Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MBEYA CITY: Safari ya kushuka, kupanda ilivyogeuka pande mbili

Muktasari:

  • Timu hiyo yenye historia kubwa kwenye soka nchini, ilishuka daraja msimu wa 2022-2023 kupitia ‘play-offs’ ilipoondoshwa na Mashujaa kwa jumla ya mabao 3-1 na sasa inarudi upya.

USIYEMPENDA kaja. Ndivyo unavyoweza kuelezea kurejea kwa Mbeya City ndani ya Ligi Kuu Bara baada ya kupotea misimu miwili, huku ikiweka rekodi na heshima jijini Mbeya.

Timu hiyo yenye historia kubwa kwenye soka nchini, ilishuka daraja msimu wa 2022-2023 kupitia ‘play-offs’ ilipoondoshwa na Mashujaa kwa jumla ya mabao 3-1 na sasa inarudi upya.

Mbeya City inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, inakumbukwa kwa historia iliyoandika kwa mara ya kwanza ilipopanda Ligi Kuu msimu wa 2013-2014 na kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo.

Kama haitoshi kabla ya kushuka daraja, timu hiyo ilidumu miaka 10 katika Ligi Kuu, huku ikionyesha ushindani mkubwa kwenye mashindano yote na kuzipa upinzani Yanga, Simba, Azam na nyinginezo.

Kwa sasa timu hiyo imerejea Ligi Kuu baada ya kujihakikishia kumaliza ndani ya nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa Championship kwa pointi 65 nyuma ya Mtibwa Sugar, ikibaki mechi moja. 

SIASA ZINAHUSIKA

Moja ya sababu zilizoishusha daraja timu hiyo ilikuwa ni siasa na hizo ndizo zimeirejesha tena Mbeya City Ligi Kuu kutokana na hamasa ya viongozi wake namna walivyokuwa sambamba na chama lao.

Mara kadhaa tulishuhudia viongozi wa kisiasa wakijitolea pesa zao mfukoni kulipia viingilio kwa mashabiki hadi kufikia 1000, hali ambayo iliwapa mzuka mwingi wachezaji kucheza na ‘vibe’ jukwaani.

Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa, Mbunge wa Mbeya mjini Dk Tulia Ackson walikuwa sehemu ya baadhi ya wadau na viongozi wa kisiasa waliokuwa pamoja na timu hiyo kuhakikisha wanarejea Ligi Kuu.

Mbali na viongozi hao, Mbeya City iliwaweka pamoja madiwani wa jiji hilo na wabunge wa Mkoa wa Mbeya ambao kila mmoja kwa nafasi yake alichangia kitu kufikia malengo.

Mashabiki nao hawakuwa mbali kuisapoti timu hiyo kutokana na idadi kubwa iliyokuwa ikijitokeza viwanjani kuunga juhudi za viongozi kuhakikisha City inarejea Ligi Kuu.


UONGOZI MPYA KIBOKO

Pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na uongozi wa awali chini ya mtendaji mkuu, Emanuel Kimbe aliyepambana timu kudumu miaka 10 Ligi Kuu, uongozi mpya wa sasa nao ni haki upewe maua yake.

Mbeya City baada ya kushuka daraja Kimbe aliamua kujiweka pembeni na kuteuliwa mtendaji mpya, Ally Nnunduma ambaye ameweka rekodi mpya ya kuongoza kwa kipindi kifupi na kuipandisha timu Ligi Kuu.

Nnunduma alikabidhiwa timu hiyo ikiwa Championship msimu uliopita ikiwa na michezo tisa ambapo ilimaliza nafasi ya sita kwa pointi 43, huku Ken Gold na Pamba Jiji zikipanda daraja.

Mtendaji huyo baada ya kukabidhiwa mikoba hiyo, aliahidi timu kurudi Ligi Kuu akieleza kuwa mkakati wake ni kuiweka karibu timu na mashabiki ambao aliamini wanayo nguvu kubwa kufikia malengo.

