Maeneo ya kujificha ukiwa Morocco kuenjoi Afcon 2025
Muktasari:
- Mashindano ya Afcon 2025 yataanza Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026. Katika uzoefu wa kuandaa mashindano makubwa, Morocco ni mahali panapopendelewa kutokana na miundombinu yake bora ya ukarimu na mfumo wa usafiri ulio imara, vitu vinavyotarajiwa kuvutia maelfu ya mashabiki kwenye mashindano hayo.
CASABLANCA, MOROCCO: MAMBO iko huku, unaweza kusema hivyo. Katika kuelekea mashindano ya Afcon 2025, Morocco imeandaa maeneo mazuri na ya kuvutia kwa ajili ya kuwahudumia wachezaji na mashabiki watakaoenda kwenye mikikimikiki hiyo.
Mashindano ya Afcon 2025 yataanza Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026. Katika uzoefu wa kuandaa mashindano makubwa, Morocco ni mahali panapopendelewa kutokana na miundombinu yake bora ya ukarimu na mfumo wa usafiri ulio imara, vitu vinavyotarajiwa kuvutia maelfu ya mashabiki kwenye mashindano hayo.
Nchi hiyo ya Afrika Kaskazini imeonyesha uwezo mkubwa kwa miaka mingi wa kuhudumia kikamilifu timu za taifa, mashabiki na wapenzi wa mchezo wa soka. Kabla ya mashindano haya ya Afcon 2025, Morocco imewahi kuandaa CHAN, AFCON U17 na U23, AFCON ya wanawake, pamoja na Ligi ya Mabingwa ya Wanawake.
Mwaka 2019, Ufalme ulizindua akademia, kituo cha mafunzo kwa wanasoka chipukizi ambacho FIFA ilikitambua kuwa moja ya akademia kubwa na zenye mafanikio makubwa zaidi duniani. Mwaka huo, Morocco ilipokea zaidi ya watalii milioni 12, waliopangishwa katika vyumba zaidi ya 90,000 vilivyosambaa katika miji ya nchi hiyo. Serikali ya Morocco haikuridhika na hatua hizo tu, mwaka jana ilizindua mpango wa kuboresha hoteli za nchi kwa awamu mbili.
Mpango huo unaojulikana kama ‘Cap Hospitality’, unalenga kuboresha taasisi za malazi (EHTC). Kupitia mpango huo mikopo ya hadi dirham milioni 100 itatolewa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya hoteli, huku serikali ikilipa riba yote. Mikopo hiyo inayodumu hadi miaka 12 inalenga kuboresha vyumba 25,000, ikiwa ni pamoja na ukarabati, ununuzi wa samani na programu za kutumia nishati kwa ufanisi.
Miji itakayotumika Afcon 2025
Casablanca – Stade Mohammed V
Rabat – Uwanja wa Prince Moulay Abdellah
Marrakech – Grand Stade de Marrakech
Tangier – Stade Ibn Batouta
Agadir – Stade Adrar
Fez – Complexe Sportif de Fès
Uchaguzi wa miji hii ulizingatia ubora wa kiutendaji na kiufundi, hasa katika miundombinu ya michezo, malazi na usafiri inayokidhi viwango vya CAF.
Uwezo wa viwanja hivyo
Tangier: 60,000
Fes: 35,000
Rabat: 45,000
Casablanca: 45,000
Marrakech: 45,000
Agadir: 45,000
Kila mji una uwanja wa ndege wa kimataifa na unaweza kusafiri kirahisi kwa treni kwani miji yote imeunganishwa kwa reli. Morocco ina reli ya kasi (LGV) inayounganisha Tangier na Casablanca, iliyozinduliwa mwaka 2018 na Mfalme Mohammed VI, ikiwa ya kwanza barani Afrika.
Morocco, maarufu kwa urithi wake wa kitamaduni, mandhari maridadi na ukarimu, inatoa machaguo mengi ya malazi kwa kila aina ya msafiri. Iwe unataka hoteli za kifahari, malazi nafuu au sehemu za kipekee za Kimorocco, mwongozo huu utakusaidia kupata mahali pazuri pa kukaa wakati wa mashindano.
Chaguo za malazi
1. Hoteli za kifahari
Hizi ni hoteli za kiwango cha juu zenye vyumba vya kisasa na huduma za hali ya juu. Wakati wa baridi kali au joto la kiangazi, hoteli hizi kwa kawaida zenye bei ya juu, hutambulika kwa njia za kupoza au kupasha joto vyumba na maji ya moto ya kutosha. Bei ya malazi kwa usiku mmoja ni kati ya Dola 590.
Casablanca: Four Seasons Hotel Casablanca, Hyatt Regency Casablanca
Rabat: Sofitel Rabat Jardin des Roses
Marrakech: La Mamounia, Royal Mansour Marrakech
Tangier: Hilton Tangier Al Houara Resort & Spa
Hoteli hizi hutoa huduma bora, mandhari ya kuvutia na muunganiko wa ubunifu wa Kimorocco na starehe za kisasa.
2. Hoteli za kati
Bei kwa usiku mmoja ni takriban Dola 430, ambayo ni malazi ya bei za wastani.
Hoteli hizi ni kwa ajili ya wasafiri wanaotaka faraja kwa gharama ya wastani.
Mfano wa hoteli za kati ni Movenpick Hotel Casablanca, Kenzi Tower Hotel, ONOMO Hotel Rabat Terminus, Hotel Sahrai (Fez), Kenzi Europa (Agadir), Best Western Odyssee Park Hotel (Agadir), Kenzi Solazur (Tangier) na Mnar Castle Apartments (Tangier)
3. Malazi ya bajeti ndogo
Bei ya usiku mmoja ni karibu Dola 30. Haya ni malazi nafuu na mazuri kwa wasafiri wanaotafuta kuokoa gharama.
Mfano wa makazi hayo ni Hostel Maïssa (Casablanca), Ibis Casablanca City Center, Hotel Ali (Marrakech), Rodamon Riad Marrakech, Dar Al Batoul (Rabat), Funky Fes (Fez), Dar Hafsa (Fez), The Medina Hostel (Tangier) na Dar Nakhla Naciria (Tangier).
Katika baadhi ya maeneo, wageni hutumia magodoro kwenye paa au chini ya hema kubwa za Kiberber, chaguo la bei nafuu lakini lenye mvuto wa kitamaduni.
4. Riads
Riads ni nyumba za jadi za Kimorocco zilizo na bustani ya ndani. Mara nyingi huhusishwa na hadhi ya kifahari na huduma za kiwango cha hoteli ya nyota nne. Zinapatikana sana Marrakech na sasa nchini kote. Riads ni maarufu duniani kwa mtindo wao wa kipekee, ukarimu wa karibu, mandhari ya kuvutia na chakula kizuri.
Ndani ya riad unaweza kupata; Vyumba vya kimahaba, huduma binafsi, mandhari nzuri ya jiji kutoka kwenye paa, kiamsha kinywa kitamu na wakati mwingine chakula cha jioni. Ni sehemu nzuri kwa msafiri anayetaka utulivu ndani ya mji mkongwe (Medina).