Boban afunguka ya moyoni kuhusu Simba, awauma sikio wazawa, Chama…
Muktasari:
- Alikuwa kiungo fundi hasa na moja ya kumbukumbu zake zilizoko vichwani mwa wengi ni rafu. Ukimchezea rafu ujue atakutafuta arudishe. Wengi walimjua kwa hilo ingawa mwenyewe anasema walimtafsiri vibaya na hawajui ni mtu wa aina gani uwanjani na nje ya uwanja.
KAMA kuna wachezaji waliokuwa wanaangaliwa sana uwanjani kama watatoka bila ya kadi, mmoja wao ni Haruna Moshi ‘Boban’, kiungo wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars ambaye pia aliwahi kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kwenye klabu ya Gefle IF ya Sweden.
Alikuwa kiungo fundi hasa na moja ya kumbukumbu zake zilizoko vichwani mwa wengi ni rafu. Ukimchezea rafu ujue atakutafuta arudishe. Wengi walimjua kwa hilo ingawa mwenyewe anasema walimtafsiri vibaya na hawajui ni mtu wa aina gani uwanjani na nje ya uwanja.
Mwanaspoti lilimtafuta na kumfanyia mahojiano na anasema tofauti na wanaomfikiria ila ana huruma na ukarimu na asiyependa visasi.
Amefunguka pia mambo kuhusu timu yake ya zamani ya Simba ikiwamo maisha ya ndani na nje ya uwanja na anachokifanya kwa sasa.
Kuhusu kurudishia rafu alizochezewa anasema ni mambo ya ujana tu na ya uwanjani na kuna wakati ilimbidi afanye hivyo lakini sio kama ndio maisha yake na huwa hapendi vinyongo kwa watu na ni mtulivu hasa nje ya uwanja.
Anasema kwa kusisitiza: “Kwanza ule ulikuwa ni ujana tu.”
Anasita kidogo na kuongeza; “Siwezi kuwashauri vijana wa sasa kufanya hivyo. Nimeona sana mitandaoni wakisema Boban akicheza rafu wanasubiri kuona nitarudisha. Ule ni ujana.”
Pia anasema alikuwa akitoka uwanjani, anamfuata mchezaji aliyemchezea rafu na kumwambia wafanye kazi waachane na mambo yasiyo na msingi, ambayo yanawanyima watazamaji burudani.
“Mambo ya uwanjani, yalikuwa yanaishia uwanjani, sikuwahi kumuwekea mtu yoyote kinyongo.”
ALIZINGUANA NA VIONGOZI
Ingawa hataki kuweka wazi ni viongozi gani na timu gani lakini anafichua tabia yake kubwa ni kupenda haki na masilahi ya wengine jambo ambalo wengi hawajui na hilo lilimfanya hadi kuonekana mbaya kwa viongozi hao.
“Sipendi kuona jasho la mtu linapotea bure, kama mchezaji amefanya kazi kwa nini wasilipwe kwa wakati, nilikuwa nikiona hivyo kwa baadhi ya timu nilikuwa nalisemea kwa nguvu,” anasema na kuongeza;
“Kuna wakati wachezaji walikuwa wananishangaa, nilikuwa naweka nyuma masilahi yangu, natanguliza ya kwao na usingeniuliza nisingesema, kwa sababu dini yangu ya Kiislamu inasema ninapotoa kitu, mkono mwingine usishuhudie, hata huko mtaani nikitoa msaada wao ndio wanaosema siyo mimi.”
Anashauri viongozi kuhakikisha wanatumia vizuri nafasi zao kiunua masilahi ya wachezaji ili hata baada ya kutundika daruga wajivunie uwepo wao na sio kuandaa kizazi cha watu wenye malalamiko.
MAFISANGO HAMTOKI MOYONI
Analisimulia tukio la maumivu, lisilomtoka moyoni mwake ni kifo cha rafiki yake aliyekuwa kiungo wa Simba, Patrick Mutesa Mafisango.
“Kabla ya ajali iliyosababisha kifo chake, tulizungumza mambo mengi, ikiwemo na jinsi ambavyo alikuwa anavutana na viongozi wa Simba kuhusu kumwongezea mkataba mpya,” anasema na kuongeza;
“Aliniambia Boban naondoka nchini, naweza nisirudi kama hatutaelewana na viongozi wa Simba, kwani alikuwa amezungumza na timu ya Rayon Sports ya Rwanda, ambayo ilikuwa inamsubiri maamuzi yake ya kusaini, tulipiga stori nyingi za kimaisha, huku na kule nikasikia kifo chake.
