Leo FC zasherehekea uteuzi wa Papa Leo

Muktasari:
- Kama ilivyo kwa mujibu wa utaratibu wa Vatican, Papa mpya amechagua jina analotaka kulitumia. Nalo ni Papa Leo wa 14.
HABARI kubwa ya hivi karibuni duniani ni kifo cha Papa Francis na kuchaguliwa kwa Kadinali Robert Prevost (69) wa Marekani kushika nafasi hii kubwa ya uongozi ya Kanisa Katoliki.
Kama ilivyo kwa mujibu wa utaratibu wa Vatican, Papa mpya amechagua jina analotaka kulitumia. Nalo ni Papa Leo wa 14.
Jina la Leo sio tu lilipokewa kwa furaha na shangwe na waumini wa Kanisa, bali pia na klabu mbalimbali za soka duniani ambazo majina yao ni Leo.
Mara tu baada ya Papa mpya kutangazwa kwa jina la Leo baadhi ya klabu zilifanya sherehe kubwa kufurahia jina hilo, ambalo pia ni ufupisho wa jina la supastaa wa soka, Lionel Messi anayechezea klabu ya Inter Miami baada ya kutamba akiwa na Barcelona na PSG.
Hili jina la Leo lina maana moja katika lugha mbalimbali na zote zikimaanisha ni simba. Katika lugha ambazo maana ya Leo ni simba ni pamoja na za Kiingereza, Kifaransa, Kilatino, Kirusi, Kihispania, Kihindi (Gujerati), Kigiriki na Kireno.
Miongoni mwa klabu hizi ni Leo FC ya Gibraltar, eneo lenye majabali la rasi (kama kisiwa) linalomilikiwa na Uingereza liliopo kusini mwa Hispania.
Wengine hutamka Leone kumaanisha ni simba na ndio maana zipo timu zenye jina la Leone FC kama ya Colombia ambayo sare yake ni chapa ya simba juu na chini.
Hata logo za timu hizi huwa na mchoro wa simba, kama ilivyo kwa Simba ya Tanzania.
Tafsiri ya jina la Siera Leone iliopo Afrika Magharibi ni amani. Nchi hii ilikuwa na simba wengi, lakini wametoweka na wa mwisho alionekana mwaka 2017.
Katika eneo hili lenye ukubwa wa kilomita 6.8 za mraba wanaishi watu karibu 40,000 na lina klabu kama 20 za kandanda na kati ya hizi 11, ikiwamo Leo FC, ndio zinaocheza Ligi Kuu.
Klabu hizi zinazo wachezaji kutoka Misri, Jamhuri ya Kati ya Africa na Congo.
Kabla ya hapo Leo FC iliyoanzishwa mwaka 2004 mwanzo iliitwa Santos & Sons, jina la mtu ambaye ni maarufu katika eneo hilo na aliwahi kuwa meya na mchezaji kandanda aliyetegemewa.
Jina la utani la klabu hii ambayo sare yake inayo chapa ya simba ni ‘Blue Lions’ (Simba wa Buluu).
Klabu nyingine ni Leo Futsal ya Armenia ambayo inashiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo yenye ukubwa wa kilomita za mraba 29,743 na yenye watu milioni 3.
Leo Futsal ambayo ilianzishwa mwaka 2019 inao uwanja wake ambao unaingia watu 6,500 na sare yake ni rangi nyekundu.
Klabu hii hivi sasa inashika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu ya nchi hiyo inayoshirikisha timu 11. Armenia ambayo idadi ya watu wake ni milioni 3 inazo klabu 163 za kandanda za wanaume na nne za wanawake.
Mara baada ya kutangazwa Papa mpya klabu hii ilifanya sherehe za siku mbili kwenye uwanja wake wenye kuchukua watu 7,000 na kutoa zawadi mbalimbali kwa watoto.
Katika jiji la St. Louis , Marekani ipo klabu inayoitwa Leo. Hii ni St Luis Leo ambayo inaendeshwa na kanisa tokea kuundwa kwake 1908.
Hii ni moja ya timu kongwe za soka Marekani na katika miaka ya nyuma ilishiriki katika mashindano makubwa, lakini sasa inacheza katika daraja la chini kwa burudani na haipo katika ligi yoyote ile.
Katika nchi ndogo ya Suriname (watu 740,000) iliopo kaskazini mashariki ya ukanda wa pwani wa Amerika ya Kusini ipo klabu inayoitwa SV Leo Vitor.
Klabu hi iliundwa mwaka 1934 na wafanyakazi wa kampuni ya sigara na katika mwaka 1934 ikawa klabu ya kwanza kuingia katika mashindano ya Shirikisho la Kanda la Amerika ya Kati na Caribbean.
Hivi sasa ipo nafasi ya tatu katika ligi inayoshirikisha klabu. Nchi hii ina watu karibu 600,000 na uwanja wake unachukua watu 4,000. Nembo ya klabu hii ni chapa ya simba. Mashabiki wa timu hii mara nyingi huvaa fulana zenye chapa ya simba zilizoandikwa Leo FC na wengine huenda uwanjani wakiwa wamebeba sanamu za simba na wanawake huvaa vidani vyenye simba wa bati, shaba, fedha au dhahabu.
Sehemu kubwa ya Suriname ina misitu, lakini haina simba ila wapo chui wachache na kima kila pembe ya nchi ambao huingia majumbani kuiba chakula kama wanavyofanya paka hapa kwetu. Miongoni mwa vituko vya timu za Suriname ni wakati mwingine timu ikiona mwamuzi anawaonea basi huamua kujifunga wenyewe. Una maoni? Tuma ujumbe au piga namba 0658-376 417