Prime
Mambo matano yanayoipa Yanga ugumu
MASHABIKI wengi wa Yanga wamekuwa hawana furaha kutokana na mwenendo wa kikosi chao msimu huu, tangu ilipoishia hatua ya makundi na kushindwa kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku kikisuasua kwenye Ligi Kuu Bara hali inayoweka rehani nafasi ya kutetea ubingwa wao.
Yanga ndiyo inayoongoza msimamo wa ligi na pointi 30 na haijapoteza mechi hata moja msimu huu sawa na Azam FC, hata hivyo, endapo hali itaendelea kuwa hivi, huenda ikapoteza uongozi wake.
Wengi wanajiuliza shida iko wapi kutokana na kupoteza ubabe wake wa kushinda kila mechi kama awali na tangu itolewe na Ligi ya Mabingwa Ulaya, imecheza mechi nane za Ligi Kuu Bara zenye jumla ya pointi 24, lakini imekusanya 20 na kuacha nne zikipotea baada ya kushinda nne sawa na sare ilizopata.
Mbaya zaidi, Yanga imetoka sare mechi tatu mfululizo, matokeo ambayo si mazuri kwao kama bingwa mtetezi anayepambana kubeba kombe tena.
Kuporomoka kwa kiwango cha Yanga kuna mengi yanazungumzwa kwenye maeneo mbalimbali ambayo yanaweza kuwa yamesababisha, lakini hebu tuangalie yale matano makubwa.
USAJILI
Kitu cha kwanza kabisa ambacho Yanga lazima wakikubali ni uongozi wao msimu huu haukuwa na jicho zuri kwenye usajili.
Ukifanya tathmini ya kina, utagundua wachezaji wengi waliosajiliwa viwango vyao vilishindwa kuhimili presha ya kikosi hicho.
Msimu huu Yanga imesajili wachezaji 17 kuanzia dirisha kubwa kabla ya kuanza msimu na lile dogo la Januari 2026.
Wachezaji walioingia dirisha kubwa ni Frank Assinki, Moussa Bala Conte, Celestin Ecua, Mohamed Doumbia, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Offen Chikola, Andy Boyeli, Lassine Kouma, Nizar Abubakar ‘Ninju’, Abdulnasir Abdallah ‘Casemiro’.
Kati ya hao, Tshabalala pekee ndiye amepenya kikosi cha kwanza na amepata muda mwingi wa kucheza kuliko wenzake, huku Boyeli akirudishwa Sekhukhune United alipochukuliwa kwa mkopo. Wengine wametolewa kwa mkopo ambao ni Chikola (Singida Black Stars), Conte (Raja Casablanca), Ecua (JS Kabylie) na Doumbia (Marumo Gallants).
Dirisha dogo wakaingia Laurindo Aurelio Depu’, Emmanuel Mwanengo, Buba Jammeh, Allan Okello, Mohammed Damaro na Hussein Masalanga.
Hapo pia, Depu, Okello na Damaro wanapata nafasi kubwa zaidi ya kucheza kuliko Mwanengo, Buba na Masalanga. Pia Yao Kouassi Attohoula amerudishwa kwenye mfumo baada ya kupona majeraha yake, hata hivyo, hajarudi kama yule aliyekuwa mwanzo akikichafua sana, makali yamepungua.
Kwa maana hiyo, kati ya nyota 17 wapya walioingia Yanga msimu huu, ni wanne pekee ndio wamepata nafasi kubwa ya kucheza. Katika usajili, hii ni hasara kwani hata nusu ya matarajio hayajafikiwa.
Hili ni eneo kubwa ambalo Yanga, baada ya kumaliza msimu huu, lazima wajue walikosea wapi na kipi kimewakwamisha, hali ya kuwa ilikuwa ni timu ambayo ilisifika kwa jicho zuri la kuona wachezaji walio bora.
Wakati wanaongezwa wachezaji hao, kulikuwa na matumaini makubwa watakuja kuziba nafasi ya wale waliotoka, hususan ile ya Khalid Aucho, lakini bado viatu vyake vimekuwa vizito kwa wachezaji kama Conte na Damaro ambaye naye hana uhakika sana wa kucheza.
MIFUMO YA PEDRO
Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves hawezi kukwepeka kwenye lawama za hiki kinachoendelea katika timu, licha ya kwamba yapo maeneo amefanya vizuri. Ukitazama utaona ni kweli kikosi chake hakijapoteza mechi na kinaongoza ligi, hapo utampongeza.
Ukigeukia namna Yanga inavyokwenda sasa, utagundua suala la kuja kupoteza ni ishu ya muda tu kwani mifumo yake imekuwa ikiipa wakati mgumu timu na amekuwa ni kocha anayetaka sana iwe imara kwenye kulinda.
