Luhende: Kashfa dawa za kulevya ziliniharibia, Mecky Mexime akaniokoa
Muktasari:
- Hayo huwezi kuyajua kama hayajakukuta, lakini unaweza kujifunza kupitia aliyekuwa beki wa Yanga, David Charles Luhende ambaye aliwahi kukutwa na kashfa ya matumizi wa unga (Dawa za kulevya).
MAISHA yanaweza kubadilika wakati wowote bila hata kutarajia ni muda gani na yatakuaje. Mbaya zaidi ukiwa mtu maarufu kwani ukubwa wa jina lako unaweza kuwa sawa na tatizo lako.
Hayo huwezi kuyajua kama hayajakukuta, lakini unaweza kujifunza kupitia aliyekuwa beki wa Yanga, David Charles Luhende ambaye aliwahi kukutwa na kashfa ya matumizi wa unga (Dawa za kulevya).
Anafunguka namna ilivyokuwa ngumu kwake kupita katika kipindi hicho kigumu kilichomfanya arudi nyumbani na kuona safari yake ya soka imeingia doa.
Licha ya kucheza soka kwa misimu 13, lakini yapo mengi ambayo aliyapitia kwa kipindi chote ikiwemo mafanikio kama kuingia katika kinyang’anyiro cha beki na kikosi bora, changamoto na hata kumbukumbu mbaya.
YANGA YA SASA
David ambaye aliitumikia Yanga misimu miwili anaweka wazi utofauti wa wakati alipokuwa akicheza na sasa ni upi.
“Mpira umebadilika na Yanga ya sasa imeongezewa motisha hata sehemu wanapoishi na mazingira kwa ujumla ni mazuri, wakati wetu hata malipo hayakuwa makubwa kama ilivyo sasa.
Nakumbuka sana wingi wa mashabiki, kwa upande wangu napenda kucheza kukiwa na mashabiki wengi kuna kitu wanakiongeza na nikicheza kinyume na hapo basi huwa nahisi kama niko mazoezini.”
KOCHA NISIEMSAHAU
David ambaye aliwahi kuitumikia Yanga lakini hakuondoka vizuri baada ya kupata sifa mbaya anamtaja Kiongozi asiyemsahau.
“Kocha ambaye sitamsahau ni Mecky Mexime kwa sababu alikuwa na mimi kipindi kigumu ambacho nilipata kashfa ya kuwa natumia unga lakini bado hakuniacha.
Nilirudi nyumbani lakini alinifuata na kunirudishia heshima na kunipa imani iliyonifanya nijihisi kama nina nafasi, jambo ambalo lilinifanya nisikate tamaa katika safari yangu ya soka.”
KILICHOKWAMISHA DILI LA YANGA
Baada ya kutoka Yanga beki huyo aliwahi kuhitajiwa tena lakini mwisho safari ya kurejea katika klabu hiyo haikuzaa matunda na anasema sababu.
“Dili la kurudi kweli lilikuwepo lakini kipindi Yanga inataka nirudi pale viongozi wangu nao waliniita tena kutaka kufahamu ofa niliyopewa ila wakaona mimi ndiye mwandamizi hivyo sio rahisi kutoka ijapo mkataba umekwisha kumalizika.
Kweli nilikuwa naipenda Yanga ule wingi wa mashabiki ila kilichotokea hakikunipa amani moyoni ndiyo maana sikutaka tena ingekuwa Simba ningeenda.”
BEKI BORA
Luhende ambaye aliwahi kuwa na rekodi ya kuwania tuzo ya beki bora wa msimu wakati yupo Yanga anafunguka na kuwataja wachezaji wanaocheza katika nafasi yake ambao kwake anawaona kuwa ni bora
Anamtaja beki wa Simba Mohamed Hussein kama ndio bora zaidi kwake licha ya kuwepo kwa chipukizi wengine ambao wanauwasha vizuri tu katika timu zao.
Tshabalala anarekodi ya kuitumikia Simba misimu 13 akitokea Kagera Sugar ambayo Luhende ndio anaichezea kwa sasa.
“Kwa Tanzania beki bora kwa muda niliocheza mimi na yeye lakini bado watu wanatuzungumzia mazuri na kwa kiwango alichocheza.
Hivyo wakati najipongeza lazima na yeye nimpe maua yake ni Tshabalala kwani amekuwa mkongwe lakini hatari lakini kwa vijana wa sasa ni Pascal Msindo.”
MSIMU BORA
Baada ya kuchezea ligi ya Tanzania miaka 13 lakini Waswahili wanasema siku hazifanani, ndio maana anaamua kulifungukia Mwanaspoti kuhusu msimu wake bora zaidi na mbaya pia.
Anautaja msimu aliokuwa Yanga wakati alipopata nafasi ya kuwania tuzo ya beki bora wa msimu ingawa hakufanikiwa kupata ila aliingia kwenye kikosi bora cha msimu.
“Msimu bora zaidi kwake ulikuwa wa 2019/20 na nilikuwa kwenye kiwango bora mpaka kuwekwa katika tuzo za kushindani beki na niliingia kikosi bora cha msimu.”
Nilipata ofa nje za kwenda kucheza nje ya Nchi lakini haikufainikiwa ijapokuwa mpango huo bado upo,Mpango huo upo ila unapata nini cha kukufanya uendele kucheza mbali zaidi, ishu kubwa inayowafanya wengi wasiende nje ni maslahi.”
“Msimu uliopita ulikuwa mgumu zaidi kwani timu yangu mpaka inafika mwisho haikuwa na uhakika wa kusalia hivyo kwangu kama beki haikuwa rekodi nzuri.”
