Mabondia 10 bora wa kike Tanzania
Muktasari:
- Mabondia kama Zulfa Macho, Stumai Muki, Sara Alex, Debora Mwenda, Lulu Kayage na Jesca Mnanga ndiyo unaweza kusema angalau majina yao yanaweza kujulikana kwenye ngumi za kulipwa.
KATIKA mchezo wa ngumi za kulipwa Tanzania upande wa wanawake wamekuwa wa kipata nafasi ndogo ya kutambulika katika jamii licha ya juhudi zao kubwa wanazozifanya kwenye mchezo huo.
Mabondia kama Zulfa Macho, Stumai Muki, Sara Alex, Debora Mwenda, Lulu Kayage na Jesca Mnanga ndiyo unaweza kusema angalau majina yao yanaweza kujulikana kwenye ngumi za kulipwa.
Lakini ukiangalia kwenye ngumi za ridhaa ambazo ndiyo zimekuwa msingi mzuri wa mabondia wengine kupata maarifa ya kutoka ni bondia mmoja pekee ndiyo amepata nafasi ya kujulikana kutokana na juhudi na rekodi kubwa alizoziweka.
Hapo utakutana na jina la bondia Grace Mwakamele ambaye ni mwajiriwa wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutokana na kuwa bondia wa kwanza nchini mwanamke kushinda medali katika ngumi za ridhaa tangu nchi ipate uhuru.
Bondia huyo ndiye anayeshikilia rekodi kubwa akishinda tuzo ya mwanamichezo bora wa kike kwa mwaka 2023 katika mchezo huo kwenye tuzo ambazo zimetolewa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Mwanaspoti linakuchambulia mabondia kumi bora wa kike Tanzania walioorodheshwa katika ngumi za kulipwa kupitia pauni kwa pauni ‘P4P’ ambayo ipo kwenye mtandao wa boxrec unaotumika kuhifadhi taarifa za mabondia duniani.
1. Rehema Abdallah
Licha ya kupotea kwa kipindi kirefu na kupitia misukosuko ya maisha, bondia Rehema Abdallah ndiye anayeshikilia nafasi ya kwanza yaani ‘malkia wa ngumi Tanzania’ kwa sasa.
Bondia ambaye ametoka kushinda ubingwa wa Pugilistic Syndicate wa Tanzania (PST) visiwani Zanzibar kwa kumchapa Muingereza, mwenye asili ya India, Sangeeta Bird kwa pointi katika pambano lililofanyika Agosti 15, Zanzibar.
Rehema ana rekodi ya kushinda mapambano 11 huku tisa ni kwa ‘KnockOut’ na mawili kwa pointi katika mapambano 12 aliyocheza yakiwa sawa na raundi 40 ambayo kila raundi moja upande wa wanawake ikichezwa kwa dakika mbili pekee.
Bondia huyo anayeshikilia nafasi ya kwanza yaani ‘Tanzania One’ upande wa wanawake wote pia anakamata nafasi ya kwanza kwa mabondia wanawake kati ya mabondia sita wa uzani wa Light nchini lakini akiwa bondia wa 25 duniani kwenye mabondia 190.
Rehema ndiyo bondia pekee kati ya mabondia hao aliyefikia nyota moja na nusu huku uwezo wake wa kushinda KnockOut ukiwa ni asilimia 80.82.
2. Halima Vunjabei
Mmoja kati ya mabondia wa siku nyingi katika mchezo wa ngumi za kulipwa akiwa na rekodi ya kipekee kutokana na kucheza mapambano mengi zaidi kwenye mchezo huo, Halima Vunjabei ndiyo anakamata nafasi ya pili katika mabondia bora wa Tanzania.
Vunjabei amekaa kwa muda mrefu kwenye nafasi ya kwanza kabla ya kung’olewa kwenye nafasi hiyo na Rehema Abdallah akiwa na rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 28 akishinda mapambano 14 pekee kati hayo, manane ni kwa KO huku akipigwa mara 13 kati ya hizo moja ni kwa KO na ametoka sare mara moja.
