MANYASI... Mwalimu wa Historia anayekiwasha Ligi Kuu
Muktasari:
- Nyota huyo amesomea Shahada ya Sanaa na Elimu (Bachelor of Art with Education), katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, kilichopo mjini Morogoro, ambapo amepiga stori na Mwanaspoti na kufunguka mambo mengi, ambayo yatakuhamasisha maishani.
UNAPOZUNGUMZIA wachezaji wasomi katika Ligi Kuu Bara, hutoacha kutaja jina la kiungo mkabaji wa Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’, Jofrey Manyasi, ambaye kitaaluma ni mwalimu darasani aliyebobea zaidi kufundisha masomo ya Kiingereza na Historia.
Nyota huyo amesomea Shahada ya Sanaa na Elimu (Bachelor of Art with Education), katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, kilichopo mjini Morogoro, ambapo amepiga stori na Mwanaspoti na kufunguka mambo mengi, ambayo yatakuhamasisha maishani.
SIO MWAJIRIWA
Kiungo huyo anasema kwa sasa sio muajiriwa wa moja kwa moja katika taaluma yake ya kufundisha kwa sababu ameweka nguvu zaidi katika kucheza soka, ingawa mara kadhaa baadhi ya shule zinamchukua akiwa mapumzikoni ili kwenda kufundisha.
“Akili yangu nimeweka sana katika kucheza soka kwa sababu ilikuwa ni ndoto yangu, japo kitaaluma ni mwalimu, wengi wao wanajua nacheza tu ila hawajui pia nina uwezo wa kufundisha, zote ni kazi zangu na ninajivunia sana,” anasema Manyasi.
UPANGAJI WA RATIBA
Anasema moja ya vitu vikubwa vinavyomsaidia ili kufanya kazi zote kwa ufasaha ni upangaji mzuri wa ratiba yake ya siku nzima, kwa lengo la kuhakikisha majukumu yake yote yanaenda vizuri bila ya kuathiriwa na jambo lolote alilo na uwezo nalo.
“Nikijua leo nina ratiba ya kufundisha basi nawahi asubuhi sana kufanya mazoezi kisha ndio naenda kwenye majukumu yangu mengine, hali hiyo imenisaidia na sio sasa hivi tu bali hata nikiwa chuo nasoma hivyo, ni muhimu kwa kila mmoja wetu.”
SOKA NDOTO YAKE
Manyasi anasema licha ya kitaaluma ni mwalimu darasani, kucheza mpira ni mojawapo ya ndoto zake kubwa tangu utotoni, hivyo, anashukuru kwa hatua aliyofikia sasa, kwani ukiamini katika jambo lolote na kulifanyia kazi ni rahisi kufanikiwa.
“Kwangu ni heshima kubwa kuona nacheza, lakini natumia ujuzi wangu nilionao kuwapa wengine, katika jambo lolote ukiwa na imani utafanikiwa, hivyo niwasihi vijana wenzangu tuendelee kupigania ndoto zetu na Mungu atatuongoza,” anasema Manyasi.
UALIMU ULIVYOMSAIDIA
Licha ya muda mwingi kwa nyota huyo kuutumia kucheza mpira, anasema taaluma yake ya ualimu imemsaidia sana kuongeza wepesi wa kuelewa kitu chochote anachofundishwa na kocha, jambo analojivunia na anaendelea pia kulifanyia kazi.
“Kocha anavyonifundisha huwa najiona mimi nikiwa darasani nafundisha pia, hii inanisaidia kwa sababu napata ujuzi mara mbili zaidi ya nilionao, kitu kikubwa ninachozingatia nikifundishwa au kufundisha ni nidhamu ndani na nje ya uwanja.”
CHANGAMOTO
Katika safari yoyote yenye mafanikio hakukosekani changamoto na hivi ndivyo ilivyomtokea Manyasi ambaye anasema akiwa na timu ya Boma ya jijini Mbeya aliumia mguu na kuhisi asingerejea tena uwanjani, ingawa alipona na kupigania ndoto zake.
“Changamoto nyingine ni ya kwenye ratiba ya shule hasa kukiwa na mitihani ya kidato cha pili au cha nne kwa sababu muda wa kufanya mazoezi unakuwa mgumu kidogo, ila najitahidi sana kuhakikisha mambo yote yanaenda vizuri kama nilivyopanga.”
WANAFUNZI WANAVYOMUONA
Manyasi anasema wanafunzi wanamuona kioo cha jamii kutokana na kazi anazozifanya ndio maana hata wao wanatamani kufika alipo, jambo ambalo analifurahia na kumuongezea hamasa akiwa anawafundisha au akiwa uwanjani ili wafikie malengo yao.
“Wanafunzi wanatamani siku moja wawe kama mwalimu wao, nikiwa nao uwanjani wakati wa vipindi vya michezo shuleni huwa wanajisikia furaha sana na kila ninachowafundisha wanakifanya kwa kujituma kwa sababu tunaishi vizuri pia,” anasema.
NIDHAMU MPANGO MZIMA
Kiungo huyo anasema katika kazi ya aina yoyote ili ufanikiwe ni lazima uzingatie nidhamu kwa sababu hata ukiwa na kipaji ila huna maadili mazuri huwezi kufanikiwa, jambo ambalo kwake binafsi analichukulia kwa uzito ili awe mfano kwa wengine.
“Mimi nje ni mwalimu wao ila pia ni kioo cha jamii kutokana na kazi zote mbili ninazozifanya hivyo, inabidi nifanye yale matendo mazuri ambayo siku zote yatakuwa ni mfano bora wa kuigwa na wanafunzi ninaowafundisha na jamii yangu kiujumla.”
