Prime
Hivi Arajiga alisomea uamuzi na wakina nani!

Muktasari:
- Yaani thamani yake hupungua kadri mkataba unavyoelekea mwisho na wahasibu huangalia kama uwepo wake umechangia klabu au kampuni kupata faida au hasara.
KATIKA vitabu vya fedha vya klabu barani Ulaya wachezaji huingizwa kama mali na huduma yake hupimwa kama vile mali nyingine zinavyopimwa, hali kadhalika faida na hasara za mali hiyo huonekana mwishoni mwa msimu au wa mkataba wake.
Yaani thamani yake hupungua kadri mkataba unavyoelekea mwisho na wahasibu huangalia kama uwepo wake umechangia klabu au kampuni kupata faida au hasara.
Na ndio maana suala la kupanua fainali za Klabu Bingwa ya Dunia lilipata upinzani mkubwa kutoka klabu za Ulaya, ambazo zinasema mashindano hayo yameongeza mechi na hivyo kuweka afya za wachezaji hatarini, kitu ambacho klabu hizo zinasema zitaathirika iwapo wachezaji watamaliza wachovu na pengine wenye majeraha na hivyo ufungaji hesabu utakuwa mgumu.

Lakini tabia za binadamu kama bidhaa (human commodity) hutofautiana sana na bidhaa nyingine. Ukiingiza chupa za soda kiwandani zitatoka zikiwa na kichwa kilichofanana kwa kila kitu, kuanzia ladha hadi virutubisho au vitu vilivyowekwa ndani. Huwezi kwenda dukani halafu ukamuomba muuza duka akuwekee soda, ili uchague iliyo nzuri kuliko nyingine.
Unaagiza aina ya soda unayotaka na kueleza kama ni baridi au la na unakunywa bila ya tatizo, labda chupa iwe imevunjika kidogo au haina gesi.
Tabia hizo za bidhaa ni tofauti na binadamu. Ukiwaingiza binadamu 30 darasani kwa ajili ya kozi fulani, watamaliza wakiwa na uelewa na ufaulu tofauti. Wapo watakaofeli kabisa, wapo watakaopata wastani na wapo watakaokuwa bora.

Huwezi kujifananisha akili na mtu uliyesoma naye kozi moja na mwaka mmoja eti kwa sababu tu umeona amefanikiwa sehemu fulani katika ajira yake. Ubidhaa wa binadamu ni tofauti kabisa.
Wapo wachezaji wanaoanza shule za soka wakiwa watoto wadogo kabisa, lakini wapo waliohitimu wakiwa na uwezo tofauti. Si kwamba Lamine Yamal alikuwa darasani peke yake, lakini talanta yake na mafunzo aliyoongezewa, juhudi za kutaka kumuelewa mwalimu, zimemfanya awe tofauti.
Ndivyo ilivyo kwa Ahmed Arajiga, mwamuzi aliyetokea kuwa maarufu katika siku za karibuni akipanda ngazi kutoka mwamuzi wa kawaida hadi kuanza kutumiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) katika mechi kubwa.

Amejitenga na waamuzi wengi wa Tanzania kutokana na kufanya kazi yake kwa weledi bila kushawishika na shinikizo kutoka nje, hasa klabu kubwa za Simba na Yanga ambazo zinatuhumiwa kutumia kila aina ya mbinu uamuzi uende upande wao.
Yale maneno ‘makosa ya kibinadamu’ yaliyogeuzwa kuwa dhihaka, yanatumika kwa usahihi pale Arajiga anapokosea. Lakini kwa mwamuzi ambaye anaonekana amezoea kufanya makosa lakini yanayonufaisha timu moja, maneno hayo hutumika kama dhihaka.
Kwa hiyo tutakosea sana kuanza kuuliza “kwani Arajiga alipata mafunzo na kina nani?” kutokana na kuona ni nadra sana kumpata mwamuzi anayemkaribia katika kizazi cha sasa cha waamuzi.
Kwa maneno yake, Arajiga anasema ni afadhali atukanwe kwa kutenda haki kuliko kutukanwa kwa kutenda hila. Huo unaweza kuwa ndio muhtasari wa falsafa zake, kwamba atasimamia haki wakati wote bila ya kujali wanaomuangalia wanasemaje.
Wakati mwingine unajiuliza hivi hawa waamuzi wengine hawaoni jinsi Arajiga anavyojijengea umaarufu kutokana na kufanya kazi yake kwa usahihi, weledi na kujituma? Hivi hawaoni kitu cha kuiga kutoka kwake?
Au wanafanya makosa mfululizo kutokana na kushirikishwa katika mipango ya nje ya uwanja na hivyo wanajua hawawezi kuadhibiwa? Ndio maana kama kiongozi wa Shirikisho au Bodi ya Ligi amehusika kumuunganisha mwamuzi na viongozi wa klabu, huyu ataweka kiburi pale atakapofanya makosa.
Pamoja na ukweli kwamba ubidhaa wa binadamu ni tofauti na bidhaa nyingine, bado tunahitaji kuzalisha waamuzi wa angalau nusu ya kiwango cha Arajiga ili kuunusuru mchezo wa mpira wa miguu na kadhia, karaha na zaidi ya yote kuporomoka.

Ni lazima wenye mamlaka waone kwamba mpango wa kuwapandisha vijana hawa wadogo hadi kuchezesha Ligi Kuu ili waache alama (legacy) umeharibika na hivyo warudi katika kuupa mchezo sifa badala ya sifa zao binafsi.
Alama inaachwa kwa utendaji bora kama ambavyo Arajiga anafanya. Anatenda haki na watu wanakubali uwezo wake, hali ambayo itamfanya aache alama iwapo hatabadilika huko mbele.
Wenye mamlaka hawana budi kuhakikisha waamuzi wetu wanapata mafunzo maalumu ya kurekebisha kile kilichoonekana msimu huu, yaani mijadala ya kila wiki kuhusu makosa ya waamuzi na tuhuma za upendeleo.
Ni muhimu kwa Kamati ya Waamuzi kuandaa programu ya kuboresha viwango vya waamuzi ili tuzalishe waamuzi bora. Kama Eritrea, Somalia, Gambia na Comoro zinaweza kutoa waamuzi wenye viwango bora Afrika, Tanzania inashindwaje?
Lakini wakati hayo yakiendelea ni muhimu pia ukafanyika uchunguzi wa makosa yaliyofanyika msimu huu ili kutafuta tiba sahihi. Yawezekana kabisa waamuzi wanaofanya makosa hayo wanajua kuwa wanachofanya si kizuri, lakini tamaa na shinikizo kutoka nje linawasumbua.

Hizi adhabu za kuwafungia miezi miwili au mitatu zimeshazoeleka na huenda huzifanya kwa makusudi ili wapate muda wa kupumzika.
Hao wanakwenda tofauti na msimamo wa Arajiga. Kwamba wako tayari watukanwe kwa kutotenda haki. Ukishakuwa na waamuzi wenye msimamo huo unaweza kuwa na ligi bora?
Tunahitaji waamuzi wenye msimamo kama Arajiga ambao watafikia angalau nusu ya kiwango chake ili tuwe na waamuzi bora watakaopunguza kero na karaha inayozalishwa kila wiki.