Hata hivyo, mkakati huo umeonekana kuzaa matunda kwani mara kadhaa, kigogo huyo ambaye ni mchumi katika Halmashauri ya Jiji, alikuwa akiwapa nafasi wananchi kushauri masuala kadhaa kwenye timu.


USAJILI NA MOTISHA

Timu hii yenye mashabiki wengi ndani na nje ya jiji la Mbeya, haikupanda kibahati mbaya bali ni kutokana na usajili ilioufanya na benchi la ufundi lenye uwezo binafsi.

City ilianza msimu chini ya kocha Salum Mayanga ambaye alihudumu kwa zaidi ya msimu mmoja kabla ya kutimkia Mashujaa na nafasi yake kuzibwa na Malale Hamsini.

Mbali na kikosi bora ilichokuwa nacho, haikuwa mbali kuwapa nguvu ya ziada ikiwa ni motisha za hapa na pale katika njia ya kuwaongezea hamasa wachezaji kupambana katika kila mechi.

Hali hiyo iliwafanya kufika robo fainali ya Kombe la Shirikisho baada ya kufungwa mabao 3-1 na Simba, ikiwa ni rekodi bora kwao kwenye Championship.

Wachezaji kama Hashim Mussa, David Mwasa, Peter Mwalyanzi, Adili Buha, Mudathir Said, Eliud Ambokile na Chesko Mwasimba ni sehemu ya mastaa waliowahi kucheza soka la ushindani.

Wachezaji hao pamoja na kocha Malale mwenye rekodi na historia yake nchini, walisaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo ya timu hiyo na sasa miamba ya soka nchini, ijipange iwapo na ratiba ya kwenda kwenye Uwanja wa Sokoine.


YAIZIDI KENGOLD

Kupanda kwa timu hiyo kunaongeza hamasa mpya kwa soka jijini Mbeya na kuziba pengo la ndugu zao, Ken Gold walioshuka daraja msimu huu kabla ya ligi kuisha.

Ken Gold ilishuka daraja ikiwa ni msimu mmoja tu kushiriki Ligi Kuu ambapo msimu ujao itakipiga tena Championship kutafuta kurejea.

Mbeya iliwahi kuwa na timu nne Ligi Kuu na kuweka rekodi ambayo haitafutika, ikiwa ni Ihefu, Mbeya Kwanza, Mbeya City na Tanzania Prisons ambapo kwa sasa zitabaki mbili tu.


MALALE NA REKODI

Pamoja na kukuta mazingira mazuri ya kupanda, lakini huwezi kukwepa kumpongeza kocha Malale kwa kazi nzuri aliyoifanya kufikia malengo ya timu hiyo.

Kocha huyo alikuta zimebaki mechi sita ikiwamo moja ya Kombe la Shirikisho, ambapo alipoteza dhidi ya Simba, huku sare ikiwa moja dhidi ya Biashara United na kushinda miwili na sasa bado mmoja.

Katika mechi hizo alihitaji ushindi au sare, ambapo ni Biashara United pekee waliomzuia kwa kupata sare ya 1-1, akaibwaga Polisi Tanzania 1-0, Geita Gold 2-1 na kuichakaza 5-0 Cosmopolitan na kupanda Ligi Kuu.

Matokeo ya kupandisha timu kocha huyo yanakuwa endelevu baada ya kufanya hivyo kwa timu kadhaa ikiwamo Alliance FC na JKT Tanzania na sasa anafanya kweli kwa City.


UONGOZI WAFUNGUKA

Mtendaji mkuu wa timu hiyo, Nnunduma anasema anajivunia rekodi na historia aliyoweka kwani ni jambo aliloahidi kwa mashabiki na kwamba kwa sasa wanasubiri kumaliza ligi kuanza mipango.

Anasema wadau walijitoa kwa kiasi kikubwa, akiwapongeza wananchi wote ndani nje ya jiji kwa sapoti yao kuhakikisha timu inarejea Ligi Kuu akiahidi kuwa mazuri zaidi yanakuja.

“Niliahidi na tunashukuru tumefanikiwa, tukimaliza ligi tutaanza kusuka timu kwa ajili ya Ligi Kuu, kuna mambo mengi yanahitaji kufanyika.”