Prime
Nabi azungumzia kundi la Yanga CAFCL
LINAPOTAJWA jina la Nasreddine Nabi, kila shabiki wa soka anakuwa na shauku yake, lakini kwa mashabiki wa Yanga, wengi hujisikia furaha kutokana na kumbukumbu alizoacha Mtunisia huyu aliyechukua uraia wa Ubelgiji.
Nabi aliifundisha Yanga kwa mafanikio kati ya mwaka 2021 na 2023 akiipa mataji saba yakiwamo makombe mawili ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Azam Shirikisho, Ngao ya Jamii mbili na Kombe la Mapinduzi.
Ukiacha mataji hayo kumbukumbu kubwa zaidi ambayo Nabi, aliwaachia Wananchi ni baada ya kuwaongoza kucheza fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika kwenye historia ya klabu hiyo ambayo alipoteza nyumbani 2-1 kisha kwenda kushinda ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya USM Alger.
Akiwa Yanga, Nabi aliiongoza timu hiyo kwenye jumla ya mechi 88 za mashindano yote akishinda mechi 63, akapoteza nane na kutoa sare 17 kabla ya kugoma kuongeza mkataba baada ya timu hiyo kumaliza msimu wake wa mwisho alioifikisha timu hiyo fainali ya Shirikisho Afrika.
KUTIMKIA FAR RABAT
Nabi anasema alilazimika kuiacha Yanga na kutimkia FAR Rabat ya Morocco, ikiwa ni uamuzi wa kulinda heshima yake baada ya hatua ambayo waliifikia wakati wa msimu wake wa mwisho.
“Baada ya kumaliza msimu wa mwisho na Yanga nilikuwa na wakati mgumu sana wa kufanya uamuzi, kumbuka ilikuwa tumetoka kucheza fainali, Yanga ni familia yangu ambayo itaishi kwenye moyo wangu wakati wote, upendo ambao nilionyeshwa na uongozi hususani familia ya Ghalib Said Mohammed (GSM) na wasaidizi wake wote, uongozi wa klabu hususan Rais Hersi Said,”€ anasema Nabi huku akiendelea kufafanua zaidi:
“Yanga ilikuwa imecheza fainali, hatua kubwa zaidi ya hiyo ilikuwa kwenda kuchukua ubingwa wa Afrika, nilijaribu kutoa mawazo yangu, lakini kwa wakati ule ilikuwa ngumu kufikiwa kutokana na uhalisia wa mikataba ya wachezaji.
“Ngoja nikwambie Yanga ili iende mbali ilitakiwa tuchukue uamuzi mgumu wa kuwaondoa wachezaji ambao walikuwa hawawezi kwenda kutupa ubingwa wa Afrika.
“Lakini niliona mikataba yao ingekuwa ngumu kwa klabu kuyakubali maoni hayo, nashukuru kuona baadaye nyuma yangu uamuzi huo ulitimia, ilikuwa lazima ifike pale katika kujenga timu imara zaidi.
“Mwisho nikaona niende FAF Rabat, ambayo kwangu niliona ni ofa nzuri nje ya ofa nyingi ambazo wakati huo zilinifuata, ulikuwa mradi mzuri lakini bahati mbaya nilikutana na mambo ambayo nilishindwa kuwapa ubingwa tena dakika za mwisho kwa mambo ambayo siwezi kuyaweka wazi sana yaliyosababishwa na mambo ya kisiasa kutoka kwa timu pinzani.
“Kwangu mimi baada ya kuongoza ligi kwa muda mrefu FAR Rabat, ilistahili kuwa bingwa wa ligi pale Morocco lakini yale yaliyotokea hayakunifurahisha na nikaona ni bora niondoke Morocco.”
ANATUA KAIZER
Baada ya kuondoka Morocco Nabi akatangazwa kuwa kocha mpya wa Kaizer Chiefs, ambayo ilikuwa inamuwinda kwa muda mrefu hata wakati akiondoka Yanga.
“Nilipoondoka FAR Rabat nilikubali kujiunga na Kaizer Chiefs, nikiri kwamba uongozi wa klabu ulinitafuta kwa muda mrefu sana hata wakati naondoka Yanga, lakini kuna mambo nilitaka kwanza kukubaliana nao.
