Prime
Mabao 12 ‘aliyopeana’ John Noble Ligi Kuu Bara

Muktasari:
- Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Kocha wa Fountain Gate, Robert Matano alimtupia lawama za wazi kipa huyo akisema: “Kipindi cha kwanza tumepeana, golikipa amepeana kabisa, huwezi kufanya makosa kama hayo timu ikarudi kwenye mchezo. Ni ngumu sana.
TUHUMA zinazomkabili kipa wa Fountain Gate, John Noble, raia wa Nigeria hadi uongozi kumsimamisha kupisha uchunguzi ni kucheza chini ya kiwango dhidi ya Yanga huku akidaiwa kuchangia timu yake kupoteza mchezo wa Ligi Kuu Bara kwa mabao 4-0, Aprili 21, 2025, kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara.
Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Kocha wa Fountain Gate, Robert Matano alimtupia lawama za wazi kipa huyo akisema: “Kipindi cha kwanza tumepeana, golikipa amepeana kabisa, huwezi kufanya makosa kama hayo timu ikarudi kwenye mchezo. Ni ngumu sana.
“Mazoezini amekuwa akishika lakini leo (Aprili 21, 2025) ametuangusha kabisa, hawezi kufanya makosa kama yale kwa golikipa wa kariba ya juu kama yeye, ametutoa kwenye mchezo kabisa. Mechi zingine tutaendelea kucheza lakini kama mtu anapeana kama vile tutashindwa kabisa.” Kwa Wakenya neno kupeana ni kama kutoa zawadi.
Katika mchezo huo ambao Noble alitolewa mara tu baada ya kuruhusu bao la pili dakika ya 43, alionekana kucheza chini ya kiwango huku akiruhusu mabao mepesi.
Bao la kwanza ulikuwa mpira wa kutengwa ambao Stephane Aziz Ki alipiga krosi iliyogongwa na beki wa Fountain Gate katika harakati za kuokoa ukamfikia Noble ambaye alimtemea Clement Mzize na kufunga dakika ya 38.

Tukio la pili ni dakika ya 43, Noble alitoka nje ya 18 akawa anajaribu kumpiga chenga Prince Dube, ndipo akakosa balansi na kujikuta akitoa pasi kwa Aziz Ki aliyeunganisha moja kwa moja nyavuni.
Matukio hayo mawili, haraka yakalifanya benchi la ufundi likiongozwa na Kocha Robert Matano, kumtoa kipa huyo na kumuingiza Rashid Parapanda ambaye naye aliruhusu mabao mawili dakika ya 70 na 89 ingawa yake yalionekana ni sehemu ya mchezo, hivyo hakuangushiwa lawama.
Hii si mara ya kwanza kwa Noble kuruhusu mabao mepesi katika Ligi Kuu Bara kwani rekodi zinaonesha amefanya hivyo mara kumi kuanzia msimu uliopita 2023-2024 alipoanza kuitumikia Tabora United.
Noble ambaye huu ni msimu wake wa pili anacheza Ligi Kuu Bara, kwa mara ya kwanza alitua Tabora United akitokea Enyimba FC ya kwao Nigeria. Kabla ya hapo, pia alicheza ASC Kara ya Togo.
Kufuatia kiwango cha chini alichoonesha Noble dhidi ya Yanga huku ikihusishwa na masuala ya rushwa hali iliyofanya klabu yake kumsimamisha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nayo imejitosa kufanya uchunguzi wake.
Ofisa Habari wa Fountain Gate, Issa Liponda ‘Mbuzi’ anasema: “Baada ya uchunguzi kufanyika tutakuja kusema majibu ya kile tulichokipata kutokana na tuhuma zinazomwandama, hiyo ndiyo sababu ya kumsimamisha. Viongozi wa timu wameshampa barua ya kusimama kuitumikia timu, hatujui atasimama kwa muda gani.”
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Manyara, Bahati Haule anasema ofisi yao haijapata rasmi malalamiko yoyote juu ya mchezaji huyo, lakini baada ya kusikia mitaani kuwa huenda kukawa na mazingira ya rushwa yaliyotumika kwa Noble hadi kusababisha kufungwa mabao ya uzembe, wameamua kufuatilia.
