Madege: Mayele ni balaa!

ILIKUWA safari ndefu yenye kilomita 103, kutoka Tabata Mwananchi hadi Chalinze anakoishi aliyekuwa mwenyekiti wa Yanga, Iman Madega, nia ya gazeti la Mwanaspoti ni kwenda kujua mambo mbalimbali ya soka na anachokifanya nje ya michezo.
Hatimaye baada ya mwendo mrefu, timu ya Mwanaspoti inafika nyumbani kwa kigogo huyo, inapokewa kwa tabasamu na unyenyekevu mkubwa, kisha anauliza “tuketi nje ama ndani?”, anaitikiwa “nje ili tufaidi upepo mwanana wa miti”.
Madega anajieleza: “Karibuni sana, sikutegemea mngenifuata umbali mrefu kiasi hiki, sipo mjini kwa sasa nimeamua kuhamishia shughuli zangu Chalinze, nimefurahi sana kuwaona, hakika Mwanaspoti ni gazeti makini na lina vijana wachapakazi.”
Anauliza: “Hamjapata usumbufu wa bodaboda baada ya kufika stendi ya daladala?” Anajibiwa kutoka timu ya Mwanaspoti: “Tumeshangazwa na jambo moja baada ya kutaja jina lako, wakatuambia wewe ni mbunge wao, wakatuuliza kama watupeleke ofisini kwako ama nyumbani, hakika hatujapata shida.”
Anatolea ufafanuzi kwa nini wanamuita mbunge wao, kwamba amewahi kugombea kwa nyakati tofauti na bado wanamtaka achukue fomu agombee kila unapotokea uchaguzi.
Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, amefunguka mambo mengi huku akitamka kwa mara ya kwanza kwamba katika uongozi wake aliandika katiba ambayo ndani yake aliweka vipengele vya sheria ya kuilinda Yanga na mali zake kwamba na mabadiliko ya uendeshaji yalianza ndani ya utawala wake 2006-2010.
MAISHA YAKE SASA
Ni miaka mitatu tangu Madega ameamua kuyarejesha maisha yake Chalinze, uamuzi ambao anabainisha alitamani kuufanya muda mrefu, ila changamoto za hapa na pale zilimzuia.
Anaeleza anachokifanya nyumbani kwake Chalinze ni kilimo na ufugaji.
“Nafanya kilimo cha kisasa kwa kutumia trekta, mfano eneo la hapa nyumbani navuna gunia 70 za mahindi, huko Morogoro ni zaidi, nalima miwa na zipo nazi na mengineyo,” anasema Madega na kuongeza;
“Nina kuku 3000, mbuzi 50, nafuga bata, kanga na ng’ombe, kiukweli nafurahia zaidi kufanya shughuli hizi na naona nilichelewa kurejea Chalinze.”
Nje na ufugaji na kilimo, amefungua ofisi yake ya uwakili, ana hoteli na biashara nyingine.
“Kwa sasa watu wamezoea ofisi yangu ya uwakala, maana mwanzo ilikuwa ni mjini, wateja wanakuja kama kawaida, ndio maana bodaboda waliowaleta wamewauliza wawalete nyumbani ama ofisini.”
UMAARUFU MKUBWA
Madega anasema amekuwa na jina kubwa sana, tofauti na alivyokuwa anachukuliwa mjini, jambo linalomfanya kuwa mwangalifu ili kulinda heshima yake isiingie matope.
“Siwezi kujiachia kunywa ama kufanya vitu vya hovyo hovyo kwasababu nina heshima kubwa katika kijiji hiki, kiukweli inanishangaza sana ninavyokubalika,” anasema.
CHANGAMOTO KIBAO
Anasema pamoja na kufurahia kurejea Chalinze, changamoto inayomkabili ni kukosa marafiki, anaowapata akienda Dar es Salaam.
