UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kibu Denis ni mbadala wa Lomalisa?

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Kibu ni aina ya wachezaji ambao kumwelekezea mtu, inahitaji muda wa kutosha.

Huenda Kibu Dennis ndiye mchezaji Bora msimu huu mzawa wa Simba na ambaye akikosekana, watu wanashika kichwa.

Kibu ni aina ya wachezaji ambao kumwelekezea mtu, inahitaji muda wa kutosha.

Mchezaji yoyote asiyekupa namba, inahitaji ujuzi kweli wa mambo kumwelezea.

Kibu ana karibu kila kitu kinachohitajika kwa mchezaji, lakini hakupi namba. Hakuna mabao wala pasi za mwisho kwa Kibu na uhakika wa pasi.

Ni mchezaji bize zaidi uwanjani. Anakimbia dakika zote. Ana nguvu na mzuri sana kwenye kukaba lakini yeye ni kiungo mshambuliaji au winga.

Nimezisikia tetesi za Yanga kumuwinda. Huu ni wakati wa usajili, ndiyo muda wa kusikia kila kitu.

Ni kweli anaweza ndiye mchezaji bora mzawa wa Simba msimu huu lakini siioni moja kwa moja nafasi yake Yanga.

Huyu ni mchezaji mwenye nguvu na kasi ambaye kazi yake kubwa inaonekana akiwa bila mpira, sidhani kama Yanga wanahitaji mchezaji wa aina yake.

Kisiasa ni usajili mzuri kwa sababu unakwenda kumbomoa mtani lakini kiufundi sidhani kama ni chaguo sahihi.

Kisiasa itawalipa sana Yanga kwa sababu kumchukua mchezaji bora mzawa kwa mtani kwao itawapa furaha sana.

Nasubiri kuona namna Kocha Gamondi atakavyonionyesha kitu tofauti na ninachokiona kila siku kwa Kibu kama watamsajili.

Misimu miwili na nusu ya hivi karibuni, Yanga walikuwa na winga wa Kikongomani, Jesus Moloko. Hakuwa na namba nzuri sana za kushambulia.

Alikuwa na kasi na uwezo mkubwa wa kurudi kukaba lakini Yanga wamemwacha!

Pale Yanga kuna Farid Mussa mwenye uwezo wa kukaba, kasi ipo na uwezo wa kufunga pia upo lakini hatumiki.

Farid angeweza kuwa winga bora pale Yanga. Kibu sio mchezaji mbaya lakini siioni nafasi yake ya moja kwa moja.

Kwa namna Yanga ilivyo msimu huu, nadhani inahitaji winga ambaye atawapa namba pia. Mshambuliaji wa pembeni ambaye pamoja na mambo mengine ni lazima awe na uwezo wa kufunga na kutengeneza mabao.

Kibu anaweza kufanya kila kitu uwanjani lakini hana uwezo mkubwa wa kufunga wala kutengeneza nafasi.

Mipira yake mingi pasi za mwisho zimekuwa mbovu. Kama wanamsajili, basi kocha atakuwa anajua namna ya kubadilisha.

Kama kocha ndiye kamtaka basi tuheshimu taaluma ya ukocha lakini kwa kumtazama Kibu na namna Yanga inavyocheza, siioni nafasi yake ya moja kwa moja.

Kibu anang’aa pale Simba ni kwa sababu tu wachezaji wengi wazawa wamechoka! Angewakuta Hassan Dilunga, Shizza Kichuya na John Bocco pale juu, asingetajwa kabisa.

Pamoja na yote lakini haiondoi ukweli ni miongoni mwa wachezaji tegemeo simba msimu huu.

Eneo analocheza Kibu, ndipo Farid anakowekwa benchi. Kisiasa ni usajili mzuri kama watampata lakini kiufundi, namsubiri Gamondi anishangaze kwa Kibu!

Kuna tetesi Joyce Lomalisa anakwenda kutemwa mwishoni mwa msimu, lakini kama Kibu anakuja kuleta msaada kama winga mwenye uwezo pia wa kuzuia.

Mchezaji kama Kibu angekuwa na maamuzi sahihi eneo la mwisho la ushambuliaji, ingekuwa balaa.