“Ni kitu ambacho kiliniumiza sana, niliamini baada ya kumwona, nilijikuta nguvu zinaniisha, lakini nilijizuia kukufuru, mimi ni Muislamu najua ni safari ya kila mmoja, ingawa kusema ukweli siwasiliani na familia yake.”
Mafisango alifariki Mei 17, 2012 kwa ajali ya gari, iliyotokea katika eneo la Keko, Dar es Salaam, ikiwa ni siku chache kutoka kumalizika Ligi Kuu Bara msimu wa 2011/12, ambao Simba ilitwaa ubingwa.
HII DABI HATOISAHAU
Boban ni mmoja wa nyota waliocheza michezo mingi ya Dabi ya Kariakoo na kama kuna mchezo ambao hatakaa ausahau ni ya mwaka 2004 kwenye Uwanja wa Uhuru.
Anasema siku hiyo kulinyesha mvua na uwanja ulikuwa na matope ingawa mechi ilipigwa hivyo hivyo na Simba ilishinda mabao 2-1 dhidi ya watani zao Yanga kwa mabao ya Shaban Kisiga na Ulimboka Mwakingwe kwa upande wa Wekundu hao na la Wanajangwani lilifungwa na Pitchou Kongo.
WAZAWA SHTUKENI
Wachezaji wazawa pia wamepewa neno na Boban na anawaambia wana la kufanya kuwafikia mastaa wa kigeni na ni rahisi kama watajitambua.
Kaanza kwa Pacome Zouzoua, Stephane Aziz KI na Clotaus Chama, kwa kuwataja kwa uchache na kugundua hata hapa Bongo wapo na wanastahili kile wanachofanya na kupata mapro hao na wengine kutoka nje ya Tanzania.
Boban pia anasema wazawa wana la kujifunza kutoka kwa mastaa hao wa kigeni na sio kila mara wakija wanawafunika nyumbani kwani wakijitambua ni moja ya sababu ya kufanya vizuri na kuisaidia timu ya taifa.
Anasema viwango wanavyoonysha mastaa hao ni changamoto ya ushindani kwa wazawa na hivyo inabidi wapambane kweli ili kuwafikia na hata kuwa zaidi yao.
“Ni wachezaji wenye uwezo mkubwa, natarajia maskauti wa klabu mbalimbali za Ligi Kuu, watakuwa wanafanya kazi ya kuangalia viwango vikubwa vya wachezaji wa kuwasajili.”
“Pacome na Azi Ki ni baadhi tu, wapo wengi wageni ambao wanafanya kazi kubwa na nzuri. Miaka ya sasa soka linaonyeshwa wazi, hivyo kila mtu anaona wanachokifanya.
“Pamoja na kwamba wageni wanalipwa pesa ndefu, niwashauri viongozi masilahi yao yasipishane pakubwa na wazawa ambao wanafanya kazi nzuri, kwani hao ndio wanategemewa kwenye kikosi cha timu ya taifa.”
FEI TOTO BALAA
Boban amemchambua kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ alivyo tunu katika soka la Tanzania na anachokipenda kutoka kwake ni uharaka wa uamuzi katika nafasi finyu zinazokuwa zinatokea kwa timu anazokuwa anazifanyia haki.
“Kuna maamuzi baadhi anayoyafanya Fei Toto uwanjani ni kama niliyokuwa nayafanya, mfano akipata nafasi hajiulizi mara mbili anapiga, jambo ambalo linawashitukiza makipa kukutana na mpira nyavuni,” anasema.
“Kitu ninachoweza kumshauri ili Fei awe bora zaidi apunguze kucheza tachi, kwa kuwa anacheza kiungo mshambuliaji anapopiga tachi moja ya pili aachie, asiendelee zaidi ya hapo, naamini akifanya hivyo atakuwa anafunga sana.
“Kuhusu Fei Toto kuchukua kiatu cha dhahabu ni ngumu kutabiri, mechi zipo nyingi, mtu anaweza akafunga mabao manne kwenye mechi moja, hivyo hata ambaye kwa sasa hatazamwi kama yupo kwenye mbio za kuwania kiatu anaweza akawashangaza, kwa hilo tusubiri msimu uishe.”
CHAMA, KIBU WASIONDOKE SIMBA
Chama na Kibu Denis ni kati ya wachezaji wanaotajwa huenda msimu ujao, wanaweza wakaondoka ndani ya klabu hiyo, kwa mtazamo wa Boban anaona bado Simba inawahitaji mastaa hao kwa aina ya kazi kubwa walioifanya.
