Prime
Mayele na wenzake wamewapiga bao mapacha wetu

Muktasari:
- Mwaka 2018 ikanunuliwa na tajiri kutoka Saudi Arabia, Turki Al Sheikh. Na hapo ndipo ilipobadilishwa jina kuitwa Pyramids ikahamishiwa Cairo. Sheikh aliiuza kwenda kwa tajiri mwingine, Salem Al Shamsi. Kuanzia kwa Sheikh hadi tajiri wa leo Pyramids wamezoea kutia pesa pale inapohitajika.
RAFIKI yetu Fiston Mayele na timu yake ya Pyramids wametwaa kombe ambalo kwetu linabaki kuwa ndoto. Ligi ya Mabingwa Afrika. Imenifikirisha. Hawa jamaa walianzishwa 2008 tu wakitumia jina la Al Assiouty. Walikuwa na makazi yao katika manispaa ndogo ya Ben Suef
Mwaka 2018 ikanunuliwa na tajiri kutoka Saudi Arabia, Turki Al Sheikh. Na hapo ndipo ilipobadilishwa jina kuitwa Pyramids ikahamishiwa Cairo. Sheikh aliiuza kwenda kwa tajiri mwingine, Salem Al Shamsi. Kuanzia kwa Sheikh hadi tajiri wa leo Pyramids wamezoea kutia pesa pale inapohitajika.
Matokeo yake msimu huu wametwaa ubingwa wa Afrika. Hii maana yake nini? Maana yake rafiki zetu wametwaa ubingwa mbele ya wale watani wa Kariakoo, Simba na Yanga. Hawa watani mmoja alianzishwa 1935 mwingine akaanzishwa 1936.
Pyramids wametuonyesha kwamba ukitia pesa unapata mafanikio. Bahati nzuri sisi wenyewe ni mfano mzuri wa matumizi ya pesa za Pyramids. Walimtaka Fiston Kalala Mayele akiwa wa moto pale Yanga na amewapa ubingwa.

Bahati mbaya kwetu ni kwamba wakati wao wakitia pesa, sisi tunaonekana kuwa klabu ambazo bado kazi yake ni kulisha wenye pesa zao. Mayele ni mfano mwingine tu, lakini wakati fulani TP Mazembe wakiwa na matumizi makubwa ya pesa walitia pesa pale Simba na kuondoka na Mbwana Samatta ambaye alienda kuwapa ubingwa wa Afrika.
Ndivyo ilivyo. Samaki mkubwa anamla samaki mdogo. Safari hii Wydad Casablanca wameondoka na Stephane Aziz Ki. Utashangaa nini kama Aziz KI akiungana na mafundi wenzake kule Morocco na akatwaa ubingwa wa Afrika? Hauwezi kushangaa sana.
Matokeo yake tumebaki kushangilia kufika fainali za Shirikisho mara mbili katika miaka ya karibuni. Sio mbaya, lakini safari bado ni ndefu. Kama robo huwa ni mwisho katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, basi tunahitaji tuendelee kutia pesa tena na tena.

Ubingwa wa Pyramids pia umenikumbusha kwamba suala sio umri wa klabu. Suala ni uwekezaji tu. Kigingi kikubwa kwao ni ubingwa wa Ligi Kuu Misri. Pale wamekutana na fitina za Al Ahly na mara nyingi wamejikuta wakiishia nafasi ya pili.
Hapa nimewakumbuka ndugu zetu Azam. Na wao walianza 2008 kama Pyramids. Tofauti ni kwamba Azam wamewahi kuchukua mara moja ubingwa wa Ligi Kuu Bara wakati Pyramids hawajawahi. Mara nyingi Azam wamekuwa wakilalamika kwamba wakubwa wamekuwa wakiwapiga fitna katika mbio za ubingwa.
Sawa, kama unapigwa vita ndani basi unaweza kufanya kitu nje. Hiki ndicho ambacho rafiki zetu Pyramids wamewafundisha Azam. Kama marefa wa ndani wanazipendelea Simba na Yanga basi unaweza kuchezeshwa na waamuzi wa kimataifa katika mechi za CAF na ukachukua ubingwa kama una timu imara.
Azam wangeweza kukwepa fitna za Simba na Yanga kwa kufanya vizuri michuano ya CAF. Ingethibitisha namna gani huwa wananyongwa katika soka la nyumbani. Kwa hali ilivyo sasa ni ngumu kuthibitisha kwa sababu katika michuano ya kimataifa nako wanavurunda. Majuzi tu walitolewa na timu ambayo haina hata afya kutoka Ethiopia. Wakatolewa tena na APR ya Rwanda. Maisha ambayo Simba na Yanga wameshavuka.