Vunjabei mwenye hadhi ya nyota moja kamili ndiyo bondia namba moja katika mabondia wanne wa uzani wake wa bantam huku akiwa bondia wa 65 katika mabondia 225 wa uzani huo duniani huku uwezo wake wa kutoa vichapo kwa KO ukiwa ni aslimia 57.14.
3. Nasra Msami
Sifa yake kubwa ni upole akiwa amejaliwa urefu wa kutosha mithili ya Twiga wanaopatikana katika hifadhi na mbuga kubwa za wanyama nchini.
Msami ni bondia ambaye anakamata nafasi ya tatu akiwa na rekodi ya kucheza jumla ya mapambano matano ambayo ameshinda yote, huku mawili akipata ushindi wa KnockOut.
Bondia huyu anashikilia nafasi ya pili kwenye uzani wa Light nyuma ya kinara wa uzani huo Rehema Abdallah nchini huku akiwa bondia wa 38 duniani kwenye mabondia 190 wanaopatikana kwenye uzani huo.
Msami mwenye miaka 26 uwezo wake wa kushinda KnockOut ni asilimia 40 pekee kwenye mchezo huo.
4. Stumai Muki
Huyu ni mmoja kati ya mabondia ambao wanatambulika na wengi katika mchezo huo kutokana na mapambano yake mengi kupata nafasi ya kurushwa na kituo kikubwa cha luninga nchini, akifahamika zaidi kama Stumai Muki.
Muki ambaye asili yake Kigoma, amecheza jumla ya mapambano 14 ambayo sawa na raundi 90.
Bondia huyo rekodi yake imekuwa ya kipekee kutokana na kushinda mapambano kumi lakini hajui utamu wa kushinda kwa KO lakini amepigwa mara nne na moja kati ya hizo ni KnockOut.
Muki ambaye anakamata nafasi pili katika mabondia wawili wa uzani wa fly Tanzania, duniani anashika nafasi ya 56 kati ya mabondia 191 akipewa hadhi ya nyota moja.
5. Sarah Alex
Arusha katika mchezo wa ngumi upande wa wanawake imekuwa ikiwakilishwa vyema na Sara Alex kutokana na kufanya vizuri kwenye mapambano yake ikiwemo kuingia kwenye P4P ya mabondia bora wa Tanzania.
Alex ambaye pia anajulikana zaidi kama ‘Miss GB wa Arusha’ kutokana na kuvutiwa na bingwa wa dunia, Muingereza, Natasha Jonas ‘Miss GB’, ana rekodi ya kucheza jumla ya mapambano sita na kati ya hayo ameshinda manne.
Bondia huyu hajaonja utamu wa ushindi wa KnockOut katika mapambano hayo sita aliyocheza huku akiwa amepigwa mara moja na kutoka sare mara moja.
Alex ambaye ni bondia namba moja kwenye uzani wa super fly katika mabondia wawili wa uzani huo nchini, kwa dunia anashika nafasi ya 61 kati ya mabondia 171 wa uzani huo.
6. Jesca Mfinanga
Sifa yake kubwa ni kuweza kupangilia maneno mabovu ya kutia hasira kwenye mchezo wa ngumi na wala usiombe kupewa nafasi ya kupigana na Jesca Mfinanga kwani sehemu ya kwanza atakupiga kwa maneno.
Mfinanga ambaye pia ni mtoto wa mwamuzi wa kimataifa wa mchezo huo, Pendo Njau mpaka sasa amecheza mapambano tisa pekee.
Katika mapambano hayo bondia huyo ameshinda matano kati ya hayo moja ni kwa KnockOut na amepigwa katika mapambano matatu huku moja ni kwa KO na ametoka sare moja.
Mfinanga anayepanda ulingoni kwenye uzani wa fly akiwa na nusu nyota anakamata nafasi ya kwanza katika mabondia watatu wa uzani huo nchini huku akiwa bondia 88 duniani katika mabondia 240 wa uzito huo.
