MJUAJI: Dilunga aifunga Simba, atoka uwanjani

MECHI za Simba na Yanga zimekuwa na vituko na matukio mengi ya kushangaza.
Kuna matukio ya ajabu yamewahi kutokea katika mechi nyingi za timu hizo, lakini tukio la mwaka 1970 lilikuwa la ajabu na liliwashangaza wengi.
Ilikuwa mechi ya kuwania kombe kati ya miamba hiyo miwili. Ilikuwa mechi ya kwanza kwa timu hizo kukutana Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) baada ya mchezo wa mwisho uliopigwa Uwanja wa Karume na Simba kukubali kichapo cha mabao 5-0.


MABADILIKO MAKUBWA
Simba baada ya kufungwa na Yanga mabao 5-0, mechi iliyopigwa Juni Mosi, mwaka 1968 wakati huo ikiitwa Sunderland, ilifanya mabadiliko makubwa ya wachezaji.
Timu ilikuwa na wachezaji wengi vijana baada ya kuachana na wachezaji walioonekana kuwa wazee. Wachezaji kama kina Haidary Abeid, Abdallah Kibaden, Willy Mwaijibe, Saad Ali na wengine ndio waliochukua nafasi za wakongwe
Katika mechi hiyo Simba ilianza na kipa Hassan Mlapakolo baada ya kuanza kumuweka pembeni kipa namba moja, Mbaraka Hassan Mahundumla.
Baadhi ya viongozi walikosa imani na Mbaraka baada ya kufungwa 5-0 na Yanga.
Mbali na kichapo hicho viongozi na mashabiki wa Sunderland walikosa imani na Mbaraka baada ya kuruhusu mabao matano katika mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya African Sports ya Tanga.
Dhidi ya Wana Kimanumanu jijini Dar es Salaam Simba ilifungwa mabao 5-2.
Mlapakolo akaanza kuaminiwa Simba.


MASHABIKI WALINUNUA MPIRA
Siku hizi katika mechi za Kariakoo Derby makomandoo wa klabu hizo huwa na makini sana na kulinda uwanja wakihofia kufanyiana ndumba
Katika mechi hii mpira wa kuchezea katika mechi hiyo ulienda kununuliwa chini ya ulinzi wa mashabiki wa pande zote mbili yaani wale wa Simba na Yanga.
Kama haitoshi mashabiki hao walibaki na mpira ukiwa katika uangalizi wao na pande zote mbili ziliuchukua mpira huo na kuingia nao hadi uwanjani na kuuweka katikati ya uwanja. Hii yote ilikuwa ni kuulinda mpira huo na kuogopa kuhujumiana kwa imani za kishirikina.


BAO LA AJABU LA DILUNGA
Yanga ikiwa na kikosi cha kina Elius Michael 'Nyoka Mweusi', Baraka Kitenge, Boi Iddy 'Wickens', Hassan Gobbos na Omary Kapera.
Wengine ni Badi Saleh, Léonard Chitete, Abdulrahman Juma, Kitwana Manara, Maulid Dilunga na Juma Bomba.
Dakika 15 tangu mchezo kuanza, Chitete alimpindua beki wa Simba na kumpa pasi Dilunga aliyeukwamisha mpira kimiani.


AONDOKA UWANJANI NA VESPA
Mara baada ya kufunga bao hilo, Dilunga hakurudi uwanjani. Alipanda pikipiki aina ya vepsa na kuondoka uwanjani hapo.
Inadaiwa Dilunga alipotoka uwanjani hapo alienda baa huku nyuma nafasi yake ikichukuliwa na beki wa kwanza wa kati wa Yanga,  Athumani Kilambo.


USHIRIKINA WATAJWA
Kitendo hicho cha Dilunga kilihusishwa na imani za kishirikina.  Inadaiwa bao lake lilikuwa la kusawazisha lakini lilicheleweshwa na kuwa la ushindi.


MAMBO YALIKUWA HIVI
Kwanza mchezo ulicheleweshwa kuanza kutokana Yanga, kuzua mambo tofauti. Inadaiwa kucheleweshwa kwa mchezo huo uliochezeshwa na Kocha wa timu ya Taifa, Shaaban Marijani  ' Maji Mengi' au Maji Moto' ilikuwa ni janja ya Yanga kufuta mabao ya ushindi ya Simba.
Hatimaye mchezo uliisha kwa ushindi wa bao 1-0 kwa Yanga na kapteni wa timu hiyo, AbdulrahmanJuma kupanda jukwaani kukabidhiwa kombe huku kapteni wa Simba, Yussufu  Salumu akiondoka akiwa mnyonge.