Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maswali tata kwa England ya Tuchel kabla ya Kombe la Dunia

ENGLAND Pict

Muktasari:

  • Badala ya kujiimarisha, England imeonekana kupoteza uelekeo katika mechi za kirafiki, ikitoa sare ya 1-1 dhidi ya Uruguay kabla ya kufungwa 1-0 na Japan.

LONDON, ENGLAND: WAKATI dunia ya soka ikisubiri kwa hamu fainali za Kombe la Dunia 2026, macho mengi yameelekezwa kwa timu ya taifa ya England, ambayo kwa miaka ya karibuni imekuwa ikipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika mashindano makubwa. Hata hivyo, maandalizi ya mwisho ya kikosi hicho chini ya Kocha Thomas Tuchel yameibua maswali mengi kuliko majibu.

Badala ya kujiimarisha, England imeonekana kupoteza uelekeo katika mechi za kirafiki, ikitoa sare ya 1-1 dhidi ya Uruguay kabla ya kufungwa 1-0 na Japan. Matokeo hayo peke yake hayakuwa tatizo kubwa, bali namna timu ilivyocheza ikiwa butu katika safu ya ushambuliaji na kukosa ubunifu katikati ya uwanja.

Ni kweli iliwakosa nyota wake muhimu kama Harry Kane, Declan Rice, Jude Bellingham na Bukayo Saka, lakini kwa timu yenye wachezaji wengi wa kiwango cha juu, hilo halipaswi kuwa kisingizio. Ukweli unabaki, Tuchel bado anatafuta majibu sahihi kabla ya kipenga cha kwanza cha Kombe la Dunia.

ENG 06

Pengo la Kane

Kwa zaidi ya miaka kadhaa, Harry Kane amekuwa moyo wa safu ya ushambuliaji ya England. Mbali na kuwa mfungaji mahiri, uwezo wake wa kushuka chini, kuunganisha mchezo na kusaidia viungo umeifanya timu kucheza kwa urahisi.

Kutokuwepo kwake kulionekana wazi katika mechi hizi mbili. Dominic Solanke alijitahidi dhidi ya Uruguay, lakini alikosa ule ubora wa mwisho. Dhidi ya Japan, Tuchel alijaribu kumtumia Phil Foden kama mshambuliaji wa kati, jaribio ambalo halikufanikiwa kabisa.

Hii inaacha swali kubwa: je, England wanahitaji mshambuliaji anayefanana na Kane au wabadilishe mfumo mzima wa ushambuliaji? Bila jibu la haraka, timu inaweza kuingia mashindanoni ikiwa na udhaifu mkubwa mbele.

ENG 01

Kitendawili cha Foden

Phil Foden amekuwa nyota mkubwa katika ngazi ya klabu, lakini katika timu ya taifa, bado hajathibitisha ubora wake. Katika mechi hizi mbili, alionekana kupotea, akishindwa kuleta ubunifu au kuathiri mchezo.

Tatizo linaonekana ni nafasi anayochezeshwa. Kumtumia kama namba tisa kunamnyima uhuru wake wa kucheza kati ya mistari na kuunda nafasi. Hali hii inamweka Tuchel kwenye wakati mgumu, kuendelea kumwamini au kuanza kujenga mfumo bila kumtegemea.

ENG 05

Maguire au Stones: uzoefu dhidi ya ubora?

Katika safu ya beki, mjadala mkubwa ni kati ya uzoefu na ubora wa kiufundi. Harry Maguire ameendelea kuwa tegemeo kwa timu ya taifa, akionyesha uimara na uongozi.

Kwa upande mwingine, John Stones ana ubora mkubwa wa kiufundi lakini majeraha yamekuwa kikwazo. Katika mashindano mafupi kama Kombe la Dunia, hali ya utayari ni muhimu kuliko sifa pekee.

Hii inamwacha Tuchel akihitaji kufanya maamuzi magumu kuhusu nani wa kuamini katika mechi muhimu.

ENG 04

Tatizo la mabeki wa pembeni

Soka la kisasa linahitaji mabeki wa pembeni wenye uwezo wa kushambulia na kulinda kwa kiwango sawa, lakini England bado haijapata suluhisho.

Upande wa kulia, Ben White ameonyesha kiwango cha kupanda na kushuka, huku Djed Spence akionekana kuwa na nguvu lakini bado hajakomaa. Tino Livramento naye hajathibitisha ubora wake kikamilifu, huku majeraha ya Reece James yakizidisha tatizo.

Kushoto, Lewis Hall ameonyesha matumaini, lakini bado anahitaji uzoefu zaidi. Hakuna mchezaji aliyejihakikishia nafasi, jambo linaloweza kuwa hatari dhidi ya timu zenye winga hatari.

ENG 03

Namba 10: Bellingham tegemeo pekee?

Nafasi ya kiungo mshambuliaji imekuwa na changamoto pia. Jude Bellingham anaonekana kuwa chaguo bora zaidi, lakini kutokuwepo kwake kumefichua udhaifu mkubwa.

Foden, Cole Palmer na Morgan Rogers walijaribu kujaza nafasi hiyo bila mafanikio makubwa. Hii inaonyesha utegemezi mkubwa kwa Bellingham, hatari kwa timu inayolenga ubingwa.

ENG 07

Rashford vs Gordon: nani aanze?

Upande wa kushoto, ushindani uko kati ya Marcus Rashford na Anthony Gordon. Katika mechi za karibuni, Rashford ameonekana kuwa na makali zaidi, akitumia kasi na uwezo wake wa kupenya.

Gordon ameonyesha juhudi lakini bado hajawa na athari kubwa. Kwa sasa, Rashford anaonekana kuwa mbele, lakini ushindani huu bado uko wazi.

ENG 02

Tuchel ana kibarua kizito

Kwa jumla, maswali haya sita yanaonyesha England bado haijajipanga kikamilifu licha ya kuwa na kikosi chenye vipaji vikubwa. Tatizo si ukosefu wa wachezaji, bali ni mfumo, muunganiko na maamuzi sahihi.

Kwa Tuchel, muda si rafiki tena. Akiwa na miezi michache kabla ya mashindano, anatakiwa kupata majibu ya haraka na sahihi.

Kombe la Dunia halisubiri na historia inaonyesha timu zinazoshinda ni zile zilizo na mwelekeo, uthabiti na maamuzi sahihi kabla ya mashindano kuanza. Ikiwa England itaingia ikiwa na maswali mengi kuliko majibu, basi ndoto yao ya ubingwa inaweza kuyeyuka mapema.

Swali kubwa linalobaki: je, Tuchel ataweza kupata majibu kwa wakati au England itaendelea kuwa timu ya “karibu kufanikiwa” bila kufika kileleni?