Liverpool, Man United utamu upo hapa Anfield
Muktasari:
- Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Liverpool imekutana na vipigo vitatu mfululizo kwenye michuano yote.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL pengine imejeruhiwa, lakini Manchester United itahitaji kuwa fiti kwenye maeneo mengi kupata matokeo ya uwanjani Anfield, Jumapili.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Liverpool imekutana na vipigo vitatu mfululizo kwenye michuano yote.
Mechi yao ya mwisho, kikosi hicho kinachonolewa na Arne Slot kilichapwa na Chelsea, shukrani kwa bao la dakika za majeruhi la mtokea benchi Estevao.
Man United kwa upande imeshinda mechi ya mwisho kabla ya kuingia kwenye mapumziko ya mechi za kimataifa baada ya kuichapa Sunderland 2-0 uwanjani Old Trafford.
Ushindi unaamini utamwondolea presha kocha Ruben Amorim. Ushindi pia utaifanya Man United kupanda kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Lakini, jambo hilo litakwenda sambamba na kumweka kwenye wakati mgumu kocha Slot kwenye kibarua chake huko Anfield.
Katika mechi hiyo, Man United inaweza kutumia njia kadhaa kupeleka majanga kwa kocha Slot na kumweka hatarini kupoteza kibarua chake.
- Jinsi gani kutumia udhaifu wa Van Dijk
Virgil van Dijk amekuwa mmoja wa mabeki bota kabisa wa kati kuwahi kutokea kwenye Ligi Kuu England. Lakini, katika mechi za karibuni, Mdachi huyo ameonekana kuwa dhaifu na tatizo kubwa kwenye safu ya ulinzi ya Liverpool. Van Dijk amekuwa akipangwa sambamba na Ibrahima Konate. Mabeki hao kwa sasa hasa Van Dijk ameonekana kutokuwa na uwezo wa kupambana jino kwa jino na washambuliaji wasumbufu.
Hiyo ina maana, washambuliaji wa Man United kama Bryan Mbeumo, Matheus Cunha na Benjamin Sesko watakuwa na nafasi kubwa ya kuiweka safu hiyo ya Liverpool kwenye wakati mgumu muda wote.
Dhidi ya Chelsea, ilionekana Moises Caicedo alifunga bao la mbali, lakini alipata nafasi hiyo baada ya makosa ya Van Dijk. Man United pia inaweza kutumia nafasi hiyo kwa kumtumia Sesko kumvuruga Konate, ili kuwaruhusu Bruno Fernandes na Mason Mount kufunga kwa mbali.
2. Jinsi ya kufunika sehemu ya kiungo
Man United inaingia uwanjani kucheza dhidi ya timu yenye kundi kubwa la wachezaji mahiri kwenye sehemu ya kiungo. Lakini, inaweza kutawala eneo hilo na kushinda vita endapo kama itamtumia Kobbie Mainoo.
Endapo kama ataanzishwa kwenye kikosi cha kwanza, Mainoo ana uwezo mkubwa wa kuzivunjavunja nguvu za viungo wa Liverpool kutokana na uwezo wake wa kukaa na mpira na kupiga pasi. Hilo litakuwa muhimu katika Man United kuanzisha mashambulizi ya ushindi wakati itakapofanikiwa kuurudisha mpira kwenye himaya yao kutoka katikatika ya uwanjani. Mainoo ataweza kumpunguzia mzigo Fernandes, ambaye mara nyingi amekuwa akijaribu kufanya mambo mengi uwanjani. Nahodha huyo wa Man United anacheza eneo kubwa sana kwa ajili ya Man United, hivyo wakati mwingine anakuwa hayupo kwenye maeneo muhimu kitu ambacho Mainoo anaweza kuficha huo udhaifu na kuifanya Man United kutawama kwenye eneo hilo la katikati ya uwanja.
Faida moja ya Fernandes ni kwamba atakwenda kuwaongezea mzigo Liverpool upande wa pembeni na hapo itafanya Man United kutengeneza nafasi za kushambulia. Amorim anapaswa kumwaamini Mainoo.
3. Amorim apite kwenye nyayo za Crystal Palace
Kocha Oliver Glasner amekuwa akipata mafanikio makubwa huko Crystal Palace alioongoza timu hiyo kushinda Kombe la FA msimu uliopita na Ngao ya Jamii. Alicheza fomesheni ya 3-4-3 kama ya Amorim, lakini alikuwa na namna tofauti. Mtindo wake ulifanya kazi nzuri dhidi ya Liverpool, Septemba, ambapo Palace ilishinda 2-1 uwanjani Selhurst Park. Glasner alitumia mtindo wa kuwakabia kwa juu Liverpool na hivyo kuwafanya wafanye makose mengi, huku udhaifu wa mabeki wa miamba hiyo ya Anfield uliipa faida Palace. Kocha Amorim amekuwa na mtindo tofauti, timu yake inakabia chini na kutumia zaidi mashambuliaji ya kushtukiza.
Kwenye mchezo huo wa Anfield, kocha Amorim anaweza kuiga namna Palace ilivyoikabili Liverpool na kupata matokeo mazuri ili kupeleka majanga zaidi kwa kocha Slot.
4. Tatizo la Mo Salah
Mohamed Salah hayupo kwenye kiwango bora sana cha soka lake tangu msimu huu ulipoanza. Staa huyo wa kimataifa wa Misri amefunga mara mbili katika mechi saba alizocheza kwenye Ligi Kuu England hadi sasa. Na kinachoelezwa ni kwamba tatizo linalomkabili Salah kwa sasa ni kukosekana kwa Trent Alexander-Arnold, kwenye upande wa kulia kutokana na staa huyo wa England kutimkia zake Real Madrid.
Salah alikuwa akifaidika sana na uwezo wa Alexander-Arnold kupiga pasi na kumfanya akimbie nyuma ya mpira, lakini sasa hapati huduma kama hiyo msimu huu akiwa anacheza na beki mpya wa kulia, Jeremie Frimpong.
Na kingine, Frimpong anacheza pembeni sana na hivyo anashindwa kumfanya Mo Salah kupata nafasi ya kutosha kuingia ndani ya boksi ili kwenda kuleta madhara kwa wapinzani. Kitu kingine ni kwamba Mo Salah amesogezwa mbali kidogo na goli kutokana na ujio wa washambuliaji Alexander Isak na Hugo Ekiktie, ambao wamekuwa wachoyo wakitaka kufunga wao kwanza ili kutengenezea mazingira mazuri kuliko kumpa pasi Mo Salah. Tofauti na ilivyokuwa kwa Darwin Nunez na Roberto Firmino, ambao walikuwa wakimtengenezea Mo Salah nafasi za mabao, lakini kwa sasa mkali huyo wa Misri yupo kwenye matatizo makubwa.