Beki Yanga azungumzia ishu ya kutumia dawa za kulevya

Muktasari:
- Mwanaspoti linakutana kwa mazungumzo na mmoja wa mastaa wa Yanga ambaye pia jina lake lipo kwenye kumbukumbu nzuri za timu ya taifa 'Taifa Stars.
JUA linawaka polepole katika viunga vya Kianga, Unguja, Zanzibar kwenye kona ya uwanja wenye majani yaliyonawiri
Mwanaspoti linakutana kwa mazungumzo na mmoja wa mastaa wa Yanga ambaye pia jina lake lipo kwenye kumbukumbu nzuri za timu ya taifa 'Taifa Stars.
Hata hivyo, ndani ya mazungumzo hayo, ishu kibao zinaingia ikiwamo namna soka la Bongo linavyosonga kwa kasi, lakini katikati anagusia ishu ya dawa za kulevya, suala ambalo limemuachia mateso makubwa moyoni.
Mazungumzo hayo yanamhusisha beki wa zamani wa Yanga na timu ya taifa la Tanzania (Taifa Stars), Haji Mwinyi Ngwali na waandishi wa makala haya.
Hapatoshi. Mahojiano haya hayafanyiki hotelini wala studio ya runinga, bali ni mazungumzo katika uwanja uleule aliokuwa akicheza akiwa peku kipindi ambacho akiwa na miaka 15.
"Hapa ndipo nilipoanza ndoto zangu. Hapa ndipo nilifukuzia ndoto zangu za kuichezea Yanga. Mnavyoniona leo na maumivu yangu yote bado hii ardhi inanipa nguvu ya kuendelea kuamini,” anasema Haji huku akitazama kwa mbali vile uwanja huo ulivyokeuka kuwa pori.
Ndivyo yalivyoanza mahojiano hayo na mchezaji huyo ambaye bado ana ndoto, lakini amepitia maumivu, shutuma, vikwazo na aibu ambayo si wengi wanaweza kuivumilia.

Katika mahojiano hayo Haji amefunguka kwa ujasiri kuhusu hali yake ya sasa, historia ya soka, majuto, mafanikio na ndoto za kurejea tena kwenye soka la ushindani.
PLUIJM ALITOA GIZANI
Kwa sauti ya heshima, Haji anamtaja Hans van der Pluijm kuwa kocha aliyemtoa gizani, akamvusha bahari hadi Bara akisema alikuwa kocha asiyeangalia jina, bali uwezo na nidhamu ya mchezaji.
“Yule mzee hakuniita kwa bahati. Aliniona, akanifuatilia. Alinipa nafasi. Yeye ndiye aliyenivusha (bahari),” anasema kwa msisitizo huku macho yakionyesha shukrani isiyoisha.
Pluijm hakuwa tu kocha, bali mlezi na msimamizi wa vipaji. Aliona mbali kuliko wengine. Haji anasema mara ya kwanza alipofika kambini, kocha huyo alimwita pembeni na kumwambia, "kijana wewe ni zaidi ya unavyojiona. Jifunze, vumilia, fanya kazi."
Kauli hiyo anadai ilimjenga na kumfanya ajione kuwa na thamani licha ya kutoka katika mazingira ya kawaida.
Kwa Haji, mafanikio ya Yanga kati ya 2015 hadi 2017 hayawezi kuzungumzwa bila kumtaja Pluijm akisema kocha huyo alijenga timu kwa msingi wa nidhamu, mshikamano wa ndani na maadili na kwamba hakuvumilia uvivu wala majivuno.

