Mastaa hawa ushindi upo mikononi mwao

TAYARI Ligi Kuu Bara imechanganya. Timu zote zimecheza mechi sita na kuvuna kile walichokipanda hadi kufikia sasa ikiwa ni ligi dume yenye timu 16 tu.

Mwanaspoti linakuletea uchambuzi wa mastaa wa kila timu ambao kwa kiwango walichokionesha hadi sasa, ni dhahiri ndio wameshika kwa kiasi kikubwa matokeo ya timu zao na jukumu limebaki kwao kuchagua kusuka au Kuonyoa.


YANGA

Msimu huu wako moto kila idara lakini kiufupi mabomu yao ya kumaliza mechi yapo kwa kipa Djigui Diara, viungo Kharid Aucho, Yannick Bangala na Feisal Salum ‘Fei Toto’ pamoja na mshambuliaji Fiston Mayele.

Licha ya kwamba kila mchezaji ana mchango kwenye kuipa Yanga ushindi lakini wachezaji hao hadi sasa ndio wanaonekana kuamua mechi kutokana na ubora wao na namna wanavyocheza.


SIMBA

Kama ulidhani Simba ni ya kawaida, basi sahau! Ujio wa kocha mpya Mhispania Pablo Franco umekuja na kasi mpya kikosini hapo kwa msimu huu.

Aishi Manula, Rally Bwalya, Meddie Kagere, Pape Sakho, Kibu Denis, Duncun Nyoni na Benard Morrison ndio mastaa wa chama hilo ambao kama watakuwa kwenye viwango bora basi wapinzani wajipange kuwakabili licha ya kuwa Simba bado ipo bora kila idara.


AZAM

Pamoja na kuanza ligi kwa kusuasua na kujikuta ikivuna alama saba kwenye mechi tano za awali, kuna baadhi ya mastaa wa Azam ambao wana kazi ya ziada kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri zaidi.

Kipa Mathias Kigonya, mabeki Yvan Mballa na Daniel Amoah, viungo Sospeter Bajana na Keneth Muguna sambamba na washambuliaji Iddi Nado, Idris Mbombo na Rogers Kola ndio wamevikwa mabomu kuhakikisha Azam inashinda.


BIASHARA UTD

Wanajeshi hawa wa mpakani wamekamilika kila idara lakini Kipa James Ssetuba, mabeki Lenny Kissu, Abdulmajid Mangaro, viungo Ramadhan Chombo, Denis Nkane, sambamba na mshambuliaji Atupele Green ndio mastaa wa chama hilo.

Nyota hao wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanaibeba mabegani timu hiyo na kumaliza msimu ikiwa nafasi nne za juu kama msimu uliopita ilipomaliza nafasi hiyo.


POLISI TANZANIA

Msimu huu hawa jamaa wamepania kinoma, hadi sasa wapo nafasi ya tatu kwenye ligi baada ya kucheza mechi tano na kuvuna alama 10 nyuma ya vinara Yanga na Simba.

Metacha Mnata, Kelvin Yondan, Juma Makapu, Tariq Simba, Adam Adam, Vitalis Mayanga na Tariq Seif ndio mastaa walioshikilia hatma ya Polisi hadi sasa kutokana na ubora wao uwanjani.


DODOMA JIJI

Uwanja wa Jamhuri Dodoma wanaoutumia walima zabibu hawa, msimu huu umewekwa taa na sasa zinapigwa mechi za usiku.

Sasa kazi ipo kwa mastaa wa timu hiyo, Seif Karihe, Salmin Hoza, George Wawa, Nassoro Macheza, Cleophace Mkandala, Hamis Mcha, Emannuel Martin na Jamal Mtegeta kuhakikisha wanawafurahisha wanadodoma.


MBEYA KWANZA

Hili ni chama jipya kwenye Ligi Kuu msimu huu lakini mziki wake sio wa kitoto chini ya mastaa Salum Chuku, Minza Christom, Paul Peter, Willy Mgaya na Chrispin Ngushi.

Pamoja na kuwepo kwa mastaa wengine kikosini hapo lakini wachache hao ndio wanaonekana kuwa na kazi ya ziada kuhakikisha timu hiyo inakiwasha zaidi Ligi Kuu.


MBEYA CITY

Haroun Mandanda, Keneth Kunambi, Mpoki Mwakinyuke, David Mwasa, Juma Luizio, Eliud Ambokile na Paul Nonga ndio mastaa wa Mbeya City wanaotazamiwa kuibeba timu msimu huu.

Wakali hao wa Mbeya chini ya kocha Mganda Mathias Lule msimu huu wamejipanga kupambana na kutafuta kumaliza nafasi nne za juu.


KMC

KMC bado hawajakaa sawa msimu huu. Wamecheza mechi tano za awali bila kupata ushindi hata mara moja lakini bado kuna wachezaji ambao ndio wana jukumu la kuipa ushindi timu hiyo ya Kinondoni.