“Soka la kisasa, linahitaji aina ya uchezaji wa Kibu, huenda wanaweza wakawa wanamhukumu hajafunga mabao mengi, ila kafanya kazi kubwa kuliko kufunga, anakaba, anashambulia, ana kasi na kutumia nguvu,” anasema na kuongeza;
“Ninachokiona Simba inapaswa kusajili mastraika wengine, kiungo na beki wa kati ambao watawaongezea nguvu kina Kibu na Chama, pia itamsaidia Kibu kumpunguzia majukumu analazimika kufanya majukumu ya wengine ambao wanajisahau.”
Boban akimtazama anavyocheza kiungo wa Simba, Chama anapenda utulivu wake, maamuzi, akili ya kipi akifanye kwa wakati gani.
“Napenda wachezaji watulivu ambao hawana papara na mpira, Chama amekamilika kuitwa mchezaji bora na mwenye thamani, hakuna asiyejua kazi yake katika nchi hii, tangu alipoanza kucheza Ligi Kuu Bara,” anasema Boban ambaye shangilia yake alikuwa akipandisha soksi na kupeleka mpira kati.
SIMBA, YANGA, AZAM ZIPEWE UPINZANI
Kwa ushindani na vipaji vikubwa anavyoviona Ligi Kuu Bara, anaona kuna haja ya klabu nyingine ziwe na nguvu kiuchumi, ili ushindani uzidi kuwa bora na timu yoyote iweze kunyakua ubingwa.
“Mfano Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Coastal Union na timu nyinginezo, zikiwa na nguvu kiuchumi ama wadhamini wa kutosha, basi hawatakuwepo wachezaji wanaotamani Simba, Yanga na Azam FC kwani watakuwa wanapata kila kitu,” anasema na kuongeza;
“Zamani timu zilikuwa na nguvu, ndio maana timu kama Tukuyu Stars, Mtibwa haikuwa ishu kunyakua taji la ubingwa, zilikuwa na ushindani ambao ulifanya wachezaji wawe bora zaidi.”
MRITHI WA BOCCO APIKWE
Anavyoona mrithi wa straika John Bocco wa Simba ambaye ana mabao 154 wapo wengi ingawa ni klabu yenyewe kujua inataka mchezaji wa aina gani. Pia anaona ni vyema klabu zikawajenga wachezaji kwani wakitengenezwa ndio wanakuwa wazuri hata kama wana vipaji.
“Kuna washambuliaji wengi wenye vipaji, shida inakuja wanaangalia wale wenye majina na hawawezi kukuza vipaji vingi.
“Kuna wachezaji wapo mkoani huko ni wazuri, halafu mchezaji hata kama ana kipaji kiasi gani, atatakiwa kumjenga ili awe mzuri zaidi, ila sijaliona hilo kwa asilimia kubwa.”
MASTAA WANAANGUSHWA NA HILI
Anasema kutokana na sayansi na teknolojia anaona vijana wengi wanaathiriwa na mitandao ya kijamii, hasa kipindi wanapopata majina wakiwamo mastaa wa soka, kitu ambacho mwishowe huwatoa mchezoni.
“Kuna wachezaji wana vipaji vikubwa, niwashauri waishi maisha halisi, waachane na maigizo ya mtandaoni, hayawezi kuwasaidia kitu, wanatumia muda mwingi kuona watu wanawazungumziaje, nafikiri kitu kizuri kazi zao ndizo zizungumziwe zaidi,” anasema na kuongeza;
“Wanatakiwa wapate muda mzuri wa kulala, wale vyakula vya asili, wafanye mazoezi ya kutosha, wanywe maji, wakifanya hayo, watakuwa na nguvu ya kucheza kwa kiwango kwa muda mrefu.
“Lakini akili zao zikiwaza baada ya mechi wanataka kujua watu wanaongea nini juu yao, waposti kitu gani, hayo yanaweza yakawatoa mchezoni, ndio maana mtu akiniuliza ulicheza kwa kiwango muda mrefu, hata nikiwa kambini nilipenda kulala kwa wakati, kula kwa wakati tena vyakula sahihi, sikuwa na mambo mengi,” anasema Boban ambaye anasema huwa akitulia anapenda kusikiliza muziki aina ya Reggae kwani unazungumzia uhalisia wa maisha ya kweli na siyo maigizo.
“Napenda muziki wa Ragge kwa sababu ni halisi, aina ya maisha yangu ni halisi, sipendi makandokando, ndio maana mtu akitaka kuwa rafiki yangu asitoke kwenye misingi yangu nje na hapo hatuwezani.”
Anaongeza yupo kwenye mitandao yote ya kijamii, ila ni ngumu kuona anaposti picha zake ama vitu anavyovifanya, anaishia kuangalia vitu vinavyoendelea duniani na kunyamaza.