“Tatizo kubwa la huku, wengi wao wameniweka daraja la juu sana, kiasi kwamba wanaogopa kunizoea, japokuwa wapo baadhi ninabadilisha nao mawazo ya hapa na pale, ila najihisi upweke, marafiki zangu wa zamani nakutana nao nikienda Dar es Salaam,” anasema.
JAMBO HILI HATOSAHAU
Anasimulia huku akicheka, anasema 2009 alipewa jukumu la kumsajili kiungo fundi Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye alimfuata Uwanja wa Muhimbili ambako walikuwa wanafanya mazoezi, alichomfanyia staa huyo, kilimfanya aandikwe kwenye magazeti kwa kuachwa njia panda.
Anasema alifika katika uwanja huo mida ya jioni, wakati huo Boban alikuwa amemaliza mkataba wake na Simba, alishangaa amekaa hadi usiku hamuoni mchezaji.
“Niliumia sana kumkosa Boban, maana nilimvizia sana niliamua kumfuata hadi katika mazoezi Uwanja wa Shule ya Msingi Muhimbili, aliponiona tu akasepa, najua waliotibua mambo ni Kaburu (Geofrey Nyange) na Mulamu Nghambi maana walikuwepo eneo hilo,” anasema Madega na kuongeza;
“Nilibakia kushangaa tu na kesho yake kwenye gazeti nilijikuta nimeandikwa Boban atoweka amchomesha mahindi Madega, nikasema sikubali nikawapiga bao la mwaka wa kumsajili kipa wao namba moja, nilimtumia mdogo wangu Beka aliyekuwa rafiki wa Juma Kaseja.”
Anasema Beka alifanikiwa kumshawishi Kaseja ambaye walimng’oa Simba kwa dau kubwa, jambo ambalo mashabiki wa Wanamsimbazi walishindwa kuamini.
“Beka alinipigia simu usiku, nilikwenda kumalizana na Kaseja muda huohuo, kibao kikageuka badala ya kuchomeshwa mahindi wakachomwa wao,” anasema.
YANGA YA SASA
Madega anasema, Yanga ya sasa ya kina Fiston Mayele, Khalid Aucho, Yannick Bangala na wengineo ni nzuri na ina ushindani mkubwa, lakini isibweteke kuongoza ligi ikafikiri ubingwa ndio wameishaupata.
“Mimi katika maisha yangu sio muumini wa kutoa sana sifa, ninachoweza kusema Yanga tuna timu nzuri sana, kila mchezji ana uwezo mkubwa kuanzia wanaoanza hadi wa benchi, hilo lisiwafanye kuiona Simba haina mpango wa ubingwa, waongeze umakini na upambanaji zaidi,” anasema.
ALIVYONG’ATUKA
Baada ya kutoka Kampala mashindano ya Cecafa Kagame Cup aliamua kufanya uamuzi mgumu wa kujiuzulu nafasi ya ujumbe ndani ya klabu ya Yanga wakati huo mwenyekiti wao akiwa ni Abbas Tarimba.
Anasema walienda kushiriki michuano hiyo na timu ikaondolewa mapema, jambo ambalo liliwakera Wanayanga, akaona uungwana ni kujiweka kando na kama kiongozi inampasa awajibike.
“Timu inapofanya vibaya anayestahili kuwajibika ni kiongozi, maana ndiye anayeandaa timu, ukisema ukae kimya sasa atawajibika shabiki? Kitu hicho hakiwezekani. Ingawa tulitimiza majukumu na kuweka bajeti kabisa ya michuano hiyo, nilifanya hivyo kwa lengo la kuleta amani,” anasema.
Anasema kitendo cha kujiuzulu kilimjengea heshima ya kuchaguliwa kwa mara nyingi hadi kuwa mwenyekiti mwaka 2006-2010.

HAKUYAPENDA HAYA
Anasema kwenye uongozi wake alikuwa hapendi idadi kubwa ya watu, jambo lililofanya aajiri katibu ambaye alikuwa ni marehemu Lawrence Mwalusako.