“Ni kweli hata sisi tumesikia kuwa magoli aliyofungwa huyo kipa yalikuwa na utata kwamba bao la kwanza alipigiwa shuti dogo akatema mpira kwa uzembe na goli la pili alirudisha mpira golini,” anasema Haule.
Anasema wanafanya hivyo kwa mujibu wa sheria ya Takukuru kifungu cha 15 kilichofanyiwa marekebisho na kupitishwa na Bunge mwaka 2024.
“Sheria hiyo imeongezewa suala la kuwa rushwa ya uchaguzi, rushwa michezoni, kamari na michezo ya kubahatisha na mambo ya burudani,” anabainisha Haule.
Fountain Gate msimu huu imekuwa na rekodi mbovu ya kuruhusu mabao mengi zaidi kwenye Ligi Kuu Bara yakifika 51, KenGold inafuatia kwa nyavu zake kutikiswa mara 50 baada ya zote kucheza mechi 27.
Katika mabao hayo 51, yametokana na kufungwa makipa wanne tofauti wa kikosi cha Fountain Gate ambao ni John Noble aliyecheza mechi 16 akiruhusu mabao 31 na kupata clean sheet mbili huku akionyeshwa kadi nyekundu moja katika mchezo dhidi ya Simba uliomalizika kwa sare ya 1-1, Februari 6, 2025.
Fadhili Kisunga amedaka mechi mbili na kuruhusu mabao matatu wakati Rashid Parapanda amecheza mechi moja ambayo alitokea benchi na kuingia dakika ya 44 dhidi ya Yanga, akaruhusu mabao mawili.
Fikirini Selemani Bakari ambaye alikuwa hapo kwa mkopo akitokea Singida Black Stars na sasa anaichezea Tabora United pia kwa mkopo, alidaka mechi tisa akiruhusu mabao 16 akipata clean sheet moja. Mechi ya mwisho alidaka Novemba 5, 2024 dhidi ya Pamba Jiji, Fountain Gate ilichapwa 3-1 nyumbani, ikaonekana ameruhusu mabao kirahisi ndiyo ikawa mwisho wake.
MABAO 12 ‘ALIYOPEANA’
Kama alivyosema Kocha Matano, John Noble alipeana mabao dhidi ya Yanga katika kipigo cha 4-0 akimaanisha aliwapa zawadi wapinzani wao kutokana na kufungwa kirahisi, tunakukumbusha namna ambavyo mabao 12 aliyofungwa kipa huyo kati ya 62 katika jumla ya mechi 42 za Ligi Kuu Bara alizocheza ndani ya misimu miwili. Katika mabao hayo 12, manane yalikuwa msimu uliopita akiwa Tabora United, huku manne akifungwa ndani ya Fountain Gate msimu huu.
Ikumbukwe kuwa, msimu uliopita 2023-2024, Noble akiwa Tabora alidaka mechi 27 za ligi na kuruhusu mabao 31, huku msimu huu 2024-2025 amedaka mechi 16 na kuruhusu idadi hiyohiyo ya mabao na kufanya jumla misimu miwili amefungwa mabao 61. Ana cleansheet 11, tisa alizipata msimu uliopita na mbili msimu huu.

SEPTEMBA 15, 2023
Katika mchezo huu uliochezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, wenyeji Tabora United waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Tanzania Prisons. Mabao ya Tabora United yalifungwa na John Ben dakika ya 42 na 90+2 na Eric Okutu (dk 58). Lile la Tanzania Prisons mfungaji ni Samson Mbangula dakika ya 70.
Bao hilo la Mbangula linaonekana kuwa rahisi kufungwa Noble kufuatia mabeki kujichanganya na kumkuta mfungaji ambaye hakupiga shuti kali sana, likapita tobo kwa kipa huyo akiwa amesimama hana la kufanya, na kujaa wavuni.
OKTOBA 6, 2023
Tabora United iliichapa Dodoma Jiji mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi. Wenyeji walitanguliwa kwa bao la Yasin Mgaza dakika ya pili baada ya Noble kushindwa kutokea mpira mrefu uliopigwa eneo lake na kumuachia beki apambane na mfungaji huku yeye akibaki golini, ikawa rahisi kufungwa.
