Maimuna kiungo Yanga aliyeishinda vita ya mjomba

KUNA msemo unasema' ukisema cha nini, wenzako wanasema watakipata lini' ndivyo ilivyotokea kwa kiungo wa zamani wa Simba Queens, Maimuna Hamis 'Maynaco' ambaye kwa sasa anaichezea Yanga Princess.
Maimuna hakuwa akipata nafasi ndani ya kikosi cha Simba jambo lililosababisha baada ya msimu uliopita kumalizika uongozi wa klabu hiyo kuamua kumuacha lakini amegeuka lulu kwa watani zao wa jadi Yanga kwani tangu atue kikosini msimu huu hajawahi kukaa benchi katika mechi zote ambazo timu hiyo imecheza hadi sasa.
Maimuna ameanza kikosi cha kwanza mechi zote na amecheza kwa ubora mkubwa akiwa kiunganishi muhimu kwa timu yake eneo la katikati huku akiwaweka bechi wachezaji wengi  wakiwemo wa kimataifa.
 
 

KUONDOKA SIMBA
"Ulipomalizika msimu uliopita nilipokea simu kutoka kwa meneja wa timu akaniambia kuwa wanataka wanitoe kwa mkopo kwenda timu yoyote ambayo nitataka na nitakuwa huru kuichezea.
"Mimi niliwakatalia na kuwaambia kuwa nina uamuzi wangu na siwezi kwenda timu yoyote kwa mkopo ninachowaomba waniache tu huru nikatafute changamoto nyingine sehemu ninayotaka na ndipo wakakubali na tukaachana kwa amani, "anasema Maimuna.
Anasema baada ya kuachana na Simba hakukaa muda mrefu akasajiliwa na Yanga kwa sababu walikuwa wanajua uwezo wake,
"Nilivyoachana na Simba tu kocha Edna Lema aliniita na kufanya mazungumzo nae na akanitaka nijiunge na Yanga kipindi hicho yeye bado anafundisha timu hii na nikakubali nikazungumza na uongozi hivyo nikapata nafasi ya kusajiliwa.
Anasema anafurahi kuwa Yanga na anamshukuru Mungu anapata mara kwa mara nafasi ya kucheza huku akiahidi kuendelea kupambana ili kucheza kikosi cha kwanza.
"Sio kwamba sikuwa na uwezo wakati niko Simba ndio maana nilikaa sana benchi lakini nafikiri kwa wakati huo kocha alikuwa na mipango yake na alikuwa anajua anataka nini kwa wakati huo.
"Nimekuja Yanga nimejiwekea malengo binafsi kwamba nimetoka Simba nilikuwa sichezi nimefika timu mpya lazima nifanye vizuri,"anasema Maimuna na kuongeza;
"Muhimu ukiweka malengo kisha ukiyaishi utafanikiwa tu.Nilivyotoka kule nilijiuliza kwa nini nilikuwa sipati nafasi, je nini tatizo, mapungufu yangu yalikuwa wapi ndipo  nikajituma, nikayafanyia kazi mapungufu yangu na namshukuru Mungu mambo yananiendea vizuri kwa sasa.


USHINDANI WA NAMBA
Yanga msimu huu imesajili buana, yaani ni full mziki katika kikosi hicho, ina wachezaji 10 wa kimataifa hivyo kuchangia ushindani mkubwa wa namba katika kikosi hicho lakini hilo wala halimpi shida Maimuna.
"Kukiwa na ushindani wa namba kwenye timu ni jambo zuri kwani inasaidia mchezaji kutobweteka kwani wengine wakishakuwa wanacheza sana wanaanza kujiona yeye ni yeye hata iweje atacheza tu na hata akiumwa atachomwa sindano na atacheza.
"Lakini kukiwa na ushindani kila mtu atakuwa makini kwani ataona nikikosea tu hapa mwenzangu anaweza kuchukua nafasi na nikapotea mazima hivyo hiyo inaongeza upambanaji kwa wachezaji wote, "anasema Maimuna na kuongeza.
"Pia uwepo wa wachezaji wengi bora kikosini kunaleta ushindani ambao pia utakuwa na manufaa kwa timu kwani wote mkijituma kwa bidii timu nayo inafanikiwa na kutimiza malengo yake.
Maimuna hakuelezea ushindani uliopo katika kikosi chao tu bali pia alisifu ushindani uliopo msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara.
"Msimu huu sio mchezo, ushindani wa ligi ni mkubwa tofauti na zamani kwani timu zilikuwa zikipigwa hata mabao 15 au 10 kwenye mechi moja lakini sasa hivi ukishinda  basi ni 1-0 au sare.
"Kikubwa ni kuyaomba makampuni mbalimbali na watu binafsi kujitokeza kudhamini ligi ya wanawake, kwani licha ya kwamba TFF wanajitahidi kwa sasa mdhamini yupo mmoja na hatoshi bado kuna matatizo mengi kwenye timu za wanawake
"Ligi yetu hivi sasa inaelekea kwenye ubora mkubwa hivyo wadhamini waje ili kuifanya ligi kuwa juu zaidi Afrika , "anasema Maimuna.


