Mastaa hawa wamemaliza msimu mapema!

Muktasari:
- Kuna wachezaji wamemaliza msimu mapema kutokana na sababu mbalimbali huku wengine wakiwa wanaandamwa na majeraha yanayowaweka nje na wengine wanakumbwa na adhabu kutoka timu zao.
KUNA mastaa Ligi Kuu Bara wameanza kula bata kabla ya msimu wa 2024/25 kutamatika Juni 22, mwaka huu kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).
Ipo hivi. Kuna wachezaji wamemaliza msimu mapema kutokana na sababu mbalimbali huku wengine wakiwa wanaandamwa na majeraha yanayowaweka nje na wengine wanakumbwa na adhabu kutoka timu zao.
Mwanaspoti linakuletea nyota ambao wameanza mapumziko huku wengine wakijiuguza majeraha ili kujipanga na msimu mpya.

BENO KAKOLANYA
Kakolanya amemaliza msimu mapema baada ya kusimamishwa kwa kile kinachodaiwa ni utovu wa nidhamu huku akisubiri hatma yake baada ya suala lake kupelekwa kamati ya maadili. Mchezaji huyo anaitumikia Namungo kwa mkopo msimu mmoja akitokea Singida Black Stars ambapo mkataba na Singida Black Stars unamalizika mwisho wa msimu.
Mara ya mwisho kipa huyo kukaa langoni ilikuwa Februari 5 kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Tabora United ugenini ambapo Namungo ilikubali kichapo cha mabao 2-1. Tangu ajiunge na timu hiyo mwanzoni mwa msimu huu, Kakolanya amecheza mechi nane za ligi akishuhudia ikishinda moja, sare moja na kupoteza tano. Matokeo ya mechi hizo ni Tabora 2-1 Namungo, KenGold 2-3 Namungo, Kagera Sugar 1-1 Namungo, Namungo 0-2 Yanga, Mashujaa 1-0 Namungo, Singida BS 2-0 Namungo, Dodoma Jiji 1-0 Namungo na Namungo 0-2 Dodoma Jiji.
YACOUBA SONGNE
Majeraha yamekiweka rehani kibarua cha staa wa zamani wa Yanga, Yacouba Sogne baada ya upasuaji wa goti Morocco kukamilika akarejea nchini kwao Burkina Faso ili kujiuguza na atakuwa nje ya msimu wote.
Yacouba ambaye alitua Tabora United msimu huu akitokea AS Arta Solar ya Djibouti, alisaini mkataba wa mwaka mmoja ambao unakwisha mwezi huu atakosa mechi 10 za ligi.
Msimu huu kaichezea Tabora United katika mechi 13, akifunga mabao manne tangu alipoumia Novemba 29, 2024 kwenye mchezo wa ugenini dhidi ya KMC ambao alifunga bao la kwanza dakika ya 41 kwenye ushindi wa mabao 2-0 katika Uwanja wa KMC Complex.

KOUASSI YAO
Yao aliyekuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu kutokana na kuumia nyama za paja, alianza mazoezi na wenzake, lakini alijitonesha na kumfanya aendelee kukosekana uwanjani, huku ikielezwa kuwa mechi zilizosalia za kufungia msimu sio rahisi kuziwahi tena.
Beki huyo raia wa Ivory Coast amekuwa akiandamwa na majeraha tangu kuanza kwa msimu huu na kumfanya atumike katika mechi saba za Ligi Kuu timu hiyo inayoongoza msimamo, ambapo pengo lake limezibwa na Israel Mwenda aliyeingia dirisha dogo na wakati mwingine Kibwana Shomari.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinaeleza Yao ni kama hatacheza tena msimu huu baada ya kujitonesha jeraha hilo lililokuwa limeanza kupona.
Kibwana hadi sasa ametumika katika mechi saba kati ya 25 akitumia dakika 533 akitoa asisti moja, wakati Mwenda amecheza mechi nane akitumia dakika 675 na kufunga mabao mawili bila kuwa na asisti yoyote.

JOHN NOBLE
Kipa wa Fountain Gate, raia wa Nigeria, John Noble amesimamishwa kutokana na kufanya makosa mara kwa mara langoni na anadaiwa kuwa ameshaondoka ndani ya kikosi hicho, ingawa atarejea ili kujua hatima yake kama ataendelea kusalia au la.
Hatua ya kipa huyo kuondoka ilijiri baada ya makosa mawili aliyodaiwa kuyafanya katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga iliyopigwa Aprili 21, 2025, jambo lililosababisha kupelekwa kwenye kamati ya maadili ya klabu hiyo ili kujibu tuhuma zinazomkabili. Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Manyara, Noble aliruhusu bao la Clement Mzize dakika ya 38 baada ya kuutema mpira uliopigwa kichwa na Prince Dube aliyeunganisha frii-kiki iliyopigwa na Stephane Aziz KI.
Noble anasema kwa sasa hayupo katika timu hiyo kwa sababu ameenda kupumzika kutokana na presha kubwa aliyopitia kisha atarejea ili kujua hatima yake. Mwanaspoti linatambua mchezaji huyo anayemaliza mkataba mwisho mwa msimu huu hataongezewa tena licha ya kuwapo kwa kipengele kinachoruhusu kuongezewa, huku ikielezwa viongozi hawana mpango wa kuendelea naye msimu ujao.

