Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MASTAA: Modest anataseka asaidiwe, mpenzi wake wa zamani afunguka

Muktasari:

  • Kumbuka Alphonce yupo kitandani kwa miaka mitano sasa, lakini  akiwa na kumbukumbu ya mambo mengi ya sasa na zamani na hapa akifunguka mambo kadhaa, huku mastaa mbalimbali wakiwamo waliowahi kucheza naye enzi hizo, wakiwaangukia Watanzania kujitokeza kumsaidia kwa hali na mali. Endelea...!

TOLEO lililopita tuliona baba mzazi wa beki wa zamani wa kimataifa, Alphonce Modest aliyewahi kuwika na timu za Pamba, Simba, Yanga na Mtibwa Sugar sambamba na Taifa Stars, Mzee Modesti Songoro alivyofunguka mambo mbalimbali kuhusu mwanawe, Alphonce Modest akiwaomba Watanzania wamsaidie ili apate matibabu yatakayomfanya arejee katika hali yake ya kawaida kiafya.

Kumbuka Alphonce yupo kitandani kwa miaka mitano sasa, lakini  akiwa na kumbukumbu ya mambo mengi ya sasa na zamani na hapa akifunguka mambo kadhaa, huku mastaa mbalimbali wakiwamo waliowahi kucheza naye enzi hizo, wakiwaangukia Watanzania kujitokeza kumsaidia kwa hali na mali. Endelea...!


TUKIO ASILOSAHAU

Anasimulia kituko alichokifanya uwanjani; "Timu ya taifa ilikwenda kucheza na Ethiopia, sikuwa na timu wiki nzima kwani sikutaka kwenda kucheza ile mechi, kutokana na changamoto zilizokuwa zinanikabili. Kocha Kayuni alikuwa ananiamini sana, nikaitwa siku moja kabla ya safari, nikaungana na wenzangu, kwanza hali ya hewa ya Ethiopia ilikuwa inanichanganya, nilibanwa na mafua nikitoa kamasi zinatoka damu, kifupi ilitusumbua wachezaji wote na kitendo cha mimi kutofanya mazoezi kilifanya niteseke zaidi.

"Kocha akanipanga nianze kikosi cha kwanza, sasa kuna mchezaji aligundua sipo fiti mashambulizi yakawa yanatokea kwanza, nilipoona nimefanya makosa mara mbili, nikamwambia kocha anitoe akafumba macho kama hanioni, nilichokifanya nikajiangusha, nikatoa viatu nikalala na kujifanya nimezimia, ikabidi anitoe, kwani sipendi kabisa kuwa sababu ya kufungwa, ndiyo maana sikutaka niikosti timu."

Anasema anakumbuka wakati timu ya taifa inaitwa, alitoka kucheza michuano ya Mataifa Huru akiwa na Simba, nchini Afrika Kusini na walishinda mabao 2-0 dhidi ya Sudan.

"Wakati nipo na Simba, Afrika Kusini nilipigiwa simu, kulikuwa na changamoto ya mtu kutaka kuuza uwanja wangu, ndiyo maana nikataka nipate muda wa kushughulikia hilo, ingawa kocha Kayuni akaamua kukomaa na mimi hadi mwisho," anasema Modest ambaye katika maisha yake ya uchezaji aliwahi kupata kadi nyekundu moja tena ya kusingiziwa kwa kosa la mchezaji mwenzake akiwa Simba.


KIKOSI CHA ZAMANI

Kikosi cha Modest kwa wakati wote enzi akicheza anakipanga namna hii; Mohamed Mwameja, Deo Mkuki, Kenneth Mkapa, Mustapha Hoza, George Masatu, Hussein Masha, Nico Bambaga, Sekilojo Chambua, Said Mwamba 'Kizota/Madaraka Seleman 'Mzee wa Kiminyio', Nteze John na Edibily Lunyamila, huku kocha akiwa ni Sunday Kayuni.