7. Zawadi Kutaka
Inaelezwa kwa sasa amekuwa mbali na mchezo wa ngumi za kulipwa kutokana na kubanwa na masuala ya mafunzo ya kijeshi, lakini bado haijamfanya bondia Zawadi Kutaka apoteze nafasi yake kwenye orodha ya mabondia bora wa Tanzania.
Kutaka ana rekodi ya kucheza jumla ya mapambano saba akiwa ameshinda manne kati ya hayo mmoja akipata ushindi wa Knockout huku akiwa amepigwa mara mbili moja kati ya hizo ikiwa ni Knockout na moja akitoka sare.
Bondia huyo mwenye hadhi ya nusu nyota anakiwasha kwenye uzani wa Superfly, anakamata nafasi pili nyuma ya kinara Stumai Muki huku akiwa bondia wa 75 duniani katika mabondia 191 wa uzani huo.
Kutaka amepewa asilimia 25 ya kuweza kushinda Knockout katika mapambano yake kwenye mchezo huo.
8. Tatiana Ezekiel
Moja ya vitu vikubwa ambavyo amebarikiwa bondia Tatiana Ezekiel ni uwezo kutawala ulingo.
Rekodi zinaonyesha amecheza jumla ya mapambano manne katika mchezo huo na ameshinda pambano moja na kupoteza moja huku mawili akiambulia sare.
Bondia huyo mwenye hadhi ya nusu nyota, anacheza kwenye uzani wa feather huku yeye akiwa ni bondia namba moja katika mabondia wawili wa uzani huo nchini.
Tatiana anakamata nafasi ya 84 duniani katika mabondia 202 wa uzani huo huku kiwango chake cha kushinda kwa Knockout ikiwekwa sifuri.
9. Najma Isike
Ukitaja idadi ya mabondia wavumilivu au wenye usugu ndani ya ulingo basi jina la Najma Isike haliwezi kukosa kutokana na kuwa bondia asiyekubali kupotea haraka.
Najma ana rekodi ya kucheza jumla ya mapambano manane ambayo ni sawa na raundi 89 za dakika mbili kwa kila raundi ambapo ameshinda mapambano matatu na amepigwa mara tano kati ya hizo mbili ni kwa Knockout na wala hajawahi kutoka sare.
Bondia huyo wa uzani wa super feather ndiyo anashikilia rekodi ya kuwa bondia pekee kwenye uzani wake nchini, lakini ni wa 74 duniani katika mabondia 192 wa uzani huo.
Najma hajawahi kuonja au kutambua utamu wa ushindi wa Knockout hali ambayo imemfanya kupewa asilimia 0 kabisa licha ya kuwa na hadhi ya nusu nyota.
10. Grace Mwakamele
Mshindi wa tuzo ya mwanamichezo bora upande wa wanawake kwa mwaka 2023 bondia Grace Mwakamale ndiyo amefunga dimba la mabondia kumi bora wa Tanzania kwa mujibu wa mtandao boxrec.
Bondia huyo ambaye ni askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) anashikilia rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 13 ambayo sawa na raundi 51.
Mwakamele ambaye amepata tuzo kutokana na mafanikio yake katika ngumi za ridhaa, ameshinda mapambano tisa kati ya hayo sita ni kwa Knockout na mapambano matatu akipata ushindi wa pointi.
Bondia huyo amepoteza katika mapambano manne kati ya hayo mawili ni kwa Knockout ambapo ndiyo bondia namba moja katika uzani wa super walter nchini akifuatiwa na Fatuma Yazidu na Happy Daud huku akishika nafasi ya 27 katika mabondia 57 duniani wa uzani huo.
Mwakamele mwenye hadhi ya nusu nyota, uwezo wake wa kuchapa wapinzani wake kwa Knockout ni asilimia 66.67, kwa mujibu wa mtandao wa viwango vya mabondia duniani wa Boxrec.