ADOLF MTASINGWA
Panga pangua kikosi cha kwanza cha Azam FC amekuwa mhimili kwenye safu ya kiungo cha ulinzi tangu ajiunge na timu hiyo na hatakuwa sehemu ya dakika 270 za mechi zilizobaki kumalizia msimu kwani tayari ameshauaga.
Kiungo huyo aliumia mfupa mdogo wa kidole kidogo cha mguu na kufanyiwa upasuaji mdogo ikitazamiwa jeraha lake litapona wiki ya sita tangu kuanza kwa matibabu. Mara ya mwisho kiungo huyo mkabaji kucheza ilikuwa Februari 15, mwaka huu dhidi ya Mashujaa ambapo walishinda 2-0 katika Ligi Kuu Bara.
Tangu aumie amekosekana kwenye mechi nane kati ya hizo Azam imeshinda tatu sare tatu na vipigo viwili dhidi ya Coastal Union 0-0, Simba 2-2, Namungo 1-1, ushindi dhidi ya Tanzania Prisons 4-0, KenGold 2-0, Kagera Sugar 4-2 wakati vipigo ni Yanga 2-1 na Singida Black Stars 1-0.

ABDALLAH MASOUD ‘CABAYE’
Baada ya KenGold kushuka daraja ikiwa na mechi tatu mkononi na kukiri kuwa Abdallah Masoud ni sehemu ya wachezaji waliosimamishwa kwa kosa la utovu wa nidhamu imebainika kuwa licha ya wenzake kurudi kumalizia mechi zilizobaki yeye hatakuwa sehemu ya timu hiyo.
Chanzo cha kuaminika kutoka kwa rafiki wa karibu wa mchezaji huyo kimeliambia Mwanaspoti kuwa Cabaye amegoma kurudi akidai kuwa anahitaji kujipa mapumziko na kujiepusha na kupata majeraha mechi chache zilizobaki.

AISHI MANULA
Msimu wa 2017-2018, Simba ilimsajili Aishi Manula akitokea Azam akafanikiwa kuwa namba moja kwa misimu sita mfululizo kabla ya uliopita na huu mambo kuwa magumu.
Manula ambaye anashikilia rekodi ya kuwa kipa aliyeshinda tuzo nyingi za Ligi Kuu Bara (5), amekosa kucheza kikosi cha kwanza tangu aliposajiliwa Ayoub Lakred kutokea FAR Rabat ya Morocco msimu uliopita. Ujio wa Moussa Camara kutoka AC Horoya ya Guinea msimu huu ukaongeza balaa zaidi kwa kipa huyo mzawa ambaye hajacheza mechi yoyote ya mashindano kati ya 49. Mara ya mwisho Manula kusimama langoni Simba ilikuwa Agosti 31, 2024 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Al Hilal uliomalizika kwa sare ya bao 1-1. Pia alikaa benchi Aprili 13, 2025 Simba ikishinda 2-1 dhidi ya Mbeya City hatua ya robo fainali ya Kombe la FA. Mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.

GEORGE MPOLE
Licha ya kwamba usajili wake Kagera Sugar umekwamishwa, bado haijafahamika hatima ya George Mpole kwani hajarejea Pamba Jiji ya Mwanza. Jambo hilo linaacha maswali kuhusu mustakabali wa mshambuliaji huyo.
Mpole ni mchezaji halali wa Pamba Jiji baada ya kujiunga akitokea FC Saint Eloi ya DR Congo na ilipanga kumpeleka kwa mkopo Kagera Sugar, lakini mambo hayakwenda vizuri kwa sasa haijulikani yupo wapi.

SAMSON MBANGULA
Mchezaji huyo msimu uliopita aliifunga Simba mabao mawili katika mchezo wa kwanza wa ligi uliopigwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro uliomalizika kwa Prisons kushinda 2-1. Mara ya mwisho kuonekana uwanjani katika kikosi hicho ilikuwa Oktoba 26, 2024 timu yake ilipofungwa mabao 2-1 na KMC katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya na baada ya hapo hajacheza tena kutokana na maumivu ya goti la kulia. Kutokana na ukubwa wa majeraha hayo, nyota huyo amelazimika kufanyiwa upasuaji utakaomfanya arejee uwanjani, Julai, mwaka huu.