“Naona kila kinachoendelea, ila huwezi kuniona kama nipo kwenye mitandao hiyo, kwani haijawahi kunilevya, isipokuwa naangalia vitu vilivyopo duniani,” anasema na kufichua pamoja na kuwa staa hakuwa na mambo ya ajabu ikiwamo skendo za wanawake na hakuwa akipenda.
“Hayo hayakuwa mambo yangu kabisa, kwanza sikuwahi kukaribisha hizo ishu, ndio maana hamkuwahi kunisikia kwenye skendo za wanawake.”
MAMA AMPA MZUKA WA SOKA
Anasema yeye ni kitinda mimba kwenye familia yao, mama yake alikuwa hapendi acheze soka na yeye alikuwa hataki kusoma, hivyo alijikuta anachapwa fimbo za kila wakati, hata hivyo yote hayo yalimjenga na mama anajivunia kutokana na soka lake.
“Nimezaliwa na mama muuza vitumbua, muda wa kwenda kusaga unga wa vitumbua, mimi nilikuwa nakwenda kucheza, nikirejea nyumbani fimbo zilikuwa zinanihusu, lakini ilifikia muda mama alipokuwa akisikia nina kipaji kikubwa aliamua kuniacha,” anasema na kuongeza;
“Baada ya kuanza kupata umarufu hadi alikuwa ananiangalia kwenye tv, aliniambia mwanangu songa mbele, jitume, ongeza nidhamu, lakini yote katika yote namshukuru baba yangu alitusaidia sana tuzifikie ndoto zetu za soka.
Anasema kwa sasa mama yake anaishi kama malkia, jasho lake la soka, lilibadilisha maisha yake.
“Soka limenipa mambo mengi, ila kubwa zaidi ni kufahamiana na watu mbalimbali, ambao ni muhimu maisha mwangu,” anasema Boban ambaye anafunguka jina hilo ‘Boban’ alipachikwa na mashabiki, lakini alilifurahia kwani, lilitokana na kiungo wa Milan, Zvonimir Boban aliyekuwa anampenda jinsi anavyocheza na alikuwa anamfuatilia.
“Sikulichukia jina hilo, mtu ambaye walinifananisha naye ni aikoni kwangu, halafu ukitaka kujibizana na mashabiki ndio watazidisha kukutania, ndio maana hukuwahi kuona najibu jambo lolote, sikuona sababu ya kufanya hivyo,” anasema.
NI SHABIKI WA FRIENDS RANGERS
Anasema timu ambayo ipo kwenye moyo wake ni Friends Rangers na imehusika pakubwa kutengeneza wachezaji mastaa akiwamo yeye.
“Hii timu ina historia kubwa kwa mastaa wengi Tanzania, ingekuwa nchi nyingine Heri Mzozo angepewa heshima ya kusaka vipaji.
“Mzozo ameibua vijana wengi na bado anaendelea kuibua, shida inakuja je, wanathamini mchango wake, ndio maana anajiweka pembeni, lakini tunaojua thamani yake, hatuwezi kuacha kumheshimu kwenye maisha yatu.”
AWAVULIA KOFIA MASTAA HAWA
Anasema hana kikosi cha kwanza kila mchezaji anayecheza vizuri kwake ndio wanaostahili, ila miongoni mwa aliokuwa anapenda kuwaona wakicheza ni Shaban Kisiga, Said Sued, Juma Nyoso, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ na Mwinyi Kazimoto.
“Hao ni baadhi kuna wachezaji wengi wazuri, ndio maana nasema siwezi kutaja kikosi cha kwanza, maana nitakuwa sitendi haki, hata hao niliowataja ni baadhi tu,” anasema.
KITAA ANAFANYA NINI
Boban ameshastaafu soka baada ya kutesa kwa miaka mingi akizichezea timu mbalimbali za Tanzania na nje ya nchi. Kwa sasa anajihusisha na kukuza vipaji vya vijana wa mtaani kwake na aliwahi kuhudhuria kozi ya ukocha ya FIFA ya Grassroots iliyofanyika Makao Makuu ya TFF, Karume, Ilala na akiwa nyumbani anapenda kujumuika na wenzake kwenye mamboi mbalimbali au kulala.
“Nikiwa nyumbani napenda kutulia ndugu, jamaa na marafiki ambao ndio wanaojua mimi ni mtu wa aina gani, ndio maana wananielewa, tofauti na wengine wanavyonichukulia,” anasema Boban ambaye alikuwa anapenda aina ya uchezaji wa Patrick Vieira, mchezaji wa zamani wa Arsenal,Juventus,Inter Milan, AC Milan na Manchester City, uwezo wake na moyo wa kujitolewa kwa timu.