MJUAJI: Mgogoro Yanga - Tambwe ataka mastaa wanne

WIKI iliyopita katika mfululizo wa simulizi ya mgogoro mkubwa uliowahi kuikumba Yanga miaka ya 1970 na kuona namna walivyoilalamikia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) juu ya kuwachunia barua yao kwenda Romania.
Leo tunaendelea na sehemu ya tatu ya simulizi hili tukirejea kwenye pambano la Klabu Bingwa Afrika kati ya vijana wa Jangwani na Enugu Rangers. Endelea nayo...!
Baada ya mchezo wa Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa) mwaka 1975 kati ya Yanga na Enugu Rangers ya Nigeria ndipo lilipoibuka sakata jipya la Kocha Tambwe Leya na mchezaji wake, Sunday Manara.
Awali, Mwenyekiti wa Yanga, Mangara Tabu Mangara alitishia kugomea mchezo huo kutokana na timu yake kutopewa huduma za Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kama ilivyokuwa zamani kwa timu zinazowakilisha nchi kuhudumiwa na baraza hilo.
Mwenyekiti Mangara alijitokeza mbele ya wanahabari na kusema, Yanga itacheza mchezo huo. Hata hivyo, kiongozi huyo alisema hakuwa akitishia aliposema haitacheza mchezo huo kama haitaachiwa kuusimamia na fedha za mchezo kuingia kwenye akaunti ya klabu.
Alisema iko siku jambo hilo litatimia kwa Yanga kugomea kuingiza timu uwanjani kama mambo hayatabadilika. Yanga ililazimika kuwaweka wachezaji wake kama dhamana katika Hoteli ya Bahari Beach ili waweke kambi hotelini hapo na kuendelea na mazoezi.
Hata hivyo, mgogoro huo kati ya Hoteli ya Bahari Beach ambayo ilikuwa ikiidai pesa BMT na kuzuia wachezaji wa Yanga kuweka kambi ulimalizwa baada ya wasimamizi wa hoteli hiyo, (Tanzania Hotels) kupewa barua na Hazina na kuhakikishwa madeni yote ya BMT yatalipwa.
YANGA YATOLEWA
Enugu Rangers iliyokuwa inakuja Tanzania kucheza na Yanga katika mchezo wa marudiano baada ya sare tasa nyumbani kwao ilianza kujiimarisha.
Enugu iliwaita wachezaji wake wawili - beki na mshambuliaji ambao walikuwa Marekani kwa ajili ya masomo ili kuongeza nguvu katika mchezo wa Dar es Salaam. Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 na kutolewa kwa bao la ugenini.
BIFU LA TAMBWE, MANARA UPYAA
Siku 19 tangu Yanga itolewe na Enugu katika michuano hiyo ya Afrika, Kocha Tambwe aliibuka na kutema nyongo.
Kocha huyo raia wa DR Congo (zamani Zaire) alitishia kujiuzulu iwapo wachezaji wanne maarufu hawatafukuzwa kabisa katika klabu hiyo. Tambwe alidai wachezaji hao (ambao hakuwataja majina) walifanya vitendo vya aibu kambini (hotelini Bahari Beach).
CHANZO CHA KUTOLEWA
Kocha huyo aliongeza wachezaji hao ndio chanzo cha timu yake kutolewa na Enugu katika mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam akidai walichelewa kuingia kambini baada ya kurudi kutoka Lagos, Nigeria.
Tambwe aliwataja wachezaji tisa tu ambao ndio waliowahi kambini baada ya kurudi katika mchezo wa awali dhidi ya Enugu.
Wachezaji hao ambao hawakupangwa katika mchezo wa marudiano ni Juma Pondamali ‘Mensah’, Bona Max, Juma Matokeo na Juma Shaaban.
Wengine ni Nondo, Mohammed Rishard ‘Adolf’, Mohammed Mkweche na Ahmed Omary.
Kocha huyo alisema wachezaji wengine ambao ndio tegemeo la timu walichelewa kuripoti kambini kwa siku tano.
Kocha Tambwe alisisitiza anataka wachezaji hao wafukuzwe kwa sababu walijiingiza katika vitendo vya anasa wakiwa kambini bila ya kujali maslahi ya mchezo dhidi ya Enugu Rangers.
Tambwe alimsifu sana mchezaji Kitwana Manara kwa kuonyesha jitihada kubwa uwanjani na kama angepata msaada wa wenzake, Yanga ingeibuka na ushindi katika mchezo huo na kuitoa Enugu.
Aliwaambia viongozi wa Yanga wawatimue wachezaji hao kwa kuwa timu hiyo sio ya wachezaji wawili au watatu kwani ina wachezaji wengi wazuri sio hao wanaojiona wao ndio wao. Pamoja na Kocha Tambwe kutowataja wachezaji hao, tetesi ziliwataja kuwa ni Sunday Manara, Gibson Sembuli, Omary Kapera na Idd Boi ‘Wickens’.
Kwa taarifa yako ndugu msomaji wachezaji hao ndio waliokuwa nyota na katika timu kiasi kwamba ni vigumu kuweza mtu yeyote kukubali kuwafukuza klabuni.
UONGOZI WAPIGWA SHOTI
Mwenyekiti wa Yanga, Mangara alisema uongozi wa klabu hiyo umeshtushwa na taarifa ya Kocha Tambwe ya kuwataka kuwafukuza wachezaji hao wanne.
Kiongozi huyo alisema viongozi wa Yanga watakutana na kulizungumza jambo hilo kabla ya kuchukua hatua ambazo kocha wao anawataka wazichukue. Aliwatuliza wanachama wa Yanga kutulia wakati uongozi unalitafakari jambo hilo zito.
Hata hivyo, siku ambayo uongozi ulipanga kulizungumza jambo hilo ilishindikana na kulisogeza mbele zaidi.
Unajua Nini kilitokea? Usikose Jumapili ijayo.