Mechi ambayo sitaisahau ilikuwa ya Simba na Yanga ambapo ulimalizika kwa sare ya 3-3 kwani bosi alitaka turudishe mabao matano tuliyowahi kufungwa na kuanzia hapo angetuoa bonasi kubwa kama tungevuka yale tuliyofunga.”
KIZAZI HIKI
Ukongwe wake kwenye tasnia unatosha kabisa kuonyesha kipaji kikubwa alichonacho kwani kwa miaka yote 13 bado amesalia kwenye kiwango kile kile.
Anafunguka sababu za wachezaji wengi wa enzi zake kama Hussein Shabalala, Jonas Mkude, Shomari Kapombe na wengineo ambao ni wa muda mrefu lakini mpaka sasa wanatumika.
“Vijana wa sasahivi watakaochezwa kwa muda mrefu kama sisi basi watahitaji pongezi maana wakati wetu hatukuwa na vitu ambavyo vinaweza kuchukua muda mwingi kuliko mazoezi.
Vitu kama Simu walikuwa wanavyo watu wachache sana, lakini kuwa na Wanawake wengi ambao wanachangia kudhoofisha kipaji cha wachezaji, kuna vitu vingi lakini starehe zimekuwa nyingi nje ya mpira na imekuwa ngumu kwao kuacha.”
KUHUSU LIGI
Wakati Staa huyo alipoanza mpira Ligi ya Tanzania haikuwa juu kama ilivyo sasa, mpaka kushika nafasi ya tano kwa ubora Afrika.
Anasema Ligi sasa imekuwa sana na ni faida kwa wachezaji kwani maslahi yanaongezeka, kwani wakati huu mchezaji mgeni anapokea pesa ndefu kuliko wa sasa.
“Hii ni Ligi bora sana ndio maana watu wengi wa nje wanaikimbilia, na kukua kwake kunaongeza maslahi kwa wachezaji.
Wakati nipo Yanga malipo ya mchezaji wa juu kabisa haikuzidi Milioni nane kwa mwezi na hakuwa mzawa, lakini ukuaji wa ligi yetu sasa unasikia watu wanapata pesa nzuri tu.
MWISHO LINI
Baada ya kulitumikia Soka kwa muda mrefu anafunguka kuhusu mipango yake, huku akisisitiza kuwa hana hata mawazo ya kustaafu kwa sababu bado anahitajika.
“Siwezi kusema safari yangu itaishia Kagera au lini kwani bado nina mkataba wa mwaka mmoja na kama msimu ukiisha nitajua muelekeo.
Bado nipo sana sifikiri kuacha mpira kwa sasa licha ya kucheza misimu 13 lakini bado najiona naweza kufanya makubwa.”
UJIO WA KOCHA
Kagera ambayo ilimleta kocha mpya hivi karibu ambaye amekwisha kucheza mechi tatu ambazo zimetoa matumaini mapya, Beki huyo wa muda mrefu anafunguka kumuhusu anasema kuwa;
“Kocha mpya ameongeza kitu ndio maana ili uitwe Mwalimu ni lazima kuwe na vitu vingi, Pia ni Mzazi hivyo kuna wakati anakuwa mkali hasa uwanjani na mazoezini na akikukosea basi utamuona anakuomba msamaha baadae.”
WAZAWA WANAKWAMA HAPA
Kumekuwa na maswali mengi kwa mashabiki juu ya wachezaji wazawa kuzidiwa kete na wakigeni ambao wanakuja kucheza katika timu za hapa Tanzania.
“Wacheza mpira hakuna kwa sasa ijapokuwa riziki imekuja tofauti na zamani, Mtu anaweza kununua gari kwa pesa ya bonasi.
Kikosi cha kwanza timu kubwa wazawa wanaoanza inaonyesha tu nguvu ya wachezaji wa nyumbani ilivyo, wageni wengi wanaokuja wanapiga kazi kwa sababu wanajua hakuna familia ya kuwasaidia.
Ukienda ugenini lazima uishi kwa tahadhari na kujifunza sana ili usikosee, ila ukiwa nyumbani unaweza kufanya lolote bila kujali kwa sababu huna cha kupoteza.”
SOKA LA TANZANIA
Kutokana na uzoefu mkubwa alionao juu ya soka la Tanzania Luhende anaweka wazi kuwa kuna mambo anayoyaona hayanyooka bado.
“Tuwe wa kweli, kwani kuna vitu vingi ambavyo tunadanganyana, hakuna uzalendo hasa kwa viongozi kwani wao ndio wanakuwa wa kwanza kuchukua wachezaji kwa sababu ya jina la mtu sio kiwango chake.
MAFANIKIO
Kila mtu kwenye maisha yake anapenda kuona anapatan mafanikio kwenye kila anachofanya ili kuwavutia wengine hasa na kwa kipindi hiki ambacho vijana wengi wanakimbilia kucheza soka.
Luhende anasema kuwa, mafanikio hayakosekani na anafurahi kwa sababu mpira umemfanya aweze kusimama na kujitegemea kama kijana.
“Kwa miaka 12 sasa wazazi wake hawajui kula yake wala kuvaa kwake jambo ambalo ni la mafanikio zaidi nje na yale ambayo sitaki kuyaweka wazi.
Kuwa na nyumba kwa wachezaji ni kitu cha kawaida sana, kwani sasahivi wengi wanamiliki lakini sio kila kitu kwenye maisha na kiufupi nina mafanikio mengi.”