“Maana sikuona sababu ya watu kukaa klabuni bila kufanya kazi, sipendi uvivu, nilitamani mashabiki wa Yanga wawajibike kutoa michango inapotokea, ingekuwa ngumu kama wanashinda klabuni, pia kumuajiri katibu, nilikuwa na kazi zangu za uwakili, hivyo nisingeweza kupatikana muda wote kazini,” anasema.
Anaongeza: “Nilikuwa sina pesa za kuwapa sijui mabaunsa, ndio maana nilikuwa sipendi kuendekeza hayo mambo, watu wachape kazi, inapotokea klabu inahitaji mchango wanatoa.”
OFISI YA UWAKILI
Sio jambo dogo kuhamisha ofisi kutoka sehemu moja kwenda nyingine lakini kwa upande wa Madega aliweza kufanya hivyo kuitoa ofisi yake ya uwakili kutoka Dar es Salaam kwenda Chalinze.
Anasema hata alikohamia kazi yake ipo na anapata wateja katika ofisi yake japokuwa sio kwa kasi kubwa kama alipokuwa mjini.
KINARA WA MABADILIKO
Akiwa Mwenyekiti wa Yanga alianzisha wazo la kutaka mabadiliko na anajivunia kuona limepata mwamko wa kwenda kutimiza kile alichokuwa amekipanga miaka mingi nyuma.
“Kwanza kabisa hata siku Yanga wanaingia makubaliano na LaLiga kwa ajili ya mabadiliko walinialika na nilikwenda, niliona nimepewa heshima ya kipekee ya kuenzi kitu ambacho nilikiweka misingi imara ambayo inakwenda kuwa kwenye matendo,” anasema Madega
Anaongeza: “Sio hilo tu hata baada ya mchakato kuanza waliniweka kwenye kamati ya mabadiliko, naamini tutafika mbali sana kwa kuwa tuna nia ya dhati ya kufanikisha hilo.”
Anasema hata kabla ya kuwa mwenyekiti wa Yanga mwaka 2006-2010 alikuwa anapenda kuichangia Yanga ambapo wakati huo kulikuwana makundi mawili Seneta ambao walikuwa wanachanga pesa kubwa (laki mbili) na kundi la kawaida (Sh 10,000).
“Nilikuwa kundi la seneta ndio maana waliniambia nigombee na nikafanikiwa kuwa mwenyekiti, maana nilipenda zaidi kutoa kuliko kupokea,” anasema.
Anaongeza: “2002 kulikuwa na (makundi mawili yanayovutana) Yanga Kampuni na Yanga Asili, mwenyekiti alikuwa Tarimba, ndio maana hata wakati nimekuwa kiongozi nikayaweka kwenye mpangilio mzuri hayo mabadiliko,” anasisitiza.
Anasema makundi ya Yanga Asili na Yanga Kampuni yalileta mpasuko mkubwa klabuni hapo.
“Ilipelekea hadi marehemu (Reginald) Mengi kuingilia kati ili kuinusuru Yanga, muunganiko wa Yanga Asili na Yanga Kampuni ndio ukaja kuzaa uongozi wangu mimi, na nilipoingia madarakani jukumu langu la kwanza ilikuwa ni kutengeneza mfumo mpya, ishu ikaja nani awe mkubwa kati ya klabu au kampuni,” anasema na kuongeza kuwa 2010 ndio wakabadilisha katiba ikapita Yanga Kampuni.
“Pia nilifanikiwa kutengeneza sheria za kulinda nembo ya Yanga, thamani ya klabu ndio maana katika mabadiliko yanayoendelea kwa sasa wapo hatua ya kujua thamani ya mali za klabu kabla ya kuingia kwenye mfumo huo,” anasema.
URAIS TFF
Mwaka 2017 Madega alikuwa miungoni mwa wanamichezo waliojitosa kumng’oa Jamali Malinzi katika nafasi ya urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Anasema kutokana na uwezo wake mkubwa katika michezo ikiambatana na misimamo yake mikali aliona ni vyema kujitosa kuwania kiti hicho japokuwa hakuweza kufurukuta.