KIPIGO CHA MJOMBA
Maimuna alianza soka wakati akiwa shule ya msingi na baadae kupata ufadhili wa masomo ya sekondari katika shule ya Lord Baden inayomilikiwa na Kanali mstaafu,Iddi Kipingu baada ya kuonyesha kiwango kizuri kwenye mashindano ya Umisseta.
Baada ya kumaliza kidato cha nne akajiunga na timu ya Mburahati Queens alikocheza mwaka mmoja tu na mwaka 2017 akajiunga na timu ya JKT Queens ambapo aliisaidia kuchukua ubingwa msimu miwili mfululizo 2017/2018 na 2018/2019.
Msimu uliofuata akajiunga na Simba Queens aliyoichezea mpaka msimu uliopita walipoamua kuachana nae.
"Nikikumbuka hadi nafikia hapa namshukuru Mungu kwani nilikuwa na vita kubwa kutoka kwa mjomba wangu ambaye alikuwa ameishika sana dini na hakutaka mimi nicheze mpira.
"Mimi nimelelewa na bibi licha ya kwamba wazazi wangu wote wapo, sasa tangu nasoma nilikuwa napenda mpira wa miguu, mjomba alipokuwa akija nyumbani alikuwa ananipiga sana na kuchoma moto nguo zangu mazoezi, hakutaka kabisa nicheze mpira lakini niliendelea kukomaa na nashukuru bibi yangu alikuwa akiniunga mkono na hata wazazi wangu hadi leo wananiunga mkono, "anasema Maimuna.


MAHUSIANO
Wachezaji wengi wa kike wanaocheza mpira soka wamekuwa ni wagumu kuweka mahusiano yao wazi na wengine wala hawana mpango na mahuisno wala kuwa na familia na hata nilipomuuliza Maimunauko kwenye mahusiano au ndoa? aliishia kucheka tu.
"Najua kuna maisha nje na mpira, nahitaji familia, mume, watoto lakini kwa sasa mda bado haujafika ila nina malengo ya kuwa na familia yangu hapo baadae, "anasema Maimuna mabye anapenda sana kutazama katuni na picha za kutisha

 
UDUME JIKE
Tabia ya wachezaji wengi wa kike kuvaa mavazi ya kiume, kunyoa staili zinazoonekana kama za kihuni na wengine hata kutembea kidume ni jambo linalowakwaza wadau wengi wanaofuatilia soka la wanawake na hali hiyo inapelekea hata wazazi ambao watoto wao wana vipaji vya kucheza soka kuhofia kuwaruhusu kucheza mchezo huo kutokana na jambo hilo.
Hata hivyo msimu huu umeonekana kuwa na mabadiliko makubwa kwa wachezaji wengi kuonekana nadhifu kwa kujiweka kama wanawake ikiwemo kusuka mitindo mbalimbali ya nywele wanapokwenda kwenye mechi mbalimbali jambo ambalo linawavutia mashabiki wengi kwenye viwanjani.
"Kwanza tujipongeze kwa kipindi hiki tumebadilika kwa asilimia kubwa tofauti na zamani, sasa hivi hata wanaume wanavutiwa kuja uwanjani kuangalia mpira na wanaweza hata kutafuta mchumba na wakapata, "anasema huku akicheka na kuongezaa;
"Jambo tunalotakiwa kujua ni kwamba mpira wa wanaume haukubadilishi wewe muonekano haukubadilishi wewe maumbile yako hivyo sisi wenyewe binafsi tubadilike, tuishi kwenye misingi yetu, unaweza kucheza mpira na usiwe katika hayo mazingira.
"Najua wengine hali ya mtu kuwa kama dume dume ni kutokana na mazoea tukiwa kambini au mazoezini unakuta umevaa bukta au umevaa suruali ya nichezo sasa hali hiyo imewaingia taratibu lakini muhimu tubadilike kwani kuna muda unashusha hadhi na watu wanaanza kutuzungumzia tofauti,"anasema Maimuna ambaye anavutiwa zaidi na msanii Zuchu.
 

KOCHA EDNA HANA BAYA
"Namshukuru sana kocha Edna ukiacha kuwa ni mwalimu lakini pia ni mzazi, dada yaani ni mshauri mzuri sana kwa wachezaji wa kike.
"Tangu nikiwa JKT mwaka 2017 alikuwa akinifuatilia na kunishauri, nilipojiunga na Simba hivyo hivyo na hata wakati nakuja hapa amekuwa akinishauri vitu vingi ili niendelee kuwa bora, "anasema Maimuna ambaye pia amefurahi kukutana na kocha wake Sebastina Nkoma ambaye msimu uliopita alikuwa naye Simba Queens.