ISHU YA MADAWA
Kwa Haji mojawapo ya sehemu ngumu zaidi katika maisha yake ni pale jina lake lilipoanza kuhusishwa na matumizi ya dawa za kulevya. Hakuwahi kutiwa hatiani wala kukamatwa, lakini kelele mitandaoni zilitosha kumuumiza kisaikolojia.
"Maisha yangu yalichafuka, watu waliniona kama mlevi wa dawa. Kisa? Maisha yangu yalibadilika tu si kila anayepotea uwanjani ni mlevi. Wengine tunavamiwa kwa majungu. Mpaka leo siwezi kumsamehe mtu aliyeniweka kwenye hiyo picha chafu. Kwa maneno yake tu, aliharibu jina langu akawafanya hata wazazi wangu wakose raha,” anasema mkongwe huyo.
Haji anasema shutuma hizo zilianza kuibuka wakati akiwa Yanga na aliwahi kupelekwa kupimwa (iwapo anatumia dawa hizo) na hakuwahi kukutwa na hatia, lakini anakumbuka vile habari hizo zilivyosambaa na kuandikwa katika gazeti na hadi leo ametunza nakala ya gazeti husika.
"Yule mwandishi siwezi kumsamehe, huo ndio ukweli," anasema.

MIMI NI YULE YULE
Kwa wale waliovunjwa moyo na kupotea kwake kwenye ramani ya soka, Haji anawaambia kwa sauti ya matumaini kwamba bado yupo sana tu.
“Ninarudi. Naomba wanishike mkono. Waache kusikiliza maneno ya mtaani. Mimi bado ni Ngwali wa Jangwani.”
Haji anasema hakupotea kwa sababu alichoka, bali kwa sababu maisha yalimbadilisha mwelekeo ghafla. Aliumia, alipoteza fomu, akakumbana na changamoto binafsi, lakini hakuwahi kupoteza mapenzi yake kwa mpira.
Anasema alibaki akijifua akisubiri muda wake urejee. Wengi walimtenga, wachache walibaki na anawashukuru waliobaki.

SIMBA WAMEVUKA MALENGO
Haji anaisifu Simba kwa kiwango ilichoonyesha katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambayo ilipigwa kwenye Uwanja wa New Amaan mjini humo, akisema: “Simba wamevuka malengo yao. Walianza msimu wakiwa na lengo la kufika nusu fainali, lakini leo hii tunazungumza timu iliyocheza fainali ya CAF. Hili ni jambo la kihistoria, si kwa klabu yao tu bali hata kwa Tanzania.”
Anasema kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wa Simba katika fainali hiyo kilikuwa cha kimataifa na kwamba licha ya kadi nyekundu kwa kiungo wake Yusuph Kagoma, bado timu haikuyumba.
“Kadi haikutarajiwa, lakini hawakupaniki. Walicheza kwa nidhamu na kuonyesha kwamba waliandaliwa vizuri. Tshabalala (Mohammed Hussein) kila mechi anaendelea kuwa bora zaidi. Huyu ni mchezaji wa fainali,” anasema. Hata hivyo, Haji anawataka wachezaji wa Simba kutoridhika na hatua hiyo, bali kuifanya iwe mwanzo wa mafanikio mengine makubwa siku za usoni.