Hata hivyo, Tabora United ilijipanga upya, ikasawazisha kupitia Erik Okutu dakika ya 50 kisha Abas Athuman akafunga la ushindi dakika ya 90+5.
DESEMBA 23, 2023
Kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Tabora United iliikaribisha Yanga, mchezo huo ulifanyika hapo baada ya Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kufungiwa. Aziz Ki alifunga bao pekee lililoipa Yanga ushindi wa 1-0, hata hivyo bao hilo lilionekana kuwa ni uzembe wa kipa Noble ambaye alisogea mbele na kuacha nafasi iliyotumiwa vizuri na Aziz Ki kumchungulia kwa mbali akafunga faulo ya moja kwa moja.
FEBRUARI 6, 2024
Kichapo cha mabao 4-0 ilichokipata Tabora United kwenye uwanja wake wa nyumbani Ali Hassan Mwinyi, kilikuwa na mabao ya kiufundi lakini moja lilionekana uzembe wa kipa Noble.
Pa Omar Jobe alianza kufunga dakika ya 20, kisha Sadio Kanoute (dk 36), Che Malone Fondoh (dk 60) na Freddy Michael (dk 87).
Bao la Che Malone ndilo lililozua maswali mengi kufuatia Noble kwanza kushindwa kudaka mpira wa kona uliopigwa na Saido Ntibazonzkiza ambao uliteleza mikononi mwake na kumfikia Clatous Chama aliyeurudisha eneo la hatari, kisha mfungaji akapiga shuti hafifu na kufunga kirahisi huku akimuacha kipa ameganda.
FEBRUARI 11, 2024
Sare ya bao 1-1 kati ya Tabora United dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, ilifanya Noble pia kuonekana akiendelea kufanya makosa yaleyale ya kuruhusu mabao rahisi. Erick Okutu alianza kuifungia Tabora United dakika ya 11, kabla ya Pius Buswita kusawazisha dakika ya 37 ambapo bao lake hilo lililotokana na faulo iliyopigwa mpira ulionekana unakwenda nje, Noble akaufuata juu na kujaribu kuudaka akajikuta anaurudisha uwanjani na kumtengea mfungaji ambaye hakufanya kosa, akafunga

FEBRUARI 28, 2024
Kwa mara nyingine, Noble anarudia kosa la kumtemea mfungaji mpira baada ya kushindwa kudaka shambulizi la kwanza. Hiyo ilitokana na faulo iliyopigwa langoni mwake, Samson Mbangula akaunganisha kwa kichwa na Noble kuupangua mpira uliomfikia Zabona Mayombya na kuitanguliza Tanzania Prisons dakika ya 21. Katika mchezo huo, Tanzania Prisons ikiwa nyumbani Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, ilishinda 2-1. Bao lingine lilifungwa na Mbangula dakika ya 88. Lile la Tabora United mfungaji akiwa Eric Okutu dakika ya 17.
MACHI 10, 2024
Wakati Wazir Junior anapiga hat trick katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Dar huku KMC ikishinda 4-2 dhidi ya Tabora United, Noble alifanya kosa lingine la ‘kupeana’.
Ilikuwa ni bao la kwanza lililofungwa na Daruesh Saliboko dakika ya 44 ambapo alishindwa kucheza krosi na kumtengea mfungaji, akauweka nyavuni.
Katika mchezo huo, mabao mengine ya KMC yalifungwa na Wazir Junior dakika ya 49, 60 na 67. Yale ya Tabora United yalifungwa na Daniel Lukandamila dakika ya 84 na 90+2 kwa penalti.
APRILI 13, 2024
Bao alilofungwa Noble katika mchezo huu ambao Tabora United ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, linafikirisha sana.
Heritier Lulihoshi aliiweka mbele Tabora United kwa bao la dakika ya 72, ikaonekana wenyeji wanakaribia kabisa kuondoka na pointi tatu, lakini kilichotokea dakika ya 90+2 ilibaki kuwa maumivu makubwa kwao.
