Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Michael B Jordan aweka rekodi tuzo za Oscars

Muktasari:

  • Hilo ni toleo la 98 la tuzo hizo zilizofanyika Ukumbi wa Dolby Theatre uliopo Hollywood, jijini Los Angeles, Marekani tangu kuanzishwa kwake mwaka 1929.

USHINDI wa mwigizaji wa Marekani, Michael Jordan katika kipengele cha muigizaji bora wa tuzo za Oscar zilizotolewa usiku wa kuamkia jana umeibua mjadala mkubwa baada ya kumshinda mpinzani wake mkubwa Timothee Chalamet aliyeonekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda.

Hilo ni toleo la 98 la tuzo hizo zilizofanyika Ukumbi wa Dolby Theatre uliopo Hollywood, jijini Los Angeles, Marekani tangu kuanzishwa kwake mwaka 1929.

Katika usiku huo ulioshuhudiwa na watu mbalimbali maarufu tuzo mbalimbali za kutambua thamani ya sanaa ya uigizaji zilitolewa lakini ile ya Jordan aliyoshinda  kupitia filamu ya ‘Sinners’ ilivutia zaidi watazamaji kutokana na ushindani wa waigizaji hao.

Sinners iling’ara usiku huo kwa kuchukua jumla ya tuzo nne ikiwemo ya muigizaji bora, Uandishi Bora wa Hadithi Asilia ikienda kwa mwandishi Ryan Coogler, Picha Bora ya Filamu (Cinematography) muongozaji, Autumn Durald Arkapaw na Muziki Bora wa Filamu, Ludwig Göransson.

Hii ni mara ya kwanza kwa Jordan kuchaguliwa kuwania tuzo hiyo na kushinda  tangu aanze kazi ya uigizaji mwaka 1999, miaka 27 bila tuzo hiyo.


USHINDI ULIVYOBADILI UPEPO

Kabla ya hafla hiyo wachambuzi wengi wa filamu walikuwa wakimpa nafasi kubwa ya kushinda Chalamet kutokana na mafanikio yake katika filamu na tuzo mbalimbali alizoshinda awali.

Nyota huyo alikuwa ameshinda tuzo za Golden Globe Awards pamoja na Critics’ Choice Awards, mafanikio yaliyomfanya kuwa na nafasi kubwa ya kuinyakua.

Hali ilibadilika baada ya Chalamet kukosa tuzo ya BAFTA Awards zinazotolewa kila mwaka Uingereza na tuzo hiyo ilienda kwa Robert Aramayo.

Mambo yakawa magumu zaidi baada ya Mmarekani huyo mwenye asili ya Ufaransa kukosa tena tuzo muhimu ya Screen Actors Guild ambayo alishinda Jordan na kubadili taswira ya nafasi kubwa ya  Chalamet kushinda.

Kwa kawaida, tuzo hizo mara nyingi huendana na matokeo ya Oscars kwa sababu hupigiwa kura na waigizaji wenyewe, ambao ni sehemu kubwa ya wapiga kura katika Akademia. Ushindi huo ulimpa Jordan nguvu kubwa kuelekea usiku wa Oscars.


MARA TATU MFULULIZO

Hii ni mara tatu mfululizo Chalamet kupoteza tuzo hiyo licha ya kuwa miongoni mwa waigizaji wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda kila mwaka.

Mara ya kwanza Chalamet kukosa tuzo ya Muigizaji Bora ilikuwa mwaka 2018, alipochaguliwa kuwania kupitia filamu ya ‘Call Me by Your Name’. Katika tuzo hizo, ushindi ulienda kwa Gary Oldman kupitia filamu ya Darkest Hour.

Hata hivyo licha ya kukosa lakini uteuzi huo ulimfanya Chalamet kuwa mmoja wa waigizaji vijana zaidi kuwahi kuwania tuzo ya Muigizaji Bora katika historia ya Oscars.

Mara ya pili kupoteza ilikuwa mwaka 2025 na Chalamet aliingia kwenye Oscars akiwa na matumaini makubwa baada ya kushinda tuzo za Screen Actors Guild katika kipengele hicho. Licha ya mafanikio hayo kabla ya Oscars, tuzo ya Muigizaji Bora ilichukuliwa na Adrien Brody.

Mwaka huu Chalamet alikosa tena tuzo hiyo baada ya kunyakuliwa  na Jordan aliyeshinda kupitia filamu ya Sinners. Hivyo kushindwa huko kumefanya nyota huyo kuwa na rekodi ya kupoteza mara tatu mfululizo katika tuzo za Oscars.