TAALUMA NYINGINE MUHIMU
Anasema kila mmoja mwenye uwezo ni muhimu kuwa na taaluma zaidi ya moja katika maisha ya sasa, kwa sababu itamrahisishia kufikia malengo yake, kwani inatoa wigo mpana wa kuchagua jambo atakalolifanya tofauti na kutegemea kitu kimoja pekee.
“Ukiwa na taaluma zaidi ya moja inasaidia sana kwa sababu hata nafasi za ajira zinapotoka unaweza ukakosa sehemu moja ila kwingine ukapata, hivyo, ni muhimu pia kusomea mambo mbalimbali ili pale fursa zinapotokea tuweze kuzichangamkia.”
USHAURI KWA WANAFUNZI
Manyasi anasema moja ya mambo anayopenda kuwashauri wanafunzi ni kutambua kwamba licha ya michezo kuwa ni afya, pia ni ajira, hivyo, wasikate tamaa katika kupigania ndoto zao kwa sababu kila jambo linawezekana ukiwekeza jitihada zaidi.
“Mipango mingine ni ya Mwenyezi Mungu, lakini tusichoke kuishi katika ndoto zetu, nikiwa na wanafunzi wanazungumzia sana kutaka kufika mbali, ila mojawapo ya jambo ninalowasihi ni kupambana na wasikatishwe tamaa kwenye kufikia malengo yao.”
AKIACHA SOKA ANAFUNDISHA
Anasema akiacha kucheza soka atawekeza nguvu zaidi katika kutumia akili yake ya kufundisha moja kwa moja tofauti na sasa ilivyo, kwani ualimu ni kazi anayoipenda na siku zote anajivunia kutokana na mazingira anayoishi na jamii inayomzunguka.
“Nikistaafu nitajielekeza zaidi kufundisha moja kwa moja tofauti na sasa ambavyo ninafanya, ualimu ni wito na kiukweli nimeona tofauti kubwa ya kuishi na watu, kwa sababu jamii inaniheshimu hivyo, nami najikuta nikiishi kwa maadili mema.”
HISTORIA YA SOKA
Nyota huyo anasema safari yake ya soka ilianzia jijini Mbeya katika Wilaya ya Kyela, ambapo alianzia kucheza kwenye timu ya Boma, kisha baadaye kujiunga na Geita Gold, Ihefu kwa sasa Singida Black Stars, Kagera Sugar na sasa Coastal Union.
“Boma ndio timu ambayo naweza kusema ilitangaza jina langu na kuonekana hadi na wengine, kipindi hicho nilikuwa nacheza kwa lengo la kujitangaza, hivyo, nashukuru nilitimiza malengo hayo baada ya viongozi wengi kuvutiwa na kipaji changu.”
KOCHA ALIYEMUIBUA
Manyasi anasema licha tu ya kufundishwa na makocha wengi, hatokaa akamsahau kocha, Geofrey Katepa, kwa sababu ndiye aliyechangia kufika hapo alipo leo, kutokana na misingi bora aliyomjengea katika safari yake ya soka kuanzia utotoni.
“Nathamini sana mchango wa makocha wengi walionifundisha hadi sasa, ila Katepa ni zaidi kwa sababu misingi yote bora kwa maana ya kiuchezaji alianza kunifundisha yeye, kwangu atabaki miongoni wa watu bora ambao sitokaa nikawasahau maishani.”
ROLE MODEL WA GAUCHO
Anasema miongoni mwa wachezaji waliomvutia kucheza mpira ni pamoja na aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Brazil, Ronaldo de Assis Moreira ‘Ronaldinho Gaucho’, aliyetamba na klabu ya Barcelona ya Hispania na PSG ya Ufaransa.
Gaucho aliyetamba pia na timu mbalimbali kwa mafanikio makubwa zikiwamo, AC Milan ya Italia, Gremio, Flamengo, Atletico Mineiro zote za kwao Brazil na Queretaro ya Mexico, ni miongoni wa nyota waliomvutia Manyasi na kutamani kucheza soka.
“Gaucho sio tu alikuwa mchezaji ninayemuangalia zaidi ila alikuwa namba moja kwangu kutokana na aina yake ya uchezaji, nilikuwa napambania ndoto zangu kupitia yeye kila nikimuangalia, kiukweli alikuwa mmoja wa nyota bora kuwahi kuwaona.”
BOBAN, NIYONZIMA SIO MCHEZO
Manyasi anasema wachezaji waliocheza Ligi Kuu aliokuwa anavutiwa nao kutokana na uchezaji wao ni Mtanzania, Haruna Moshi ‘Boban’ na Mnyarwanda Haruna Niyonzima, ambao kwa kiwango kikubwa walichangia kuitangaza pia Tanzania ndani na nje ya nchi.
“Unapomtaja Boban au Niyonzima kwa vijana wa sasa hivi wanaweza wasielewe ninachomaanisha, ila ni wachezaji waliofanya mambo makubwa katika Ligi yetu na hata kuchangia kuitangaza, watabakia miongoni mwa watu ninaowakubali maishani mwangu.”
Boban ni miongoni mwa nyota waliofanya vizuri na timu kubwa hapa nchini zikiwamo za Simba, Yanga, huku akizichezea pia, Mbeya City, African Lyon, Friends Rangers na Moro United, wakati soka lake la kulipwa nje aliichezea Gefle IF ya Sweden.
Kwa upande wa Niyonzima, amejizoelea pia umaarufu hasa kupitia timu za Yanga na Simba za hapa nchini, ingawa pia ameichezea Al Ta’awon ya Libya, sambamba na miamba wa Etincelles, Rayon Sports na APR FC zote za kwao Rwanda kwa mafanikio makubwa.