MAKAPU NA NINJA
Katika chumba cha kubadilishia nguo Jangwani, Haji alijenga udugu wa kweli na baadhi ya wachezaji waliokuwa zaidi ya marafiki kwake akiwakumbuka zaidi Said Makapu na Abdallah Shaibu 'Ninja' kila wakati siyo kwa sababu walikuwa wakali uwanjani, bali namna walivyokuwa bega kwa bega nje ya uwanja.
“Tulililia mpira pamoja. Tulishinda, tukafungwa, tukafukuzwa kambini. Tulikula pamoja. Wale sio marafiki ni ndugu,” anasema Haji akieleza kuwa urafiki wao ulikuwa zaidi ya matokeo ya uwanjani.
Haji anakumbuka siku moja baada ya kufungwa mechi ya kimataifa walikaa wote watatu hadi usiku kambini wakitafakari walikosea wapi. “Makapu alisema ‘bora tushindwe kwa damu kuliko kwa kutojituma’ maneno hayo yalinijenga sana,” anasimulia kwa uchungu. Urafiki wao ulikuwa wa uhalisia hawakufichana ukweli na walikosoana kwa upendo.
Leo hii, kila mmoja akiwa na njia zake maishani, Haji anasema uhusiano huo haujapotea. Bado wanawasiliana, huombeana dua na humtaja Mungu wakiamini kuwa udugu wa mpira ni zawadi adimu isiyopimika kwa fedha.
UMAARUFU UNACHANGANYA
Haji anakumbuka kipindi ambacho jina lake liliitikisa mitandao ya kijamii na mitaani akidai zimu zilipigwa kila wakati, hasa kutoka kwa wanawake. “Nilikuwa sina mke, lakini maisha yale yalikuwa hatari. Simu zaidi ya 20 kwa siku. Ukikosa nidhamu unapotea,” anasema huku akitabasamu kwa mbali.
Anasema kuna kipindi alitamani kuzima simu kwa wiki nzima ili apumzike kutopokea ujumbe. “Umaarufu hauji na mwongozo. Nilijifunza kwa maumivu. Rafiki zako wanabadilika, maadui wanajifanya marafiki. Ukiwa huna msimamo unaanguka,” anasema. Alijifunza kumwamini kocha, familia na wachache waliomtakia mema bila kuelemewa na mbwembwe za umaarufu wa ghafla.
NDOTO HAITAFUTIKA
Nyota huyo anakumbuka kwa fahari siku alipoitwa Taifa Stars mara ya kwanza ikiwa ni wiki chache baada ya kutua Yanga. Ilikuwa siyo tu ndoto yake, bali ya mtaa aliotoka, familia, walimu na kila aliyemuona akicheza katika viwanja vya vumbi.
“Nilihisi kama ndoto. Kuvaa jezi ya taifa ni heshima. Niliipigania. Sikutegemea huruma, niliistahili,” anasema kwa sauti ya kujivunia.
Haji anakumbuka aliambiwa asitegemee nafasi kwa jina kikosini, bali kwa juhudi akilazimika kufanya mazoezi ya ziada na kuwa na mipango ya lishe na usingizi.
Kutokana na hilo kila mechi ya ligi alijituma kana kwamba alikuwa akiwania nafasi ya kwanza maishani na ndiyo maana ndoto ya kuvaa jezi ya taifa haikujengwa kwa bahati, bali kwa jasho na uvumilivu.
KUONDOKA KWA AZIZ
Licha ya mchango mkubwa wa Stephanie Aziz Ki tangu alipojiunga na Yanga 2022 akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast, Haji anasema klabu hiyo haina sababu ya kuogopa au kujiona dhaifu kwa kuondoka kwake kwenda kujiunga na Wydad Casablanca ya Morocco kwa kuwa bado ina hazina kubwa ya vipaji.
“Yanga haiwezi kuwa na pengo la Aziz Ki. Ameondoka akiwa ameacha alama kubwa, lakini wapo wachezaji wenye uwezo mkubwa ambao wanaweza kuvaa viatu vyake,” anasema.
Haji anasema wachezaji wanaoweza kurithi majukumu ya Aziz Ki ni Pacome Zouzoua na Clatous Chama akieleza kuwa wawili hao wamewahi kuonyesha viwango vya juu katika mechi muhimu na wana uzoefu wa kutosha wa michuano ya ndani na kimataifa.
“Zouzoua ana uelewa mzuri wa mpira, anapiga pasi za mwisho kwa akili na ana uwezo wa kufunga. Chama naye tumemuona mara nyingi akiwa Simba ni mchezaji wa mechi kubwa. Sasa akiwa Yanga atakuwa na nafasi ya kuonyesha makali zaidi,” anaongeza.
Zouzoua ambaye amekuwa akishambulia akitokea pembeni msimu huu amefunga mabao tisa na kutoa asisti nane katika Ligi Kuu, wakati Chama aliyewahi kuibeba Simba katika mechi nyingi kubwa za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho CAF anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji bora namba 10 katika ukanda wa Afrika Mashariki.
CHANGAMOTO ALGERIA
Haji anazungumzia pia changamoto walizokutana nazo akiwa na Yanga nchini Algeria ambapo anasema, “nchi tuliyokutana na changamoto ambazo sitazisahau kwenye maisha yangu ya soka ni Algeria kwani tutiliwa dawa vyumbani ambazo zilikuwa maalumu kwa ajili ya kupunguza nguvu.
"Ukiachana na hilo pia marefa walikuwa hawapo pamoja na sisi. Kila tulipokuwa tunaenda kucheza tulikuwa tunakutana na figisu.”