Jesse Owens: Mwamba aliyeandika rekodi isiyofutika medali Olimpiki

Muktasari:
- Hata hivyo, thamani ya medali zinapouzwa miaka baada ya kutunikiwa mwanariadha hasa za Olimpiki, Jumuiya ya Madola au Kombe la Dunia la Fifa katika nchi za Ulaya na Marekani huwa kubwa kiasi cha kushangaza.
MEDALI na hasa ya dhahabu katika mashindano ya michezo ya kimataifa ni tuzo iliyojaa fahari kwa mshindi na inayosaidia kuitangaza nchi ya mshindi husika.
Hata hivyo, thamani ya medali zinapouzwa miaka baada ya kutunikiwa mwanariadha hasa za Olimpiki, Jumuiya ya Madola au Kombe la Dunia la Fifa katika nchi za Ulaya na Marekani huwa kubwa kiasi cha kushangaza.
Naamini medali za wanamichezo wa Afrika, Asia au nchi za Kiarabu zikiuzwa hazitakaribia hata robo ya thamani inayotolewa kwa medali za wanariadha wa Ulaya na Marekani.

Kwa mfano, kama mwanariadha wa Tanzania, Filbert Bayi ataamua kuuza medali zake za dhahabu, basi fedha atakazopata ni ndogo ukilinganisha na za wenzake kama Sebastian Coe wa Uingereza na John Walker wa New Zealand waliokuwa wapinzani wake wakubwa katika mbio za maili moja na mita 1,500 katika miaka ya 1970 na 1980.
Katika huo mwenendo wa kuuza medali - rekodi ya thamani kubwa ya kuuza medali hizo katika mnada ni ile moja ya medali nne alizonyakua mwanariadha wa Marekani mwenye asili ya Afrika, Jesse Owens, katika michezo ya Olimpiki ya 1936 iliyofanyika Berlin, Ujerumani.
Medali hiyo iliuzwa 2013 kwa Dola 1.5 milioni za Marekani (takriban Sh4.03 bilioni). Zaidi ya nusu ya hizo fedha zilitumiwa na familia yake kusaidia kuwasomesha watoto wa masikini wa Marekani wenye asili ya Afrika, yatima, wajane na watu wenye ulemavu.
Medali mbili nyingine ziliuzwa miaka michache iliyopita katika Jiji la Texas kwa Dola 500,000 (takriban Sh1.3 bilioni). Hivi sasa familia yake inatayarishiwa mnada wa kuuza medali ya mwisho ya dhahabu iliyobaki ya Olimpiki ya Berlin na kubakisha medali alizoshinda katika mashindano mengine.
Owens anakumbukwa kwa kufanya mambo ambayo hayasahauliki na yamekuwa sehemu muhimu ya historia ya michezo ya Olimpiki na mingine.
Akifahamika kama James Cleveland “Jesse” Owens alikuwa stadi katika michezo mingi na kushinda medali nne za dhahabu ambazo ziliweka rekodi tatu za dunia na kuwa sawa na nyingine katika michezo ya 1936 iliyofanyika Berlin.
Hii ilikuwa katika mbio za mita 100 na 200, mbio za kupokezana vijiti za masafa ya 4x100 na kuruka kwenye mchanga.
Owens aliyejulikana kama J.C alikuwa kitinda mimba katika familia ya watoto 10 (wanawake watatu na wanaume saba) alizaliwa Septemba 12, 1913. Alipokuwa mdogo alifanya kazi mbalimbali kama kupanga vitu madukani, kubeba mizigo na kushona viatu huku akipenda kukimbia.
Alipata umaarufu akiwa mwanafunzi wa shule ya sekondari ya mji wa Cleveland alipotumia muda sawa na rekodi ya dunia wa sekunde 9.4 katika mbio za mita 91 na kuruka futi 24 na mita 7.56 katika mchanga kwenye mashindano ya shule za sekondari yaliyofanyika Chicago 1933.

Aliendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Ohio na huko alifanya vizuri katika riadha na kuweka rekodi za dunia - mojawapo ikiwa ni ya kuruka mchanga futi 26 na mita 8.13 iliyodumu kwa miaka 25.
Mwaka 1936 yeye na wenzake walipanda meli kwenda Ujerumani kushiriki Olimpiki na huko watu wengi walikuwa na hamu ya kumuona kwa vile alipata umaarufu dunia nzima.
Alipofika Ujerumani Adi Dassler (aliyemiliki kampuni maarufu ya viatu vya michezo ya Adidas) alimuomba atumie viatu vinavyotengenezwa na kampuni yake. Hii ilimfanya Owens kuwa mwanariadha mweusi wa kwanza kutumia viatu hivyo.
Katika mashindano alifanya hayo maajabu ya kushinda medali nne za dhahabu na kuweka rekodi tatu za dunia. Mafanikio yake yalimuudhi mtawala wa Ujerumani, Dikteta Adolf Hitler aliyesema inakuwaje mtu mweusi anamshinda mtu mweupe katika michezo.
Hata hivyo, Hitler alijikaza na kumpa mkono akimwambia hongera huku akisisitiza kuwa alishangazwa na mafanikio yake. Aliporudi Marekani kutoka Ujerumani alipokewa na gwaride lililotayarishwa na Meya wa New York, Fiorello LaGuardia.
Wakati akiangalia gwaride, mzee mmoja wa Kizungu alimpa mkoba wa karatasi na alipoufungua alishtuka kuona ndani yake kulikuwa na zawadi ya Dola 10,000 na karatasi iliyokuwa na maandishi ya ‘Ahsante’.
Kauli ya Hitler ilikumbukwa katika harakati za kupinga ubaguzi na unyanyasaji wa polisi zinazoendelea Marekani hivi sasa. Rekodi ya Owens ya kushinda medali nne za dhahabu haikufikiwa hadi 1984 ilipofanyika michezo ya Olimpiki huko Los Angeles, Marekani.
Aliyefanya hivyo alikuwa Carl Lewis wa Marekani ambaye pia ni mwenye asili ya Afrika. Wakati hayo yalipotokea Owens alikuwapo uwanjani kama mtazamaji.
Owens alikipenda Chama cha Republican ambacho sasa kinaongozwa na Rais Donald Trump na kuwaomba watu weusi kujiunga na mara nyingi alihutubia katika mikutano ya kampeni.
Mafanikio ya Owens yalizifanya nchi nyingi zikiwamo za Ghuba kutoa stempu ya picha yake kumheshimu na alipewa tuzo zaidi ya 100 na viongozi wa nchi mbalimbali, kampuni na vyuo vikuu.
Alipostaafu riadha alifanya biashara na kuwa mkurugenzi wa kampuni ya magari ya Ford ya Marekani na kuifanya kazi hadi 1946. Baada ya hapo alifungua klabu ya michezo kwa vijana Marekani wenye asili ya Afrika, lakini baadaye hali yake ya maisha ilibadilika na kumfanya 1965 kuuza mafuta katika kituo kimoja ili kujikimu kimaisha. Baya zaidi lililomtia unyonge ni kufunguliwa mashtaka ya kukwepa kodi.

Hata hivyo, walitokea watu waliomsaidia na serikali ya Marekani ilimchagua kuwa balozi wa michezo na kusafiri katika nchi nyingi. Mwaka 1972 alitoa kitabu kiitwacho ‘I Have Changed’ (Nimebadilika) kilichoelezea masikitiko yake kwa kutounga mkono kwa nguvu harakati za kupinga ubaguzi na kwa kuiunga mkono Republican ambayo viongozi wake hawakuwathamini watu weusi.
Owens alialikwa Munich, Ujerumani katika Olimpiki 1972 na kukutana na kansela wa nchi hiyo, Willy Brandt ambaye alimuelezea kuwa mmoja wa wanamichezo bora waliowahi kuwapo duniani.
Miezi michache kabla ya kifo chake aliongeza uvutaji wa sigara na kuifanya hali yake kuwa mbaya akalazwa hospitali akisumbuliwa na kansa ya mapafu. Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 66 na kuzikwa huko Chicago, Machi 31, 1980.