MJUAJI: Sababu Simba, Yanga kutocheza wikiendi

KUNA watu wanalalamika kwanini Simba na Yanga leo hii hazipangiwi ratiba ya kucheza michezo ya Ligi Kuu saa 8 mchana.

Lakini walishawahi kushuhudia Simba na Yanga zikicheza mechi zao za Ligi Kuu au mashindano mengine (zikipambana zenyewe) katikati ya wiki?

Yaani itokee mchezo wa Simba na Yanga uchezwe labda Jumatano, Alhamisi, Jumanne au hata Ijumaa? Sio kama haijawahi kutokea, imeshawahi kutokea lakini kwa miaka ya sasa hiyo mechi lazima itachezwa usiku.

Kamwe haiwezi kuchezwa kuanzia saa 10 jioni ni lazima itaanza saa 11 jioni kama sio saa 1:00 usiku.

Mchezo uliokuwa uchezwe Juni 21, 1973 ilikuwa siku ya Alhamisi lakini asubuhi tu, habari zikaibuka kwamba mchezo huo hautachezwa siku hiyo. Siku hiyo, magazeti yote yaliyotoka yaliibuka na habari kubwa ya kukanusha kuwepo kwa mchezo huo.

Habari zilisema hivi, mchezo uliokuwa uchezwe leo, Alhamisi hautakuwepo na badala yake umepangwa kuchezwa Juni 23 ambayo ilikuwa Jumamosi.

Taarifa kutoka Makao Makuu ya Chama cha Soka cha Tanzania (FAT) iliyotolewa na Katibu Mkuu, Martin Mgude usiku wa Jumatano (Juni 20, 1973) ilitangaza kuahirishwa kwa mchezo huo.


SABABU HIZI HAPA

Taarifa ya Mgude ilisema kuarishwa kwa mchezo huo kulitokana na hofu ya wafanyakazi wengi kutoroka kazini na kwenda uwanjani kushuhudia mchezo huo.

Habari za ndani zinasema taarifa iliyotoka serikalini ilisema FAT ihakikishe mchezo huo hauchezwi siku hiyo.

Serikali ilipatwa na hofu kwa kuwa ilitambua kwamba watu wengekuwa na hamu ya kusikiliza au kuutazama mchezo huo uliokuwa uanze saa 10 jioni.

“Kwa vyovyote vile watu hawataweza kustahimili, tunajua jinsi wananchi wanavyozipenda timu zao za Simba na Yanga,” taarifa nyeti ilibainisha.

Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyoufanya mchezo huo usichezwe kwa kuwa mashabiki wengi wa Simba na Yanga wangetoroka mapema kazini na kuwahi kushuhudia mchezo huo.

Pia, hata viongozi wengi wa serikalini nao wasingeweza kustahimili kwa sababu nao wamegawanyika katika ushabiki wa timu hizo.

Sababu hizi zimekuwa zikitumika hadi leo hii kuzifanya timu hizi zisicheze katikati ya wiki.


SIMBA ILIGOMEA

Awali mchezo huo ulipangwa kuchezwa Uwanja wa Karume, Ilala ulihamishiwa Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) kutokana na sababu za usalama na kuwapa nafasi watazamaji kushuhudia mchezo huo vizuri zaidi.

Hata hivyo, wakati hali hiyo ikijitokeza, Simba ilikuwa imeweka mgomo wa kucheza mchezo huo katika Uwanja wa Taifa.

Katibu Mwenezi wa Simba, Jimmy David Ngonya alisema timu yake ingeweza kucheza mchezo huo katika Uwanja wa Taifa kama FAT ingetoa sababu nyingine za kuuhamisha mchezo huo kutoka Karume hadi Uwanja wa Taifa, tofauti na zile za kiusalama.

“Hatuoni sababu za kuuhamisha mchezo huo katika dakika za mwisho, tunajua utachezwa Uwanja wa Karume,” alisema Ngonya.


YANGA KIROHO SAFI

Katibu Mwenezi wa Yanga, Mshindo Mkeyenge alisema hawawezi kusema lolote kwa sababu jambo hilo lilikuwa mikononi mwa watendaji wa mashindano hayo.

“Ni jukumu la waandaaji kuona kuona kama wataona kuna umuhimu wa kuuhamisha mchezo huo katika Uwanja wa Taifa,” alisema Mkeyenge.

Kwa maoni yake Mkeyenge alisema haoni kwanini baadhi ya watu watoke uwanjani wakiwa wameshindwa kuuona mchezo huo vizuri ukichezwa Uwanja wa Karume kutokana na udogo wa uwanja huo.

Mkeyenge alisema mchezo huo ni kama mwingine wowote ambao timu yake imekuwa ikicheza.


Vikosi vilivyotarajiwa kupangwa hivi

Simba: Athumani Mambosasa, Mohamed Kajole, Shaban Baraza, Athur Mambeta na Omary Choggo.

Wengine ni Khalid Abeid, Willy Mwaijibe, Haidar Abeid, Abbas Dilunga, Abdallah Kibaden ëKingí na Sentala.

Yanga: Muhidin Fadhili, Seleman, Ali Yussuf, Gobbos, Kapera, Abdulrahaman Juma, Chitete, Sunday Manara, Kitwana Manara, Gibson Sembuli na Maulid Dilunga.


SIMBA SC YAJIKOMBOA

Baada ya kuarishwa kwa mchezo huo, ulichezwa Juni 23, 1973 kama ulivyopangwa katika Uwanja wa Taifa na Simba iliyokuwa ikipoteza mara kwa mara dhidi ya Yanga iliibuka kidedea kwa ushindi wa bao bao 1-0.

Bao la Simba lilifungwa na Haidari Abeid ‘Muchacho’ katika dakika ya 68.

Kwa maoni na ushauri, tuwasiliane kwa namba 0713 900 017.