Kwa nguvu na kasi yake kama angekuwa mzuri sana wa kumalizia mashambulizi pengine ndiye angekuwa kinara wa mabao kwenye ligi yetu.

Angeweza hata kutumika kama mshambuliaji wa kati lakini ngoja tumwachie Gamondi na kama kweli Yanga wamemtaka.

Dennis Nkane na Farid wamekosa nafasi pale Yanga, Kibu atakuwa na kazi kubwa zaidi.

Kama Yanga wanataka kuja kushindana hasa kaına Mamelodi Sundowns, Al Ahly na TP Mazembe kuna kazi kubwa mbele yao ya kufanya.

Huwezi kumfunga Ahly nje ndani kwa usajili wa Kibu.

 Inaonekana tuna tatizo kubwa sana la wachezaji wazawa. Klabu nyingi hazizalishi wachezaji bora wazawa.

Mtibwa Sugar wamekuwa wakilisha sana timu kubwa wachezaji wazawa na Azam FC.

Pia moja ya sababu zinazoitesa Simba kwa msimu wa tatu sasa ni kukosa wachezaji wengi wazawa wenye ubora.

Wachezaji wengi wazawa waliopo ni ama wametumika sana au wamechoka!

Enzi za kina Mzamiru Yassin kwenye ubora wake, Hassan Dilunga, John Bocco, Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Zimbwe Jr, hakuna mtu angemuwaza Kibu.

Lakini mpira ni mchezo wa zama. Huu ni muda wa Kibu ingawa kuna vitu vingi bado vinakosekana kwenye miguu yake.

Simba bado wanajitafuta ndiyo maana ni rahisi sana kwa mchezaji kama Kibu kung’aa.

Yanga wameshajipata, inahitaji mtu bora sana kupenya kikosi cha kwanza. Kibu anaweza kwenda kama kuna kitu tofauti anachoona kocha kutoka kwenye miguu yake.

Ni mchezaji mzuri lakini siioni nafasi yake Yanga, ni bora angebaki Simba mahali ambapo hana Presha na timu bado inajengwa.

Yanga hawatokuwa na muda wa kumsubiria gari lichanganye, watu watataka matokeo ya haraka kitu ambacho kitakuwa kigumu kwake.

ŞKibu ana uwezo wa kuzuia na kukaba. Kimsingi hizi sio sifa za mchezaji anayecheza nafasi ya ushambuliaji! Kwa Dunia ya leo ni kazi sana kuheshimika kama hauna namba.

Mchezaji wa ushambuliaji, watu wataangalia mabao au pasi za mwisho.

Hata ukabe kwa kiasi gani, hata uwe na mbio kiasi gani, hakikisha unafunga.

Mambo ya kuhesabu mikimbio yapo kwenye riadha tu. Tuisila Kisinda alichemsha pale Yanga kwa sababu ya kukosa namba.

Kila kitu kilikuwa sawa lakini maamuzi yake ya mwisho mara nyingi sana hayakuwa na msaada kwa timu.

Yanga wanahitaji mchezaji atakayewapa namba zaidi. Kibu Yanga, sidhani kama utakuwa ni uamuzi mzuri kwa timu labda kama kuna kitu cha kitofauti amegundua Gamondi.

Walau Simba anacheza moja kwa moja kila mechi, pale Yanga hali itakuwa tofauti. Yanga wana utajiri wa wachezaji kwa sasa karibu kwenye kila nafasi.

Kupata nafasi ni mapambano haswa na bahati mbaya, Gamondi ameshapata timu yake ya ushindi.

Sio kocha anayependa kila mchezaji acheze. Yeye analinda kibarua chake. Ana wachezaji wachache sana wa ushindi ambao huwa hawabadiliki mara kwa mara.

Ni wale wale kila mechi na wanampa matokeo. Kibu akienda Yanga, anakwenda kwenye vita kubwa ya kugombea nafasi kuliko alikotoka.

Sina shida na Kibu lakini ni lazima aongeze namba. Sina tatizo naye kabisa lakini ni lazima aanze kufunga.

Ni lazima aongeze umakini kwenye pasi zake za mwisho. Kibu ni mchezaji mzuri lakini kwa Yanga, naona utakuwa ni usajili wa kisiasa zaidi kuliko ufundi.

Nipe mrejesho wako unaonaje makala za safu hii.