Messi alivyowapa raha makocha waliomnoa Barca

Thursday April 08 2021
messi pc

BARCELONA, HISPANIA. Zama mpya zinaendelea Barcelona baada ya uteuzi wa Kocha Ronald Koeman.

Agosti 19, 2020, Koeman alichaguliwa kuwa kocha mpya wa Barcelona kwa mkataba wa miaka miwili utakaofika tamati Juni 30, 2022.

Kocha huyo Mdachi ametua Nou Camp kuchukua mikoba ya Quique Setien, aliyefutwa kazi baada ya kichapo cha mabao 8–2 na Bayern Munich kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mechi yake ya kwanza ya kiushindani, Koeman alishuhudia Barcelona ikishinda 4-0 dhidi ya Villarreal kwenye La Liga, kabla ya kukumbana na kipigo chake cha kwanza cha bao 1-0 dhidi ya Getafe, Oktoba 17, 2020.

Oktoba 24, alikumbana na kichapo cha kwanza kwenye El Clasico wakati Barcelona ilipopigwa 3-1 uwanjani Nou Camp na mahasimu wao Real Madrid.

Lakini, kwenye mechi zote hizo, maisha ya Koeman yamekuwa yakitegemea kwa kiasi kikubwa mchango wa supastaa wa maana kabisa kwenye soka la dunia, Lionel Messi.

Advertisement

Kinachoelezwa ni Messi ndio Barcelona yenyewe. Kuthibitisha hilo ni kutazama idadi yake ya mabao ambayo amekuwa akifunga kwa makocha wote waliopita kwenye timu hiyo yeye akiwa mchezaji.

Kwa msimu huu wa 2020/21, Barcelona ikiwa chini ya Koeman, Messi amecheza mechi 38 na kufunga mabao 29 kwenye michuano yote, huku akiasisti pia mara 11. Lakini, kabla ya hapo alikuwa chini ya Setien, ambaye alifunga mabao 15 katika mechi 24 alizocheza chini ya kocha hiyo.

Huu hapa umuhimu wa Lionel Messi kwenye kikosi cha Barcelona kwa kila makocha waliopita kwenye kikosi hicho cha Nou Camp na kucheza chini yao, mara yake ya kwanza kuitumikia timu hiyo ilikuwa mwaka 2004.

Mkataba wa Messi utafika tamati mwishoni mwa msimu huu na jambo hilo linawafanya mabosi wa miamba hiyo ya Nou Camp kupambana kuhakikisha anabaki kwenye kikosi chao na hilo linatokana na lile ambalo amekuwa akifanya kwa makocha wote waliopita kwenye timu hiyo. Huduma ya Messi haina ubaguzi.


Frank Rijkaard (Juni 2003 - Juni 2008)

Mechi: 110

Mabao: 42

Asisti: 24

Kocha, Frank Rijkaard ndiye aliyempa kibali Messi cha kuanza kuchezea timu ya wakubwa ya Barcelona na hakika hakumwaangusha. Chini ya kocha huyo, Messi alicheza mechi 110, akifunga mabao 42 na kuasisti mara 24.

Mafanikio aliyopata ni kushinda La Liga mara mbili, Supercopa de Espana mara mbili, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja huku tuzo binafsi ikiwa ni Golden Boy, Don Balon mara mbili, Kinda Bora wa mwaka wa FIFPRO mara mbili kutokana na ubora wake moto kabisa ndani ya uwanja.


Pep Guardiola (Juni 2008 - Juni 2012)

Mechi: 219

Mabao: 211

Asisti: 88

Chini ya Pep Guardiola, Lionel Messi alionyesha kiwango bora zaidi katika maisha yake ya soka kwa muda wake aliokuwa kwenye kikosi cha Barcelona.

Chini ya kocha huyo Mhispaniola, alicheza mechi 219, akifunga mabao 211 na kuasisti mara 88. Mafanikio yake, alishinda La Liga mara tatu, Copa del Rey mara mbili, Supercopa de Espana mara tatu, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili, UEFA Super Cup mara mbili na Klabu Bingwa Dunia mara mbili.