Madega aliwahi kuwa Mjumbe wa TFF, chini ya Leodgar Tenga ambaye anakiri ni kiongozi aliyekuwa na misimamo kama yake na mwenye kuweka uwazi wa mambo.
“Tenga ni kiongozi sana, yule, hapendi konakona, ndio kama mimi, napenda vitu vilivyonyooka ukipinda pinda hatuelewani,” anasema.
Amewataka viongozi wa TFF kufanya kazi na kuacha mapenzi japokuwa anatambua mapenzi ya hizo timu hayaepukiki hivyo wajitahidi kubadili hilo.
“Uongozi wa Tenga hakukuwepo malalamiko mengi kama ya viongozi waliofuata, viongozi wa Simba na Yanga walimuogopa sana kwani alikuwa mnyoofu na muumini wa kuzingatia kanuni,” anasema.
HATAMSAHAU MANJI
Anasema wakati huo kulikuwepo na sintofahamu wakati wa udhamini wa Yusuf Manji, ambaye wakati mwingine alikuwa anapenda kuendesha klabu wakati yeye alikuwa tajiri tu.
“Niliondoka kwa sababu nilihitaji unyoofu, kuna baadhi ya mashabiki walikuwa wakipewa pesa tu wanayumbishwa, jambo ambalo halikuwa zuri sana, niliweka mipaka uongozi na udhamini, siyo mdhamini aanze kuipangia klabu hiyo siyo sawa, nikaona ya nini, hilo linajidhihirisha baadaye akawa mdhamini na mwenyekiti pia,” anasema.
UKAME MIAKA MINNE
Anasema kitendo cha Yanga kushindwa kutamba kwa watani zao Simba miaka minne mfululizo iliyopita hadi sasa, kinaumiza Wanayanga, lakini ana imani ni upepo tu na wao watafanya vizuri.
“Hata mwaka huu nawashauri sana Yanga wajitahidi kupambana na kujituma na kila idara ifanye majukumu yake ipasavyo naamini timu yetu itafanya vizuri,” anasema akikumbushia Yanga ilivyowanyanyasa Simba kwa kutwaa mataji saba katika miaka 10 iliyotangulia kabla hii minne ambayo Wekundu wa Msimbazi wameshinda taji hilo mfululizo. Ndani ya miaka 10 hiyo kuanzia 2008 hadi 2017, Simba ilitwaa taji hilo mara mbili tu na nyingine ikibebwa na Azam wakati Yanga ililitwaa mara saba.
NENO KWA WANACHAMA
Madega anasema, katika vitu ambavyo vinamkwaza ni tabia mbaya ya mashabiki kuweka ubaguzi kwa viongozi kama hana pesa hata akipigania maslahi yao, wanakuwa hawamuungi mkono na kuwageukia matajiri hata kama wanajali maslahi binafsi.
“Tatizo katiba yetu haisemi kiongozi bora anatakiwa kuwa na shilingi ngapi, na niliweza kuondoa hali hiyo kwa kuwa mimi kwanza nilikuwa najiamini na pia naipenda Yanga, ilipelekea nikatoa neno kuwa ‘tajiri baki na mali zako ila tuachie timu yetu’, nilikuwa najiamini, uongozi na pesa ni vitu viwili tofauti,” anaisistiza.
ASHIRIKIANA NA SIMBA
Anasema yeye ni muumini mkubwa wa ukweli na uwazi na ndio maana alikuwa akishirikiana vilivyo na viongozi wa Simba na wanakaa meza moja na kuyajenga.
“Mimi na watu wa Simba wala hatuna shida hata kidogo, kwa kuwa hatuna uadui, utani maana yake wanafanya marafiki na siyo maadui, niliwahi kusaini mkataba wa Kilimanjaro ambao Simba ndio waliniita tukakaa na kufanikisha na ulikuwa udhamini mkubwa na mzuri uliotusaidia wote.”