Alipoulizwa akipange kikosi cha sasa kwa jinsi anavyoifuatilia Ligi Kuu akiwa kitandani, Modest huku akitabasamu anakitaja hivi; Moussa Camara, Yao Kouassi, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Ibrahim Bacca, Abdulrazack Hamza, Yusuph Kagoma, Clatous Chama/Debora Fernandes/Aziz Ki/Pacome Zouzoua.

"Hapo yeyote anaweza kuanza, mfano Leonel Ateba akishambulia, nyuma yake anaweza akasimama Pacome, kulia Aziz Ki na kushoto Chama. Sijamuanzisha Djigui Diarra kwa sababu atapewa changamoto na Camara, kiungo sijamuweka Jonas Mkude kwani kwa sasa hachezi mara kwa mara, ila akiwa katika piki lazima ataanza kikosi cha kwanza," anasema Modest.


MASTAA WAOMBA ASAIDIWE 

Zamoyoni Mogella ambaye ni staa wa zamani anasema Modest aliipenda sana klabu ya Wanamsimbazi: “Modest kuichezea Simba haikuwa kazi pekee, bali aliipenda na aliitumikia kwa moyo, niwaombe viongozi kuliangalia jambo hilo, namna ya kumsaidia mchezaji wao wa zamani.

“Pia kaichezea Stars kwa miaka tisa,naamini Watanzania ni wakarimu watafanya jambo kwa ajili yake,nimeona katika gazeti lenu, wanaonekana familia wana hali ngumu, inayohitaji msaada zaidi.

“Binafsi nitafanya hivyo kwa kile nitakachojaaliwa, kuona namshika mkono, ili mradi asipungukie pesa ya kula na vitu vingine vidogo, inaumiza mtu alikuwa na nguvu zake, alikuwa anajitafutia mwenyewe, leo hii yupo kitandani anasubiri asaidiwe kila kitu, maradhi yanaweza yakamkuta binadamu yeyote, hivyo leo yamemkuta Modest hatujui kesho nani atapitia changamoto nyingine.”

Kiraka wa zamani wa Simba, Steven Mapunda anasema kuna kila haja ya kumsaidia Modest, ili kupata pesa za matibabu na matumizi yake, kutokana na hali yake ya sasa.

“Baada ya kuona gazeti la Mwanaspoti, hali yake imenisikitisha sana, napanga safari kuja jijini Dar es Salaam, ili nikazungumze na wadau, ambao naamini waweza wakafanya jambo kwa Modest.

“Vijana wa sasa ni ngumu kumfahamu, nimecheza naye Simba na Stars, alikuwa mchezaji mkubwa na mwenye heshima yake,nilipoona hali yake imeniumiza naona anahitaji vitu vingi vya kumsaidia.”

Mdau wa soka kutoka Moshi, anayejulikana kwa jina la Felix Kauta alichapisha bango lililokuwa linasomeka ‘Save Alfonce Modest’ huku akieleza jinsi anavyomkumbuka wakati anacheza.

“Namkumbuka Modest walivyotwaa taji la Challenji mwaka 1994 akiwa na Taifa Stars pia Stars ilivyoifunga Sudan mabao 2-0, alikuwa na msaada mkubwa sana kwa taifa lake, nawaomba wadau kumsaidia mwenzetu, pia nalishukuru gazeti la Mwanaspoti kuibua hali yake,” anasema.


MTIBWA SUGAR WAMZUNGUMZIA

Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mtibwa Sugar, Jamal Byser anasema: “Ni mchezaji wa kuigwa licha ya vijana wengi wa sasa hawajamuona, ila ni kati ya wachezaji bora waliowahi kutokea Tanzania, alikuwa anaji tolea sana kwa ajili ya timu, popote anapokuwepo amani inatawala, alipenda kuwaona watu wanacheka.

“Modest alistaafu akiwa na kiwango cha juu, aliniambia kiongozi nimecheza kwa muda mrefu naipisha damu changa, aliyekuja kumrithi nafasi yake, alikuwa Idris Rajabu.