Ilipigwa krosi ambayo Noble aliruka juu na kuudaka vizuri mpira, lakini alipotua chini, akauachia mpira ukawahiwa na Ismail Aziz Kader, kisha Noble akamfanyia faulo ndani ya boksi, ikawekwa penalti. Said Ndemla akaenda kupiga, Noble akapangua lakini Martin Kigi akamalizia kwa kuuweka mpira kambani, mechi ikaisha 1-1.
OKTOBA 28, 2024
Baada ya kutoka Tabora United, 2024-2025 Noble ametua Fountain Gate ambapo ameendelea kufanya makosa yaleyale ya kupeana. Katika mchezo uliomalizika kwa sare ya 2-2 kati ya Fountain Gate dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, alifunga bao mpira uliopita palepale akiwa amesimama akibana mwamba. Mfungaji alikuwa Hassan Hadji ‘Cheda’ dakika ya 28. Bao lingine la kawaida alifunga Seif Karihe dakika ya 15. Yale ya Fountain Gate wafungaji ni Nicholas Gyan dakika ya 3 na Salum Kihimbwa ile ya 90+3.
DESEMBA 13, 2024
Licha ya Fountain Gate kushinda 3-2 dhidi ya Coastal Union, lakini Noble aliruhusu bao moja la kizembe lililofungwa na Maabad Maulid dakika ya 79 baada ya kuutema mpira mbele yake kutokana na shuti la Maulid Shaban. Lucas Kikoti alifunga bao lingine la Coastal kwa penalti dakika ya 44. Huku Wenyeji Fountain wakiwa uwanja wao wa Tanzanite Kwaraa wakifunga kupitia Elie Mokono (dk 14), Edgar William (dk 47) na Nicholas Gyan (dk 54 kwa penalti).
APRILI 21, 2025
Fountain Gate ikiwa nyumbani Uwanja wa Tanzanite Kwaraa ilifungwa mabao 4-0 na Yanga, mchezo huo ndio umezua sekeseke zaidi.
Bao la kwanza, Noble alifungwa baada ya mpira wa faulo uliopigwa na Stephane Aziz Ki katika harakati za beki wa Fountain Gate kuokoa, ukamfikia Noble ambaye alimtemea Clement Mzize na kufunga dakika ya 38. Kisha bao la pili dakika ya 43, Noble alitoka nje ya 18 akawa anajaribu kumpiga chenga Prince Dube, ndipo akakosa balansi na kujikuta akitoa pasi kwa Aziz Ki aliyeunganisha moja kwa moja hadi nyavuni. Mabao mengine mawili alifungwa Rashid Parapanda dakika ya 70 na 89, baada ya kuingia kipindi cha kwanza kuchukua nafasi ya Noble.

MSIKIE IVO, FATHER
Kipa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Ivo Mapunda, amezungumzia makosa aliyofanya Noble katika mchezo dhidi ya Yanga, ambapo anasema: “Nikizungumzia kiwango katika mchezo huo kilikuwa chini, hali hiyo inamshushia heshima kama kipa wa kigeni ambaye anatakiwa afanye zaidi ya kile kinachotakiwa kufanywa na wazawa ndiyo maana mashabiki wamekuwa na wasiwasi naye ingawa kiufundi nikiwa kama kocha naona ni makosa ya kizembe.
“Mfano bao la pili baada ya kutoka ndani ya 18 alipaswa aupige mpira mrefu, sasa akawa anataka apige chenga alirudi nao ndani, wakati anafahamu anacheza na Yanga iliyo na washambuliaji hatari, mechi kubwa za Simba na Yanga ndizo alitakiwa aoneshe ukubwa wake na ukomavu wa kuibeba timu.”
Naye kipa wa zamani wa Simba na Taifa Stars ambaye aliwahi kufundisha makipa wa Simba, Idd Pazi ‘Father’ anasema: “Mara nyingi nasema sifa za kipa wa kigeni lazima awe na kiwango bora zaidi ya wazawa, mfano bao la pili kulikuwa na haja gani ya kupiga chenga wakati anajua Yanga ina washambuliaji hatari kama siyo kuwataka maneno ya watu kumshambulia.
“Tanzania tuna makipa wazuri zaidi ya hao kina Noble, mfano mzuri huyo Parapanda licha ya kufungwa mabao mawili ila alionesha uhai wa kuwepo golini.”