Mambo mawili natamani kuyachunguza baada ya Pyramids kutwaa ubingwa wa Afrika. Nataka kuchunguza kama ubingwa huu umepokewa vizuri na mashabiki na viongozi wa timu mbili kubwa za Misri - Al Ahly na Zamalek. Sidhani kama Pyramids watakuwa wamenuniwa kwa kutwaa ubingwa huo.
Ninachofahamu ni kwamba mashabiki wa Al Ahly na Zamalek huwa hawapendani wenyewe kwa wenyewe. Ni kama ilivyo kwa Simba na Yanga. Ukienda Cairo ukamfunga Zamalek, basi inakuwa raha kubwa kwa mashabiki wa Al Ahly. Vivyo hivyo ukimfunga Al Ahly unajikuta unaangukia kuwa rafiki kipenzi wa Zamalek.
Mwaka 2003 wakati Simba ilipoiondosha Zamalek pale Cairo kwa mikwaju ya penalti mashabiki wa Al Ahly walifurahi. Hiki ni kama kinachotokea katika mpira wetu. Simba kafungwa fainali na RS Berkane, lakini waliofurahi ni Yanga. Sidhani kama Pyramids watakuwa wamenuniwa kwa kutwaa ubingwa huu. Labda Waarabu wa Misri watakuwa wameona fahari kuwa ubingwa umeendelea kubakia katika ardhi yao. Haya yote siyafahamu vizuri. Labda Watanzania wanaoishi Misri wanaweza kutusaidia. Huku Tanzania nadhani hakutakuwa na shida kama Azam wakitwaa ubingwa wa Afrika au Shirikisho. Sehemu pekee ambayo wanaweza kununisha watu ni kama wakichukua ubingwa wa ligi. Lakini na hapo inategemea na anakimbizana na nani. Kama anakimbizana na Yanga huku Simba wakiwa mbali kuna uwezekano mashabiki wa Simba wakasimama na Azam na kufurahia ubingwa wao.

Kitu kingine ambacho kinahitaji uchunguzi ni aina ya mkataba wa mauzo ambao Yanga wameingia na Pyramids. Kwa wenzetu ubingwa wa Pyramids ulikuwa fursa kwa Yanga kuambulia chochote kama wangeingia mkataba kama wa wenzetu wa nje.
Wale wenzetu huwa wanaweka kipengele kuwa endapo mchezaji atatwaa taji fulani, basi klabu yake ya zamani itapokea kiasi fulani. Kuna namna mbili hapa. Kwanza ni kwa klabu yake ya zamani kunufaika, pili ni hata mchezaji mwenyewe. Tukiachana na bonasi ya kawaida ambayo Mayele atapata na wenzake kwa kutwaa taji hilo, lakini Mayele alipaswa kuwa na kipengele katika mkataba wake ambacho kinaweza kumpa fedha kama akitwaa ubingwa wa Afrika.
Wenzetu ndio maana mazungumzo ya mkataba huwa yanachukua muda mrefu tofauti na sisi. Kuna mambo mengi ya kujadili na vipengele vingi kama hivi ambavyo katika mpira wetu tunachukulia poa ndio maana mazungumzo ya mkataba yanafanyika usiku mmoja tu nyumbani kwa kiongozi na mchezaji anamwaga wino.