“Uongozi uliona umefanya naye kazi nzuri, ukampa kazi kiwandani sehemu ya ulinzi kama Afisa ulinzi, hadi pale alipoona hawezi tena anapaswa kurejea kwao Kigoma.”


HASSAN DALALI ANENA

Kipindi Modest anajiunga na Simba, Hassan Dalali alikuwa mwenyekiti wa matawi Mkoa wa Dar es Salaam, anamzungumzia akisema, “alikuwa beki hatari,alipendwa na mashabiki, mcheshi, alijitoa kwa ajili ya timu, ndio maana Yanga waliona anaweza akawasaidia wakamwazima, kikubwa tunamuombea Mungu amponye maradhi yake.”


MPENZI WAKE WA ZAMANI

Baada ya Modest kukiri alimuumiza aliyekuwa mpenzi wake wa zamani Mwanaspoti lilimtafuta mwanamke huyo aliyejitambulisha kwa jina la Hadija Kanyowe, alikuwa na haya ya kusema:

“Mapenzi yetu yalianzia utotoni, familia yake ilinifahamu, nikaja nikaumia baada ya kuanza kupata umarufu kumpenda mwanamke mwingine, sikukata tamaa nikawa namfuata na kumshauri.

“Ni mwanaume ambaye nilimpenda sana, nilitamani muda wote nikae karibu naye, hata baada ya kurejea Kigoma akiwa anaumwa nilienda kumuona, nikampa moyo kwamba atasimama tena.

“Nina mtoto ila sijaolewa, niliwahi kwenda kuiomba familia yake nikamuuguze, lakini mhusika alikataa, niseme ukweli moyo wangu ni mweupe kwake, ikitokea akanikubali hata sasa nipo tayari kumchukua na kuishi naye kwangu.

“Ninachotamani ni kumuona baadhi ya viungo vyake vinafanya kazi, ili aweze kujisaidia baadhi ya mambo mwenyewe, mimi naishi mtaa wa Kilima Hewa, naweza kutembea kwa bodaboda natumia Sh.1500, lakini tofauti na ningekuwa naishi naye, kwa upande wangu sijali ndugu, natamani kuona ana furaha.

“Huwa nikienda tunaanza kutaniana mambo ya zamani, namwambia atainuka tena, namwambia napenda kumuona karibu yangu, yote hayo nafanya ili asijisikie vibaya.”


MWANASAIKOLOJIA

Mwanasaikolojia Charles Nduki, anasema: “Jambo lingine kupitia imani yake, wanapaswa kumjenga kuamini Mungu ana nguvu zaidi ya binadamu, anaweza akamrejeshea alivyopoteza, wanaoenda kumtembelea wasionyeshe sura za huzuni, badala yake tumaini la kumuonyesha atavuka hali aliyo nayo.

“Asikilize zaidi vitu vinavyoleta matumaini, iwe katika redio, mazungumzo ya watu wanaomzunguka, akiangalia move ziwe zile za ushindi na siyo za kuibua huzuni moyoni mwake.

“Kwa upande wa mahusiano kama amekimbiwa basi, anapaswa kukubaliana na ukweli, kisha awaweke karibu wanaomtengenezea furaha itakayofanya asahau, ama kama kuna mpenzi mwingine yupo naye amuonyeshe anampenda na anamtegemea siku moja atarudi katika hali ya kawaida hilo ni muhimu zaidi, pia hapaswi kuzingatia watu wanamuonaje isipokuwa yeye anajionaje.”


USHAURI WA DAKTARI

Mmoja wa madaktari aliyewahi kumuuguza kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kumshauri kurejea Kigoma kupumzika alisema: “Mgonjwa aliyepooza, unapaswa kumchua katika vifundo vya miguu na mikono na kumnyoosha nyoosha mikono, hiyo ndio tiba yake ya kujisikia vizuri.”

MWISHO