Mambo yaliyozingua mwanzo tu Ligi Kuu

LIGI Kuu Bara imeanza kwa kishindo huku kila timu ikionyesha ushindani ambao unauhitajika katika Ligi Kuu Bara ingawa vituko navyo haviishi.

Ni ukweli uliowazi kuwa ligi hii ni bora Afrika Mashariki kwani inawavutia wachezaji wengi kuja kucheza nchini.

Katika michezo ya kwanza imeshuhudia vituko vingi jambo ambalo limeibua mijadala ya aina yake.

Yapo mambo mengi ambayo yamejiri kwenye mechi za ufunguzi yanayotia aibu mwanzo huo wa ligi na Mwanaspoti linakudokolea machache kati ya mengi yaliyoibuka viwanjani.


NYAVU ZA GOLI

Huenda hii ndio inatofautisha ligi ya Bongo na kwingineko kwani vituko hivi utavipata Tanzania katika soka ambalo linapiga hatua kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na hata Bara la Afrika.

Mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/22 ulishuhudia tukio hilo katika Uwanja wa Mabatini, Kibaha mkoani Pwani wakati Mtibwa Sugar ikikipiga dhidi ya Mbeya Kwanza.

Unaweza kucheka ingawa sio kwa furaha, bali kwa masikitiko ukijiuliza tangu ligi ilipomalizika msimu uliopita maofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wanaokagua viwanja walikuwa wapi? Mpaka Ligi Kuu inaanza upya na kushuhudia madudu kama hayo? ama kweli hii nd’o Bongo.

Nyavu za Uwanja wa Mabatini zilikuwa zimetoboka, hivyo mpira ulikuwa unasimama na waamuzi wa mchezo huo walikuwa wakizishikiza kabla ya mchezo kuendelea, hivyo kutumia muda wa mchezo bila sababu za msingi.


KIBENDERA KONA TATIZO

Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya michezo ya mwanzo tu kushuhudia vichekesho ambavyo hutusaidia kuongeza siku za kuishi kama wasemavyo wahenga.

Hili la kibendera kuwa kibovu lilionekana katika mchezo wa Mtibwa Sugar dhidi ya Mbeya Kwanza, lakini pia katika Uwanja wa Karume uliopo Musoma mkoani Mara wakati wa mchezo kati ya Biashara United na Simba.

Kwa mechi ambazo huchezwa saa nane mchana humlazimu mwamuzi kutoa dakika kadhaa kwa wachezaji kupata maji, hii ni kwa sababu ya jua kali muda huo, lakini pia muda huo pia ulitumika kurekebisha kibendera cha kona. Mambo hayo!


HAMISHAHAMISHA YA TIMU

Hakuna kitu kizuri kama maandalizi kwenye jambo lolote zuri, kwani inaonyesha wazi Ligi Kuu ilipoishia msimu uliopita ndipo inapoendelea msimu huu - yaani kwa kifupi ni kama hakuna mabadiliko yoyote.

Ubovu wa viwanja umesababisha timu kuondoshwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine ikiwa tayari imekwishaanza hali inayosababisha bajeti ya timu kuongezeka kwa kutopewa taarifa mapema.

Mchezo wa Mtibwa Sugar na Mbeya Kwanza lilitokea hilo, ambapo mechi hiyo ilipangwa kufanyika Uwanja wa Jamhuri Mjini Morogoro, ila cha kushangaza ilihamishiwa Mabatini-Kibaha na kujikuta timu zikifika usiku ikiwa ni siku moja kabla ya mechi. Inaelezwa pia kwamba bado hamahama hiyo inakuja.


MAJINA YA WACHEZAJI

Katika mchezo wa Biashara United na Simba ilishuhudiwa takriban wachezaji wanne wa Biashara United jezi zao zikiwa na majina kama ilivyokuwa utaratibu, lakini jambo la kushangaza ni kwamba wengine hawakuwa na majina, jambo ambalo unaweza kujiuliza maswali mengi bila majibu.

Sio vyema na utaratibu mzuri kwa soka la kisasa ni kuona na kuwajua kwa majina wachezaji wote wanaoshiriki mchezoni. Siku zote kuiga jambo zuri ni vyema na fahari.


WASIKIE WADAU

Akizungumzia suala la kuhamishwa viwanja dakika za lalasalama, msemaji wa timu ya KMC, Christina Mwagala anasema ili kupiga hatua katika soka inabidi kurekebisha upungufu uliopo kwani bado Tanzania inakabiliana na safari ndefu kufikia mafanikio ya juu zaidi.

“Changamoto hiyo imetutokea pia na sisi, ukiangalia mchezo wetu na Polisi Tanzania tulipangiwa kucheza Ushirika - Moshi, ghafla tukahamishiwa Sheikh Amri Abeid - Arusha, ila hatujakaa sawa tunapelekwa tena Karatu (Arusha), kwa kweli inachosha maana tunatumia gharama kubwa,” anasema.

Kocha wa zamani wa Lipuli FC na Ndanda FC, Meja mstaafu Abdul Mingange anasema matatizo ya viwanja yanahusu wamiliki, hivyo haoni shinda kwa (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) kupiga ‘stop’ visitumike vinavyoonekana kuwa vibovu wakati ligi ikiendelea, huku akilitaka shirikisho hilo kuwagusa zaidi mameneja wanaovisimamia viwanja hivyo.

“Viwanja vyetu vingi ni changamoto nchini, hivyo nadhani ni muda kwa TFF kuwa wakali kwa mameneja ili kufikia malengo ya kuendelea kuinua soka letu,” anasema.