Prime
Miaka 32 baadaye, Mnyama kashindwa kupata mwali Unguja

Muktasari:
- Tulikuwa na dakika 180 tofauti kati ya zile za Uwanja wa Manispaa wa Berkane na hizi za Unguja. Kule RS Berkane walikuwa kila kitu. Huku Simba walikuwa kila kitu. Simba walitamanishwa kitu, lakini kikawa kinaponyoka kadri dakika zinavyoyoyoma.
HAIKUWEZEKANA. Na bahati mbaya zaidi ni kwamba haikuwezekana katika namna ambayo ilikaribia kuwezekana. RS Berkane imeondoka na ubingwa wa Shirikisho katika ardhi ya Unguja huku ikiacha msiba mkubwa kwa Wanasimba nyuma yake.
Tulikuwa na dakika 180 tofauti kati ya zile za Uwanja wa Manispaa wa Berkane na hizi za Unguja. Kule RS Berkane walikuwa kila kitu. Huku Simba walikuwa kila kitu. Simba walitamanishwa kitu, lakini kikawa kinaponyoka kadri dakika zinavyoyoyoma.
Walau kama Berkane ingefunga bao mapema basi tungetambua kwamba fainali imekwisha. Lakini Simba ndio iliyoanza kufunga mapema. Bao la mchezaji bora wa mechi, Joshua Mutale. Huwa wanamuita SGR.
Alikuwa na siku njema. Bao lile alikuwa katika nafasi sahihi, wakati sahihi, dakika sahihi na katika mechi sahihi. Akafunga. Kuanzia hapo aliwayumbisha vilivyo Berkane. Ghafla amebadilisha upepo. Mwanzoni mwa msimu hadi katikati ya msimu ungewauliza mashabiki wa Simba kama wanamhitaji Mutale msimu ujao katika kundi la watu ishirini wote wangesema hawamtaki.
Sasa hivi hali imekuwa tofauti. Ukiwauliza kama wanamhitaji nadhani watagawanyika kama kura za maoni zinazokaribia katika Uchaguzi Mkuu ujao nchini. Si ajabu Mutale akapata kura nyingi za ‘ndio’ na kumuacha mpinzani wake mwingine, Jean Charles Ahoua ambaye naye Simba wana wasiwasi na uwezo wake licha ya kuwa na namba nzuri.

Mechi ikaendelea. Berkane wa Unguja walikuwa wamechoka kuanzia dakika ya kwanza ya mchezo hadi dakika ya mwisho. Kwamba walizidiwa uwezo na Simba? Inawezekana. Kwamba joto la Unguja lilikuwa kali sana kwao? Inawezekana.
Shomari Kapombe akapoteza nafasi ya dhahabu. Yeye na nyavu. Aliudundisha mpira wa kichwa chini badala ya kuupiga kama ulivyo. Nafasi ile ataiota kwa miaka mingi. Unatamani Steven Mukwala angekuwepo katika nafasi ile.
Wakati wa mapumziko tukaona ugomvi wa Fabrice Ngoma na kipa Moussa Camara. Nabashiri kwamba ugomvi huu ulitokana na tukio la kipindi cha kwanza wakati Camara alipokwenda katika kibendera na mpira halafu akajaribu kuoshea mpira ndani. Mpira ukakatika na kutua karibu na lango la Simba huku yeye mwenyewe akiwa hayupo langoni.
Camara alipaswa kufanya kitu rahisi tu. Kufuata misingi. Angeutoa mpira nje kisha akakakimbilia langoni. Nadhani hapo ndipo alipomtibua Ngoma. Hata hivyo, baada ya kumchunguza Ngoma kwa muda mrefu sasa nimegundua kwamba Ngoma akiongea basi kwa heshima tu wachezaji wote wa Simba wanapaswa kukaa kimya. Ngoma ni kiongozi uwanjani, mzoefu, mfia timu, ana moyo na timu. Camara baada ya kumsugulisha benchi kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula kuna wakati anajisahau na kufanya makosa madogo madogo uwanjani.
Tulipotoka mapumziko Simba ilikuwa inadaiwa bao moja la kuiweka mechi sare baada ya Shomari kushindwa kufanya hivyo kipindi cha kwanza. Hapo ndipo mechi ilipoanza kuharibika baada ya kukumbana na makali ya mwamuzi wa Mauritania, Dahane Beida.
Katikati ya utamu wa mechi alimzawadia kadi ya pili ya njano, Yusuf Kagoma. Hadi sasa nina mkanganyiko wa mawazo. Haikuwa rafu mbaya isipokuwa Kagoma alijaribu kuucheza mpira kutokea nyuma. Mara kadhaa nimeona inaweza kuwa kadi ya pili ya njano. Mara kadhaa pia nimewahi kumuona mwamuzi akimuita mchezaji na kumuonya kwa mdomo kwamba anaweza kumpa kadi nyingine ya njano na awe makini.
Wakati mwingine sheria na kanuni zinakuwepo. Wakati mwingine mwamuzi anaamua mambo kwa busara zake. Angeweza kutomuonyesha kadi ya pili Kagoma na mechi ikaendelea vizuri kwa sababu hata Berkane hawakuonekana kumlalamikia mwamuzi ampe kadi Kagoma. Labda walimchanganya na hawakujua kuwa ana kadi ya njano tayari.

