MJUAJI: Pan Africans iligomea ligi 1982

SUALA la timu za Ligi Kuu kuwa na viporo vingi kwa kisingizio cha mechi za kimataifa halikuanza leo wala jana, lilikuwepo tangu kitambo.
Suala hili lilikuwa likizihusisha sana timu za Simba na Yanga kwa kulalamikiwa na timu nyingine za ligi hiyo.
Hata hivi karibuni kumekuwa na malalamiko kwa Ligi Kuu kusimama wiki nzima bila ya sababu za msingi hadi juzi iliporudi tena.
Tukio kama hilo liliwahi kutokea na Pan Africans kutishia kugomea Ligi ya Taifa. Ulikuwa ni mwaka uleule ambao umekuwa na matokeo mengi ya soka, mwaka 1982.
Kama wewe ni msomaji mzuri wa makala hizi utagundua nimeandika mambo mengi sana kuhusu mwaka huo.
MENEJA WA PAN
Klabu ya Pan iliamua kugomea au kutishia kuendelea kucheza Ligi ya Taifa (sasa Ligi Kuu Tanzania Bara) na sababu kubwa ilikuwa ni klabu ya Yanga Africans.
Meneja wa Pan, wakati huo Omari Juma alikitaka Chama cha Soka cha Tanzania (FAT) kuhakikisha timu zote zinacheza michezo sawa ili kuondoa uwezekano wa kupanga matokeo.
Juma alisema timu yake ilikuwa inajipanga kupeleka barua FAT na vyombo vingine vya juu vya michezo kuhusu ligi hiyo ilivyokuwa ikiendeshwa.
“Kuna timu zinacheza mara kwa mara na nyingine zimesimama hazichezi bila ya sababu ya msingi,” alisema.
SIMBA, COASTAL NAO
Kabla ya suala hilo kuvaliwa kibwebwe na Pan African, timu za kwanza kulalamika zilikuwa ni Simba na Coastal Union.
Timu hizo zilidai hali ya timu moja kutocheza kwa muda mrefu ingeweza kuisaisia kutwaa ubingwa.
KISA YANGA
Hadi wakati Pan inalalamika ilikuwa tayari imeshacheza michezo saba, sawa na Tumbaku ya Morogoro na kubakisha michezo mitatu tu. Coastal Union ya Tanga ilikuwa imecheza michezo sita, huku Simba na CDA Dodoma ‘Watoto wa Nyumbani’ walikuwa wamecheza michezo mitano.
Yanga iliyokuwa bingwa mtetezi ilikuwa imecheza michezo minne tu huku ikibakisha michezo sita.
Juma alidai, FAT ilikuwa na njama kwa sababu ilikuwa ikibadilisha ratiba ya ligi hiyo mara kwa mara, mabadiliko ambayo yalikuwa yanazifanya timu nyingine baadhi ya timu kama Pan kucheza michezo mingi.
Kiongozi huyo alisema Pan isingecheza mchezo wowote wa ligi hadi timu zote ziwe na michezo sawa.
“Hatari yake timu ambazo zitacheza mechi zake nyingi mwishoni zinaweza kupanga matokeo ya kutoshuka daraja ua kutwaa ubingwa,” alisema Juma.
Kiongozi huyo alikikataa kisingizio cha Yanga kutocheza ligi kwa sababu ya kuwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.
ILIKUWA KLABU BINGWA
Wakati huo, Yanga ilikuwa ikishiriki klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika). Lakini hata Pan ilikuwa ikicheza Kombe la Washindi Afrika (iliungwanisha na michuano ya Kombe las CAF kuwa Kombe la Shirikisho la sasa).
“Mbona sisi tumecheza mechi nyingi pamoja na kwamba tulikuwa tukishiki Kombe la Washindi? Alihoji.
Yanga ilitolewa raundi ya pili na Al Ahly kwa kichapo cha jumla ya mabao 6-1. Awali ilitoka sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam na kwenda kushindiliwa mabao 5-0 Cairo, Misri.
Kabla ya hapo, Yanga iliitoa Textil do Pungue kwa jumla ya mabao 4-1. Ilishinda ugenini 2-1 na nyumbani 2-0.
Pan ilitolewa raundi ya kwanza kwa penalti baada ya kushinda nyumbani 1-0 dhidi ya Power Dynamos na kufungwa 1-0 Ndola, Zambia.
FAT YAMJIBU
Katibu Mtendaji wa FAT, Patris Songora aliiambia Pan kama itagomea na kutekeleza tishio lake basi, timu hiyo itahesabika imepoteza mchezo na timu pinzani kupewa ushindi. Na kama haitoshi chama hicho kitachukua hatua dhidi ya timu hiyo.
Hata hivyo, Songoro alisema kwa kuwa tatizo hilo lilikuwa limelalamikiwa na timu nyingi, basi chama chake kingekaa na kuangalia namna ya kufanya marekebisho.
EL- MAAMRY AWA MKALI
Mara baada ya majibu ya Katibu Mtendaji huyo, Mwenyekiti wa FAT, Said El Maamry aliibuka na kuishtumu Pan kwa kutoa vitisho.
Kwanza alisema chama chake hakipo kwa ajili ya kuipendelea timu yoyote. Lakini alisema barua ya Pan kwa FAT ni kama vitisho na chama hicho hakiwezi kubabadilisha ratiba kutokana na vitisho vya klabu moja.
“FAT haiwezi kutishwa, bali itazingatia kufanya mabadiliko ikiona kama kuna uwezekano wa kufanya hivyo,” alisema El Maamry.
Wiki ijayo usikose, mchezaji aliyefariki uwanjani na kuzua utata. Unamjua ni nani? Usikose wiki ijayo!