Miongoni mwa tuzo zake binafsi, Messi alishinda Ballon d’Or mara tatu kipindi chake alichokuwa chini ya Guardiola kwenye kikosi cha Barcelona, hiyo ikiwa ni sehemu tu ya tuzo binafsi nyingi alizobeba kwa kipindi hicho.


Tito Vilanova (Juni 2012 - Julai 2013)

Mechi: 43

Mabao: 54

Asisti: 14

Kocha, Vilanova hakudumu sana Barcelona, aliinoa timu hiyo kwa mwaka mmoja tu kabla ya kuugua maradhi ya kansa na kufariki duniani.

Lakini, chini ya Vilanova, Messi aliendelea kuonyesha ubora wake kwenye kikosi cha Barcelona, akifunga mabao 54 katika mechi 43 alizocheza, huku akiasisti mara 14 katika mechi hizo.

Mafanikio ya timu nzima, Barca ilibeba taji la La Liga chini ya Vilanova, wakati tuzo binafsi alizoshinda Messi ni Ballon d’Or mara moja, Mchezaji Bora wa La Liga, Mshambuliaji Bora wa La Ligax, Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya na Kiatu cha Dhahabu cha La Liga maarufu kama Pichichi.


Gerardo Martino (Julai 2013 - Mei 2014)

Mechi: 38

Mabao: 35

Asisti: 11

Hiki ni kipindi Messi alipata bahati ya kuwa chini ya Muargentina mwenzake kwenye kikosi hicho cha Barcelona.

Gerardo Martina alipewa mikoba ya kuinoa Barcelona baada ya Vilanova na hakika mambo yake yalikuwa matamu kabisa kwa kuanzia, akipata huduma bora kutoka kwa Messi na katika mechi 38 alizocheza chini yake, alifunga mabao 35 na kuasisti mara 11.

Katika kipindi ambacho Barcelona ilikuwa chini ya Martino, haikupata mafanikio makubwa sana, ikibeba taji la Supercopa de Espana pekee na ndiyo maana kocha huyo alifutwa kazi kabla ya msimu kumalizika.


Luis Enrique (Mei 2014 - Mei 2017)

Mechi: 134

Mabao: 133

Asisti: 51

Luis Enrique ni kocha mwingine aliyepata umaarufu mkubwa kwenye kikosi cha Barcelona kutokana na mafanikio yake ya uwanjani.

Kakika, Mhispaniola huyo ni miongoni mwa watu waliopata huduma bora kabisa kutoka kwa Messi, ambapo kwenye mechi 134 alizocheza chini ya kocha huyo, alifunga mabao 133 na kuasisti mara 51.

Chini ya kocha huyo na huduma matata kabisa ya Messi, Barca ilishinda La Liga mara mbili, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja, Copa del Rey mara tatu, UEFA Super Cup mara moja, FIFA Club World Cup mara moja huko tuzo binafsi, Messi alishinda Ballon d’Or mara moja, Mchezaji Bora wa mwaka wa Uefa, Mchezaji Bora wa La Liga, Mshambuliaji Bora wa La Liga, Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya, Mfungaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na Pichichi.


Ernesto Valverde (Mei 2017 - Januari 2020)

Mechi: 109

Mabao: 103

Asisti: 39

Kocha Valverde naye ni mmoja wa watu waliopata huduma bora kabisa kutoka kwa supastaa Lionel Messi.

Chini ya kocha huyo, Messi alicheza mechi 109 na kufunga mabao 103, huku akiasisti pia mara 39 na kuonyesha ubabe mkubwa kabisa ndani ya uwanja.

Kwa kipindi hicho, Barcelona ilishinda La Liga mara mbili, Copa del Rey mara moja, Supercopa de Espana mara moja, huku tuzo binafsi alizobeba chini ya kocha huyo ni Ballon d’Or.

Mchezaji Bora wa Fifa, Mshambuliaji bora wa Msimu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya, Mfungaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na Pichichi mara mbili.

Messi alimshukuru pia Valverde kwenye mtandao wa Instagram kwa kile alichokifanya kwenye timu hiyo huku ikielezwa kwamba wawili hao walikuwa na uhusiano mzuri kwelikweli kama kipindi ambacho Messi alikuwa chini ya Guardiola.

Advertisement