Kaizer Chiefs haikuwa nafasi ambayo nilitakiwa kukubali kwa haraka kutokana na ofa, ile ni klabu kubwa sana, lakini bahati mbaya ilihitaji nguvu kubwa kwa kuwa kikosi chao kilikuwa kimebomoka sana, ilihitaji bajeti kubwa sana kuirudisha kwenye ubora wake.
“Tulikubaliana kwamba tutalifanya hilo kwa awamu, lakini niseme haikuwa rahisi sana kutokana na ubora wa timu shindani kama Mamelodi Sundowns, Orlando Pirates ambao walikuwa na vikosi bora zaidi yetu.
“Tulihitaji wachezaji wakubwa ambao walikuwa sahihi kwa timu na ilihitaji bajeti kubwa, hivyo tukawa na mwendo ambao haukuwa sahihi sana kwa mashabiki, lakini nilifurahi msimu uliopita tulianza angalau kuona picha ya ile Kaizer Chiefs, ambayo tunaitaka hasa baada ya kuchukua ubingwa wa Nedbank na baadaye tukapata tiketi ya kurudi kwenye mashindano ya Afrika.
“Kwangu mimi ubingwa ule na kuirudisha timu mashindano ya Afrika, ilikuwa kubwa sana bahati mbaya mwanzo wa msimu huu, tukafikia uamuzi wa kuachana ambao sitaki kuuongelea hili kwa undani kwa kuwa kuna makubaliano kati yangu na uongozi, itoshe kwa kuwatakia kila la kheri itafanikiwa huko mbele.”
ANATAJWA SIMBA, YANGA, AZAM
Kila klabu za Simba, Yanga na Azam zinapoachana na makocha jina la Nabi huibuka kwa nguvu kama ambavyo ilitokea hivi karibuni baada ya timu hizo kuachana na makocha wao.
“Ni kweli huwa napata presha sana kutoka kwa klabu za Tanzania kunihitaji, kwangu mimi huwa ni furaha ikionyesha kwamba hiyo ni nchi ambayo nimeishi vizuri na kuna heshima ya kazi yangu niliyoifanya.
“Niliwahi kufanya mazungumzo na wamilikiwa Azam FC, lakini wakati ule kuna mambo yalikuwa yananizuia, ila niseme Azam ni timu kubwa yenye kila kitu ambacho kocha yeyote angeweza kutamani kufanya kazi.
“Ofa ya Simba, ndio imewahi kuja, lakini nayo sio hivi karibuni baada ya kuondoka Fadlu (Davids) niliona tu watu wanasema, lakini haikuwa na uhalisia wowote kutoka kwangu hakuna kiongozi ambaye niliongea naye hivyo hivyo Yanga ilikuwa ni presha tu kwa mashabiki na vyombo vya habari, lakini hakuna ambaye alinitafuta kwa maana ya uongozi.”
KILICHOMRUDISHA TANZANIA
Nabi anaweka wazi kwamba mashabiki wa mpira wasifikirie tofauti wanapomuona Tanzania kwani hapa ni kama nyumbani.
“Mimi Tanzania ni nyumbani wakati wowote nikipata nafasi huwa nakuja. Ukiangalia tangu nilipoondoka Yanga, nimekuwa na safari za kuja hapa ambazo nyingi ni binafsi sana hazikuwa za kuitwa na timu yoyote, nakumbuka nilipokuja hivi karibuni niliona watu wanasema nimekuja Yanga au Simba haikuwa hivyo.
“Nilikuja Tanzania kuangalia maendeleo ya shule ya watoto wa dini ambayo naijenga kule Kimbiji, niliishi sana kule Kimbiji nikaona namna watoto wanakosa sehemu sahihi ya kujifunza dini.
“Nikachukua uamuzi wa kujenga madrasa ambayo ipo kwenye hatua za mwisho kumalizika, nilisema nijenge hii ili iwe alama yangu na familia yangu kwa kuishi vizuri Tanzania, hii madrasa niliomba ipewe jina la mama yangu mzazi itaitwa madrasa Zakia.
“Ujenzi bado unaendelea tupo kwenye umaliziaji kwahiyo bado nitakuja sana Tanzania, hata wakati wa kuifungua nitakuja tena lakini hapa ni nchi ambayo napenda sana mazingira yake kuna vivutio vingi, huwa nakuwa na amani sana nikiwa hapa Tanzania.”
