Prime
Manula amerejea Azam na utamu wake
Muktasari:
- Manula amerudi nyumbani pale Azam Complex, sehemu ambayo ilimkuza akitokea Mkamba, Kilombero, akichukuliwa na matajiri hao wa Chamazi akiwa kijana mdogo sana kwenye kliniki ya soka la vijana. Akakulia hapo na kupandishwa timu ya wakubwa akiwa mmoja wa wachezaji waliokuwa tegemeo wakati huo.
UMEKIONA kiwango cha kipa Aishi Manula pale Azam FC? Jamaa ni kama amezaliwa upya. Yupo kwenye kiwango bora utasema ndio ameanza sasa kuonyesha makali yake kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini kumbe ni mzoefu wa kiwango cha kutosha.
Manula amerudi nyumbani pale Azam Complex, sehemu ambayo ilimkuza akitokea Mkamba, Kilombero, akichukuliwa na matajiri hao wa Chamazi akiwa kijana mdogo sana kwenye kliniki ya soka la vijana. Akakulia hapo na kupandishwa timu ya wakubwa akiwa mmoja wa wachezaji waliokuwa tegemeo wakati huo.
AZAM WAMPOTEZA KIZEMBE
Mwaka 2017, wakati msimu wa 2016/17 unamalizika, Azam ilifanya hesabu mbovu za kuwaondoa wachezaji wake waliowalea kwa muda mrefu kwa kugoma kuwaongezea mikataba. Wakiwemo aliyekuwa nahodha wao mshambuliaji John Bocco, kiungo kiraka Erasto Nyoni, beki Shomari Kapombe pamoja na Gadiel Michael ambao waliambiwa hawataweza kupewa fedha nyingi za kuongeza mikataba.
Wachezaji hao walipoona mambo magumu Azam wakaanza kujitafutia maisha mapya, na klabu ya kwanza kupata taarifa hiyo ilikuwa Yanga, lakini bosi wao mmoja wa zamani akaweka ngumu kuwasajili akidai nyota hao walikuwa wazee.
Simba iliposikia taarifa hiyo, wakafanya maamuzi ya haraka kwa kuwachukua Bocco, Manula, Nyoni na Kapombe ambao walikwenda kuungana na mastaa wengine na kutengeneza Simba ngumu ambayo ilipasua kwa mafanikio ndani ya Tanzania na hata Afrika.
SHIDA ILIANZIA HAPA SIMBA
Aprili 7, 2023 Simba ikicheza na iliyokuwa Ihefu FC pale Azam Complex kwenye mchezo wa FA, Simba ilishinda kwa mabao 5-1 lakini Manula hakumaliza mchezo huo. Aliumia dakika ya 73 na kutolewa dakika mbili baadaye nafasi yake ikichukuliwa na Beno Kakolanya.
Ilionekana kama aliumia kidogo lakini hakuweza kurudi tena uwanjani kwa haraka na anguko lake likaanzia hapo. Licha ya kufanyiwa upasuaji, hakuweza kurejea kwa haraka kupigania nafasi yake ndani ya kikosi hicho.
SIMBA ILIKOSEA HAPA
Kama ilivyo kawaida ya klabu kubwa, Manula hakuonekana tena kama kipaumbele. Licha ya jitihada za kipa huyo kupambana kurudi uwanjani, Simba ilionekana kuelekeza akili kwenye hesabu za makipa wengine.
PRISONS, YANGA WAMTIBULIA
Bahati mbaya zaidi, Manula kuna wakati alipambana na kufanikiwa kurudi uwanjani lakini akakutana na mechi mbili ambazo zilimharibia, akionekana kama hafai tena kuidakia timu hiyo. Mchezo wa kwanza ulikuwa wa nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons SC pale Jamhuri Morogoro ambapo wekundu hao wakapoteza kwa mabao 2-1 na lawama nyingi zikaangukia kwa kipa huyo.
Mbaya zaidi Manula alikuwa golini tena kwenye mchezo dhidi ya Yanga ambao Simba ilipoteza kwa mabao 5-1 Novemba 5, 2023. Nako lawama zikawa kwake.
Baada ya hapo hakuonekana tena langoni kwa Simba mpaka alipokuja kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Al Hilal Omdurman huku akionyesha kiwango bora kwa dakika 45 tu za kipindi cha pili alizopewa chini ya kocha Fadlu Davids.
Simba wakati huo Manula hakuonekana kipa muhimu tena. Thamani kubwa ilikuwa kwa Moussa Camara aliyekuwa chaguo la kwanza ambapo hata kipa huyo raia wa Guinea alipokosekana langoni alionekana Ally Salim huku Manula akikosekana.
Wakati wote huo taarifa zilikuwa za kutofautiana sana ambapo Simba ilikuwa inadai kwamba kipa huyo alikuwa majeruhi, lakini upande mwingine watu wa karibu na Manula walidai hakuwa na shida yoyote ya kiafya na kwamba ilikuwa inapotoshwa.
AZAM WAJILIPUA
Dirisha kubwa la usajili lililopita, Azam FC ikarudi kwa Manula na kumsajili kipa wao huyo wa zamani akitokea Simba ambako alidumu kwa misimu nane, wakimrudisha nyumbani.
Alisajiliwa sambamba na kipa wa kigeni kutoka Al Hilal, Issa Fofana, wakiungana na kinda wa matajiri hao Zuber Foba. Manula alianza taratibu lakini sasa ameonyesha kwamba kiwango ni kitu cha muda lakini ubora ni wa kudumu, akirudi na kiwango bora kama ambavyo alikuwa kabla
wakati akifanya makubwa na Simba.
KIWANGO KIMERUDI
Manula kiwango alichoonyesha kwenye mchezo dhidi ya Wydad Athletic Club kule Morocco, licha ya Azam kupoteza kwa mabao 2-0, lakini kipa huyo alifanya kazi kubwa ya kuokoa mashambulizi saba ya hatari.
Achana na mechi hiyo, Azam ikiwa ugenini dhidi ya Prisons dakika za jioni kabisa ilikapigwa shambulizi la kushtukiza kwa wenyeji, lakini Manula aliokoa shuti kali ambalo kama si mikono yake timu yake ingepoteza kwa mkwaju huo.
Kiwango ambacho Manula anaendelea kukionyesha akiwa na Azam ni wazi kwamba mabosi wa matajiri hao wanachekelea na kujiona wameshinda vita.
Lakini kwa upande mwingine kule Simba lazima watakuwa wanainama chini wakiona namna walivyompoteza kipa muhimu aliyekuwa anatakiwa kubaki kwenye kikosi chao.
AZAM INAPETA HAPA
Kurejea kwa kiwango cha Manula ni wazi kwamba timu hiyo itashusha presha ya kuachana na kusajili makipa wa kigeni. Sioni kama Fofana ataendelea kubaki klabuni hapo hasa wakati huu ambao wananufaika na kazi ya Manula, huku pia wakiwa na Foba ambaye yupo vizuri.
Hesabu hizi hazikwenda vizuri Simba ambao baada ya kuumia kwa Camara na Yakoub Mohamed ilihitajika kutafutwa kipa mwingine bora na kurudi kusajili mchezaji mwingine wa kigeni akija Djibrilla
Ujio wa Kassali ukailazimisha Simba kumuacha Camara ambaye alikuwa bado hayuko sawa. Lakini kama Simba ingekuwa na jicho la mbali kwa Manula basi maamuzi hayo magumu wangeyakwepa kirahisi, ukizingatia kanuni za Ligi Kuu Bara zinazuia timu kuwa na makipa wawili wa kigeni.