Alipokuwa Dar es Salaam maskani yake kubwa ilikuwa ni Break Point ya Kijitonyama ambayo ni ya watu wa Simba na ni kijiwe kikubwa cha tawi la Friends of Simba.
“Nakumbuka jiko lilikuwa la Magori, aliyekuwa kama patna ni Harrison Mutembei alikuwa mwekahazina wa Simba, Daud Machumu mwenye eneo hilo naye alikuwa Simba, na ndiyo ilikuwa sehemu sahihi, na niliwahi kupata matatizo nikionekana na watu wa Simba, lengo langu nilikuwa najaribu kuondoa dhana ya uadui kwenye michezo.
“Mimi niliwauliza Rais wetu Kikwete ni Yanga, lakini mbona alimpa uwaziri Juma Kapuya na hakuna shida? Hawakuwa na la kunijibu na nilichokipenda kwa sasa cha wazi wazi Haji Manara kutoka Simba kwenda Yanga,” anasema.
Pamoja na ushirikiano waliokuwa wanaufanya katika kujenga maendeleo ya soka, anasema Simba iliwasaliti baada ya kukubaliana wasishiriki michuano ya Kombe la Kagame, jambo ambalo aliingia kwenye mgogoro na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholaus Musonye.
“Tulikubaliana tugome baada ya Musonye kuonekana kutaka kuchukua mapato mengi lakini wenzetu Simba wakasaliti waliamua kupeleka timu walitukwaza sana kusema ukweli ilikuwa 2010 kama sijasahau,” anakumbuka.
KUMBE SAKATA LA IVO
Anasema kuna mechi walichezea Morogoro, Ivo Mapunda alifungwa bao ambalo Wanayanga wakaona kama amechukua mlungula Simba, baada ya kumuona wanamzonga, akamfuata ili ampeleke kambini kwa usalama wake, lakini akakaidi na kupanda gari lake kurejea Dar es Salaam.
“Wanachama wanamzonga kutaka kumfanyia vurugu halafu yeye hataki kutii, nikajiuliza je, wakimzuia njiani wakamuumiza tutaonekana viongozi na wazembe, maana mimi niliamini matokeo yale ni moja ya yale matatu, kufungwa, kushinda na sare ndio maana nikawapongeza Simba maana ndio uungwana wa mchezo,” anasema.
“Tuliporejea Dar nikamuita akagoma, nikakaa na kamati nikamfungia miezi sita, alikuwa kipa namba moja Yanga na Stars, nilipata changamoto lakini nikasema atadaka Jackson Chove na akafanikiwa kufanya vizuri tukachukua ubingwa, Mapunda aliona kwamba nipo sawa ni kati ya wachezaji ambao wananiheshimu sana kila ninapokutana naye,” anasema.
KAMATI ZA UFUNDI ZIPO
“Ni kweli hizo kamati zipo, lakini mie siziamini sana, kwa kuwa mambo yanabadilika lakini ndio mambo ambayo tumeyakuta katika timu na yanaleta utulivu mkubwa, na kuna watu wanaamini hata kama una benchi zuri na wachezaji wazuri lakini kamati ya ufundi muhimu.
“Nakumbuka ilinitokea, kulikuwa na mechi moja hivi, usajili wetu ulikuwa unaonekana dhaifu, Azam walikuwa bora na Simba pia, lakini mechi ya kwanza ya Simba na Azam Simba alipigwa, mchezo uliofuata Yanga na Azam wale wazee (waganga) wakati mechi inakaribia nilidhani watanipigia kuchukua hela ya kazi lakini haikuwa hivyo.
“Wakanijibu washaona tumechukua hela Azam, na eti waliichungulia mechi wakaona Azam itashinda, basi tukawaacha, tukaandaa timu bila kuroga na tukashinda 3-0.”