YANGA ANAIONAJE
“Yanga ni timu nzuri siku zote nimekuwa nasema hili, hii hali ambayo inapitia sasa ni kawaida kwenye maisha ya soka, nimeona wamemuondoa kocha siwezi kuwaingilia sana uongozi lakini kiujumla nilivyoiona timu ni kikosi kizuri kinahitaji kocha mkubwa ambaye atapambana kuirudisha timu kwenye utulivu.”
KURUDI YANGA
Nabi anasema kuna uwezekano wa yeye kurejea tena Tanzania, kwani maisha yake ya soka bado hayajafika mwisho.
“Mimi ni kocha siwezi kusema sitaweza kurudi Yanga, hii ni klabu ambayo imepanda kitu kikubwa kwenye moyo wangu, hatua ya kurudi inategemea na mtazamo wa uongozi wa klabu, kama wataona nahitajika nitaongea nao, lakini sijakaa mezani au kuongea na kiongozi yeyote juu ya kurejea Yanga.
“Hivi karibuni nilikutana na ndugu yangu Waziri Mavunde (Antony), ni rafiki yangu wa muda mrefu sana, hata nilipoondoka Yanga tuliendelea kuwasiliana kwahiyo kuna mambo binafsi tulionana na kuzungumza, haikuwa kuhusu Yanga kabisa, lakini kuna mambo nitamsaidia kuhusu lile eneo ambalo analiongoza na namtakia kila la kheri.”
SOKA LA TANZANIA
“Soka la Tanzania linazidi kupiga hatua kadiri ya muda unavyosogea, nimeishi Tanzania najua ugumu wa mechi za ligi ya Tanzania, unaweza kuona kama mechi ni rahisi lakini mchezo ukianza utagundua sio rahisi kuona timu yako inashinda, unaona sasa kuna timu nne zinaweza kuingia hatua ya makundi mashindano ya Afrika hii ni uthibitisho kwamba ligi ya hapa inakua kwa kasi sana.
“Huhitaji kuja Tanzania ili ujue soka la Tanzania, kuna fursa ya mechi kuonyeshwa kwenye televisheni hii inasaidia na kuwatangaza wachezaji wengi, unajua kila mchezaji anaona akija Tanzania atapata nafasi ya kuonekana mataifa mengine kirahisi, nadhani kama usimamizi kama huu utaendelea Tanzania itazidi kupiga hatua.”
GSM SHUJAA YANGA
Akizungumzia umwamba ambao Yanga inaendelea kuuonyesha kwa kuchukua mataji ya ndani na pia kung’ara kimataifa, Nabi anasema, kama kuna mtu anatakiwa kupongezwa ni udhamini na ufadhili wa Ghalib Said Mohammed kwenye klabu hiyo.
“Yanga ina uongozi mzuri ndio maana mnaona mambo yanabadilika, lakini mimi naangalia pia kwa umbali zaidi, nimekuwa hapo kama kuna mtu amesimama imara kutaka kuona timu inabadilika na kufanya vizuri ni GSM, amekuwa na nguvu kubwa sana ya kuifanya Yanga isimame imara.
“Nimekuwa nazungumza naye sana. Na kila ukiongea naye unaona namna akili yake inawaza kutamani kuiona Yanga inakuwa na kikosi imara cha kubeba ubingwa wakati wote na inabeba taji la Afrika.
“Aliwahi kuniambia akiona Yanga imeanguka uwanjani, anaumia sana na sio yeye tu. Ngoja nikupe siri, hata familia yake inafurahi sana timu ikifanya vizuri, kiukweli watu wa Yanga ukiondoa viongozi wao wanatakiwa kumshukuru sana GSM kwa namna anavyoendelea kuipa nguvu timu yao.”
HESABU BAADA YA KAIZER
Nabi anasema kwa sasa amerudi nyumbani na anahitaji kumpumzika kwani amefanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika.
“Kwa sasa nimerudi nyumbani, akili yangu nimeona inahitaji kupumzika, nahitaji kupumzika kidogo, lakini pia nipate muda wa kukaa na familia yangu, nimekuwa napata muda mfupi sana wa kuangalia mambo ya familia, baadaye nitafanya uamuzi, nina ofa nyingi sana, lakini huu sio wakati wa kuamua wapi kwa kwenda.”€