Yanga imepata sare tano msimu huu, lakini ni sare moja tu ambayo haitamuhusu Pedro, ambayo ni ile dhidi ya Mbeya City wakati huo kikosi hicho kikifundishwa na kocha Romain Folz, lakini nyingine nne zitamhusu kocha huyu raia wa Ureno.
Ukitazama sare hizo nne za Pedro, utaona Yanga haikucheza vizuri sana kama timu kubwa kuanzia ile ya Simba, Azam, TRA United na Mtibwa Sugar. Ni vigumu kuona haraka Yanga inacheza soka la falsafa ipi kama makocha wa nyuma walivyokuwa wakijitambulisha.
Ukweli ni Pedro ameijenga Yanga kuwa ngumu katika ulinzi kwani imeruhusu mabao matatu pekee katika mechi 16 za ligi ikiwa ndiyo timu iliyoruhusu mabao machache zaidi. Pia Yanga inaongoza kwa mabao mengi ikifunga 32.
Hata hivyo, kuna baadhi ya mechi Pedro anaingia kwa uoga, anajilinda zaidi kuliko kushambulia zikiwamo zile alizotoka sare kwani ukiachana na ya juzi dhidi ya Mtibwa Sugar iliyokuwa 1-1, zingine zote matokeo yalikuwa 0-0 dhidi ya Simba, Azam na TRA United.
MAJERAHA
Mguu mwingine mbaya ambao Yanga iliingia nao msimu huu ni janga la wachezaji majeruhi ambalo limeendelea kuitafuna timu hiyo ikiwa na wachezaji wanane ambao ni majeruhi kama washambuliaji Clement Mzize, Depu, Prince Dube, kipa Abubakar Khomeni, mabeki Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Chadrack Boka. Pia winga Edmund John.
Bahati mbaya sana wachezaji wengi ni wale ambao walikuwa tegemeo kikosini. Kule mbele ni Mzize ambaye hataweza kucheza tena msimu huu, lakini wamo Depu na Dube ambao walikuwa kama ndiyo watoto pekee waliosalia kwenye familia baada ya kuumia kwa Mzize. Hili limeiyumbisha sana Yanga, ikipoteza nguvu kubwa eneo lao la kushambulia.
Pia kwenye ulinzi kuna tatizo, mabeki wa kati tegemeo, Job na Bacca ni majeruhi huku Job ikielezwa anaweza asicheze tena msimu huu kutokana na jeraha lake.
Hapo bado haujawaweka wengine ambao walishakaa nje kwa muda kisha wakarudi kama Pacome Zouzoua na Mudathir Yahya.
Msimu uliopita, pia Yanga ilipitia kipindi kama hiki, ilikwenda kucheza mechi mbili mfululizo za ligi dhidi ya Azam na Tabora United (sasa TRA United) ikiwa na wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza majeruhi wengine wakitumikia adhabu.
Katika mechi dhidi ya Tabora United ambayo Yanga ilifungwa 3-1, ikalazimika Denis Nkane acheze beki wa kulia wakati ni winga. Pale mabeki wa kati alisimama Bakari Mwamnyeto na Aziz Andabwile, baada ya Job na Bacca kukosekana pia.
Mechi hizo mbili ziliitibulia Yanga msimu uliopita, safari hii imejirudia tena, mechi hizo zimefuata lakini sasa Yanga haijapoteza, imetoka sare licha ya changamoto hizo za majeraha, lakini bado imeshindwa kutibu ugonjwa wake.
PEDRO NA MASTAA WAKE
Kuna eneo lingine ambalo Pedro lazima ahusishwe kwa namna anavyoishi na wachezaji wake.
Wakati ambao Yanga imekumbwa na majeruhi wengi, anaonesha kushindwa kuwajenga wachezaji waliopo baadhi kwenye hali ya kuwa tayari kutumika.
Wengi wanajiuliza inawezekana ni kweli wachezaji kama Farid Mussa, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Aziz Andambwile na Kibwana Shomari wakashindwa kucheza kipindi ambacho kuna rundo la majeruhi, pia wakati wa mechi mfululizo ili kupunguza hatari ya waliotumika sana kuumia.
Kumbuka wakati mwingine majeraha ya wachezaji hutokea kutokana na kutopata muda mwingi wa kupumzika.
KOCHA WA VIUNGO
Vuta picha Yanga wakati makocha wa viungo walikuwa Helmy Gueldich, Taibi Lagrouni, timu hiyo ilikuwa inaonyesha wachezaji wake wako fiti muda wote wa mchezo.
Msimu huu mambo yamekuwa tofauti, wachezaji wengi wamekuwa wakiumia sana, hali ambayo inatafsiriwa kwamba hawako fiti kwa kiwango kikubwa.
Hapa lazima kuangaliwe upya endapo kutaonekana kuna shida kwa kocha wa viungo aliyepo sasa Chyna Mokaila au kuna ishu nyingine tofauti.