Kenny Ally, Andrew Vicent ‘Dante’, Charles Ilamfya, Sadala Lipangile, Awesu Awesu na Miraji Athuman ni mastaa ambao kama wakiamua kujitoa kwa asilimia kubwa kuipambania timu basi KMC itakuwa shoo shoo.


MTIBWA SUGAR

Wanatuliani hawa hali yao imekuwa mbaya misimu miwili iliyopita na msimu huu haijapata ushindi katika mechi tano za awali.

Pamoja na kusuasua huko lakini ndani ya kikosi hicho kuna majembe kama

Aboutwalib Msheri, Said Ndemla, Abdi Banda, Ibrahim Ame, Stive Nzigamasabo, Kelvin Sabato na Riphat Hamis ambao hatima ya kuiheshimisha Mtibwa iko mikononi mwao.


KAGERA SUGAR

Hili chama kwa sasa lipo na kocha fundi Fransis Baraza ambaye misimu miwili iliyopita aliwika akiwa na Biashara United na ndani ya timu kuna mastaa kibao ambao anawaaminia.

Ramadhan Mfuko, Stephen Duah, Meshack Abraham, Nassor Kapama, Erick Mwijage na Mbaraka Yusuph kwa msimu huu ndio mastaa wa Kagera ambao wameshika hatma ya chama hilo hadi sasa.


GEITA GOLD

Matajiri hawa wa Dhahabu, huu ni msimu wao wa kwanza kwenye ligi na tayari wamemtimua aliyekuwa kocha wao mkuu Ettiene Ndayiragije kutokana na mwenendo mbaya na sasa mikoba amekabidhiwa Felix Minziro aliyeipandisha timu hiyo.

Licha ya kuwa ni mpya kwenye ligi lakini katika kikosi chake kuna mastaa wazoefu na wengine ni wapya kama Amosi Kadikilo, Kelvin Nashon, Maka Edward, Juma Mahadhi, Chilo Mkama, Venance Ludovic na Daniel Lyanga ambao wana jukumu la kuiweka timu kwenye mstari.


TANZANIA PRISONS

Wajelajela hawa msimu huu hawajaanza vizuri lakini bado mashabiki wa kikosi hicho wanaamini kuwa chama lao litafanya vizuri zaidi mechi zijazo.

Vedastus Mwihambi, Jumanne Elfadhili, Salum Kimenya, Benjamin Asukile, Lambert Sabiyanka na Ezekiel Mwashilindi ni miongoni mwa maafande ambao hatima ya timu hiyo ipo mikononi mwao kwa msimu huu.


COASTAL UNION

Wagosi wa kaya msimu huu wamejipanga kweli kweli licha ya kutopata ushindi kwenye mechi tano za awali wakitoa sare nne na kupoteza moja.

Usajili wao sio wa kitoto na tayari nyota kama Mussa Mbissa, Victor Akpan, Amani Kyata, Jacob Benedictor, Mtenja Albinos na Isa Abushee wamevikwa mabomu ya kulitetea chama hilo kutokana na ubora wao kwa msimu huu.


RUVU SHOOTING

Wazee wa mpapaso nao mambo si haba! Unaambiwa msimu huu wamepania kinoma na tayari mastaa wao washakula kiapo cha kuipambania timu mwanzo mwisho.

Nyota kama Mohamed Makaka, Zuberi Dabi, Shaban Msala, Pius Buswita, Marcel Kaheza, Rashid Juma, Fully Maganga na Santos Mazengo ndio kwa sasa wanaonekana kuvikwa mabomu ya kuliwakilisha chama hilo.


NAMUNGO

Hawa jamaa msimu huu wana mastaa kibao wenye viwango vya juu lakini Jonathan Nahimana, Shiza Kichuya, Abdulaziz Makame, Reliants Lusajo, Obrey Chirwa, Jacob Masawe, William Charles na Baraka Mtuwi ndio wameshikilia hatma ya timu.

Uzoefu na ubora wa mastaa hao ndio utaamua Namungo inayonolewa na kocha Hemed Seleman ‘Morocco’ imalize ligi ikiwa nafasi gani.


SIKIA HAWA

Miongoni mwa wadau wa soka waliozungumzia hatima ya timu kuwa kwa baadhi ya wachezaji kwenye vikosi vyao ni Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Baraza na Kiungo wa Polisi Tanzania, Tariq Simba.

“Licha ya kwamba kila mchezaji ni muhimu kikosini lakini kuna ‘key players’ ambao mara nyingi mbinu na mifumo huanzia kwao na mara zote wao ndio wanakuwa na jukumu la kuichezesha timu hivyo wasipofanya vizuri kuna uwezekano mkubwa wa timu kukosa matokeo chanya,” alisema Baraza.

Kwa upande wa Simba alisema; “Uwanjani kunakuwa na wachezaji 11 na kila mmoja anajitoa kuipambania timu yake na inategemeana na mechi kwani kuna muda mechi moja itahitaji aina ya wachezaji fulani na kama itawakosa basi mambo yanakuwa magumu pia sifa kubwa ya kuwa bora au staa kwenye timu ni kuweza kukabiliana na aina tofauti tofauti za kiuchezaji.”