisema FAT iliuambia uongozi wa timu hiyo sheria za mwaka huo za soka zilikuwa hazitumiki na kulikuwa na sheria mpya ambazo ingezitangazwa muda wowote.


ISHU YA BAWAZIRI

Simba ilifafanua, sababu ya kugomea mchezo huo ni kitendo cha African Sports kumchezesha kipa Salim Bawaziri akiwa anakutana na timu hiyo mara tatu ndani ya msimu mmoja.

“Februari 22, 1969 tulicheza dhidi ya Sports na kutoka nayo sare ya bao 1-1. Katika mchezo huo kulikuwa na makosa. Kipa wa Sports ya Tanga, Bawaziri kwanza alikuwa ni mchezaji wa Klabu ya Ujamaa.

“Tumewahi kucheza na Ujamaa katika raundi ya kwanza na ya pili zote kipa akiwa Bawaziri na sasa tumecheza naye mara ya tatu akiwa anaitumikia Sports baada ya kujiunga na timu hiyo katika raundi ya pili,” ilisema sehemu ya taarifa ya Sunderland.


SPORTS YATOA MAELEZO

Klabu ya African Sports ya Tanga ilisema imeshangazwa na kitendo cha Sunderland kugomea mchezo dhidi ya Yanga kwa kuwa wao waliruhusiwa kumtumia kipa wao Bawaziri kwa sheria za Ligi ya Taifa.

Katibu Mwenezi wa Sports alisema wanazo nakala za barua walizowasilisha FAT na ile ya chama hicho kuwaruhusu kumtumia kipa huyo.

“Mbona tulicheza na Yanga na Bawaziri alikuwapo langoni kwetu lakini hawakulalamika,” alihoji kiongozi huyo.

Hata hivyo, sasa mwaka uliofuata baada ya sakata hilo, yaani 1970 Bawaziri aliihama Sports a.k.a Wana Kimanumanu na kutua Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ a.k.a Wana Mangushi, aliyonayo hadi leo akiwa mmoja wa wanachama na viongozi waliowahi kushinda nyadhifa mbalimbali.


KWANI SHERIA INASEMAJE?

“Sheria namba ‘B-C’ kifungu cha 2 cha Ligi ya Taifa ya Tanzania ya mwaka 1968 na 1969 inasema hivi:

“Ni marufuku kwa mchezaji wa timu yoyote inayoshiriki Ligi ya Taifa kujiunga na timu inayoshiriki ligi hiyo katika raundi ya pili, iwapo mchezaji atafanya hivyo, timu yake itapoteza mchezo na pointi kupewa timu inayocheza nayo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo hiyo.


FAT ILISEMAJE?

“Hivyo tumedai kupewa ushindi dhidi ya African Sports kwa mujibu sheria namba 20 ya Ligi ya Taifa ya Tanzania ambayo inasema- Timu yoyote inaweza kupinga au kudai ushindi baada ya siku tatu baada ya mchezo husika.”

Sheria iliitaka Sunderland kuandika barua na kuambatanisha na Sh100 na kiasi hicho cha pesa kilitakiwa kurudishwa ikiwa madai ya timu hiyo yatafaulu na kutorudishwa kama hayatafaulu.

FAT iliijibu Sunderland na kuirudishia Sh100 na kukiri kitendo cha Bawaziri kuichezea Sports kilikuwa ni makosa.


FAT YARUDISHA Sh100

Hata hivyo, FAT ilisema sheria hizo za Ligi ya Taifa ni za zamani ambazo sio madhubuti na kuiambia Sunderland iendelee kucheza michezo mingine ya ligi mpaka pale sheria mpya za soka zitakapokuwa zimetolewa.

Pamoja na FAT kuirudishia Sunderland kiasi chake cha Sh100, lakini ikagoma kuipa ushindi katika mchezo wake dhidi ya Sports.

“Kwa jibu hilo la FAT tumeamua kutocheza mechi zote za Ligi ya Taifa hadi pale sheria mpya zitakapotolewa.

“Hatuwezi kucheza ikiwa hakuna sheria yoyote ya ligi hiyo kwa sababu hata Ligi za Jangwani na Buguruni zina sheria zake. Leo itakuwa kinyume kuona National League ichezwe bila ya kufuata sheria,” ilihitimisha taarifa hiyo ya Sunderland.

Mchezo wa Sunderland na Yanga ulikuwa unasubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wa soka na kiingilio chake kilikuwa ni Sh7/=, 5/=, 3/= na Sh2/=.

Unajua kama Yanga ilishawahi kuifunga Brazil mabao 3-1 na kuwa habari kubwa sana hapa nchini?

Basi kama unataka kuipata habari hiyo kwa kina usikose kusoma Mwanaspoti Jumapili ijayo.