Berkane walikuwa hoi juzi. Jaribu kufikiria kama Simba wangekuwa wamepungua kule Berkane. Nadhani hali ingekuwa mbaya mno kwa Simba. Lakini Unguja Simba walikuwa wamepungua na bado wakaendelea kuleta rabsha.
Ni rabsha hii ndio ilileta bao la Mukwala lililokataliwa na VAR. Na baada ya bao hili kukataliwa kumekuwa na hisia mbalimbali. Kuna mashabiki wa Simba wakakukumbuka kwamba mwamuzi huyu alikuwa amelikataa bao halali la Stephane Aziz Ki alilofunga kule Pretoria katika pambano la robo fainali dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Hapa namtetea Dihane. Mabao yanayokataliwa na VAR yanakuwa nje ya uwezo wake. Watu waliokuwa katika chumba cha VAR ndio wanapaswa kulaumiwa kama tunahisi tumeonewa. Kuanzia bao la Aziz KI, hili la juzi, pamoja na yale matukio yaliyotokea katika mechi ya Simba na Stellenbosch hatua ya nusu fainali.
Mwamuzi anasikiliza tu kile ambacho anaambiwa na watu walio katika chumba cha VAR. Naweza kumuona hayupo sawa katika tukio la Kagoma, lakini hili la bao lililokatiliwa kwa VAR kama lile la Aziz Ki ni vitu ambavyo anapokea maelekezo kutoka katika chumba cha VAR.
Mwishoni Simba wakaruhusu bao ambalo lilivunja ndoto na mioyo. Makosa ya safu ya ulinzi ya Simba yakaipeleka mechi mbali zaidi na dakika hazikuruhusu. Pale Simba ilipaswa kushinda 4-1 ili ivuke. 3-1 isingeisaidia kwa sababu Afrika bado tunatumia kanuni ya bao la ugenini. Mechi ikawa imeishia miguuni mwa Soumaila Sidibe staa kutoka katika nchi ya Mali.
Miaka 32 iliyopita Simba ilifika fainali ikiwa na mfadhili, Azim Dewji. Ikafungwa 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) kwa mabao ya staa wa Stella Abidjan, Boli Zozo. Juzi walikuwa wametoka sare na kukosa ubingwa chini ya mfadhili anayeitwa Mohamed Dewji.
Jioni ile ya mwaka 1993, mgeni wa heshima alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati Ally Hassan Mwinyi. Safari hii mgeni wa heshima alikuwa mwanae, Dk Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar. Hata baada ya miaka 32 bado kura zetu hazijatosha kuleta kombe hili nyumbani.

Hapo katikati Yanga ilijaribu, lakini kura hazikutosha. Juzi Simba imejaribu lakini kura hazikutosha. Hata hivyo, ninachoona ni kwamba hatuko mbali sana na ubingwa huu.
Tuongeze uwekezaji katika timu zetu. Bahati mbaya wakubwa wanazidi kutunyofoa. Juzi wameondoka na Aziz Ki. Kabla ya hapo waliondoka na Fiston Mayele. Na unaweza kusikia kuna wakubwa wengine wanamtaka Ellie Mpanzu. Unadhani Al Masry na pesa zao hawakuomuona? Hata hivyo, tusichoke. Tuendelee kuwekeza. Hatuko mbali sana na hili taji kama ilivyokuwa hapo awali.