MJUAJI: Al Merrikh ni mechi ya Sure Boy

MWAKA 1981 Kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Rud Gultendof alikuwa akizunguka na winga wa timu hiyo, Said George katika Fukwe ya Bahari ya Hindi.

Ilikuwa kando kidogo ya Hoteli ya Bahari Beach ambapo Taifa Stars ilikuwa imeweka kambo yake kwa ajili ya michuano ya Kombe la Challenge.

Gultendof ambaye kwa sasa ni marehemu, alikuwa akimjenga kisaikolojia Said George ili aweze kufanya vizuri katika mchezo ambao alikuwa akitarajia kumpanga.

Kocha huyo raia wa Ujerumani alikuwa akimwambia Said George aliyekuwa akiitumikia Coastal Union kwamba wakati alipokuwa na umri kama wake alikuwa akitegeemwa na timu ya taifa lake.

Kocha huyo alikuwa anakiona kitu katika miguu ya Said George, hivyo alikuwa akimjenga kisaikolojia ili mchezaji huyo aweze kukionesha kitu hicho kwenye mchezo ambao alikuwa akitarajia kumpa nafasi. Nimeanza na kisa hicho katika hali ya kuchombeza tu, ili kuwaonesha makocha wetu kwamba wanaweza kutumia historia ili kuwafanya wachezaji wa sasa waweze kujituma na kutumia uwezo wao wote kupata mafanikio.


HUYU HAPA SURE BOY

Jana Jumamosi katika Jiji la Kigali kulikuwa na mchezo muhimu sana wa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika, kati ya Al Merreikh ya Sudan dhidi ya Yanga ya Tanzania.

Kwangu binafsi ninaposikia mechi kati ya Al Merreikh dhidi ya Yanga nakumbuka mwaka 1986 pale katika Uwanja wa Taifa ‘Shamba la Bibi’ (sasa Uwanja wa Uhuru), pamoja na kwamba miamba hiyo imekutana katika mechi nyingi.

Wajuaji au wakongwe watakumbuka jinsi jina la Sure Boy lilivyopatikana. Ilikuwa ni kivumbi na jasho kwelikweli. Halikuwa jina la kurithi kama lilivyorithiwa sasa na Salumu Abubakari.

TUJIKUMBUSHE CECAFA 1986

Mwaka 1986, Yanga ilicheza michuano ya Kombe la Afrika Mashariki (sasa linafahamika kama Kagame Cup) na kufika fainali. Yanga ilikuwa katika Kundi A ikiwa sambamba na klabu za AFC Leopards (Kenya), Silver Strikers (Malawi), KCCA FC (Uganda) na Small Simba (Zanzibar).

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Januari Mosi, 1986, Yanga ilianza dhidi ya Silver Strikers na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1. Mchezo wa pili ikafungwa 2-1 na AFC Leoprads.

Januari 9, Yanga tena ikaifunga KCCA bao 1-0 na mchezo wa mwisho ikaifunga Small Simba 2-1.


YASHIKA NAFASI YA PILI

Katika kundi hili Yanga ilishika nafasi ya pili nyuma ya AFC Leopards iliyokusanya pointi 10, huku Yanga ikiwa na pointi tisa.

Kundi B kulikuwa na timu za Mufulira Wonderers (Zambia), Al Merreikh (Sudan), Majimaji (Tanzania), Gor Mahia (Kenya) na Wagad (Somalia).

Katika kundi hili timu mbili zilitoka za Mufulira Wonderers iliyozoa pointi 10 na Al Merreikh iliibuka na pointi nane.

YANGA YAISAKA AL MERRIKH

Januari 11, 1986 zilipigwa nusu fainali kati ya Yanga na Mufulira na AFC Leopards na Al Merreikh. Hadi dakika 90 zinakamilika sio Yanga wala Mufulira iliyopata bao katika mchezo ambao uliamuriwa kwa matuta. Yanga ilipita kwa penalti 4-2 wakati AFC Leopards ilichapwa bao 1-0. Na kuzifanya Yanga na Al Merreikh kukutana fainali.


JINA LA SURE BOY

Mapema kabla ya fainali ilipigwa mechi ya kusaka mshindi wa tatu ambapo AFC Leopards ilishinda dhidi ya Mufulira Wonderers bao 1-0.

Wakati huo, Al Merreikh ilikuwa tishio. Mpira ulipigwa mwingi na katika dakika za mapema kipindi cha kwanza, Yanga ilifungwa bao la kuongoza na kipindi cha pili ikaongezwa lingine.

Sio kama Yanga walikuwa wanyonge la hasha, kipa wa Al Merreikh, Hamid Breima alikuwa nyota wa mchezo huo kama sio mashindano ya mwaka huo kwa ujumla.

Breima alifanya kazi kubwa  kuokoa hatari nyingi sana kutoka kwa wachezaji wa Yanga. Lakini katika jitihada zake, alishindwa kuokoa mipira miwili ya kijana mdogo aliyetoka Timu ya Sigara na kujiunga na Yanga, Abubakari Salumu.

Mchezaji huyo mfupi na machachari aliingia kipindi cha pili na kuisumbua ngome ya Al Merreikh na kufanikiwa kumfunga kipa bora zaidi mabao mawili ya haraka.

Abubakari Salumu alifunga mabao hayo wakati nusu ya mashabiki wa Yanga wakiwa wameshatoka uwanjani wakiamini wmepoteza kwa mabao 2-0.

Mtangazaji aliyetangaza mchezo huo, Charles Hilaly ni kama alikuwa amepagawa kufuatia mabao hayo na hapohapo alijikuta akimpachika Abubakari Salumu jina la Sure Boy. Tangu siku hiyo akatambulika hivyo.

Hata hivyo, mechi hiyo iliamuriwa kwa penalti na Yanga ilipoteza kwa kufungwa 4-2. Je, kuna mtu ameshamsimulia mtoto wa Abubakari Salumu, Salumu Abubakari ambaye naye anajiita ‘Sure Boy’ jina hili lilipotokea?

Basi Salumu Abubakari anapaswa kufahamu kwamba ana deni kubwa sana kutoka kwa baba yake kwa kulitumia jina hilo, kama ameshindwa kufanya kitu Kigali jana dhidi ya Al Merreikh,  bado mechi haijaisha anaweza kulitendea haki jina hilo la kurithi katika mchezo wa marudiano, jijini Dar es Salaam.