ITRI: Gozi litakalotumika Morocco Afcon 2025
Muktasari:
- Ukiitwa jina la ITRI, mpira huo umebuniwa kwa hamasa ya saa ya kale ya Morocco, zellij huku ikinakshiwa na michoro na alama za kuonyesha umoja wa nchi za Afrika na mapenzi makubwa ya mchezo wa soka kwenye bara hilo.
RABAT, MOROCCO: SHIRIKISHO la soka la Afrika (CAF) kwa kushirikiana na kampuni ya vifaa vya michezo, PUMA, imetambulisha mpira maalumu utakaotumika kwenye mashindano ya Afcon 2025 yatakayoanza baadaye mwezi huu huko Morocco.
Ukiitwa jina la ITRI, mpira huo umebuniwa kwa hamasa ya saa ya kale ya Morocco, zellij huku ikinakshiwa na michoro na alama za kuonyesha umoja wa nchi za Afrika na mapenzi makubwa ya mchezo wa soka kwenye bara hilo.
Jina hilo la mpira linaelezea pia nyota iliyopo kwenye bendera ya taifa la Morocco huku michoro mingine iliyopo kwenye mpira huo ikiwakilisha utamaduni wa sanaa ya zellij.
Mpira huo wa ITRI utaanza kutumika kwa mara ya kwanza kwenye fainali hizo za Morocco. Muundo wa mpira huu una mvuto wa kipekee unaojumuisha michoro ya kijiometri ya zellij ya Kimorocco, inayotambulika kwa umbo la nyota katikati, mistari ya umbo la petali za maua na mpangilio wa mduara wenye ulinganifu. Kila sehemu ya muundo huu ina maana yake ya kitamaduni:
-Umbo la nyota linaashiria tamaa, mwanga, na utafutaji wa ubora katika hatua kubwa zaidi ya kandanda barani Afrika.
-Maumbo ya petali yanawakilisha shangwe, ukuaji na roho ya kufurahia inayobainisha mashindano ya Afcon.
-Ulinganifu wa mviringo unaakisi umoja wa mataifa 24 yanayokutana kwa ajili ya mashindano haya.
Muundo huu wa kipekee pia una michoro ya ‘Flow of Movement’, inayokamata muundo wa upekee wa mdundo na namna ya kucheza soka kwa ustadi barani Afrika. Mchanganyiko wa rangi nyekundu na kijani unaonyesha hamu, matumaini na fahari, huku pia ukilitolea heshima taifa la Morocco.
Kutoka jadi hadi ubunifu
Mchakato wa kubuni ulianza muda mfupi baada ya Morocco kuthibitishwa kuwa mwenyeji wa mashindano, na uliendelea kupitia hatua kadhaa za utafiti wa kitamaduni, ubunifu, majaribio ya utendaji na uboreshaji.
Ushirikiano huu uliunganisha timu ya ubunifu ya CAF na kitengo cha kimataifa cha usanifu cha PUMA ili kuhakikisha mpira unawakilisha kwa uhalisia sanaa ya Kimorocco huku ukiwa na mvuto wa bara zima.
Ukiwa umetengenezwa juu ya teknolojia ya PUMA Orbita 6, mpira huu unachanganya kwa urahisi urithi wa jadi na ubunifu wa kisasa, ukitoa viwango vya utendaji vinavyohitajika kwa mashindano ya kiwango cha juu huku ukisherehekea utamaduni wa Afrika.
Peter Dangl, Mkurugenzi wa Usambazaji EEMEA wa PUMA alisema: “Tunajivunia kuzindua mpira wa ITRI, mpira rasmi wa mashindano ya AFCON 2025 na ishara halisi ya roho ya kandanda la Afrika.
Kwa kuunganisha ubunifu wa sanaa ya Kimorocco na teknolojia ya juu ya utendaji. ITRI unasherehekea urithi wa taifa mwenyeji na umoja wa bara zima. Ushirikiano wetu na CAF unaonyesha dhamira ya muda mrefu ya PUMA kwa soka la Afrika na jamii zinazolipa uhai.”
Mashindano ya Afcon 2025 Morocco yataanza Desemba 21, 2025 ambapo mataifa bora zaidi ya kandanda barani Afrika yatachuana kuwania ubingwa wa bara hilo katika mchezo wa soka. Mpira huo unauzwa kwa Sh373,364 za Kitanzania.