Lwanga Injini isiyoimbwa Simba

Tuesday February 16 2021
lwanga pic
By Thomas Ng'itu

MASHABIKI wa klabu ya Simba kwa sasa hata akosekane kiungo wao mahiri, Jonas Mkude hawana presha na hilo kutokana na kuwa na viungo imara katika nafasi hiyo.

Simba katika dirisha dogo ilimsajili kiungo Taddeo Lwanga ambaye baada ya kupata vibali vyake alianza kuvaa jezi za timu hiyo na kuonyesha uwezo bora anapokuwa uwanjani.

lwanga pichaaa

Uwepo wake kwenye dimba bila shaka umewafanya mashabiki wamsahau kimtindo Mkude ambaye alisimamishwa kutokana na matatizo ya utovu wa nidhamu.

Mwanaspoti limemuangalia kwa kina kiungo huyo na huu ni uchambuzi wa kina wa namna ambavyo anacheza pindi anapolipigania chama lake.


Advertisement

UTULIVU

Ukimuangalia Lwanga anapokuwa uwanjani sio mchezaji ambaye anakuwa na mambo mengi. Kazi yake kubwa huwa ni kuhakikisha kwamba kila kitu kinaenda sawa.

Lwanga anapokuwa na mpira huwa hana papara, bali ni utulivu mguuni kwake kuona namna gani ambavyo atahakikisha timu inakuwa salama.

Pia, ni mtu ambaye ana uwezo wa kuanzisha mashambulizi japokuwa anacheza kama kiungo, lakini ana uwezo mkubwa wa kuanzisha mashambulizi.


BAMPA KWA BAMPA

Licha ya kuwa ni mchezaji mtulivu anapokuwa uwanjani, asikwambie mtu huyu jamaa kumpita inabidi ufanye kazi ya ziada.

Lwanga ana spidi ya kutosha kuhakikisha eneo la kiungo la timu pinzani hamzidi mbio kirahisi na kama akipitwa, basi huhakikisha anamalizana na mchezaji wa timu pinzani mapema.

Kiungo huyu pia ameonekana kuwa mzuri katika kupiga kiatu, japo buti hizo huwa hazionekani kirahisi hivyo marefa ni ngumu kuona kwa haraka haraka.

Vilevile amejaliwa pumzi ya kutosha na mwisho wa siku amegeuka kuwa mfano wa mnyama - Punda kwa kuhakikisha anaifanya vizuri kazi yake barabara anapokuwa uwanjani.


ANAUSOMA MCHEZO

Kucheza kwake mashindano makubwa kama ya nchi za Afrika (Afcon) na kucheza soka la kulipwa nchini Misri inawezekana imechangia kwake kuwa mchezaji mwenye uwezo wa kusoma mchezo.

Lwanga ni kiungo ambaye anaendana na biti, yaani anajua mchezo husika naatakiwa kucheza vipi kulingana na viungo wa timu pinzani.

Kuna wakati huwa hana mambo mengi zaidi ya kupiga pasi na kukaba kwa juu, lakini kuna mechi unaweza usimuone hata kidogo akipiga pasi, bali atakuwa anakaba.


PASI ZA UHAKIKA

Licha ya kwamba ni kiungo mkabaji, Lwanga amebarikiwa kuwa na jicho la kupiga pasi za uhakika kwenda kwa washambuliaji au viungo wenzake.

Ni nadra sana kwa kiungo mkabaji kuwa na uwezo huo kwani mara kwa mara kazi yao inakuwa katika ukabaji na sio kitu kingine chochote.

Kiungo huyu pia sio muumini sana wa kupiga pasi za nyuma (back pass) badala yake amekuwa ni mtu wa kupiga pasi ambazo zinasonga mbele zaidi kuhakikisha timu inashambulia.


CHAMA, BWALYA WANanawiri

Lwanga katika eneo la kiungo anacheza sambamba na Clatous Chama pamoja na Lary Bwalya, lakini hao wenzake ni wazuri zaidi katika kuchezea mpira.

Kutokana na ukabaji wake anawafanya Bwalya na Chama wawe huru katika kuchezea mpira kwani wanakuwa hawana kazi kubwa ya kukaba.

Hilo pia wanapokutana na timu yenye viungo wengi muda mwingine huwa anazidiwa kwani anakuwa hana msaidizi wa kuhakikisha anafanya kazi kama yake.

Kutokana na tatizo hilo huifanya Simba kusukumiwa mashambulizi kwani kiungo kinakuwa tayari kimekatika.


Msikie pawasa

Aliyekuwa beki wa zamani katika klabu hiyo na timu ya Taifa Tanzania, Boniface Pawasa anasema Simba imepata kiungo mzuri, lakini wanatakiwa wazidi kumpa muda wa kuzoea na kujiweka fiti.

Pawasa anasema alimuona kiungo huyo katika fainali za Afcon zilizofanyika Misri akiwa na kikosi cha Uganda na ndipo alipotambua uwezo wake.

“Ni kiungo mzuri sana lakini anahitaji mtu wa kumsaidia kukaba kwa sababu wengi wanaomzunguka sio watu wa kukaba kabisa, kwa hiyo muda mwingine inampa wakati mgumu kutimiza majukumu yake,” anasema.

“Pia Lwanga ana utofauti mkubwa sana na Mkude hasa kwenye pasi zake, yeye anakuwa mtu wa kupiga pasi za mbele wakati Mkude ni mtu wa kupiga pasi za nyuma.”

Pawasa anaongeza kuwa: “Inabidi pia apewe muda mwingi wa kucheza na Simba wamvumilie kwani licha ya kufanya vizuri bado hajawa Lwanga yule ambaye nilimuona Afcon.”

Advertisement