Mechi za makundi CAF hazichezwi mdomoni
Muktasari:
- Wawakilishi wetu wakumbuke kuwa zipo nyakati timu ambazo huonekana dhaifu ziliwasapraizi kwa kuwafunga lakini zipo nyakati hizo zinaoonekana ni ngumu, zilinyooshwa nao na kuondoka kichwa chini.
WAKATI droo ya hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika ilipokuwa inachezeshwa, kila mmoja hapa kijiweni alikuwa anaombea jambo lake litimie.
Baadhi walikuwa wanaomba timu zao zipangwe kundi moja na timu fulani huku wakitamani pia zisikutanishwe na klabu nyingine fulani na kadhalika.
Hatimaye droo ikapangwa na wawakilishi wetu Tanzania ambao ni Yanga na Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam FC na Singida Black Stars zilizopo Kombe la Shirikisho Afrika wakapata wapinzani wao kwenye hatua hiyo.
Kama kawaida yetu, baada ya droo tambo kutoka kwa mashabiki wa kila upande zikaanza dhidi ya wengine na wa timu fulani wanaona kama wenzao wapo katika kundi gumu na wao wapo katika kundi rahisi.
Kuna ambao wanatamba timu yao itapenya na kuingia robo fainali na wenzao hawatofanya hivyo ilimradi tu kutotaka upande fulani uonekane una unyonge na mwingine uwe na ubabe.
Lakini mwishowe tukubaliane hapa, mpira hauchezwi mdomoni hasa hatua kama hii ngumu ya makundi ambayo tumeweka historia ya kipekee kama nchi kuingiza klabu zote nne zinazotuwakilisha.
Timu zetu zinapaswa kufanya maandalizi ya uhakika hasa ya kimbinu na kiufundi ili ziweze kukabiliana vyema na wapinzani ambao wako mbele yao badala ya kuwekeza muda na nguvu kubwa katika vijembe, tambo na propaganda ambazo mwishowe hazichezi mpira.
Ugumu au wepesi wa wapinzani wao utategemea zaidi namna timu zetu zilivyo bora na zikicheza kwa kiwango cha kawaida au cha chini kila mpinzani atakuwa mgumu lakini zikionyesha ubora wa hali ya juu, hata hao wanaoonekana miamba watashughulikiwa.
Wawakilishi wetu wakumbuke kuwa zipo nyakati timu ambazo huonekana dhaifu ziliwasapraizi kwa kuwafunga lakini zipo nyakati hizo zinaoonekana ni ngumu, zilinyooshwa nao na kuondoka kichwa chini.