Ikumbukwe nyota huyo mwenye miaka 30 hakuwahi kuchukua tuzo za Oscars tangu aanze kuigiza mwishoni mwa mwaka 2007, mashabiki wengi wanaamini kuchukua tuzo hiyo ni suala la muda kutokana na umri wake.


SAFARI YAKE HADI OSCARS

Ushindi wa Jordan haukuwa wa bahati mbaya bali ni matokeo ya kazi kubwa aliyoifanya kwa miaka mingi. Nyota huyo alianza kupata umaarufu mkubwa kupitia filamu kama ‘Creed’ na ‘Black Panther’, ambazo zilionyesha uwezo wake mkubwa wa uigizaji na kumfanya kuwa mmoja wa waigizaji wanaoheshimika katika kizazi chake.

Katika filamu ya ‘Sinners’, Jordan ameonyesha uwezo mkubwa wa kuigiza kwa hisia, nguvu ya uhusika na uwezo wa kubeba hadithi nzima ya filamu.

Wachambuzi wengi wanaamini uigizaji huo uliwavutia wapiga kura wa Oscars na kumfanya aonekane anastahili kushinda tuzo hiyo.


WA SITA

Ushindi huo umemfanya Jordan kuwa muigizaji wa sita mwenye asili ya Afrika kushinda tuzo ya Muigizaji Bora katika historia ya Oscars.

Muigizaji wa kwanza katika historia ya tuzo hizo ni Sidney Poitier alikuwa mwanamume wa kwanza mwenye asili ya Afrika kushinda tuzo ya Muigizaji Bora mwaka 1964 kupitia filamu ya ‘Lilies of the Field’. Ushindi wake uliweka historia kubwa Hollywood na kufungua milango kwa waigizaji wengi wenye asili ya Afrika.

Wa pili alikuwa  Denzel Washington, alishinda tuzo hiyo mwaka 2002 kupitia filamu ya ‘Training Day’. Washington ni mmoja wa waigizaji wanaoheshimika zaidi Hollywood.

Mwingine ni Jamie Foxx  alitwaa tuzo hiyo mwaka 2005 baada ya kumuigiza mwanamuziki mashuhuri Ray Charles katika filamu ya ‘Ray’. Uigizaji wake ulisifiwa  kwa namna alivyofanikiwa kuiga maisha ya mwanamuziki huyo.

Mwaka 2007 Forest Whitaker alishinda kipengele hicho kupitia filamu ya ‘The Last King of Scotland’, na aliigiza nafasi ya aliyekuwa rais wa Uganda Idi Amin.

Mwaka 2022 Will Smith  alitwaa tuzo hiyo kupitia filamu ya ‘King Richard’, akimuigiza baba wa nyota wa tenisi Serena Williams na Venus Williams.


HOTUBA YA JORDAN

Katika hotuba hiyo, alitoa heshima kwa waigizaji wakongwe waliowahi kuvunja rekodi katika Hollywood kama Sidney Poitier, Denzel Washington, Halle Berry, Jamie Foxx, Forest Whitaker na Will Smith.

Jordan alisema kuwa mafanikio yake yametokana na njia waliyoifungua waigizaji hao katika tasnia hiyo, kauli iliyotafsiriwa kama heshima kubwa kwa waliomtangulia.

Katika hotuba yake ya shukrani, alimpongeza Coogler kwa kumpa nafasi ya kuonyesha uwezo wake wa kuigiza.

Alisema “Wewe ni mtu wa ajabu sana. Ni heshima kubwa kwangu kukuita mshirika na rafiki. Umenipa nafasi na uhuru wa kuonekana na kuonyesha uwezo wangu.”


USHINDI HUO UNA MAANA GANI?

Ushindi wa Jordan unaashiria ushindani mkali unaoendelea katika kizazi kipya cha waigizaji wa Hollywood. Waigizaji kama Jordan na Chalamet wanachukuliwa kama kizazi kipya cha uigizaji na filamu za kisasa kila mmoja anaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza tasnia hiyo miaka ijayo.

Pia ushindi wa ‘Sinners’ katika vipengele kadhaa unaonyesha namna filamu hiyo ilivyoweza kuwashawishi wapiga kura wa Oscars, na kumfanya Jordan kuwa mmoja wa washindi wakubwa wa usiku huo.

Kwa jumla, ushindi wa Jordan katika Oscars 2026 umefungua ukurasa mpya katika kazi yake ya uigizaji.

Ni ushindi unaothibitisha kuwa juhudi zake za miaka mingi zimeanza kuzaa matunda.